WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 5, 2013

Taasisi ya Sayansi za Bahari cha Buyu chahitaji bilioni 14



 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano Samia Suluhu Hassan akipata Maelezo kwa Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Sayansi ya Bahari Dkt Narriman Jiddawi juu ya Utunzaji wa Samaki Aquarium wakati wa Ziara ya waziri huko Zanzibar
 
 Mhadhiri Mwandamizi wa Tasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chua Kikuu cha Dar es Salaam Dkt NarrimanJiddawi akimuonyesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Samia Suluhu Hassan aina ya Kasa katika chumba cha Kutunzia samaki[AQUARIUM}wakati wa Ziara ya Kutembelea Tasisi za jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizopo Unguja .
 
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Samia Suluhu Hassan akipata Maelezo juu ya Ujenzi wa Kituo cha tasisi ya Sayansi za Bahari kilichopo Chukwani Unguja kwa Kaimu Mkurugenzi Dkt Christophet Muhando wakati waziri alipofanya Ziara ya Kutembelea Tasisi za Jamhuri za Muungano wa Tanzania zilizopo Unguja [PIcha na Ali Meja]   
 
Kaimu Mkurugemzi waTaasisi ya Sayansi ya Bahari ya chuo kikuu cha Dar es Salaam Dkt Christopher Muhando akimtembeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Jengo la Taasisi ya Sayansi ya Bahari huko Chukwani Mjini Unguja wakati wa Ziara yakutembelea taasisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

ZAIDI ya shilingi bilioni 14 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa chuo cha Taasisi ya  Sayansi za Bahari kilichopo Buyu wilaya ya Magharibi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Hayo yamesemwa leo huko Forodhani mjini Zanzibar na Muhadhiri Dkt. Ntahondi Nyandwi wakati alipokuwa akisoma ripoti ya chuo hicho na rasilimali zake mbele ya Waziri anae shughulikia masuala ya Muungano Samia Suluhu Hassan aliyekuwa katika mfulilizo wa ziara yake kuzitembelea Taasisi za muungano hapa Zanzibar.

Amesema fedha hizo zitahitajika ili kukamilisha ujenzi wa  jengo lote na miundombinu  ikiwemo vifaa vya maabara, sehemu za wanafunzi wa uzamili, zamivu, kumbi za mikutano, ofisi za programu za kimataifa, ofisi za wageni wa kimataifa na mengineyo.

Dk. Nyandwi amesema kupatikana kwa fedha  hizo kutakamilisha mahitaji hayo na mengine ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia  hatua nzuri  na wameshatumia zaidi ya bilioni nne  kwa kujenga miundo mbinu mbalimbali ikiwemo  ofisi za viongozi na madarasa.

“Kwa vile pesa za kumlipa mkandarasi hazikupatikana kwa wakati na hakukuwa na uhakika kuzipata, ujenzi ulisimama Agosti 2008 na mkandarasi aliondoka lakini kwa sasa ujenzi unaendeleo taratibu”alisema Nyandwi . Aidha alifahamisha kuwa ujenzi huo unaendelea kidogo kidogo  kadri fedha zinavyo patikana baada ya kumuomba mkanda rasi awapunguzie gharama na kuweza kumaliza mipango ya awamu ya kwanza na ya pili. 

Nae Waziri wa  Nchi Afisi ya Makamu wa Rais,  Muungano  Samia Suluhu Hassan  amesema kuwa atamuagiza Mkuu wake wa kazi kuja Zanzíbar  kujionea na yeye   Jengo hilo hatua ilio fikiwa.

Aidha alisema kua ujenzi huo utaendelea kidogokidogo mpaka utapomalizika. Maendeleo ya ujenzi wa Taasisi ya sayansi Baharini ni moja ya Taasisi za Chuo  Kikuu cha Dar-es Salaam kampasi  ya Mwalimu Nyerere ambapo umuhimu wa Taasisi hiyo ulianza kujitokeza Mwaka 1978 chini ya sheria Na. 12 ya 1970 ya chuo kikuu cha Dar-slamu kwa tamko la Serikali Na. 34 lililo pitishwa tarehe 16 march 1979.

Chuo hicho kumalizika kwake kufanya kazi za kutafiti nyanja zote za Sayansi za Baharini, kutoa mafunzo ya uzamivu, uzamili katika sayansi ya Bahari ,kutoa ushauri wa kitalamu ,kutoa mafunzo ya Shahada ya kwaza  kwa kulingsana na mahitaji ya  Taifa la Tanzania   kama sehemu ya Taluma kwa vitendo.


IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR LEO 5/4/2013

FEDHA NA MALI YA UMMA ZINAVYOTAFUNWA TANZANIA

 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2011; imeendelea kufichua namna kundi la watumishi wa umma na wafanyabiashara wakubwa wanavyoitafuna Tanzania. Utouh aliwasilisha taarifa hiyo bungeni mwishoni mwa wiki. Fedha na mali za umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ama zinaibwa au zinachukuliwa kwa namna ambayo ni vigumu kuamini kama kweli viongozi wakuu wa kitaifa wana dhamira ya kutokomeza ufisadi uliovuka mipaka.
 

Kuuzwa kwa viwanja, majengo ya Serikali
 

CAG amebaini kuwa kiwanja kilichopo katika Kitalu Na. 10 katika Barabara ya Nyerere, kimeuzwa kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kinyemela. Amesema wakati uuzaji kiwanja hicho ulipaswa uratibiwe na Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC - mrithi wa PSRC), kazi hiyo ilifanywa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria.
 

Nyaraka za mawasiliano kati ya MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina zinazohusiana na uuzaji kiwanja hicho, zinaonyesha kuwa Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina ndiyo waliojihusisha moja kwa moja katika uuzaji wa mali hiyo ya umma, kwa kutoa maelekezo kwenye menejimenti ya CHC. Bodi ya Wakurugenzi haikushirikishwa kabisa.
 

Hatimaye kiwanja hicho kiliuzwa kwa MeTL kwa Sh bilioni 2.046 bila kufuatwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005.
 

Katibu wa Waziri aamuru kampuni ilipwe Sh bilioni 2.34
 

Utata wa matumizi mabaya ya fedha za umma, umemkumba aliyekuwa Katibu wa Waziri mwenye dhamana ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuhusu kiwanja namba 192 kilichopo Barabara ya Nyerere. Alimwandikia barua Mwenyekiti wa PSRC ailipe kampuni ya DRTC Sh milioni 954.72.
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa DRTC akamwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC akitaka alipwe haraka kiasi cha Sh bilioni 2.349. Kwenye barua hiyo, Meneja wa DRTC alisisitiza kuwa malipo hayo ni maelekezo kutoka serikalini, licha ya ukweli kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko madai halisi na akalipwa.
 

Kuuzwa kwa jengo la kampuni ya umma ya TMSC
 

Jengo la kampuni ya Tanzania Motors Services (TMSC) lipo katika kitalu namba 24 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Jengo hilo liliuzwa kwa kwa kampuni ya Saddiq Super Service Station (SSSS) kwa Sh bilioni 1.3. Kampuni hiyo ilitoa malipo ya awali ya asilimia 10, yaani Sh milioni 130. Baadaye Wizara ya Fedha ikaitaarifu CHC kuwa Serikali imeghairi kuliuza jengo hilo lililopo kitalu namba 24 kwa kampuni ya SSSS. Wizara ya Fedha ikaitaka CHC ikubaliane na SSSS kuwafidia, kwani tayari kampuni hiyo ilishatoa kianzio cha Sh milioni 130.
 

Kuona hivyo, kampuni ya SSSS ikawasilisha madai ya kulipwa fidia ya Sh bilioni 3.894 kwa ajili ya kupoteza biashara yake na Sh milioni 500 kama fidia kwa usumbufu. Hatimaye ikaamuliwa kuwa SSSS ilipwe Sh milioni 964 ambamo ndani yake kulikuwa na Sh milioni 130 ilizotoa awali na gharama za usumbufu.
 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikuwa Mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha malipo hayo. Akawasilisha katika Wizara ya Fedha ambayo yeye ni kiongozi, ili ilipe kiasi hicho cha fedha kwa maelekezo ya kikao alichokiongoza yeye mwenyewe.
Kwa uamuzi huo, Wizara ya Fedha ikailipa moja kwa moja SSSS Sh milioni 964.2; ilhali kama ni malipo, basi yalipaswa kufanywa na CHC. Malipo hayo, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, yanaibua maswali juu ya dhamira ya Wizara ya Fedha kulipa fedha hizo haraka haraka bila kuishirikisha Menejimenti wala Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.
 

Malipo ya kushangaza kwa kampuni ya Tantrack
 

Tantrack Agencies ilikuwa mpangaji katika jengo la TMSC lilipo kitalu namba 24, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Ilipanga kwa miaka miwili kuanzia Julai Mosi 1993. Kampuni hiyo inasema ilitumia Sh milioni 24 kukarabati jengo kwa wakati wote wa mkataba wake wa upangaji, licha ya ukweli kwamba jambo hilo halikuwamo kwenye mkataba iliyoingia na TMSC. Ikakataa kulipa ada ya pango ikisema fedha hizo zilizotumika kwenye ukarabati zitambuliwe kuwa ndiyo ada ya pango.
 

Tantrack ikafungua kesi ya madai namba 257 ya mwaka 1995 katika Baraza la Nyumba Mkoa wa Dar es Salaam (DRHT) dhidi ya TMSC, kwa kigezo kwamba TMSC ilikuwa ikivunja makubaliano. Ilifanya hivyo baada ya TMSC kuiandikia barua ikiipa notisi ya miezi sita ihame kutokana na kutotekeleza makubaliano ya mkataba.
 

Wakati hayo yakiendelea, jengo la TMSC likauzwa kwa njia ya mnada kwa African Terminal Limited (ATL) kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa Sh milioni 3. CHC ikapeleka vielelezo vyake mahakamani ikionyesha mkataba ulivyokuwa kati yake na Tantrack. Kabla rufaa haijasikilizwa, ATL ikaweka pingamizi. Sasa ni miaka 15 suala hilo likiwa halijaamuliwa.
CAG anasema imebainika kuwa kuna uzembe na kutowajibika kwa pande zote mbili zinazopambana kwenye mgogoro huo.
 

Utata Kitalu namba 33 kilichotwaliwa na Kampuni ya Maungu Seeds
 

PSRC iliingia makubaliano na kampuni ya Maungu Seeds, kwa ajili ya kununua kiwanda cha Mzizima Maize Mill kilichopo Kitalu namba 33, Barabara ya Saza katika Eneo la Viwanda Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
 

Makubaliano hayo yalitiwa saini Septemba 1, 2004; na gharama ya ununuzi ilikuwa Sh milioni 620. Malipo yalikuwa yafanywe kwa awamu tatu. Maungu ikaanza kulipa Sh milioni 200 na kutoa dhamana ya benki (TIB) ya Sh milioni 420.
Ikakubaliwa kuwa PSRC ingeikabidhi kampuni ya Maungu kiwanda hicho ndani ya miezi mitatu baada ya kutiliana saini ya ununuzi, na kwamba Maungu ingekabidhiwa nyaraka zote baada ya kukamilisha malipo. Iliyokuwa PSRC ikashindwa kukabidhi kiwanda kwa mujibu wa makubaliano kwenye mkataba kutokana na kwamba, kiwanda kilikuwa rehani kwa kampuni ya CDC London ya Uingereza tangu mwaka 1959.
 

Hatimaye, ilipofika Aprili 26, 2006 rehani ikawa imeondolewa, lakini tayari muda wa dhamana ya benki ulikuwa umekwisha. Kiasi cha Sh milioni 420 kikawa hakijalipwa. Mwaka 2010 kampuni ya Maungu ikafungua kesi ya madai na ikaamuriwa kuwa ipewe hati ya eneo yenye namba 6639. PSRC (CHC) ikaamuriwa iilipe Maungu Sh milioni 200 haraka. Fedha hizo ni zilezile ilizokuwa imetoa kama malipo ya awali na ikarejeshewa.
Kimsingi, Maungu ikawa haijalipa chochote, lakini ikawa imepewa kiwanda cha Mzizima bure kabisa bila kulipa kiasi chochote kwa mali hiyo ya umma.
 

Madeni ya Simu 2000 yafutwa kienyeji
 

CAG ameonyesha wasiwasi mkubwa kwa uamuzi wa CHC wa kufuta madeni mengi ya iliyokuwa kampuni ya Simu 2000. Kampuni hiyo iliundwa na kuongozwa na familia ya Mama Anna Mkapa, kwa ajili ya kuuza zilizokuwa mali za Shirika la Posta na Simu. Kuna habari kwamba familia hiyo ilijitwalia mali kadhaa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Miongoni mwa majengo yaliyouzwa ni maghorofa yaliyopo Ilala.
 

Ulaji Chuo cha Ubaharia (DMI)
 

Ukaguzi uliofanywa na CAG umebaini kuwa Sh milioni 83.96 zimelipwa kama takrima na fedha za kujikimu kwa viongozi bila kuidhinishwa na mamlaka za kisheria. Katika malipo hayo, maofisa wa Wizara ya Mawasiliano walilipwa Sh milioni 12; na Sh milioni 51.8 zililipwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la DMI kama posho ya madaraka (honorarium), mafuta na posho ya vikao.
Sh milioni 2.6 zililipwa kwa maofisa wa akaunti wa DMI bila wao wenyewe kuhudhuria vikao; Sh. milioni 10.4 zililipwa kwa watumishi wa DMI kama posho ya kujikimu Juni, 2009 bila wenyewe kuhudhuria kile kilichoitwa kuwa ni kikao cha kikosi kazi cha kupitia mitaala ya DMI.
 

Katika hatua nyingine, DMI ilipokea Sh milioni 385 kwa ajili ya kuwalipa wadeni wake, lakini ukaguzi umebaini kuwa ni 205.8 pekee zilizotumika. Wafanyakazi 12 wa DMI wamelipwa mishahara ya ngazi ya PGSS 5 na zaidi bila kuidhinishwa na Baraza DMI. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala amekuwa akijilipa mshahara kwa kiwango cha PHTS ambacho hakikuidhinishwa.
 

Kompyuta za msaada zaibwa, zanyofolewa vifaa
 

Ukaguzi umebaini kuwa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, kilitoa msaada wa kompyuta 25 kwa DMI kwa ajili ya maktaba yake. DMI ilimlipa wakala wa utoaji vifaa hivyo bandarini Sh milioni tatu Desemba 7, 2007. Lakini hadi ukaguzi unafanywa, kompyuta hizo zilikuwa hazijawasilishwa kama ilivyotarajiwa.
Baadaye imebainika kuwa kati ya kompyuta hizo, ni kompyuta 13 pekee zilizowasilishwa katika maktaba, na kwamba ni kompyuta nne pekee zinazoweza kukarabatiwa. Kompyuta kenda haziwezi kutengenezwa kutokana na kuibwa vifaa muhimu kama Ram, Processors, Hard disks, Power Supply na Mother Boards.
 

Bohari ya Dawa (MSD) inaingiza vifaa feki
 

Pamoja na kuwapo upotevu wa mamilioni ya shilingi zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, CAG amebaini kuwa baadhi ya vifaa na dawa vinavyosambazwa na MSD havina ubora. Ametoa mfano wa mashine za kupima shinikizo la damu na vifaa vinavyotumika kubebea wagonjwa.
 

Pia dawa kama kwinini imebainika kuwa inasambazwa nyingine ikiwa na ubora wa hali ya chini, kutokana na pengine kutohifadhiwa vizuri. Aidha, ukaguzi umebaini kuwa vitambaa vinavyotumika kunyonya damu wakati wa upasuaji huwa vipo chini ya kiwango.
 

Ukaguzi umebaini kuwa Sh bilioni 3.95, dola milioni 9.4 na euro milioni 1.5 ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD na hivyo kukiuka Sheri ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni 41 ya Tangazo la Serikali namba 97.
Aidha, imebainika kuwa MSD imefanya ununuzi kwa zabuni nane huku upitiaji wa zabuni hiyo ukifanywa na mtu mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Zabuni zilizofikwa na hali hiyo ni za Sh milioni 134.4, dola 10,000 na Euro milioni 1.5.
 

Ulaji wa kutisha Bandari ya Dar es Salaam
 

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba na kampuni ya Singapore PTE Limited kwa ajili ya kuweka ‘Radio Data Terminals’ Februari 2010 wenye thamani ya dola 339,600. Punde tu baada ya TPA kupata radio hizo, mambo kadhaa yalianza kujitokeza.
 

Kwanza, menejimenti ikabaini kuwa ‘Radio Data Terminals’ hizo  haziwezi kufanya kazi bila kile kinachoitwa kitaalamu kuwa ni ‘Access Points’ (virusha mawimbi). Hatua hiyo ikaifanya PTA iingie mkataba mwingine na Singapore PTE Limited Juni 21, 2010 kwa ajili ya kuweka virusha mawimbi 68 kwa gharama ya dola 399,000. Baada ya kununua vifaa hivyo, ikabainika tena kwamba haviwezi kufungwa juu minara ya iliyokuwapo. Kwa sababu hiyo, PTA ikaingia mkataba mwingine na CATS (T) Limited Septemba 17, 2010 kwa ajili ya kuweka minara mingine kwa gharama ya dola 133,000.
 

CAG anasema katika ukaguzi wake kwamba pamoja na kufanya yote hayo, bado ‘Radio Data Terminals’ hazikuweza kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa vile ilipaswa iunganishwe kwenye mkongo (fibre optic) kwa gharama ya dola 553,800 za Marekani. Kazi hiyo ikafanywa na EMEC.
 

Kwa kifupi, TPA ikajiingiza kwenye gharama za ziada za dola milioni 1.09 na bado kilichokusudiwa hakikuweza kupatikana kwa muda kutoka kwa mkandarasi aitwaye CATS. Hakuna gharama zozote ambazo TPA imeweza kuzidai kutokana na kucheleweshwa au kuingia gharama kubwa kiasi hicho. Hii inatiliwa shaka kuwa ndiyo ulaji wenyewe.
 

Sh milioni 100 zaliwa bila jengo la bosi TPA
 

TPA iliingia mkataba na kampuni ya AF MULT-CON LIMITED kujenga makazi ya Meneja wa Bandari Tanga kwa gharama ya Sh milioni 500. Utangazaji zabuni umebainika kuwa ulifuata taratibu zote. Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kuna uzembe katika kufuatilia taratibu za mkataba wa zabuni. CAG mwenyewe alizuru eneo lililokusudiwa kujengwa jengo hilo, na hakushuhudia malighafi wala shughuli yoyote ya kuhalalisha malipo ya Sh milioni 100 ambazo tayari mzabuni alishalipwa.
 

Mkataba mwingine wa utata TPA
 

Wakati wa ukaguzi, CAG alibaini kuwa TPA iliingia mkataba na kampuni ya Chibeshi Construction kwa ajili ya kujenga uzio katika kitalu namba moja kwenye Bandari ya Mtwara. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni 679.8. Ulitiwa saini Aprili 14, 2009 na ujenzi ulipaswa ukamilike kwa wiki 26 kutoka siku ya kutiwa saini mkataba.
Kabla ya mkandarasi kuanza ujenzi, TPA ikaamua kuvunja mkataba huo kwa maelezo kwamba hapakuwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Uamuzi huo ukaifanya TPA iingie hasara ya Sh milioni 92.6 kama adhabu au faini. Ikamlipa mkandarasi. Fedha zikachukuliwa na mkandarasi bila kufanya kazi yoyote.
 

Mkataba mwingine wa utata waingiza hasara TPA
 

Katika ukaguzi, CAG amebaini kuwa PTA iliingia mkataba na kampuni ya WiA kwa ajili ya kuweka mawasiliano ya intaneti katika Makao Makuu ya TPA, na bandari nyingine zilizo chini ya Mamlaka hiyo. Mkataba huo ulikuwa wa miezi mitatu kuanzia Julai 2010. Hata hivyo, mradi huo haukukamilika baada ya muda uliopangwa kumalizika. TPA ikaamua kumwongeza mkandarasi muda hadi Februari 28, 2011 na mkandarasi bado alishindwa. TPA ilipaswa kumtoza mkandarasi kiasi cha dola 95,000 kwa kushindwa kutekeleza mkataba kwa muda, lakini haikufanya hivyo.
 

Hazina yalipa mamilioni ya mishahara hewa
 

Wakati wa ukaguzi, CAG amebaini kuwa Hazina imeendelea kutumia mamilioni ya shilingi kuwalipa wafanyakazi hewa katika taasisi mbalimbali. Katika ukaguzi huo, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) kumekuwa na majina 42 ya watu wanaolipwa mishahara licha ya ukweli kwamba si watumishi wa chuo hicho. Imebainika kuwa kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni, 2010 MUCE ilipokea Sh milioni 612 na kuwalipa watumishi hewa.
 

Katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Hazina imeendelea kuwalipa mishahara watu ambao si watumishi chuoni hapo. Baadhi ya waliostaafu na MNMA kupeleka majina yao Hazina, wanaendelea kulipwa. Hali hiyo imesababisha Sh milioni 134.74 zitumike kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina.
Katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, orodha ya majina kutoka Hazina inaonyesha kuwa hata wale ambao si watumishi tena wa chuo hicho, majina yao yapo kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa mishahara. Kuanzi Oktoba 2010, Machi 2011, Mei 2011 na Juni 2011 Sh milioni 194.4 zimetumika kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho.
 

Imebainika pia kwamba baadhi ya watumishi waliojiuzulu au kuacha kazi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), majina yao yameendelea kuwa kwenye orodha ya Hazina ya watumishi wanaopaswa kulipwa. Sh milioni 181 zilikuwa zimetumika kuwalipa hadi wakati ambao CAG alikuwa akiandaa ripoti hii.
Katika Chuo cha Elimu Dar es Salaam nako mambo ni kama hayo. Watu 56 ambao hawapo kwenye utumishi wameweza kulipwa Sh milioni 778.7 licha ya ukweli kwamba hawapo chuoni hapo. Hakuna rekodi inayoonyesha kuwa fedha hizo zilirejeshwa Hazina.
 

Fedha za Mifuko ya Jamii hatarini
 

Ukaguzi umebaini kuwa upo udhaifu mkubwa na hatari ya kupotea kwa mabilioni ya shilingi zilizowekezwa na Mifuko ya Jamii katika miradi mbalimbali nchini.
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetumia Sh bilioni 234.054 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kati ya fedha hizo, ni Sh bilioni 35.218 pekee ambazo zilisainiwa katika ujenzi wakati wa awamu ya kwanza. Fedha zilizotolewa katika ujenzi wa awamu ya pili, hazikusainiwa. Majengo ya awamu ya kwanza yamekamilika, lakini Serikali haijaanza kurejesha fedha inazodaiwa na NSSF zenye riba ya Sh bilioni 14.157.
 

Wabunge waondolewe kwenye Bodi
 

Kwa mara nyingine, CAG amependekeza wabunge wasiwemo kwenye Bodi za Mashirika ya Umma na bodi nyingine. Anasema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba kuwamo kwao kwenye bodi husababisha mgongano wa masilahi.
Anasema ni Tanzania pekee ambayo wabunge ni wajumbe katika bodi za mashirika ya aina hiyo. Utaratibu kama huo haupatikani mahali kwingineko duniani wala katika vyombo ambavyo Tanzania ni mwanachama.
 

Uteuzi wa wajumbe wa Bodi
 

CAG anatoa mapendekezo kwamba maofisa watendaji wakuu wa kampuni/mashirika ni vizuri wakateuliwa na Bodi za Wakurugenzi badala ya utaratibu wa sasa, ambako ni Rais anayewateua. Anapendekeza Rais aachiwe madaraka ya kuteua mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi.
Mapendekezo hayo, kwa mujibu wa CAG, yanalenga kuifanya Bodi ya Wakurugenzi iweze kuisimamia vema menejimenti na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.
 

Serikali ibane ununuzi mashangingi
 

CAG anapendekeza kuwa ili fedha nyingi zielekezwe kwenye maendeleo, Serikali haina budi kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi hasa kwenye ununuzi wa magari ya kifahari, gharama za semina na kupunguza idadi ya wanaosafiri kwenye misafara ya viongozi ndani na nje ya nchi.

Tuesday, April 2, 2013

JK AKUTANA NA NAIBU RAIS WA KENYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete  amekutana na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto ambaye alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.

Akiongea na mgeni huyo katika hoteli ya Seronera iliyoko katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani Mara, Rais Kikwete amempongeza Mhe Ruto na Rais mteule wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta, kwa ushindi wao kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya.
Mhe Rais pia alimueleza Mhe Rutto furaha yake pamoja na kuridhishwa na jinsi uchaguzi ulivyofanyika kwa amani katika nchi hiyo.

Alielelezea matumaini yake ya kuwa urafiki uliopo kati ya Tanzania na Kenya utadumishwa pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mhe Rutto, ambaye aliwasili mkoani Mara wiki iliyopita akiwa na mke wake na watoto, ameondoka leo baada ya chakula cha mchana alichoandaliwa na mwenyeji wake.ru4 1a350
 
 JK akimuongoza kuelekea kwenye chakula cha mchana  Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto na mkewe Rachel Chebet katika hoteli ya kitalii ye Seronera katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani Mara. Mhe Ruto alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.


ru5 42b9a
JK akipozi na familia ya  Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto.

ru31 d84c7

JK akiongea na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto
CHANZO: IKULU

Ndugu yangu Zitto; kuhusu mimi kumfahamu Ludovic


2 40a62

Ndugu zangu,
Ndugu yangu January Makamba alipata kuyasema haya, Desemba 9, 2012 pale Nkrumah Hall;
“ Msituone sisi wanasiasa tunakumbatiana mkadhani wote tunapendana. Tukivua mashati mkaangalia migongo yetu mtaona alama za mikuki!”- January Makamba

Nilikuwepo pale Nkrumah Hall, nilimsikia ndugu yangu January Makamba akiyatamka hayo. Kuna waliocheka, lakini kuna tuliobaki tukitafakari. Nitarudi kwenye tafsiri ya kauli hiyo ya January.
Lakini kwanza, nianze kwa kukiri kuwa nimechelewa kufuatilia mjadala huu hapa jukwaani juu ya ‘ Ludo kurubuniwa’ na mengineyo kuhusiana na sakata la Ludo kama anavyojulikana humu  na Lwakatare.
Ukweli nilikuwa mapumziko ya Pasaka mbugani Ruaha kwa siku kadhaa nikiwa na familia yangu. Hivyo, kuwa mbali na mitandao na habari nyingine za dunia.
 Ndugu yangu Zitto,
Umeandika yafuatayo kwenye jukwaa hili, nakunukuu;
“Nimeshtushwa sana na habari ninazoendelea kuzipata kuhusu bwana huyu. Nimesoma pia maandiko yake hapa na hasa maandiko dhidi yangu yenye maneno makali kweli. Kikweli sikujua kabisa kama bwana huyu alikuwa kitengo muhimu kama cha usalama kwenye chama changu ambacho mimi ni Naibu Katibu Mkuu.
Hata hivyo muhimu kuacha haki itendeke. Sio vema kumhukumu sasa mpaka ukweli wote ujidhihirishe.

Napenda kukumbusha kwamba Ukweli hautengenezwi, bali hutafutwa. Mwisho wa siku tutajua huyu bwana alikuwa anafanya kazi ya nani na kwa nini? Kwa nini yeye atekwe siku moja na Mhariri Kibanda na awe miongoni mwa watu wa mwanzo kufika hospitali kumwona Kibanda.

Ningependa pia ndugu yangu Maggid aweke wazi na kinaga ubaga mahusiano yake na bwana Ludovick. “
Ndugu yangu Zitto,
Nimeamua kwa makusudi kukaa kimya na kutoshiriki kuchangia au kujibu michango ya wengine na haswa linapotajwa jina langu kwa namna moja au nyingine. Nafanya hivyo sasa nikiamini, kuwa Zitto hukuwa mitandaoni, kwamba ulikuwa kambini ( JKT) na pengine hukuweza kuyasoma maelezo yangu ya ufafanuzi wa jinsi nilivyofahamiana na Ludovick na hata hatua nilizochukua  mara sakata la Ludovick na Lwakatare pale Machi 17 lilipowekwa wazi kwenye moja ya magazeti  kuwa ni ‘ tuhuma dhidi ya kushiriki kupanga njama za ugaidi’.
Ndugu yangu Zitto,
Nakufahamu zaidi wewe kama Zitto kuliko ninavyomfahamu Ludovick ambaye nilimfahamu kaka kijana mwanaharakati aliyekuwa akifuatilia makala zangu tangu jarida la Rai. Alipata kunipigia simu na kuniomba kukutana nae kama ilivyo kwa wengi ambao hupenda wakutane na kuzungumza nami mbali ya kusoma makala zangu au kunifuatilia kwenye blogu. Bila shaka hali hiyo inakukuta wewe Zitto pia.
Ni katika namna hiyo, ikatokea kwa Ludovick kunisaidia na kazi za kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog na kunisaidia kunipelekea, kwa niaba yangu,  ankara zangu kwa Watangazaji wa kwenye Mjengwablog kama vile Vodacom na Benki ya Azania. Ni kwa sababu mimi kwa miaka kumi sasa naishi na kufanya kazi nikiwa Iringa na kwamba ofisi nyingi ziko Dar.
Ndugu yangu Zitto,
Kwa zaidi ya miaka 25 sasa, kupitia kalamu yangu ninekuwa nikifanya kazi ya jamii. Na jamii ina maana ya watu. Kuna wakati nilimwambia jamaa yangu mmoja, kuwa leo hii nikitembelea Gereza lolote lile hapa Tanzania, yumkini nitakutana na maafande wawili au watatu wa Jeshi la Magereza wanaonifahamu kupitia makala zangu pengine tangu enzi za Rai. Na kwamba, kama nitaingia kutembelea ndani gerezani, yumkini nitakutana na wafungwa hata kumi ambao wananifahamu kupitia makala zangu za tangu enzi za Rai.
Sasa nikisimama na kuongea na wafungwa hao ambao wengine wamefungwa kwa makosa ya ujambazi kuna atakayedhani kuwa Maggid huyu lazima atakuwa mhalifu na pengine jambazi, maana inakuwaje amefahamiana na wahalifu walio gerezani!
Naam, kwa kazi zetu hizi za kijamii, huwezi ukamtilia mashaka kila mwanajamii unayekutana nae barabarani, anayeongea nawe kwenye simu au anayetaka kukutana nawe mzungumze.
  1. mimi kama mtu mzima, ninapokutana na kijana wa Kitanzania anayeonyesha kufuatilia maandiko yangu na kazi zangu za kwenye blogu, kisha akaonyesha kuwa na utayari wa kunisaidia kutuma picha au ku-upload kazi za mtandaoni ikiwamo magazeti ambayo Dar yanapatikana mapema zaidi, na mimi nina shida ya usaidizi huo, ni kwa nini basi nishindwe kushukuru kujitolea kwake?
Mjengwablog inatembelewa na watu wengi. Kazi zimekuwa nyingi sana. Ni chombo cha habari kama vingine, lakini, hakifanyi mauzo kama ya magazeti na wala  hakipewi ruzuku ya Serikali,  na mara nyingi hata matangazo hatupati tukaweza kujiendesha ikiwemo kuajiri.
Hivyo, tunategemea pia watu wa kujitolea katika kuifanya kazi yetu ya kijamii. Na pale  inapopatikana posho kidogo tunawapa wanajiotolea lakini hatuwezi kuita ni  mishahara.  Ninao vijana wanaoendelea kujitolea kwenye Mjengwablog na gazeti la mtandaoni la Kwanza Jamii,  wawili wako Iringa, na kwa sasa Dar sijapata mtu wa namna hiyo. Namtafuta.
 Ndugu yangu Zitto,
 Katika Tanzania hii, kama wanahabari na wanaharakati wa mitandaoni wangepewa jukumu la kutuhumu, kukusanya ushahidi, kuendesha mashtaka na kuhukumu, basi, Watanzania wengi nikiwamo mimi nduguyo tungeshakuwa gerezani siku nyingi sana.
 Ni bahati njema vyombo vyetu vya usalama, licha ya kufuatilia ya magazetini na kwenye mitandao, vinafanya kazi zao kwa weledi. Naamini kabisa, siku ambayo vyombo vyetu vya usalama vitaona haja ya kuniita na kunihoji kuhusiana na nilivyomfahamu Ludovick, vitafanya hivyo kwa kuzingatia taaluma yao inavyowaelekeza na si kwa mashinikizo ya magazetini na mitandaoni. Mpaka sasa sijapata hata ‘ miss call’ moja  ya kutoka vyombo vya usalama, na hiyo haimaanishi kuwa hawaijui kazi yao. Kama kutakuwa na haja ya wanazo namba zangu na wanajua hata ninapoishi.
 Ndugu yangu Zitto,
Nilichojifunza kutoka kwenye kauli ya January Makamba ni ukweli, kuwa si wanasiasa tu ambao hampendani, bali hata baadhi yetu wanahabari na tunaojiiita wanaharakati hatupendani pia.
Katika hili la Ludovick na Lwakatare kuna miongoni mwetu waliohangaika na wanaozidi kuhangaika kutafuta hata ‘ link nyepesi’ tu ya kumwuingiza, kwao wao, ni  ‘ Mwanahabari na bloga maarufu Maggid Mjengwa’ kwenye hili sakata la Ludovick na Lwakatare.
Na ikiwezekana, mimi Maggid,  niorodhoshwe kama mtuhumiwa wa kupanga njama za kumdhuru Kibanda na wanahabari wengine.  Tukifika hapo ndipo kitakuwa kilele cha furaha yao. Watakunywa mvinyo na bia. Watafurahi. Halafu iweje? Unajiuliza.
Ndugu yangu Zitto,
Ndivyo Watanzania tulivyo. Tunafurahia maanguko ya wenzetu, na hasa wale tuliotoka nao chini kwenye taaluma na wakaonekana kupanda chati kwa haraka. Mimi Maggid ni raia wa kawaida tu ninayejitahidi siku zote kuishi maisha adilifu na ya kujikimu.
Lakini, kwa wengine, mimi kuwa na Mjengwablog yenye umaarufu na hata kuanzisha kijarida cha kijamii cha ‘ Kwanza Jamii’ ni nongwa kwao. Ni yale yale ya mafarisayo walipomshangaa Yesu kwa kusema; “ Hivi ni Yesu huyu huyu mwana wa Joseph Fundi Seremala?!”
Ndio, moja ya matatizo yetu ni kutokuwa na wivu wa maendeleo, bali wivu dhidi ya wenye kujaribu kupiga hatua za maendeleo.
Ndugu yangu Zitto,
Kufikiri tu wazo la kutuhumu nayo ni tuhuma. Wanaonifahamu, bila shaka nawe ukiwemo,  hawawezi  kufikiri wazo la mimi kushiriki kupanga njama ya kumdhuru mwanahabari wa Tanzania au popote pale duniani, kumdhuru  raia wa Tanzania au popote pale duniani. Ukweli huo hapo juu nilipata kumweleza ndugu yangu  Ansbert Ngurumo kupitia jukwaa hili alipohoji mimi kusitisha rasmi usaidizi wa Ludovick kwenye Mjengwa blog kuanzia Machi 17.
 Ansbert pia aliniuliza; je, kama wewe ( Maggid) utahisiwa au kutuhumiwa kuhusika na suala la Kibanda ina maana utaacha kublogu?
Ndipo nikamjibu;
Kuwa kusitisha usaidizi wa Ludovick kwenye Mjengwablog ni kumsaidia Ludovic kutokuhusishwa na yanayofanyika Mjengwablog kwa sasa ikiwamo machapisho wakati yuko kwenye kesi.
Nikasema, kuwa sisi  wenyewe ( wanahabari) kilio chetu siku zote kimekuwa kuwataka watendaji Serikalini an kwingineko wanapokumbwa na tuhuma wakae pembeni kwa maana ya kujiuzuru kupisha uchunguzi, lakini, katika hili la Ludovick hatuoni kama hilo ni muhimu!
Kwenye hoja yake ya pili nikamjibu;
Kuwa kama atatokea Mtanzania mwenye akili timamu, akatoa tuhuma dhidi yangu, mimi Maggid Mjengwa, kuwa nahusika na kuratibu au kupanga njama za kumdhuru mwanahabari wa Tanzania au popote pale duniani. Kumdhuru raia wa Tanzania au popote pale duniani, basi, hata kama atakuwa na ushahidi mmoja tu wenye mashiko, itatosha kwangu kuacha mara moja kufanya yote yale ya kijamii kwa kutumia kalamu yangu. Bahati mbaya au nzuri, ndugu yangu Ansbert hakurudi tena kuendelea na mjadala ule.
 Ndugu yangu Zitto,
 Ndio, mwenye kunifahamu hawezi kufikiri wazo la mimi kupanga njama za kumtendea uovu mwanahabari au raia wa Tanzania. Ndio maana kuna wengi pia wamenipigia simu za kunipa pole ya juu ya kilichotokea na jina langu linavyotajwa kwa dhamira ovu.
 Alfred Mwambeleko ni kijana kada wa Chama Cha Mapinduzi.  Huyu ananifahamu tangu tukiwa wote Sangu Secondary ‘ A’ Level. Yeye na mimi, tukiwa wanachama wa CCM-Youth mwishoni mwa miaka ya 80, tulishirikiana kuandaa mijadala ya wazi pale shuleni ili vijana wajizoeshe kutoa fikra zao huru mbele ya watu.
 Majuzi hapa Mwambeleko alinipigia simu nikiwa Iringa. Alisoma jarida la moja la kila wiki akiwa na wenzake kwenye ofisi ndogo ya CCM, Lumumba. Ni kuhusiana na sakata la Ludovick na Lwakatare. Alfred Alinipigia simu kunipa pole na akatamka;
 “ Nimewaambia jamaa zangu hapa, kuwa Maggid is innocent”
 Ni kwa nini basi ndugu yangu Alfred awaambie wenzake kuwa mimi ni ‘ innocent’?
 Jibu; ni kwa sababu , coverage ya jarida lile  ilionyesha kunituhumu mbele ya jamii. Na kuna jarida lingine la kila Jumapili lilifanya hivyo pia.  Niliongea na wahariri wake kuwaeleza masikitiko yangu. Walikuwa waungwana, walinielewa. Maana, huwezi kuandika fulani ni mtu wa karibu wa fulani wakati unajua kabisa maana ya ‘ Mtu wa karibu’.  Huwezi pia kuandika fulani ni mwajiriwa wa kampuni fulani wakati huna ushahidi huo na Mkurugenzi wa kampuni anapatikana kuweza kuthibitisha au kukanusha.
Ndugu yangu Zitto,
Wewe pia ni mhanga wa ninaouita  ‘Uandishi wa habari usio wa kuwajibika’. Juzi tu umekanusha habari kuu kwenye moja  ya majarida yetu ikidai kuwa kulikuwa na njama za wewe kuwekewa sumu. Ukatamka kuwa ni  Uongo Mtupu!  Nilidhani gazeti lile lingethibitisha ilichoandika ili tujue nani mkweli na nani mwongo. Halikufanyika- Irresiponsible journalism!
Imefika wakati magazeti tuliyoyategemea yatuletee habari za kina na zilizofanyiwa uchunguzi kimsingi wanatuletea ‘ udaku’. Na wenye kuandika udaku mara nyingi huwa hawataki – ku-balance story.  Kwenye udaku kubalance story ina maana ya kuua udaku wenyewe, maana hakutakuwa na story ya kidaku. Inasikitisha kwamba tumefika hapa.
Ndugu yangu Zitto,
Hata mimi nastushwa na habari ninazoendelea kuzipata kuhusu Ludovic.  Sijutii kuyafanya maamuzi niliyoyafanya ya kumsitisha  mara moja Ludovic kufanya usaidizi kwenye Mjengwablog.
Inatosha tu mtu kutuhumiwa ili kuchukua hatua. Ni kumpa nafasi pia mtuhumiwa, ni kumsaidia. Ni wajibu wa kiraia. Kizalendo.
Pale Oyesterbay Police kuna rekodi yangu ya kumripoti mdogo wangu wa tumbo moja; baba mmoja  na mama mmoja, kwa kutuhumiwa kutenda kosa la jinai.
Ni miaka kadhaa iliyopita, nilimkamata na kumpeleka mwenyewe kituoni akaandikishwe maelezo na afunguliwe mashtaka na Jamhuri.
Ndugu zangu hawakuinelewa. Lakini leo wamenielewa. Kuwa kijana yule ndugu wa damu sasa amejitahidi kuwa  raia mwema. Hajapatikana na makosa mengine ya jinai. Na kijana mwenyewe, kwa maana ya mdogo wangu, anatambua sasa kuwa nilimsaidia.
Nayasema nikiwa na maana, hakuna Mtanzania au mtu mwingine yeyote ninayeweza kushirikiana nae kufanya uhalifu au kumlinda nikigundua kuwa amefanya uhalifu. Nitamripoti.
Siku ile ya Desemba 9, pale Nkrumah nami nilipata fursa ya kuongea. Nilizungumzia mambo mamkubwa mawili; haki na wajibu.
Nikatoa mfano wa kisa cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wakati wa Tony Blair, aliitwa Jack Straw.
Ilitokea asubuhi moja, Jack Straw alisoma gazetini kuwa mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani amewatoroka maaskari wa barabarani baada ya kutenda kosa la barabarani.
Jack Straw baada ya kusoma hayo, akamchukua mwenyewe mtoto wake na kumpeleka kituo cha polisi. Waandishi wa habari walikusanyika kutaka kumsikia Waziri mwenye dhamana ya Usalama.
Jack Straw akatamka; “ Nimemkabidhi mwanangu kwenye mikono ya polisi, nikiamini kuwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi bila kujali kuwa ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani. Lakini, nimewaambia pia Polisi, kuwa wasimkandamize mwanangu , kwa vile tu ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani.”- Jack Straw.
Hapo tuna ya kujifunza juu ya haki na wajibu.
Ndugu yangu Zitto,
Nimeandika sana. Lakini nimalizie na kauli yako  kuwa; Ukweli hautengenezwi, bali hutafutwa”. Ni sahihi kabisa.
Lakini labda nichokoze swali la kufikirisha; Tunafanyaje basi pale tunapotambua ukweli mwingine, kuwa, kwa wengine, ukweli wanauumba. That, they are simply crafting lies!
Sijaufunga mjadala, ingawa sitajadili yaliyo mahakamani.
Maggid Mjengwa,
Iringa

Tunatembea duniani kote lakini hatuoni, hatujifunzi mbali na kununua bidhaa dhaifu

 
Hadi sasa rai yangu imekuwa kwamba hatuna budi kujifunza kujenga mitazami ya mbali, mitazamo inayotia maanani kwmaba sisi si wageni hapa, siis si watu wa kupita, sisi ni watu wa kudumu na tumedhamiria kuwa tutaendelea kuishi hapa kwa muda mrefu ujao, hata miaka milioni ijayo, kizazi kimoja kikikirisha kizazi kifuatacho nchi iliyo bora kuliko kilichoirithi chenyewe.

Uimara wa fikra za jamii inayojoona kama ya kudumu hujidhihirsha katika fikra za watu wake lakini pia katika matendo watendayo kutokana na fikra hizo. Jamii ya kudumu haiamki siku moja na kuamua kufanya jambo ambalo haijalitafakari kwa muda muafaka na kwa mashauriano maridhawa. Haikurupuki na kufanya maamuzi ya kukidhi haja ya leo bila kaungalia maslahi yake yataathirika vipi kutokana na maamuzi ya muda mrafu yaliyoangalia matatizo ya mpito.

Kweli, mara kwa mara, hutokea kwamba matatizo ya mpito yakawa ni kikwazo muhimu kinachoathiri maendeleo katika mtazamo wa masafa marefu, mbali, na hayana budi kushughulikiwa kama matatizo ya mpito. Hata hivyo jamii makini itayaweka bayana, na itakuwa ikijikumbusha kila mara, kwamba hatua zinazochukuliwa sasa ni za mpito zinazoshughulikia tatizo la mpito ili kupisha njia kwa hatua za kudumu kuchukuliwa.

Miaka nyuma nilikwisha kutoa mfano (katika safu hii hii) wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kuporomoka kwa shirika la Usafiri Dar es Slaaam (UDA) mwanzoni mwa miaka ya 1980, baada ya kuwa limelirithi Dar Motor Transport (DMT), lililokuwapo tangu enzi za ukoloni.

Hapa ningependa kurejea wazo langu la siku zote, kwamba katika jamii ya maendeleo, ni marufuku kabisa kwa leo kuwa duni kuliko jana kwani kila siku mpya haina budi kuwa bora kuliko ilyoitangulia, na inapotokea kwamba jana ikawa bora kuliko leo na kesho ikawa duni kuliko leo, ni dhahiri kuna ugonjwa ful;ani katika jamii husika ila tu iwapo kuna maelezo mahsusi ya hali hiyo siyo ya kawaida.

Sasa, mwaka 1983, aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania, hayati Edward Sokoine, alitangaza kuruhusu magari madogo ya abiria kutoka miji ya Moshi na Arusha kutoa huduma ya “muda wa mpito” kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam wakati serikali ikifanya “mipango ya kudumu” ya usafiri wa umma katika jiji hili linalokua kila uchao.

Leo, miaka 30 u shei imepita, na zile “dala dala” za “mpito”  za Sokoine zimekuwa ni sehemu ya sura ya kudumu ya Dar es Salaam, kama ilivyo katika miji mingine ya bara, na juhudi za kutengeneza utaratibu kudumu wa usafiri wa umma katika jiji hili ni kama vile unapigwa vita, au umeota matende, au umepatwa na kigugumizi. Alimradi, tunaweza kusema, mradi huo hauendi ilivyotarajiwa na badala yake umekuwa ni chanzo cha kero wa watumiaji wa barabara wa kila aina.    

Huwa nasema kwamba faida mojawapo ya kusafiri ughaibuni ni kujifunza kutokana na jamii nyingine zinavyofanya mambo yake na kuiga kutokana na mambo anayoyaona msafiri. Hili ndilo fundisho kubwa tunalolipata katika simulizi ya “Kusadikika” ya Shaaban Robert , ambaye (nakumbushia tena, wasanii wamejikusanya mwaka juzi wakapanga kupeana nishani za miaka50 (ya kitu gani, hata wao hawakujua), lakini yeye wakamsahau) alitufundisha kile ambacho Wazulu wa Afriki Kusini hukisema:  Ukuhamb’ukubona; kutembea ni kuona.

Sisi tunatembea lakini hatuoni, kama vile tunakwenda “shopping,’ ambayo isingekuwa  mbaya sana kama ingejumuisha pia na “kununua’ maarifa ya wenzetu ili tuyatumie na sisi kujiendeleza. Hapana, “shopping” yetu sisi ilikuwa zamani ni “sistemu” za muziki na video; hii leo ni vitasa vya milango, bawaba na taili za sakafu

Zipo nchi zilizoendelea kiasi kwamba ni kwao ndiko tunapata vifaa kama hivyo. Lakini tukiangalia kidogo tu historia tunatambua mara moja kwamba nchi hizi zimetuacha katika miongo mitatu iliyopita, kwani mnamo miaka ya 1960 tulikuwa sambamba nazo: Malaysia, Indonesia, Thailand na nyingine nyingi.

Hatuna budi kujiuliza ni kwa nini nchi hizi ambazo zilifanana na sisi si miaka mingi iliyopita leo zinatuzidi katika maendeleo, tena kwa mbali. Bila shaka yapo mambo wanayoyafanya na sisi hatufanyi Tujiulize ni nini hicho ambazo nchi nyingine zimeendelea kutoka hali zilizokuwamo pamoja na sisi na leo tunazishangaa, tukiwa tumebaki pale pale na wakati mwingine tukiwa tunarudi nyuma.

Zitakuwapo sababu nyingi mno za kujaribu kuelezea hali hii, lakini bila shaka mojawapo ni kwamba hatujajenga saikolojia ya kudumu hapa tulipo, na ishara moja ni kwamba utashi wa kujenga makazi ya kudumu. Tunajenga vibanda vyetu vya zamani, hata kama tunavijenga kwa matofali ya “blok.”  Bado tuko kwenye misonge na tembe, hatujafikia hatua ya kusimamisha majengo ya kudumu, majengo ya aushi, ya mawe na chuma, yatakayodumu miaka mia tano hadi elfu.

Katika ujenzi tunaofanya leo hii ni wa mpito, kama nilivyosema mara kadhaa. Lakini katika kufanya ujenzi huo tunasafiri kwenda kupata vifaa vya ujenzi kutoka nchi zilizokwisha kujenga majengo ya kudumu, lakini hatuoni uhusiano uliopo baina ya sisi kwenda kufuata vifaa vya ujenzi wa majengo ya muda na uwezo mkubwa wa viwanda vyao wa kuzalisha vifaa tunavyohitaji kwa vijumba vyetu hafifu.

Tunakwenda Uchina, tunakwenda Hispania, tunakwenda Italia. Huko tunanunua vigae vya sakafu, madirisha, milango,    vyote hafifu tukivilinganisha na vifaa vinavyopatikana hapa nyumbani na ambavyovingefaa zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya kudumu.

source: Raia Mwema:  Jenerali Ulimwengu

Nahodha awatolea uvivu mafisadi Zanzibar

 
Na Mwinyi Sadallah
 
Waziri Kiongozi mstaafu wa SMZ Shamsi Vuai Nahodha, amesema hoja ya kuwapo au kutokuwapo kwa hati ya Muungano kusifute azma ya kuwashughulikia viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali za umma Zanzibar .
Nahodha aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye uwanja wa Mzalendo Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani hapa.
Alisema ameshangazwa na baadhi ya viongozi wakitunisha misuli kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakati baadhi yao wakikabiliwa na tuhuma za unadhirifu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na matatizo makubwa ya matumizi mabaya ya ardhi kwani viongozi wengi walijimegea kwa maslahi binafsi na wanajulikana.
Akifafanua zaidi alikiri kuwa kero za Muungano zipo na zinaeleweka ingawa alisema baadhi ya watu wakiwamo viongozi wanatumia mwanya huo ili kuficha tuhuma za ufisadi, uporaji na kujipatia utajiri usioelezeka.
"Kuhoji kuwapo au kutokuwepo kwa hati ya muungano baada ya miaka 49 kupita ni sawa na mtu kupatwa shaka kuhusu uhalali wa cheti cha ndoa ya wazazi wake, je ikiwa kimepotea kinaweza kubatilisha ndoa na uhalali wa mtoto,?"alihoji Nahodha
Alisema wanaotaka Muungano wa mkataba nia na lengo lao ni kuvunja muungano uliopo ili wapate nafasi ya kuatamia utajiri waliopata kwa kupora mali za wananchi na serikali yakiwamo majengo ya umma kinyume na sheria.
Aidha, aliwataka viongozi wa serikali na wanasiasa kujenga utashi na ujasiri wa kuhoji kwa nguvu ya hoja na kukemea vitendo vya ufujaji vilivyokithiri na kusababisha uchumi wa Zanzibar kutoimarika.
Alisema bado kuna vitendo hatarishi katika taasisi za serikali hivyo ni jukumu la kila mwenye ujasiri akapaza sauti yake badala ya kutumia muda mwingi kujificha kwenye kivuli cha hati ya Muungano.
Nahodha ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alisema Serikali ya CCM itaendelea kutetea msimamo wake wa muundo wa Serikali mbili na kushughulikia kasoro na utatuzi wa kero zilizopo katika Muungano bila kuyumbishwa na kundi lolote.
Akizungumzia upotevu wa Sh. bilion 20 katika Shirika la Umeme Zanzibar(zecco), alisema fedha hizo ni nyingi na zingeweza kutumika kusukuma maendeleo ya kisekta na badala yake akasema zimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
"Tusijifiche chini ya kivuli cha hati ya muungano wakati baadhi yetu mikono yetu inachuruzika michirizi ya uporaji, wizi na ubadhirifu wa mali za umma na uvunjaji wa sheria,"alisema Nahodha huku akishangiliwa.
Akilizungumzia suala la vijana kukosa ajira, alisema ni hatari kulisahau kundi hilo la vijana kwa kuwa ndiyo lenye nguvu na ushawishi.
"Chama chetu kihakikishe kinachemsha bongo na kulishika kundi hilo, lipewe nafasi katika medani za uongozi wa leo, kujengewa uwezo ili liwe jeshi imara litakalokabili mapambano na kuwashinda maadui,"alisema Nahodha .
Matamshi ya Nahodha yamekuja huku Serikali ikiwa bado haijatekeleza ripoti tatu za Baraza la Wawakilishi za kuchunguza matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu ikiwamo uuzaji wa ardhi kwa maslahi binafsi na majengo ya Serikali.
Ripoti ya kwanza ilihusu uuzaji wa majengo katika hifadhi ya mji wa urithi wa dunia katika mji mkongwe aa Zanzibar, kisiwa cha changuu kilichokodishwa kwa bei ya kutupa,ubadhirifu katika Zecco na Baraza la Manispaa Zanzibar.
Ingawa ripoti zote zimesema kuna viongozi na watendaji wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuuza mali za serikali kwa kutozingatia sheria ya manunuzi na ugavi lakini hadi sasa hakuna kigogo yeyeto aliyefikishwa mahakamani
 
Chanzo - Nipashe