SIFA YA MCHEZAJI MAHIRI ANAYETAKIWA IKULU:
- MWADILIFU
- MWAJIBIKAJI
- MKWELI
- MTETEZI WA AMANI
- RAFIKI NA MTETEZI WA WANYONGE
- SHUPAVU KATIKA MAAMUZI
- AWE TAYARI KUTUVUSHA KAMA TAIFA KUTOKA KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI
- MTU WA WATU
- MKUZAJI WA DEMOKRASIA
- MWOGOPA MUNGU
- ANAYEWEZA WAKEMEA RAFIKI ZAKE MAFISADI
Taifa
letu linaelekea katika uchaguzi wa viongozi ambao kupitia vyama vyao vya siasa
wataunda serikali ya kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya
uchaguzi wa October 2015.
Mimi
jicho langu kubwa ni kwa kiongozi Yule ambaye atashika hatamu ya kuongoza Taifa
letu na ambaye atahamishia makazi yake IKULU.
Kama taifa ni wakati mzuri umewadia sasa tuweze kumchagua mtu makini, mbunifu, mwaminifu, mwadilifu na mzalendo wa kweli kwa wananchi wanyonge na masikini wa Taifa letu.Kiongozi ambaye tunamwitaji lazima atambue kuwa kuwa wananchi wana haki ya kupata chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora.
Akumbuke kuwa wanaompeleka Ikulu ni wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na sio marafiki wachache wenye pesa. Na ajue kuwa anapochaguliwa kuongoza, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri awe tayari kuongoza kwa kuonyesha njia awe ni mfano wa uwajibikaji.
Kiongozi tutakaye mchagua lazima awe na tabia ya kuongoza kwa kutofikiria zaidi maslahi binafsi wazo hili liwe mwiko. Tutataka atumie ustadi wa uongozi ambao utasimamia haki za waoongozwa; wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.
Hatuki kumchagua kiongozi ambaye baada ya kuchaguliwa ataigeuza ikulu kuwa Ni pango la wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji wa rasilimali za watanzania kwa masilahi binafsi pamoja na marafiki wachache. Tunahitaji kiongozi ambaye uadilifu kwake utakuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku bila kujali au kupendelea mtu au kikundi cha watu au vile vile awe na uwezo wa kuwajibisha viongozi watakao kuwa chini yake wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.
Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kiongozi wetu tunataka aongoze katika misingi hiyo.
Kiongozi lazima ajue kuwa hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani ataongoza watu wake wateule. Tukiangalia katika historia ya dunia sehemu nyingi, Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na kubarikiwa katika njia njia nyingi. Walipomsahau Mungu kupitia rushwa na ufisadi na dhuluma shida na dhiki zilianza.
Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana
ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Kiongozi
anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake
unapatana na Neno la Mungu.
Itakuwa jambo bora tuweze kupata viongozi ambao kwa kweli nao watakuwa bora katika kuongoza Taifa letu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila mtanzania. kiongozi kuongoza kwa uwajibikaji; kuonyesha uzalendo na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.Pengine katika msingi huu tutahitaji kiongozi ambaye anauelewa mpana wa kuelewa shida za wananchi mwenye UWEZO wa kufikiri kwa usahihi, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa usahihi wakitambua dhamana ya uongozi ambao taifa linampa. Kwa hivyo tutahitaji RAIS pamoja na mambo mengine awe na UWEZO kuongoza kwa usahihi.
Pengine tutahitaji kidogo aina ya viongozi wetu wawe wakali japo sio sahihi kutumia msemo huu lakini wakati mwingine ile tuweze kupiga hatua ya maendeleo tutahitaji viongozi wenye mawazo ya uwajibikaji chanja; ili tuweze kubadilisha kidogo maadili ya utendaji kwa Watanzania; Tunahitaji Maraisi katika serikali zetu mbili ambao wanaweza kuwawajibisha mara moja watendaji wake ambao wanashindwa kuwajibika, tuwapate viongozi ambao wanaweka pembeni huruma ambazo hazina msingi kwa Taifa;
Nafikiri itakuwa ni jambo la busara kama sisi kama watanzania na wapiga kura tukiweza kuepuka tabia ya kuwachagua viongozi wetu kwa Mazoea, Mkumbo na kwa kutumia Hisia na mapenzi binafsi juu ya wagombea. Nafikiri umefika wakati tuwachagua viongozi wetu kwa upeo wao wa kuona mambo mbalimbali nauwezo wao wa uongozi hapa nazungumzia uzoefu wa kiongozi kabla ya kuchaguliwa kuwa rais je amefanikiwa kwa kiasi gani katika idara ambayo amewahi kuongoza?
kama taifa tunafahamu kuwa taifa letu bado linaogelea sana katika tope nzito la matumizi mabaya ya rasilimali ya Taifa Rushwa na Ufisadi basi tunahitaji Rais ambaye analiona hili kuwa ni tatizo na linahitaji utatuzi wa haraka. Lazima tukubali kuwa mabadiliko yoyote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yenye kulenga kuletea faida wananchi walio wengi hayawezi kufanikiwa bila ya kutokomeza rushwa na ufisadi. Kiongozi wetu aweze kuliona hili na kuwa tayari kupambana nalo akiamini kuwa Tanzania rushwa imeshaota mizizi, umepelekea mamilioni ya watanzania kupoteza matumaini na hali zao za maisha lakini kupitia yeye ataweza kulitatua tatizo hili na kuwachukulia sheria wale wote ambao wamehusika katika uchafu huu,
Tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kuyatekeleza kwa vitendo manemo haya ya Mheshimiwa Yusuph Makamba “maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao wenyewe, kwa kufanya kazi. Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba kila kitu wanategemea kitafanywa na serikali … Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,”. Kauli hii ni nzito kiongozi wetu anayetaka kuongoza taifa hili lazima awe tayari kuwaeleza wananchi bila kuogopa kukosa kura katika kipindi kingine cha uchaguzi.
Daima tunapofikiria kuwachagua viongozi wa juu wa Taifa letu tunayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi sema kuwa kazi ya urais ni ngumu na inahitaji busara na kuchukua maamuzi magumu, ili kuweza kutimiza haki wananchi wanyonge “ walala hoi ”; aliendelea kushauri kuwa “Ole wale wanaokimbilia Ikulu, wanakimbilia nini, Ikulu hakuna biashara ya kufanya, Ikulu ni mahali patakatifu na kama kuna mtu anadhani kuwa kukaa Ikulu ni raha basi angeniuliza mimi katika kipindi cha miaka 21 niliyokaa Ikulu nimefanya biashara gani,Ikulu ni mzigo mzito”
Mwandishi Nyenyembe aliwahi andika kuwa “Kwa maana hiyo mtu anapoamua kuulilia urais,urais sio pambo la nchi,urais ni jalala, urais ni chumba cha kuhifadhia maiti,urais ni njaa,urais ni magonjwa,urais ni bakuli la kukingia machozi ya watu wanyonge wanaolia kila siku wakihitaji msaada na kama hawapati anayetazamwa hapo ni rais”
Katika demokrasia wananchi
ndio wenye dhamana na uwezo wa mwisho wa kumrejesha mwanasiasa kuendelea kuhozi
madaraka; pamoja na umaarufu wake, uadilifu na utaalam katika kushughulikia
maswala ya siasa bila ridhaa ya mwananchi sio rahisi kurejea madarakani;
Hebu tuanagalie historia ya vyama vingi na chaguzi za Zambia zinaainisha kwa ukomavu wa demokrasia ndani ya Zambia wananchi ndio wenye sauti ya mwisho wananchi wa Zambia wanapima na kuamua kulingana na utendaji wa viongozi wao na sio ushabiki wa vyama vyao;wamejitahidi sana kuweka nchi mbele vyama baadae.
Tatizo la kushabikia sana vyama ndilo linaloponza sana maendeleo ya nchi nyingi za kiafrika; wananchi wanakumbatia zaidi chama na sio utendaji wa viongozi wa vyama vyao;
Kama wananchi tunatakiwa kuanza kuangalia upya maamuzi yetu dhidi ya viongozi wetu; tunahitaji viongozi waadilifu na viongozi wa namna hii wataweza kuchukua hatua kwa maslahi ya jamii kwa manufaa ya wote, na wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo kulingana na utaratibu wa nchi husika na kukendelea kukubalika kwako kwa masilahi ya wengi; Katika mfumo wa kidemokrasia wa serikali, ambapo nguvu ya utawala ina inapatika upya kila baada ya miaka mitano na wananchi ndio wenye dhamana ya kuwarejesha madarakani.
Nchi ya Zambia imetufundisha kuwa hakuna kiongozi anayemiliki watu, hakuna chama chenye hatimiliki ya kuwa na kundi la wananchi kama itakuwa hivyo basi kuna tatizo na wananchi katika nchi hiyo; wananchi mara zote wanategemea na wanataka mabadiliko makubwa ya kiuchumi hawahitaji propaganda za chuki, wanahitaji kufaidi raslimali zao wazambia walikuwa wanashangaa utajiri wote unaotokana na shaba unakwenda wapi? Pale ambapo hawakuridhika hawakuwa na papara walisubiri tu wakati ulipofika walimweka pembeni kiongozi na kumpa dhamana kiongozi mwingine. Lazima tukubali kuwa katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika Zambia ni moja ya changamoto za mabadiliko ya kisiasa:
Maamuzi ya wananchi katika awamu tofauti Zambia umeendelea kuwashangaza viongozi walioko madarakani kuanzaia enzi Kaunda, pamoja na ukongwe wake wa kutawala kwa miaka 27 hadi awamu ya Banda; Kiini cha msukumo huu nini? Wananchi wanatamani kupata maisha bora; na kuwa viongozi wenye kiwango cha juu kabisa cha uadilifu kuweza kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo sio kwa nadharia bali vitendo;
Viongozi wetu wa vyama vya siasa wamesahau kuwa, Kimsingi, raia huzaliwa wakiwa huru dhidi ya mikingamo ya kijamii, kwa lugha ya kitaalamu tabula rasa. Lakini mikingamo hii ya kijamii huingizwa katika fikra za wananchi kupitia itikadi na elimu ya siasa katika vyama ambavyo wanafuata; na wakati mwingine hata kupitia shule na sehemu za ibada.
Cha ajabu haitoshi kuivuruga jamii peke yake tumeona na tunaendelea kuona kuwa viongozi wetu wa kisiasa hapa nchini wamekuwa wakigombana kila mara katika mambo ya msingi na yasiyo na msingi. Kugombana si kubaya kama kunaleta tija, lakini kule kugombana kunakofanywa kwa misingi ya kujitafutia umaarufu kunasabaisha viongozi kushindwa kutekeleza majukumu yao ambayo yanatokana na ahadi wakati wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, ni dhambi ambayo haiwezi kuvumilika hata kidogo.
Wakati tunaelekea katika kipindi cha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi ya uraisi kupitia vyama mbalimbali; sisi kama wananchi tuanze kujipima na kujua ni kiongozi wa namna gani tuna mwitaji; tuziangalie khali zetu za uduni wa maisha sisi bado ni masikini, tunahitaji barabara bora; huduma za afya nzuri, elimu bora kwa vijana wetu; ajira za kutosha kwa wenye sifa za kuajiriwa;
Kama Rais Kenedy wa Marekani alivyowahi kusema ‘Wewe UMELIFANYIA NINI TAIFA LA TANZANIA’ ni wajibu wa msingi kwetu kama wapiga kura kujiuliza swali hili je tumelitendea haki Taifa kwa kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya serikali zetu mbili? Yatupasa kutimize wajibu wetu kwa maisha bora kwa kila mtu kwa kuchagua viongozi bora na sio bora kiongozi. Miaka mitano ni mingi sana tukichagua kiongozi mbovu.
Wananchi tujiulize je kama taifa tumaini letu ni lipi dhidi ya viongozi wetu wa siasa ambao tunatarajia kuwachagua; tunahitaji viongozi wakuu wa nchi ambao wataweza kutupeleka kwenye nchi yenye neema na amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa, kidini .
Niliwahi andika huko nyuma
kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya tusiendelee;tukumbuke
kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe, juhudi zetu na misimamo
yetu; tukiangalia kwa ujumla wanasiasa wanpoteza muda mwingi katika propaganda na sio
kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana
na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.
Wanasiasa wetu ndio wapiga
majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia sisi
wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya utamaduni
wa siasa za Tanzania kwa kuwachagua viongozi watakao endeleza umasikini wa
Taifa letu kwa faida ya wachache.
Kiongozi tunaemtaka tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda sisi kama Taifa.
Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?
Taifa letu katika kipindi
cha miaka ya karibuni kiliingia katika vurugu za Mtwara, Dar es salaam Zanzibar
Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika; Je kiini cha vurugu hizi kimepata jibu? Kama jibu
ni hapana sasa tutahitaji viongozi wetu wakuu tutakao wachagua wawe wanaweza
kuona na kutumia muda wao katika kuleta majibu ya matatizo ya wananchi wao;
Wananchi tunatakiwa tuamke na tusiwape nafasi wanasiasa kutufanya sisi kuwa daraja lao la wao kuweza kutimiza malengo yao bila sisi kujitambua kwa haraka; matokeo yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunauwawa na tunaendelea kuwa masikini.
Imefika wakati sasa hata viongozi wengine tutakao wachagua tusirudie kosa la kuchagua viongozi ambao wanasilka na tabia ya
kuzomeana,
kulaumiana, kutukanana;mwelekeo huu hautatusaidia sisi lengo letu la kuwa na maisha
bora
Nafikiri linalowezekana leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina ya Muumba wetu tu;
Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “Kupanga ni kuchagua”. Wananchi kwa kweli inatakiwa tujipange sasa kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa masilahi yetu binafsi ili kupata viongozi wetu wakuu walio bora na makini. Tunataka tupate viongozi waadilifu kweli kweli.
Tukumbuke kuwa Uadilifu ni karama,
ya utambuzi wa kujifahamu kwa mtu binafsi hususa kiongozi wa serikali, ambaye
anatakiwa kufanya kazi zake kulingana na sheria na taratibu ambazo hujenga,
utamaduni, wa kuwajibika kulingana na
sheria husika. Kwa kufuata taratibu nzuri za utendaji kazi Uadilifu katika kazi husaidia uimarishaji wa misingi
ya utawala bora.
Kwa kujumuisha kabisa uadilifu na utimilifu kwa uhusiano wa biashara yetu inayoendelea na kufanya uamuzi, tunaonyesha kujitolea kwa utamaduni ambao unakuza kiwango cha uadilifu wa hali ya juu kabisa; ni kweli kuwa uadilifu inahitaji uaminifu binafsi wa kiongozi husika; uadilifu unahitaji uaminifu wa kupinga ubinafsi kwa kiongozi ambaye amepewa dhamana. Uadilifu unaendana na Kuwa mkweli katika utendaji na kuishi kulingana na maadili ya kazi na kuheshimu rasilimali kwa faida ya wengine.
Wajibu wa kutenda ukweli ni wajibu wa juu kabisa wa uadilifu kwa viongozi wa umma; kiongozi wa umma lazima atambue hali halisi ambayo inaendana na wajibu kwa kufuata maadili hivyo kusambaza cheche ili hata jamii nzima nayo iweze kuishi kulingana na maadili ya Taifa.
Kiongozi mwadilifu daima hutakiwa kuonyesha uhusiano kati ya maadili yake ya utendaji na kwa urahisi kabisa aweze kusema na nafsi yake ili isitawaliwe na tama ya rushwa ambayo itapingana na dhana nzima ya maadili kulingana na kiapo chake. Hapa ni jukumu la serikali kuweka mipaka bayana wa uhusiano kati ya maadili binafsi na sheria za utendaji wake kwa manufaa ya umma. Uadilifu daiama huashiria haki, ikiwa na maana kuwa kiongozi wa umma lazima aweka maslahi binafsi pembeni;
Uadilifu hujenga amani, huleta ufanisi, kwani Watumishi wa umma watakuwa
wanauwezo wa kuhakikisha matumizi sahihi, ufanisi wapesa za umma. dhana na
misingi ya uwajibikaji anatarajiwa kufanya ya viongozi wa umma kuwajibika kwa
matendo yao au kutotenda
Ni zinatakiwa kuongeza uwazi wa serikali, kusisitiza na kuimarisha mwitikio wa kiserikali na uhalali na kuboresha utekelezaji wa sera. Mwalimu Nyerere katika hija ya maisha yake, alijitahidi kutanguliza masilhai ya watu wake, bila ya kujikita katika ubinafsi, uroho na uchu wa madaraka; uchoyo na ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa viongozi wengi ndani ya Taifa letu.
Maadili ni muhimu zaidi na katika siasa na kwa maendeleo ya wananchi. Maadili ya kweli yatapunguza wanasiasa kujishughulisha na rushwa.
MUNGU IBARIKI JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA UTUVUSHE SALAMA ILI TUWEZE KUWAPATA VIONGOZI BORA KWA MANUFAA YA WATU WAKO katika uchaguzi wa mwaka huu 2015.
Ni kweli kabisa yatupasa kuachana na uchaguzi wa viongozi
ReplyDeleteWetu kwanza mazoea. Big up