KATIKA
wakati huu, Nauona umuhimu wa kukumbushana swali hili nililopata
kuliuliza. Maana, kwa mwanadamu usipojua unataka nini, basi, usishangazwe na
matokeo ya ulichokifanyia kazi. Chaweza kuwa chochote kile.
Na
swali hili la mfumo wa Serikali si mwanzo wa mwisho wa matatizo yetu yajayo
kama taifa, bali ni mwisho wa mwanzo wa tulichodhani kuwa ni kutatua matatizo
yetu ya muungano.
Tunakoelekea
si kuzuri, maana, tumeamua kuacha kutumia busara na hekima na badala yake
tunatanguliza ushabiki wa vyama na hata makundi na watu tunaowapenda. Yako wapi
mapenzi kwa nchi tuliyozaliwa?
Maana,
tulidhani ni mabadiliko makubwa yamefanyika katika nchi yetu pale
ulipozinduliwa kwa kishindo mchakato wa kupata Katiba Mpya. Wengi
wameanza kukata tamaa.
Tulidhani
yangelikuwa mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977.
Ni pale ambapo Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977
yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na hata mfumo
wa uongozi wa Serikali.
Katika dunia
hii, mabadiliko ya kijamii hupelekea mabadiliko ya kisiasa. Na
WanaShosholojia wanasema, kuwa sababu mbili zenye kupelekea
mabadiliko hayo; sababu za ndani ya jamii husika (endogenous) na sababu
za nje ya jamii (exogenous).
Kwa
upande wetu, tunaona kuwa, sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma
kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.
Na kwa jamii yetu kwa
upana wake, ingelikuwa na sababu za msingi za kuyafurahia
mabadiliko haya, maana, ni sawa na mwanadamu aliyepewa kikombe chenye nusu
ujazo wa maziwa. Utafahamu kama amefurahia au amechukizwa kwa
namna atakavyochagua kukielezea kikombe kile; anayekiona ni ’
kikombe nusu cha maziwa’ anaonyesha kutoridhika, na anayekiona
ni ’ kikombe kilichobaki nusu tu kujaa’ huyo amekifurahia
na anaonyesha matumaini kuwa iko siku kitajaa. Inahusu kuwa na matarajio chanya
(Optimism) na kuwa na matarajio hasi (Pessimism)
Na
hakika, Rais Jakaya Kikwete ameonyesha tangu mwanzo, dhamira yake ya kutuletea
mabadiliko kama taifa. Na Wajumbe wa Tume yaKatiba walifanya
kazi njema iliyotufikisha kwenye hatua ya kuwepo kwa Rasimu ya kwanza
ya Katiba na hata ya Pili.
Nimepata
kuandika, kuwa katika dunia ya sasa, hakuna anayeweza kuyazuia mabadiliko
yanayotokana na msukumo wa ndani ya jamii- Kule Urusi ya
zamani, Mikhael Gorbachev alipoanzisha mageuzi makubwa
ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi watu hawakuamini
walichokiona. Gorbachev aliuona wakati uliobadilika. Mabadiliko
yale makubwa ya kimfumo kule Urusi yalipata majina mawili; Perestroika na
Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .
Kabla
ya mageuzi yale makubwa, Urusi ilikuwa ikikabiliwa na tatizo
la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa uwazi. Jamii ilijawa
hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na usiri mkubwa.
Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa.
Gorbachev, daima atakumbukwa kwa ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya
Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.
Na
hakika, ‘ Kuzaliwa kwa Katiba Mpya’ katika
nchi ingelipaswa iwe ni sawa na ’ Taifa kujivua gamba’. Maana,
kujivua gamba huku kama taifa kunapaswa kuendane na kuanza kubadili mifumo yetu
ya kifikra. Tuanze sasa kufikiri juu ya malengo ya taifa, kwa maana ya ndoto za
taifa letu badala ya kutanguliza sana malengo ya vyama vyetu au zaidi malengo
binafsi ya vyeo na mamlaka.
Nchi
yetu ni kama nyumba kongwe. Tuendelee kwa umoja wetu kuifanya
kazi ya kuikarabati upya nyumba yetu. Ipate mwonekano mpya.
Kuikarabati upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba
yenyewe. Kutakuwa na fito na vipande vya matofali vya kurudishia.
Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio, fito na matofali
mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa
umeikarabati upya nyumba yako.
Maana,
katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii
huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu
wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine kushiriki uongozi wa
nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo
baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata
na kuwatupa. Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza?
Ni fikra za kiwendawazimu.
Nchi
yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi
kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na
busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu
yenye kuambukiza kwa haraka.
Kamwe
tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni nchi yetu.
Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi au chama cha siasa chenye haki
zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Na kwa
mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini. Na imani ya wananchi kwa
taifa na viongozi wao ni shina la matumaini yao. Inakuwaje basi mwananchi
anapokosa imani na taifa na hata kwa
kiongozi? Katiba yetu iwe chachu ya kurudisha mioyo ya uzalendo
kwa taifa letu.
Mungu
Ibariki Tanzania.
www.raiamwema.co.tz: maggid mjengwa
No comments:
Post a Comment