WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, July 11, 2014

Maximo kapotea njia Yanga


Marcio M�ximo

Kocha wa Chelsea ya Ligi Kuu ya England, José Mourinho (51), aliwahi kusema: "Makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe" akimaanisha makocha ndiyo wamekuwa watu wa kwanza kuchukuliwa hatua na viongozi pindi timu inapokuwa na matokeo mabaya.

Unapozungumzia makocha waliowahi kuleta mafanikio katika kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars), bila shaka hutamsahau Marcio Máximo, Mbrazil aliyetua tena nchini, lakini safari hii akitua klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Kutua kwa mtaalam huyo ni faraja kubwa kwa wapenzi wa Yanga ambao pamoja na kutolewa katika hatua ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na waliokuwa mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri, wameukosa pia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliokwenda Azam FC.

Mkataba wa miaka miwili wa kuinoa klabu ya Yanga ni habari njema pia kwa viongozi wa klabu hiyo ambao inaonekana wazi wametuliza jazba za wanachama wao walioamua kuwaongeza mwaka mmoja 'bure' wa kukaa madarani baada ya kusikia mipango ya ujio wa mtaalam huyo, Máximo.

Lakini, ajira ya kuinoa Yanga inaweza kuwa kama Mbrazil huyo amepotea njia baada ya kuamua kujishusha hadhi kutoka kuinoa timu ya taifa hadi klabu (tena inayotoka ndani ya nchi ambayo alifundisha timu yake ya taifa) kwa sababu klabu ya Yanga haina historia nzuri katika mikataba inayoingia na makocha wa kigeni.

MAFANIKIO YA MAXIMO
Maximo aliyezaliwa Aprili 29, 1962 mjini Rio de Janeiro, si tu alipandisha kiwango cha Taifa Stars ikakaribia kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2007 na kuinua hamasa ya Watanzania wengi kuingia uwanjani kuitazama timu yao ya Taifa, bali ana mafanikio makubwa katika kazi yake ya ukocha.

Akiwa ni miongoni mwa makocha waliokuwa wakiunda benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Brazil ya U-17 na U-20 kuanzia 1992 hadi 1993, Maximo alipika vijana wakali wa Kibrazil wakiwamo 'kiboko ya Wajerumani' Ronaldo de Lima na mtaalam wa chenga za maudhi Ronaldinho Gaucho. 

Juni 5, 2003, kocha huyo alijiunga na klabu ya Livingston Football ya Scotland kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza Mbrazil kuinoa timu ya taifa hilo. Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri baada ya kuingoza timu hiyo kwa mechi tisa ikishinda tatu, sare tatu na kuchezea kipigo mara tatu, akaamua kujiuzulu Oktoba 14.

Juni 29, 2006, Máximo aliteuliwa kuwa kocha wa Taifa Stars na kuiwezesha timu hiyo kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizopigwa Ivory Coast kuanzia Februari 22 hadi Machi 8, 2009. Tanzania ilifuzu baada ya kuipiga Sudan kwa jumla ya mabao 5-2.

Máximo aliongeza mkataba wake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuinoa Stars hadi July 2010, lakini mikoba yake ikarithiwa na Mdenmark Jan Poulsen kutokana na kile kilichodaiwa kuwa Mbrazil huyo hakuwa na vyeti vya ukocha vinavyotambulika kimataifa kwa muda wote aliokuwa akikinoa kikosi cha Stars.

Baada ya kuondoka Tanzania, Máximo aliajiriwa kama kocha mpya wa klabu ya Democrata ya kwao Brazil Desemba 2011, lakini alifukuzwa na klabu hiyo Februari 13, 2012.

Juni 2012, ilivumishwa kuwa Máximo angelikuwa mrithi wa Mserbia Kostadin Papic  katika benchi la ufundi la Yanga, lakini kazi hiyo ilitwaliwa na Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye baadaye licha ya kuipa ubingwa wa Kombe la Kagame klabu hiyo ya Jangwani, alifukuzwa kwa fedheha baada ya timu kutoka suluhu na Tanzania Prisons kisha kufungwa 3-0 na Mtibwa katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu Bara msimu wa 2012/13.

Novemba 2012, Máximo alichukua maamuzi ya kubaki kwao Brazil akiinoa timu ya Francana hadi Juni 28, mwaka huu alipotangazwa na kuthibitisha ametia saini mkataba wa miaka miwili kuinoa Yanga, ambayo ni moja kati ya klabu mbili kubwa na kongwe nchini.

KWANINI AMEREJEA YANGA?
Mara tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Máximo alisema ameamua kurejea nchini kwa kuwa Watanzania wanamhitaji na anawapenda.

Lakini mshahara wa dola za Marekani 15,000 unaodaiwa kulipwa kwa Máximo kwa mwezi ambao ni pungufu ya dola 2,500 tu ikilinganishwa na alivyokuwa akilipwa na serikali (dola 17,500 kwa mwezi) akiwa kocha wa Taifa Stars (kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia), pengine ndicho kilichomvutia Mbrazil huyo.

“Mshahara ni siri ya muajiriwa na muajiri, lakini Máximo analipwa na muajiri wake, klabu ya Yanga,” alisema Baraka Kizuguto, kaimu ofisa habari wa Yanga baada ya kuulizwa na NIPASHE jana kuhusu hofu ya wanachama wa Yanga juu ya malipo ya mshahara wa kocha huyo kama uongozi uliopo madarakani hautapata kura za kutosha katika uchaguzi mkuu ujao.
 
MIAKA 10 MAKOCHA 10
Tangu 1991, Yanga imenolewa na makocha 24 ndani ya miaka 23 ikiwa ni wastani wa kocha mmoja kila mwaka wakianza na 1991-1993-- Syllersaid Mziray (marehemu), 1993-- Nzoyisaba Tauzany (marehemu) raia wa Burundi, 1995 --Tambwe Leya (marehemu) raia wa DRC, 1997-- Sunday Kayuni na 1997-- Steve McLennan (Uingereza).

Mwaka 1998-- Tito Mwaluvanda (marehemu), 1999-- Raoul Shungu (DRC), 2001-- Boniface Mkwasa, 2002-- Jack Chamangwana (Malawi), 2004-- Jean Polycarpe Bonganya (DRC), 2004-- Mziray, 2005-- Kenny Mwaisabula, 2006-- Chamangwana, 2007-- Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia), 2007-- Razack Ssiwa (Kenya), 2007-- Chamangwana, 2008-- Dusan Kondic (Serbia),  2010-- Kostadin Papic (Serbia), 2011-- Sam Timbe (Uganda), 2011-- Papic, 2012-- Tom Saintfiet (Ubelgiji), 2012-- Ernie Brandts (Uholanzi), Hans van Der Pluijm (Uholanzi) na sasa Máximo (Brazil).

Máximo anakuwa kocha wa 22 kuifundisha Yanga (ukiacha makocha waliotimuliwa na kurudishwa) tangu mwaka 1991, na katika kipindi chote hicho ni makocha watatu tu waliorudishwa kazini baada ya kuondoka, ambao ni marehemu Mziray, Mmalawi Chamangwana na Mserbia Papic.

Baadhi ya makocha waliamua kuondoka wenyewe, lakini wengi wao walifukuzwa na tawala mbalimbali zilizopita katika klabu hiyo ya Jangwani katika kipindi chote hicho.

Vurugu za uongozi wa Yanga kufukuza ovyo makocha zilianza 1991, tofauti na miaka ya nyuma tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1935.

Mapema 1991 Yanga ilimchukua Mziray, ambaye aliondoka kwa watani wao wa jadi, Simba baada ya kushushwa cheo kutoka Simba A hadi Simba B.
Marehemu Mziray aliiongoza Yanga kwa miaka miwili akisaidiwa na Mkwasa na akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Muungano mfululizo huku ikitinga fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ambako walifungwa kwa matuta  na Simba.

Mziray aliondoka Yanga baada ya kupata ofa nzuri kutoka Pan African na Yanga iliajiri tena kocha wa kigeni baada ya muda mrefu, ikimleta Mrundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ 1993 (marehemu) ambaye aliendelea kufanya kazi na Mkwasa na katika mwaka wake wa kwanza, akaiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda.

Tauzany aliporejea katika Ligi Kuu akaendelea vizuri na kazi, lakini haikuchukua muda akaingia kwenye mgogoro na mfadhili wa klabu hiyo wakati huo, Abbas Gulamali (sasa marehemu).

Tauzany alitumia vyombo vya habari kupambana na Gulamali na ilifikia hadi akawa anachafua jina lake kwa kudai alikuwa anafanya biashara haramu. Ilikuwa vita kali na mbaya zaidi Mrundi huyo alikuwa anakubalika mbele ya wanachama, hivyo kumfukuza ikawa tabu.

Gulamali alimrejesha kocha ambaye alifanya kazi na kupendwa mno Yanga, Tambwe Leya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye awali alifanya kazi mwaka 1975 na 1976, akiiwezesha Yanga kuifunga Simba katika mechi ya kihistoria Nyamagana kabla ya kuipa Kombe la kwanza la Kagame 1975, kwa kuwafunga hao hao Simba 2-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Tambwe alitua nchini mwishoni mwa 1994 na jukumu lake alilopewa ni Ukurugenzi wa Ufundi, ambapo yeye akaamua kutengeneza timu nzuri ya vijana, iliyopewa jina Black Stars.

Tauzany na kikosi cha Yanga chenye nyota kibao nchini wakati huo, akafungwa mabao 4-1 na Simba na hapo ndipo timu nzima na kocha wao wakafukuzwa; walibakishwa wachezaji saba tu ambao waliunganishwa na yosso wa Tambwe kutengeneza kikosi kipya kilichofanya vizuri hadi kutinga Robo Fainali ya Kombe la Washindi 1996.

Tambwe naye akaondolewa kwa visa na badala yake akaajiriwa kocha mzalendo, Sunday Kayuni 1997 ambaye naye pia hakudumu kwani alifukuzwa na akaajiriwa kocha wa muda kutoka Uingereza, Steve McLennan mwaka huo huo.

McLennan, kocha Mzungu wa kwanza, aliondolewa na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa msaidizi wake, Juma Pondamali ‘Mensah’.

Yanga ikaajiri kocha wa muda, ambaye alikuwa hajulikani kabisa, Tito Oswald Mwaluvanda (sasa marehemu) ambaye katika kujikosha kwa wanachama, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu pia) akawa anamtambulisha kama msimamizi wa mazoezi, wakati timu inatafuta kocha.

Msimamizi wa mazoezi alichukua ubingwa wa Ligi Kuu na Ligi ya Muungano 1998, tena akiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi katika Ligi ya Bara, mabao 8-0 waliyoifunga Kagera Shooting Stars (sasa Kagera Sugar), tena ikiwa inafundishwa na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo, Zacharia Kinanda ‘Arrigo Sachi’ (sasa marehemu), Edibilly Jonas Lunyamila akifunga mabao matano peke yake.

Hata hivyo, 1998 mara tu baada ya Yanga kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, marehemu Mwaluvanda aliyekuwa anasaidiwa na Felix Minziro, waliondolewa na akaajiriwa kocha kutoka DRC, Raoul Shungu aliyeingia na msaidizi wake, Abeid Mziba ‘Tekero’.

Shungu aliipa Yanga Kombe la tatu la Kagame, katika michuano iliyofanyika mjini Kampala, Uganda 1999, lakini 2000 akaondolewa na akaajiriwa Mkwasa, ambaye naye mwishoni mwa 2001 akatupiwa virago.

Baada ya Mkwasa, akaajiriwa Mmalawi Chamangwana ambaye 2003 alifukuzwa na 2004 akaajiriwa kocha kutoka DRC, Jean Polycarpe Bonghanya ambaye naye hakudumu, mwaka huo huo akaondolewa na Mziray alirudishwa. 

Hata hivyo, Mziray alikuwa anasoma ishara za nyakati, alipoona upepo unaelekea kuwa mbaya, alimwachia timu aliyekuwa msaidizi wake, Mwaisabula.

Mwaisabula aliendelea hadi 2005, lakini baadaye mwaka huo akaondolewa kisha Chamangwana kurejeshwa. Mmalawi huyo alifanya kazi hadi 2007 alipompisha Mserbia Micho.

Micho aliondoka kwa sababu ambazo hadi leo bado hazieleweki, kwani alikubalika na timu ilikuwa inafanya vizuri. Baada ya kuondoka kwa Mserbia huyo, aliyekuwa kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa alikabidhiwa timu.

Ssiwa aliiongoza Yanga kutwaa Kombe la Tusker mwaka 2007 mjini Mwanza, lakini aliporudi kwenye ligi, timu ikafanya vibaya, akatupiwa virago kisha uongozi ukamrejesha tena Chamangwana.  

Kocha huyo alitimuliwa kisha kuajiriwa tena Mserbia, tena Profesa Dusan Kondic, aliyekuja na wasaidizi wawili, Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan. Kondic naye akafukuzwa 2010 na kuajiriwa Mserbia mwenzake Kostadin Papic, ambaye pia alifukuzwa na kuajiriwa Mganda Sam Timbe.

Timbe, licha ya kuipa timu Kombe la nne la Kagame 2011, alifukuzwa miezi miwili baadaye na kurejeshwa Papic, ambaye pia hata kabla msimu 2011/12 wa Ligi Kuu haujamalizika, alitupiwa virago na kuajirwa Mbelgiji Saintfiet.

Saintfiet alihitimisha historia yake Yanga ndani ya siku 80, akicheza mechi 14, akishinda 12, sare moja na kufungwa  mbili- huku akiacha Kombe la tano la Kagame Yanga na kumpisha Mholanzi Brandts kufungua ukurasa mpya.

Brandts aliyeikuta Yanga ikiwa na hali mbaya, aliiongoza kutwaa ubingwa wa VPL msimu wa 2012/13  lakini uongozi wa Yanga ukatangaza kumtimua siku moja tu baada ya timu yao kufungwa mabao 3-1 na Simba katika mechi ya 'ndondo' ya 'Nani Mtani Jembe' Desemba mwaka jana.

Baada ya kumtimua Brandts na benchi nzima la ufundi, Yanga ilimleta Mholanzi Pluijm lakini kocha huyo na aliyekuwa msaidizi wake, Mkwasa wamesoma alama za nyakati na kuamua kutimkia Uarabuni, hivyo mzigo kutua kwa Máximo.

Maximo anaonekana kuwavutia Wanayanga wakiamini atakuwa suluhisho la matatizo yao, kuleta mataji mengi Jangwani na kupandisha kiwango cha timu yao kama alivyofanya kwa Taifa Stars.

Lakini ukweli ni kwamba Yanga haina tatizo la wataalam wa ufundi na imekuwa ikitimua makocha bila sababu za msingi. Makocha wengi wanatemwa na klabu hiyo kutokana na ama kuwa wakweli kupita kiasi kama alivyofanya Saintfiet kwa kukosoa viwanja vya mazoezi, hoteli na kambi ambazo timu ilikuwa ikipelekwa au kwa kushindwa tu kuifunga Simba kama ilivyomtokea Brandts.

Akisaidiwa na Minziro, Mholanzi huyo alitimuliwa huku timu yake ikiongoza ligi, kisha wakaajiriwa makocha (Pluijm, Mkwasa na Pondamali) walioishusha timu na kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili huku kukitokea migogoro ndani ya klabu hiyo ikiwahusisha pia baadhi ya wachezaji.
Je, Máximo ana kitu gani cha ziada ambacho makocha waliopita Yanga, wakiwamo maprofessa, hawakuwa nacho? 

Ni wazi kwamba Mbrazil huyo atakuwa na wakati mgumu pindi timu hiyo itakapokuwa na matokeo mabaya au kufungwa na watani wao wa jadi, Simba kama ilivyokuwa kwa makocha wengine waliopita Yanga.

Mbaya zaidi,  Máximo amerejea nchini wakati ambao kila kitu kimebadilika. Kila mtu, wakiwamo viongozi wa soka. Uongozi wa Yanga umeripotiwa ukisema kwamba hautamuingilia katika kazi yake, lakini historia inauhukumu.

Máximo hawezi kuwa suluhisho la matatizo ya Yanga kwa sababu hawezi kujenga uwanja wa kisasa, hawezi kuleta vitega uchumi Jangwani, hawezi kukomesha fitina za soka la Tanzania na hana uwezo wa kuwazuia viongozi wa Yanga kumfukuza. Hapo ndipo ukweli wa kauli ya Mourinho "makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe" inapoweza kutimia pia kwa Maximo.

Kikubwa lazima viongozi wa soka nchini waangalie upya chanzo cha kuyumba kwa soka letu la Bongo. Mfumo mbovu katika uongozi kwa kuendekeza siasa katika soka na kutowajika kwa viongozi, wachezaji na hata wanachama wa klabu za michezo kutaendelea kuitafuna sekta ya michezo nchini.

MAKOCHA YANGA TANGU 1991
1.  1991: Syllersaid Mziray(marehemu)
2.  1993: Nzoyisaba Tauzany (marehemu) (Burundi)
3.  1995: Tambwe Leya (marehemu) (DRC)
4.  1997: Sunday Kayuni
5.  1997: Steve McLennan (Uinegereza)
6.  1998: Tito Mwaluvanda(marehemu)
7.  1999: Raoul Shungu (DRC)
8.  2001: Charles Boniface Mkwasa
9.  2002: Jack Chamangwana (Malawi)
10. 2004: Jean Polycarpe Bonganya (DRC)
11. 2004: Syllersaid Mziray (marehemu)
12. 2005: Kenny Mwaisabula
13. 2006: Jack Chamangwana (Malawi)
14. 2007: Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia)
15. 2007: Razack Ssiwa (Kenya)
16. 2007: Jack Chamangwana (Malawi)
17. 2008: Dusan Kondic (Serbia)
18. 2010: Kostadin Papic (Serbia)
19. 2011: Sam Timbe (Uganda)
20. 2011: Kostadin Papic (Serbia)
21. 2012: Tom Saintfiet    (Ubelgiji)
22. 2012: Ernie Brandts (Uholanzi)
23. 2014: Hans van Der Pluijm (Uholanzi)
24. 2014: Marcio Máximo (Brazil)
Nani anafuata?
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment