Na Waandishi Wetu
Dar/Mikoani. Waziri Mdogo wa
Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika,
Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu
wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais
kwa tiketi ya CCM.
Waziri huyo aliuliza swali hilo usiku wa kuamkia
Jumatatu (Juni 14, 2015) mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati
anazungumza na Rais Kikwete kutokana na wanachama wa CCM 35 kujitokeza
kuchukua fomu za kuwania urais.
Viongozi hao walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25
wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika, kwa siku mbili, kwenye Kituo cha
Mikutano cha Sandton Convention jijini Johannesburg, Afrika Kusini na
kumalizika jana.
Makada hao wa CCM wameibua upinzani mkali kwenye
mbio za urais na hadi sasa hakuna dalili za mtu yeyote kuwa ana nafasi
kubwa ya kupitishwa, hali ambayo imesababisha vyombo vya habari
kubashiri kuwa mteule wa CCM anajulikana kwa viongozi wa juu wa chama
hicho tawala.
Wakati nchi ikijiandaa kupata kiongozi mpya
atakayeongoza Serikali ya Awamu ya Tano, mbio za urais ndani ya CCM
zimevutia idadi kubwa ya wanachama ambayo haijawahi kutokea kabla na
baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 baada ya
watu 35 kuchukua fomu hadi sasa.
Mwaka 1995, wanaCCM waliojitokeza kutaka kumrithi
Rais Ali Hassan Mwinyi walikuwa 15 na mwaka 2005 waliojitokeza kutaka
kumrithi Rais Benjamin Mkapa walikuwa 11.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu
ilisema jana kuwa mwanzoni tu mwa mazungumzo baina ya viongozi hao,
Linda alimuuliza Rais Kikwete, “Je, unaye mgombea yeyote ambaye
unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea”.
Baada ya swali hilo, kwa mujibu wa taarifa ya
Ikulu, Rais Kikwete alijibu, “Sina mgombea ninayempendelea. Wagombea
wote ni wa kwangu, ni wa chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo
kwa mujibu wa taratibu za haki katika chama chetu nitaitumia katika
vikao mbalimbali”.
Kuhusu utiriri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.
“Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya
kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea
wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka
katika nchi yetu katika miaka ya karibuni.
“Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha
mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu
wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Rais Kikwete alisema hana tatizo na wingi wa
wagombea kwa sababu haiwezekani kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa
sababu ni haki yao.
Vile vile, alisema wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na
pia ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka ndani ya chama na ni
uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa
wa mafanikio.
Uchaguzi mkuu wa Marekani utafanyika mwakani na
kwa mujibu wa taratibu zao, mchakato huanza mwaka mmoja kabla na
wagombea hupatikana Juni ya mwaka wa uchaguzi.
Hadi sasa, makada wanne wa chama cha Democrats,
ambacho kimeshika hatamu, wamejitokeza kuwania urais, wakati katika
chama cha Republican, ambacho kina nafasi kubwa ya kushika madaraka
mwakani baada ya kukaa nje kwa miaka 10, kuna makada 12 waliojitokeza.
CCM iteue kwa staili ya Papa
Katika hatua nyingine, mbunge wa Ngara (CCM),
Deogratias Ntukamazina ameitaka Kamati Kuu ya CCM kutumia mfumo wa
Vatican wa kujifungia na kuomba siku saba kabla ya kumpata Papa wakati
itakapokutana kuteua mgombea urais wa chama hicho baadaye mwezi huu.
Katika mchakato wa kumchagua Papa, Makardinali
kutoka sehemu mbalimbali duniani, hukutana kwenye mji wa Vatican na
kujifungia katika mkutano wao (Conclave) wakiomba ili apatikane Papa na
baada ya kukamilisha mchakato huo, moshi mweupe huonekana juu ya jumba
la mkutano kuashiria kukubalika kwake kwa Mwenyezi Mungu.
“Mimi siwanii tena (ubunge), lakini ninachosema,
tuache ushabiki… ninaondoka, lakini nina ushauri kwa Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu. Kwanza ninawapongeza waliojitokeza kuwania urais lakini
siyo yule msanii wa darasa la saba.
“Tuombe Mungu atupe Rais mzuri, anayependa watu,
anayependa maendeleo ya watu, lakini na Kamati Kuu muanze kuomba Mungu
kama anavyotafutwa Papa. Makardinali wanajifungia siku saba, wanaomba,
wanaomba na ninyi ombeni. Sasa na sisi tusishabikie, tuache vikao
vitaamua,” alisema Ntukamazina wakati akichangia mjadala wa bajeti
bungeni.
Membe aibukia kwa Msuya
Jana wagombea wa CCM waliendelea na safari ya
kutafuta wadhamini huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe aliibukia kwa nyumbani kwa Waziri Mkuu wa
zamani, Cleopa Msuya.
Membe alifika nyumbani kwa Msuya eneo la Usangi,
Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufanya naye mazungumzo akitokea mkoani
Tanga ambako aliahidi kuwa akibahatika kuingia Ikulu, kwanza
atashughulika na bandari ya Tanga.
Katika mazungumzo yao, Msuya alisema anamuunga
mkono Membe katika harakati zake za kugombea urais kwa kuwa anakidhi
vigezo vilivyotajwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Msuya alisema ana matumaini CCM itamteua Membe kwa kuwa ni
mgombea pekee ambaye hajawahi kukumbwa na kashfa na amekidhi sifa
zinazohitajika.
Msuya alisema chama hicho hakipaswi kumchagua
mgombea mwenye madoadoa ya ufisadi na uchafu kwa kuwa mgombea wa aina
hiyo hatawatendea haki Watanzania.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
wa ngazi za madiwani, wabunge na rais, chama kinapaswa kuwatanguliza
watu wenye sifa na vigezo ili kupata viongozi bora watakaowatumikia
wananchi.
“Kama kweli Taifa linawachukia mafisadi na wenye
kila aina ya madoadoa, chama hakipaswi kuwapitisha viongozi wa aina hiyo
kwa kuwa
wataendeleza ufisadi huku Watanzania wakiendelea kuteseka,” alisema Msuya
“Kama tunachukia ufisadi na matendo machafu haya
yanayoendelea kufanywa na baadhi ya watu katika Serikali yetu basi
mgombea mwenye madoadoa hataweza kuwatendea haki Watanzania kwani
wananchi wanahitaji mtu safi na asiyekuwa na aina yoyote ya uchafu,”
alisema Msuya.
Pinda atikisa kwao
Mkoani Katavi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameanza
mbio za kusaka wadhamini jimboni kwake Katavi ambako alipokewa kwa
maandamano na kuchangiwa Sh1 milioni za kumsaidia kuzunguka katika mikoa
mingine kutafuta wadhamini.
Pinda maarufu kama “Mtoto wa Mkulima” alipokewa
kwa mabango yaliyoandikwa “Pinda siyo fisadi… ni mtoto wa mkulima…
karibu nyumbani… wewe ndiye rais ajaye”, na alisindikizwa kwa maandamano
yaliyowafanya askari kuwa na wakati mgumu kudhibiti ulinzi.
Baada ya kupata wadhamini 9,141 katika tarafa
mbalimbali za mkoa wa Katavi, Pinda aliwashukuru na kueleza kuwa tukio
hilo ni la kihistoria na kuwaomba wananchi waendelee kumwombea ili aweze
kupata ridhaa ya chama chake na hatimaye kuwa rais.
Wasira na uchapakazi
Mkoani Njombe, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Steven Wasira amesema uchapakazi na uaminifu wake ndio
uliofanya kila Rais aliyepita ahitaji kufanya naye kazi.
Wasira, ambaye pia ni mbunge wa Bunda alisema hayo jana wakati
akitafuta wadhamini katika mkoani Njombe. Alisema asingekuwa mwaminifu,
angekuwa ameshawekwa pembeni kama ambavyo baadhi ya mawaziri wamefanywa.
“Nimekuwa sehemu ya uongozi wa Taifa letu kwa
miaka kadhaa, nimeanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akaja
Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, kwa hiyo
ni walimu wangu wanne, uzoefu nilioupata kutoka kwao ni shule tosha
kwangu ya kuliongoza Taifa hili,” alisema Wasira.
Bilohe na siri ya urais
Kada wa CCM anayewania kuteuliwa na chama hicho
kugombea urais, Edephonce Bilohe amesema hatishiki wala kuwaogopa
wagombea wanaonunua watu kwa nguvu ya fedha kwa kuwa uongozi ni tunu
kutoka kwa Mungu.
“Natambua kwamba nagombea nafasi hii kubwa zaidi
nchini nikishindana na wasomi na matajiri, lakini kamwe sitishwi na hawa
wagombea wanaojidai kuhonga viongozi na watu wengine ili wawaunge
mkono,” alisema Bilohe.
“Tangu nikiwa mdogo tulikuwa tunaambiwa kwamba CCM
ni chama cha wakulima na wafanyakazi, ndiyo maana mimi nikiwa mkulima
katika Kijiji cha Muzye na Mtala niliamua kwa moyo wangu wote kugombea
urais ili niwawakilishe maskini wenzangu ambao ndio wengi katika jamii
na sina shaka wataniunga mkono katika harakati zangu za kuingia Ikulu
kuongoza Taifa,” alisema.
Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema:
“Ni aibu nchi ya wastaarabu kama Tanzania, inayoongozwa na viongozi
wasomi bado tunashuhudia mapigano ya wakulima na wafugaji wakigombea
maeneo ya kulima na kuchungia mifugo.
“Nchi yetu ina ardhi kubwa isiyokaliwa na watu na
haijawahi kutumika tangu dunia iumbwe, iweje sasa watu wauane kwa ajili
ya ardhi? Hili nitalikomesha.”
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Habel Chidawali, Kibada Ernest, Burhani Yakub, Antony Kayanda na Rehema Matowo.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment