KATIKA sehemu ya pili ya
makala haya nilihitimisha kwamba kadri upinzani unavyokua ndivyo unavyozidi
kufanana na CCM kimuundo na matendo ya viongozi wake. Niliahidi kumalizia mada
yangu kwa kufafanua dhana hii ya upinzani kufanana na CCM.
Ninamalizia makala haya
kwa kueleza baadhi ya viashiria vunavyofanya upinzani uanze kufanana na CCM.
Kiashiria cha kwanza ni matumizi ya dhana ya usaliti. Tulipoanza mfumo wa vyama
vingi miaka ya tisini CCM walitumia sana dhana ya usaliti katika kuvidhoofisha
vyama vya upinzani. Kwamba wapinzani ni vibaraka wa wazungu na wanatumiwa
katika kuharibu amani ya nchi.
Wapinzani wakatangazwa
kwamba ni wasaliti wa nchi kwa kupingana na chama tawala kilicholeta amani, utulivu
na mshikamano. CCM hawakupinga upinzani kwa hoja, bali kwa kuwaaminisha
wananchi kwamba hawa ni watu hatari. Mwanzoni wananchi walikubaliana na dhana
hii na ilihitaji moyo mkuu katika kujipambanua kwamba wewe ni mpinzani. Lakini
ilikuwa ni suala la muda tu.
Hatimaye ukweli
ulijulikana na wananchi sasa wanaelewa kwamba kumbe hata wapinzani ni
Watanzania wenye nia njema na nchi yao, na wanashindana katika namna bora zaidi
ya kutawala na kuendesha nchi. Sasa miaka zaidi ya ishirini baada ya kuanzishwa
mfumo wa vyama vingi, upinzani nao wanaanza kutumia mbinu hiyohiyo ya dhana ya
usaliti katika kuzima sauti kosoaji ndani ya vyama vyao. Kwamba leo mwanachama
yeyote anayethubutu kuwakosoa viongozi anaitwa msaliti.
Tena usaliti wenyewe ni
pale ambapo mwanachama anathubutu kutaka kugombea nafasi fulani ya uongozi na
anaonekana kuwa na uwezekano wa kushinda hiyo nafasi anayoitaka. Mwanachama wa
namna hii atatangazwa dunia nzima kwamba ni msaliti na anatumiwa na chama
tawala katika kudhoofisha upinzani. Lakini ukweli ni kwamba dhana nzima ya
demokrasia imejengwa katika hoja kinzani na ushindani katika chaguzi. Uimla na
uhodhi ni dhana za kikomunisti.
Katika mfumo wa kikomunisti, viongozi wapo
sahihi wakati wote na yeyote anayewakosoa anakuwa msaliti mkubwa. Vilevile
katika mfumo wa kikomunisit viongozi hutokana na kundi dogo la wateule wa
uongozi na yeyote asiyeteuliwa na kundi hili ni msaliti na hafai. Hivi ndivyo
CCM ilivyojengwa huko nyuma na ndio maana akina Oscar Kambona ilibidi wakimbie
nchi pale walipotamani kukwea ngazi za juu za uongozi wakati walikuwa hawatoki
katika kundi la wateule.
Sasa leo hii wakati dunia
nzima ikiachana na ukomunisti, vyama vya upinzani ndio kwanza vinavaa utamaduni
wa kikomunisti wa kuwambambikizia usaliti wanachama wao wanaodiriki kukosoa
viongozi na kutamani nafasi za juu za uongozi ndani ya vyama vyao. Dhana ya
usaliti katika vyama vya upinzani inajengwa pia kwa wabunge wanaokwenda kinyume
na misimamo ya vyama vyao.
Kwa mfano, sasa hivi kuna
baadhi ya wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda kundi la UKAWA wameamua
kwenda kinyume na vyama vyao kwa kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba
vinavyoendelea mjini Dodoma. Wabunge hawa wametangazwa dunia nzima kwamba ni
wasaliti na wameambiwa watafukuzwa wakati wowote ili wabaki kuwa wabunge wa
mahakama. Hii nayo ni dalili ya ushamba na kutokuelewa dhana ya demokrasia
katika mfumo wa vyama vingi. Ukweli ni kwamba katika utamaduni wa mfumo wa
vyama vingi kuna wabunge wachache hutokea kuwa na misimamo huru na vyama vyao.
Hii ni kwa sababu dira ya utumishi wa mbunge wakati wote huongozwa na mambo
manne, ambayo ni utashi wake mwenyewe, wananchi wa jimbo lake, taifa na chama
chake.
Inapotokea kwamba kuna mgongano wa kiutashi
baina ya mambo haya, mbunge ana haki ya kuamua kadri nafsi na uelewa wake
unavyomtuma. Kwa sababu nilizozieleza hapo juu ni jambo la kawaida sana wabunge
duniani kwenda kinyume na misimamo ya vyama vyao. Kwa mfano, mwezi Aprili mwaka
huu wabunge 20 wa Chama cha Conservatives cha Uingereza walipinga muswada
uliokuwa umependekezwa na Waziri Mkuu, David Cameron wa kuruhusu vyombo vya
dola kuingia umbali wa mita 500 wa nyumba za watu binafsi wakati wowote kwa
ajili ya upekuzi kwa sababu za kiusalama.
Muswada huu ulipita kwa
mbinde baada ya kuungwa mkono na wabunge wa chama cha upinzani cha Labour.
Vilevile mwezi Machi mwaka jana, wabunge wa Conservatives, akiwemo Waziri wa
Mazingira, Owen Paterson, walipinga muswada wa ushoga uliopendekezwa na
serikali na ulipita tu baada ya kuungwa mkono wa wabunge wa chama cha Labour.
Lakini wabunge hawa wa Conservatives
hawakuitwa wasaliti. John McCain ni mbunge maarufu na mkongwe wa chama cha
Republicans nchini Marekani. Huyu anajulikana kama ‘maverick’ kwa sababu ya
misimamo yake ya kuwa mbunge huru ambaye amekuwa akienda kinyume na misimamo ya
chama chake, hasa wakati wa utawala wa Rais George Bush. Huyu hakuitwa msaliti
na hata alipata fursa ya kugombea nafasi ya urais. Kwa ushamba wetu wa dhana ya
demokrasia ingekuwa kwetu angefukuzwa siku nyingi na angeitwa msaliti kwa
kutumiwa na chama pinzani.
Ni aibu kwamba vyama vya upinzani vinazidiwa
hata na CCM katika kuwavumilia wakosoaji wao. Kwa tabia ya uhodhi, uimla na
ufashisti inayojionyesha ndani ya upinzani, wabunge kama akina Deo
Filikunjombe, Kangi Lugola, Samweli Sitta, n.k. wangeshafukuziliwa mbali kama
wangekuwa wanachama wa upinzani kwa misimamo yao ya kwenda kinyume na chama
chao mara kwa mara.
Tutakumbuka kwamba
Filikunjombe ni miongoni mwa wabunge waliosaini waraka wa kutaka kumng’oa
waziri mkuu. Lakini hakuitwa msaliti na chama chake. Sijui hali ingekuwaje kama
ingetokea mbunge wa upinzani angesaini waraka wa kutaka Kiongozi wa Upinzani
Bunge ang’olewe! Pengine jambo la kutisha zaidi ni kauli iliyotolewa na Katibu
Mkuu wa CHADEMA hivi karibuni kwamba chama hiki sasa kilikuwa kinaachana na
uanaharakati na sasa kinajiandaa kuwa chama dola.
Kauli za namna hii ni za
hatari na zinatoa tu kiashiria cha dhamira ya baadhi ya viongozi katika
muktadha wa demokrasia katika mambo mawili. Mosi, dhana pana ya neno harakati
ni ile hali ya kupigania haki za watu au kundi fulani la watu, hasa wanyonge,
na ni kazi mojawapo muhimu sana kwa chama chochote cha siasa, na hasa chama cha
upinzani. Sasa chama kinapotangazia dunia kwamba kinaachana na harakati maana
yake ni kwamba kimeamua kuachana na kupigania haki za watu.
Pili, sababu mojawapo ya kutaka kuiondoa CCM
madarakani ni ukweli kwamba chama hiki ni chama dola ambacho kimejipenyeza
katika kila maisha ya umma. Kwa muundo wake, ni vigumu kwa CCM kuendelea kuwepo
bila dola na vyama vya aina yake vilikufa mara moja baada ya kupoteza dola kama
ilivyotokea kwa KANU na UNIP. Chama hiki kilitengeneza mazingira kwamba mtu
yeyote afanyaye kazi katika utumishi wa umma, kwa mfano, sharti aunge mkono na
kuisaidia CCM.
Wafanyabiashara nao wanahisi kwamba biashara zao
haziwezi kwenda bila mkono wa chama hiki. Sasa tunapambana ili kuwaweka huru
watu wote wasijikute wanaishi maisha ya ufungwa kwa kulazimika kuunga mkono
chama fulani cha siasa. Ndio maana hatuhitaji tena vyama dola katika siasa zetu
kwa sababu vyama vya namna hii ni vyama vya kikomunisti. Kwa hiyo Katibu Mkuu
anapotuambia kwamba wanataka kubadilisha chama chao kiwe chama dola maana yake
anatuambia kwamba anatutengenezea CCM nyingine katika maisha yetu!
Sijui kama alielewa dhana ya chama dola vizuri
wakati anatoa hii kauli. Lakini upinzani unafanya makosa yote haya kwa sababu
viongozi wakewamefuga washabiki ambao kazi yao kubwa ni kushangilia kila
walisemalo na wanalitendalo. Katika vyama hivi wanachama na wafuasi wanaoitwa
kwa kiingereza ‘critical followers’ hakuna na wakijitokeza wachache
wanashughulikiwa. Kwa hiyo kwa muundo wake na matendo ya viongozi wake, vyama
hivi haviwezi kuzalisha akina ‘John McCain’, na kwa sababu hiyo havina
wakosoaji wanaoweza kuwafanya wajitazame. Kwa sababu hii vimejenga kiburi cha
kupendwa kwamba hata wakifanya mambo ya kipuuzi watashangiliwa. Athari za muda
mrefu ni kwamba wananchi watashindwa kuvitofautisha na CCM.
Ndio maana katika utafiti wa shirika la
Twaweza uliotolewa wiki iliyopita ulionyesha kwamba asilimia sabini (70%) ya
watanzania hawaamini kwamba upinzani utafanya tofauti na CCM katika kupambana
na rushwa! Ujumbe wangu ni kwamba lazima upinzani ufanye kazi ya ziada katika
kutengeneza taswira chanya kwa kukumbatia demokrasia kwa uhalisia wake, na
kuacha kufanya mambo ya ki-CCM. Vinginevyo, wananchi watatuone ni walewale tu! –
www.raiamwema.co.tz/kiburi-cha-kupendwa-kimefanya-upinzani-kuvaa-u-ccm-iii
- Dr. Kitila Mkumbo
No comments:
Post a Comment