Wakati ule tulionya kwamba misimamo hiyo isingetuwezesha kupata Katiba Mpya. Badala ya kujadili hoja zilizotokana na mijadala kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge iliyowasilishwa na Kamati ya Muda ya Kanuni, wajumbe wengi walijikita katika kutetea misimamo ya vyama na kuyakataa baadhi ya mapendekezo muhimu yaliyowasilishwa na Kamati ya Kanuni.
Mvutano huo katika Bunge hilo ulikuwa mwendelezo wa hali ya kutovumiliana tuliyoishuhudia wakati Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokuwa likijadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011. Pamoja na Muswada huo kupitishwa na Bunge katika mazingira ya kisiasa, sheria hiyo ilibidi ifanyiwe marekebisho baada ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupelekwa bungeni kutokana na upungufu uliotokana na wabunge kuweka mbele itikadi na misimamo ya vyama vyao vya siasa.
Hivyo, Bunge la Katiba lilipoanza awamu ya pili baada ya kumchagua mwenyekiti wa kudumu lilishindwa kubadili mwelekeo huo hasi. Hivyo wajumbe kuendeleza matusi ya nguoni, kejeli, mipasho, uchochezi na kauli za kibaguzi. Kasi ya mitafaruku miongoni mwa wajumbe pia iliongezeka na kufuta kabisa ndoto za kupata mwafaka wa kitaifa ambao ni muhimu katika kuandaa Katiba Mpya. Tulipata fursa ya kuonya kwamba, katika mazingira hayo tusitazamie muujiza wa kupatikana Katiba Mpya.
Pamoja na kuongezewa muda hadi siku 90 za majadiliano na hatimaye kutoa rasimu ya mwisho ya Katiba Mpya ili ipelekwe kwa wananchi kupigiwa Kura ya Maoni, Bunge lilimaliza muda huo likiwa mikono mitupu, kwa maana ya kutopiga hatua yoyote ya maana na likiwa limetumia zaidi ya Sh40 bilioni za walipakodi. Rais Jakaya Kikwete aliliongezea siku nyingine 60, lakini kutokana na kuwapo kwa ratiba ya Bunge la Bajeti, likaahirishwa hadi mapema mwezi ujao.
Hata hivyo, mpasuko kati ya wajumbe wa chama tawala na wale wa baadhi ya vyama vya upinzani waliokuwa tayari wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulikuwa mkubwa hadi wajumbe wa Ukawa wakasusia Bunge na kusema hawapo tayari kurudi bungeni hadi chama tawala kitakapoheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Tume ya Warioba.
Pande zote zinazokinzana zimekataa kulegeza misimamo. Kwa maana hiyo, Katiba Mpya imeshindikana na inabidi sasa ufanyike uamuzi mgumu. kutokana na ukweli kuwa inahitajika theluthi mbili za wajumbe kutoka sehemu zote mbili za Muungano ili kupitisha Rasimu ya Katiba.
Kwa kuwa bila ya Ukawa theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar haiwezi kupatikana, tunadhani suluhisho mwafaka ni kubadili muundo wa Bunge hilo ili idadi kubwa ya wajumbe itokane na asasi za kiraia badala ya wanasiasa ambao wanaweka mbele itikadi za kisiasa kuliko matakwa mapana ya Taifa.
SOURCE:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment