Uongozi hauji na akili
MOJA ya tunu kubwa ambayo Mwalimu Julius Nyerere alituachia kama taifa ni
kuwaamini sana viongozi. Mwalimu tulimpenda na tulimwamini karibu kwa kila
jambo alilosema na kutenda. Kilichofanya Watanzania tumwamini sana mwalimu sio
kwamba alikuwa ni malaika.
Mwalimu Nyerere aliaminika kwa sababu tatu
kubwa kwa maoni yangu, ambazo ni ukweli, uhalisia na kujua mambo. Mwalimu kama
kiongozi alikuwa ni mkweli, mhalisia na alijua kikamilifu alichokisema na
kukitenda. Hizi ni bidhaa adimu kabisa katika uongozi uliofuata baada ya
Mwalimu.
Kwa kuwa tulimwamini sana Mwalimu Nyerere, na
kwa kuwa alikuwa anajua mambo mengi na kwa upana wake, tulimsikiliza sana na
kukubaliana na karibu kila kitu alichokizungumza na kukifanya. Hata pale
tulipojua Mwalimu alikosea hatukumsuta kwa sababu tulijua hakukosea kwa kutaka
au kwa makusudi. Tulimpa kile wazungu wanakiita ‘benefit of doubt’ kwa sababu
ya ukweli na uhalisia uliokuwa dhahiri. Kwa imani yetu kwa Mwalimu ilifika
mahala kama vile ‘tukajiuzulu’ kufikiri, kwa sababu tulikuwa na mtu anayefikiri
kwa niaba yetu.
Kwa hiyo nchi ikiwa katika msukosuko,
tulisubiri kusikia Mwalimu anasemaje katika hili. Ndivyo ilivyotokea kwa vita
ya Kagera. Kabla ya Mwalimu hajazungumza, taifa lilikuwa limezizima tusijue cha
kufanya, lakini alipozungumza wote tulikubaliana naye. Ndivyo vile vile
ilivyotokea wakati taifa lilikuwa kama halijui likubali mfumo wa vyama vingi au
la. Viongozi wengi wa CCM walikuwa wamepinga vikali kuanzishwa kwa mfumo wa
vyama vingi, lakini mara baada ya hotuba ya Mwalimu kwa vijana huko Mwanza,
wote tukageuka na kukubaliana na mfumo wa vyama vingi.
Kwa hiyo Mwalimu alipandikiza mbegu ya
uaminifu kwa viongozi. Tumeendelea kuwaamini viongozi hata baada ya Mwalimu
kuondoka madarakani na duniani. Tumeendelea kuwaamini kwamba tuna viongozi
wanaofikiri kwa niaba yetu na sisi hatuna sababu ya kuhangaisha bongo zetu
zaidi ya kuchangamkia matamasha ya Fiesta ambayo nayo yanafunguliwa na viongozi
wetu huko mikoani.
Tunadhani kwamba mtu
akishapewa uongozi anapewa na akili! Kwa hiyo hatuwapimi viongozi wetu kwa
uwezo na historia yao kabla na baada ya kupewa uongozi, bali kwa sababu ni
viongozi wanajua na wanaaminika, kwa sababu moja tu - ni viongozi. Sisi
tunaendelea kuamini kwamba kila aliye kiongozi ana akili za kuongoza! Ambacho
hatujang’amua ni kwamba yale ambayo yalitufanya tumwamini Nyerere ni mambo
adimu sana katika uongozi wa leo. Utakuwa na bahati kubwa ukikutana na kiongozi
aliye mkweli, mhalisia na anayejua mambo katika nchi hii. Na hapa sizungumzii
tu uongozi serikalini; ni kote –katika serikali, mashirika ya umma, vyama vya
siasa na maeneo mengine mengi.
Viongozi wetu wengi wana
akili za kuagizwa. Ukimuuliza kwa nini unafanya jambo hili la ovyo kabisa, jibu
lake ni kwamba wakubwa wameamua. Mkubwa naye ukimuuliza anakwambia hivyo hivyo,
kwamba wakubwa wameamua. Yote hii ni kwa sababu si wa kweli, si wahalisia na
wala hawajui sawa sawa mambo wanayoyasimamia. Na hawajui kwa sababu hawajishughulishi
kujua wakiamini kwamba kwa kuwa wao ni viongozi wanajua!
Ni kwa sababu ya kuwaamini
sana viongozi wasio wa kweli, wasio na uhalisia na ambao hawajishughulishi
kujua mambo tumeanza kushuhudia mambo ya ajabu katika nchi hii. Tumefika mahala
watu wanauawa mbele ya viongozi kama ilivyotokea huko Iringa. Lakini kwa sababu
ya kutokuwa wa kweli na kukosa uhalisia, viongozi wetu wanajaribu kusema uongo
bila aibu kwamba kilichomuua marehemu ni kitu kizito kilichorushwa kutoka kwa
raia. Kiongozi huyu anafanya hivyo kwa sababu anajua kwamba ataaminiwa kwa
sababu Watanzania walipandikiziwa mbegu ya kuamini viongozi siku nyingi.
Kiongozi mwingine naye
anakurupuka bila aibu na kutangaza kwamba nitakifuta chama fulani kwa sababu
kinasababisha vurugu katika nchi. Kiongozi anajua anadanganya kwa sababu anajua
fika kwamba vurugu zinasababishwa na vyombo vilivyopewa jukumu la kuzuia
vurugu. Lakini kiongozi huyu anapata ujasiri wa kusema uongo kwa sababu si
mkweli wala mhalisia, lakini muhimu zaidi ni kwa sababu anajua kwamba
Watanzania watamwamini kwa sababu ni kiongozi.
Utamaduni wetu wa kuwaamini sana viongozi ndio
uliosababisha mashirika ya umma kufa kwa sababu viongozi walikuwa wanafanya
mambo ya kipuuzi huku wafanyakazi wakiwaangalia kwa sababu ni viongozi. Na sasa
wafanyakazi wa mashirika ya umma wanaendelea kushuhudia mashirika yakifa kwa
sababu ya imani waliyonayo kwa viongozi wao wanaofanya upuuzi. Vinginevyo,
tutaelezaje kitendo cha mashirika kama ATC, Bandari na TANESCO kufika hapo
yalipofika huku wafanyakazi (wazalendo?) wakiwapo? Ni kipi kilichowafanya
wafanyakazi wa mashirika haya kuvumilia upuuzi uliokuwa ukifanywa na viongozi
hadi mawaziri walipoingilia kati kwa sababu za kisiasa?
Hatua muhimu ya kuwafanya viongozi wetu kuamka
ni kupunguza imani yetu kwao. Tukipunguza imani yetu kwao watafanya bidii ili
waweze kuaminika. Na ili waweze kuaminika itabidi wajifunze ili kupanua uwezo
wao wa kiakili na kiutendaji. Tatizo tulilonalo sasa ni kwamba viongozi wetu
wengi hawana bidii ya kujifunza. Ni wachache wanaosoma vitabu. Hawaandiki, na
kwa hivyo hatujui wanachokifikiria. Kibaya zaidi, hata mambo madogo kama
kuhudhuria makongamano na mijadala mbalimbali hawapo, na hasa makongamano
yasiyo na posho. Kwa hivyo, sisi kama wananchi hatuna njia ya kujua viongozi
wetu wanafikiri nini na wanajua nini. Tumeendelea kuwaamini kwamba kwa sababu
ya imani yetu ya muda mrefu kwamba viongozi wanajua.
Ukweli ni kwamba uongozi
haumpi mtu akili, bali unaweza kumpatia fursa ya kujifunza kama anataka
kujifunza. Ndio kusema kama mtu ni mjinga leo, ataendelea kuwa mjinga hata kama
atapewa nafasi ya uongozi kesho kama hatafanya bidii ya kujielimisha. Uongozi
hauondoi ujinga. Kwa hiyo tuache kuamini kila jambo linalosemwa na viongozi kwa
sababu tu ni viongozi. Hii ni muhimu zaidi katika kipindi hiki ambacho taifa
lina uhaba mkubwa wa ukweli na uhalisia miongoni mwa viongozi wa kizazi cha
leo. Kwa maneno mengine, hakuna Nyerere wa kufikiri kwa niaba yetu na ni lazima
sasa tuanze kujitegemea katika kufikiri. -
No comments:
Post a Comment