Profesa Seithy Chachage
anasema;
“ Haitoshi kabisa kulifahamu jambo. Kuambiwa ni habari
tu, unaambiwa na unafahamu, unajua kwamba tukio fulani limetokea. Gumu zaidi ni
kuelewa mantiki ya hilo jambo, na hata baada ya kufikiria na kulifahamu, ugumu
mwingine huja pale ambapo inabidi ulieleze lieleweke na maelezo yakajitosheleza
yenyewe na kumfanya kila asikilizaye kuridhika kwamba jambo linaeleweka.
Haitoshi wewe kulielewa,
bali na wewe kulielezea na mtu mwingine akaelewa. Hapa umuhimu wa kufikiria
unachukua nafasi ya pekee. Hii ndiyo maana ya mawasilino.” – Profesa Chachage
Seithy Chachage ( Makuadi Wa Soko Hurua, ukurasa 117)
Naam, mengine tuandikayo tulishayaandika
zamani. Tunayarudia maana yanayotokea sasa ishara zake tulishaziona, isipokuwa,
tu mahodari sana wa kupuuzia.
Haya ya UKAWA na CCM kuna
ambao tunaweza kuyapuuzia leo tukidhani hayatuhusu, kumbe, yatatudhuru sote. Ya
UKAWA na CCM ni mgogoro wa kisiasa. Ni sharti umalizwe kwenye meza ya
mazungumzo.
Unahusu Katiba mpya, na ni
busara na hekima, kuwa Katiba hiyo ipatikane kwa pande zinazohusika, kuanza na
mazungumzo ya kindugu na kufikia maridhiano yatakayozaa Katiba ya Maridhiano.
Maana, kwetu wanadamu, mengi yanayotufanya
tufarakane na hata kugombana yanatokana na sisi wenyewe wanadamu. Na ndivyo
ilivyo hata kwa ndege na wanyama.
Ukiwaona ndege wanagombana, ukiwaona kuku
wanagombana, na hata ng’ombe, basi, sababu kubwa ni ya viumbe hao wenyewe. Na
mara nyingi, kugombana huku hutokana na kugombania kisichotosha.
Hivyo basi, suluhu ya yale tunayogombania kama
wanadamu yapaswa itokane na sisi wanadamu wenyewe. Na tangu karne ya 17 kuna
wanadamu walioliona hili.
Mwanafalsafa Thomas Hobbes alibainisha, kuwa
migogoro mingi miongoni mwetu hutokana na ushindani wa kugombania kisichotosha.
Kwa vile sote tuna mahitaji yenye kufanana, basi, Thomas Hobbes anasema, kuwa
migogoro hii itaendelea, kugombania kisichotosha.
Na Hobbes huyu anaamini, kutokana na hatari
hii, basi, jukumu muhimu na kubwa kwa Serikali yeyote ile iwe ni kulinda amani
ya nchi. Kwamba kwa kutofanya hivyo, jamii itarudi katika hali ya kutokuwa na
taratibu; vurugu, kuuana, umasikini na kupelekea maisha mafupi.
Hata hivyo, tunaamini pia, kuwa siku zote,
pasipo haki na usawa hakuna amani, ingawa, katika jamii yeyote ile, uwepo wa
amani na utulivu ni msingi mzuri katika kutafuta haki na usawa, kwa njia ya
majadiliano.
Nimepata kusimulia kisa
cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.
Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya
uliowekwa na mwenye nyumba uvunguni mwa kitanda. Panya yule akamwendea jogoo wa
mwenye nyumba. Akamwambia:
“Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa
kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote."
Jogoo akajibu: "Ondoka zako, mie mtego wa
panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda?"
Panya
yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia:
"Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa
panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua
kabla haujatudhuru sote."
Mbuzi akajibu: "Hivi
tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya
haunihusu mie mbuzi."
Panya akaenda hadi kwa
ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia: "Ewe ng'ombe wa Bwana, kuna mtego wa
panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla
haujatuletea madhara."
Ng'ombe akajibu akionyesha mshangao!
;"Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike
na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."
Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia
chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa
nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika. Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha
akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka
aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu. Sumu kali
akamwachia. Mwenye nyumba akafa.
Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu
walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo. Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba. Jogoo
akachinjwa. Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia.
Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba. Mbuzi akachinjwa. Na siku ya maziko watu
wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Naye akachinjwa!
Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe
wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu
wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya!
Kuna cha kujifunza kutoka kwenye kisa hiki.
Tutafakari hili tukiyaangalia na ya kwetu yanayotokea sasa bungeni Dodoma,
Zanzibar na kwingineko.
Source: raiamwema.co.tz/ya-katiba-na-kisa-cha-mtego-wa-panya-
Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment