Baada ya kejeli, shutuma na udhalilishaji uliofanywa dhidi yao, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ‘wamekikaanga’ Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukionya kisithubutu kubadili rasimu yenye maoni halisi ya wananchi.
Wajumbe wa tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, Humphrey Polepole na Awadhi, wametoa angalizo hilo wakati wa mdahalo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam kuhusu Katiba Mpya.
Wengine waliokuwa wazungumzaji katika mdahalo huo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Umma), Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kwa kipindi cha zaidi ya siku 60 la Bunge Maalum la Katiba linaloongozwa na Samuel Sitta, wajumbe wake hususani waliotokana na CCM, waliikejeli tume hiyo na kusema miongoni mwa wajumbe wake, hawana nia njema kwa nchi.
Karipio la Polepole na Awadhi linatokana na kuwapo mzozo unaohusishwa na pendekezo la kuwapo kwa muundo wa serikali tatu ambao unapingwa na CCM.Ingawa walipata muda mfupi katika mdahalo wa jana ulioandaliwa kupitia kipindi cha ‘Tanzania tunayoitaka,’ Polepole na Awadhi, waliionya CCM kutoichakachua rasimu halisi huku wakiwaasa Watanzania kufuatilia mchakato huo kwa makini.
AWADHI
Awadhi, alisema tume ya Jaji Warioba ilikusanya maoni ya wananchi katika wilaya 143, ikifanya mikutano 12 kwa kila wilaya ya Tanzania Bara na 22 huko Zanzibar, hivyo kufanya jumla yake kuwa 1,700.
Pia, alisema kulikuwa na mabaraza ya katiba 177 na kwamba asasi za kiraia 614 ziliunda mabaraza ambapo kwa ujumla wake, yalifanikisha kupatikana kwa rasimu halisi, hivyo akahoji, “iweje misingi yake ipinduliwe na kiundwe kitu kipya kwa watu 612?”
Hoja hiyo ilikuwa ni kujibu kauli tofauti zilizotolewa na Wasira ambaye alitumia takwimu kadhaa kuikosoa tume ya Warioba na kuhalalisha mabadiliko yanayofanywa na Bunge Maalum la Katiba.
Hata hivyo, Awadhi alipingana na Wasira kwa maelezo kuwa tume ya Warioba haikufikia kuandaa rasimu kupitia takwimu pekee.
“Tume ilichukua sampuli ya maoni, sasa kama wao (CCM) wanasema waliotaka serikali tatu ni wachache, wewe unapitisha serikali mbili kwa takwimu zipi?” alihoji.
Alisema, wajumbe wa iliyokuwa tume ya Jaji Warioba, wana haki ya kuendelea kuuzungumzia mchakato huo, licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwakejeli na kumtaka Jaji Warioba ‘afunge mdomo.’
HOFU
Awadhi alisema ipo hatari kubwa kwa taifa ikiwa rasimu halisi ‘itachakachuliwa na kuruhusu kuwapo kwa serikali mbili.
“Serikali mbili ina mambo mengi ambayo rasimu inayojadiliwa haina,” alisema na kutaja miongoni mwa hayo kuwa ni haki za adhi, serikali za mitaa na rasilimali za umma, kwa kadri ilivyowasilishwa na wananchi.
“Maoni ya wananchi yaliyogusia haki hizo na nyingine yalizungumzwa kwa misingi mikuu ambayo huwezi kwenda kudai kupitia rasimu hii (iliyochakachuliwa,” alisema.
WENGI NA WACHACHE:
Awadhi, alisema hoja dhana ya ‘walio wengi’ na `wachache’ ni matokeo ya mifumo mikongwe na Katiba ya sasa inayolalamikiwa, na kwamba kutumia (mifumo mikongwe) izalishe Katiba Mpya italiingiza taifa kwenye matatizo.
POLEPOLE: HATUKUWA NA MISIMAMO YA KISIASA
Naye Polepole, alisema wajumbe wa tume ya jaji Warioba, hawakuongozwa na misimamo ya kisiasa, bali maoni ya wananchi.
Hata hivyo, alisema kuna mambo mengi hayamo kwenye rasimu na hayakujitokeza, hali inayowaumiza mioyo, na kwamba mengine yalitajwa kwenye mdahalo huo.
“Si vema na haki kinachoendelea sasa hivi ingawa Katiba Mpya ni mchakato wa kisheria na siasa, lakini hiyo haina maana kwamba umilikiwe na vyama vya siasa,” alisema.
Alisema Katiba Mpya inahitaji kujenga muafaka, kufikia maridhiano, kuweka nidhamu kwenye mjadala, ushiriki makini unaozingatia uhuru wa wajumbe, mambo aliyosema hayajaonekana hadi sasa.
Alisema mchakato huo ukiachwa kwa vyama vya siasa kwa kudhani wana dhamana ya kuleta Katiba Mpya, hakutalitendea haki taifa hili.
PINDA: VIONGOZI WA DINI WAOMBEENI UKAWA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaomba viongozi wa dini nchini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili warudi bungeni kumaliza mchakato wa katiba.
Alitoa ombi hilo wakati wa ibada maalumu ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ruvuma, Amoni Mwenda, kwenye kanisa hilo Usharika wa Songea, ambako mamia ya waumini pamoja na viongozi, wakiwamo maaskofu, mawaziri na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu walihudhuria.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment