Mbeya/Moshi. Rais Jakaya Kikwete amesema msimamo wa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umemweka njiapanda sawa na Watanzania wengine wanaoshangaa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipohutubia waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) waliokusanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini. (MWANANCHI)(FS)
“Kwa sasa matumaini pekee ya Ukawa kurejea bungeni ni mazungumzo yanayoendelea, yanayovihusisha vyama vinne vikubwa nchini chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,” alisema Rais Kikwete.
Kauli ya Rais Kikwete ni ya pili kwa kiongozi wa juu kuwazungumzia Ukawa kuiweka Serikali njiapanda baada ya ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa Juni 26 mkoani Tanga.
Pinda alisema hatima ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea uamuzi wa wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni. Alikuwa akizungumza na mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa.
Awali Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais alimwomba kuingilia kati kuhakikisha Bunge la Katiba linatimiza matakwa yaliyokusudiwa.
Askofu Mtokambali alimsihi Rais kukwamua mgogoro uliopo kwa kuhakikisha wajumbe wa Bunge la Katiba wanaungana na kutekeleza matakwa ya sheria, kanuni ya kupata Katiba Mapya.
Akijibu, Rais Kikwete alisema masikitiko ya Askofu huyo na Watanzania wengine ni sawa na masikitiko yake na kwamba rai yake ni kuwasihi wajumbe hao wajipange kurejea kwenye mkutano ujao wa Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alifafanua kwamba hatua pekee ambayo inatoa mwanga wa kuleta suluhu ni ile aliyoichukua msajili wa vyama vya siasa nchini kuwaita viongozi wakuu wa vyama vya CUF, Chadema, CCM na NCCR-Mageuzi hivi karibuni ambako viongozi hao wameonyesha ukomavu katika mazungumzo mazuri na yenye mwelekeo wa matumaini.
“Nampongeza msajili wa vyama vya siasa kwa hekima aliyoitumia kwa kuanzisha mazungumzo hayo na nawashukuru sana viongozi wa vyama vya siasa husika kwa kujadili kwa busara yenye mwelekeo wa kutatua tatizo hilo,” alisema.
Alisema vyama vinavyoshiriki kwenye mazungumzo hayo ndiyo vikubwa nchini na kwa vyovyote vile mambo yatakwenda vizuri hata hivyo alifafanua kuwa mazungumzo ya aina hiyo pia yanatarajiwa kuwashirikisha wadau wengine.
Nawaomba maaskofu, masheikh, wachungaji, maimamu, manabii kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba Mpya warudi bungeni Agosti 5 kukamilisha kazi ndani ya siku 60 nilizowaongezea bila kuomba nyingine tena,’’ alisema.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment