WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 29, 2014

Mambo manne yaliyotikisa kamati za Bunge la Katiba


Siku 15 za kamati 10 kati ya 12 za Bunge la Katiba ambazo zilikuwa zinajadili vifungu mbalimbali vya Rasimu ya Katiba zimekamilika na sasa wenyeviti wake wapo kwenye hatua za uandishi wa ripoti kwa ajili ya kuiwasilisha ndani ya Bunge Septemba 02, mwaka huu ili mjadala wa wazi uanze .

Kamati zilianza kufanya kazi hiyo Agosti 06, mwaka huu, katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na zilijikita katika kujadili, kuboresha na kuongeza masuala mbalimbali kwenye Rasimu hiyo.

Wakati kamati hizo zikiwa zimejichimbia katika kumbi hizo, kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), limesusia mchakato huo tangu Aprili 16, mwaka huu, kwa kile walichoeleza ni kutoridhika na mwenendo wa Bunge hilo ambalo linaundwa na wajumbe wengi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM)

Umoja wa Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF ambao kwa nyakati tofauti wameapa kutorejea ndani ya Bunge hilo huku wakishinikiza kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa hauwezi kuleta Katiba bora.

Mambo manne yaliyojadiliwa kwa kina na kuumiza vichwa vya wajumbe na kuamua kuunda kamati ndogo ndani ya kamati na kwenye kamati ya uongozi ambayo wajumbe wake ni wenyeviti wa kamati zote.

Muundo wa Bunge, uraia pacha, Mahakama ya Kadhi na kamati ya pamoja ya fedha kati ya Bara na Zanzibar ndiyo mambo yaliyoumiza vichwa vya wajumbe hao kwenye kamati na kusababisha mpasuko mkubwa.

Kamati namba moja, Tatu, tano, nane na kumi zilijitokeza mbele ya waandishi wa Habari na kueleza jinsi suala hilo lilivyokuwa na mjadala mpana huku mapendekezo ya wajumbe yakitofautiana.

Mapendekezo ya wajumbe wanaopinga muundo wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linajumuisha wabunge wa Bara na wachache kutoka Zanzibar, wametaka kuwepo kwa Bunge litakaloshughulikia masuala ya Muungano pekee, Bara kuwa na Bunge lao la kuzungumzia masuala yao na Zanzibar kuendelea na Baraza la Wawakilishi.

Wengine wametaka kuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na chemba mbili kwa ajili ya masuala ya Zanzibar na Bara ambayo yataamuliwa majina na mahali pa kukutana.

Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, anasema kamati yake imeshindwa kufanya maamuzi juu ya suala hilo kwa kuwa wapo wajumbe wanaokubaliana na muundo wa sasa na wengine wanapinga.

" Matatizo ya nchi hayawezi kutatuliwa kwa muundo wa mabunge matatu, mfumo uliopo unatosha kabisa kutatua matatizo ya nchi na siyo kutaka kuwepo kwa Bunge jingine la Tanganyika," anasema Makamu Mwenyekiti, Prof. Makame Mbalawa.

Pia, Mahakama ya Kadhi, wajumbe wengi wametaka liingizwe kwenye Rasimu hiyo ili iweze kuhudumiwa na serikali huku wajumbe wengine wakitaka liachwe kwenye dini husika na siyo serikali kuingilia.

Mwenyekiti wa kamati namba nane, Job Ndugai, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la Seneti na mabunge mawili kwa ajili ya Bara kujadili masuala yao na Zanzibar wajadili masuala yao.

Anasema wabunge wa Bunge la Seneti ambalo litakuwa na jukumu la kujadili mambo nyeti ya nchi ikiwamo ya Muungano na wabunge wake watoke kwenye pande za Muungano.

" Wajumbe wengi walisema Zanzibar imepata nafasi ya kuwa na Baraza la Wawakilishi ambalo hujadili masuala yao, bado wanaingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo hujadili masuala ya Bara," anasema.

Mwenyekiti wa kamati namba tatu, Dk. Fransis Michael, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la juu na chembe mbili ambazo zitaruhusu Bara kujadili mambo yao na Zanzibar pia na wachache kuwakilisha kwenye Bunge la juu.

"Muundo wa Bunge zilikuja nadharia nyingi, wabunge wa Zanzibar wanapokuwa huku na miswada ikitoka Bungeni lazima iridhiwe na Baraza la Wawakilishi kwanza, tukakubaliana tuwe na Bunge lenye session mbili, ya kwanza wajadili ya Bara, ya pili wajadili ya Zanzibar na wachache waingie kujadili ya Muungano," anasema.

Mwenyekiti wa kamati namba 10, Anna Abdalah, alisema kamati yake nimeridhika na muundo wa Bunge uliopo na imefuta vyeo vya kuteuliwa ambavyo kwenye Rasimu vimetajwa kuwa viongozi wake lazima wathibitishwe na Bunge.

Anasema kusema kila upande uwe na Bunge lake ni dhambi ya ubaguzi ambayo haitakiwi kwa kuwa muundo uliopo sasa siyo kero.

" Tubaki na muundo uliopo sasa hauna tatizo lolote, kutaka mabunge matatu hata uyape majina gani ni sawa na kutaka serikali tatu ambazo zitavunja Muungano, haikubaliki kamati yetu tunajadili Rasimu kwa maudhui ya serikali mbili hivyo tunaondoa mambo yote yanayohusu serikali tatu," anasema.

Anasema kufanya hivyo ni mwingiliano wa mihimili kwa kuwa muhimili mmoja hauwezi kuwajibisha mtu ambaye hawana mamlaka naye.

" Bunge siyo mwarobaini wa mambo kila mtu ana sehemu yake, kuna muhimili wa serikali, Mahakama na Bunge, tusiingiliane kila mmoja athibitishe watu wake...mfano Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Uwajibikaji athibitishwe na Bunge na wakati huo huo anawasimamia wabunge itatoa nafasi ya kujipendekeza ili achaguliwe," anafafanua.

Makamu mwenyekiti wa kamati namba 11, Hamad Yusuph Masauni, anasema kamati yake imependekeza kuwepo kwa Bunge la Muungano na mabunge mengine ambayo yatajadili masuala ya nchi husika na kukutana kwenye masuala ya pamoja pekee.

Masuala mengine yaliyozua mjadala mkali ni uraia pacha, kiasi cha Bunge kukaribisha mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Boneventure Rutinwa, ambaye alitoa elimu ya suala hilo lakini bado halikuafikiwa kwenye kamati zote na kupelekwa kwenye kamati ndogo ya uongozi.

Hamad Rashid Mohamed, Mwenyekiti wa Kamati namba tano, anasema walijadili kwa kina kwa kujiuliza iweje mtu aliukana uraia wake na kutaka apate haki nyingine na kuliangalia kwa jicho la pana,'' anasema

Masauni anasema kwenye kamati yake wamepitisha uraia pacha, lakini mtu asiwe na haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi.

Baadhi ya wajumbe wamepinga muundo wa sasa wa Bunge kwa madai kuwa Zanzibar inapata upendelea kuliko Bara na wabunge wake kushiriki, kupiga kura na kuamua juu ya masuala ambayo hayawahusu.

Mjumbe wa kamati namba moja, Alli Kessy, anasema ili kuondokana na kero za Muungano ni lazima kuwe na mabunge matatu ambayo ni Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi na Tanganyika.

Bunge la Muungano wabunge wake watokane na mabunge ya chini kwa kila moja kuwa na wabunge kumi na kukutana kwa ajili ya kuzungumza masuala ya msingi yanayozikabili nchi husika.

"Kwa sasa wabunge wa Zanzibar wanaingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na kujadili masuala yasiyowahusu kama ya Tamisemi, kilimo, ujenzi na Mifugo ili hali mambo yao wanayajadili kwenye Baraza la Wawakilishi ambalo hakuna Mbunge wa Tanzania anaingia," anasema.

" Lazima Bara tupewa haki yetu ya kujadili masuala yetu kama ilivyo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo hatuliingilii kabisa, iweje Mbunge wa Mkajageni apate nafasi ya kujadili na kuamua masuala ya Nkasi ambayo hayamuhusu nami sipati nafasi ya kujadili masuala yao," anafafanua.

Mjumbe mwingine, Ester Bulaya, anasema ni lazima watanganyika wawe na Bunge lao kwa maana ya kuwa na mabunge matatu ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar ili kutoa nafasi kwa kila upande kujadili masuala ya msingi ya eneo lao.

" Si lazima tuwe na serikali tatu bali mabunge matatu, yale ya Muungano tuyazungumze kwenye Bunge la pamoja, wenzetu wana Baraza la Wawakilishi wanajadili na Bara hakuna anayeingia ila inapokuwa kujadili masuala ya bara wanashiriki ilihali hayawahusi," alifafanua.

Anasema kuendelea na Bunge la sasa ni kuwanyima haki watu wa Bara hivyo wakati umefika kupewa nafasi ya kujadili na kupanga mambo yao bila kuingiliwa na kuamuliwa.

" Sipati nafasi ya kujadili masuala ya Dole ila wao wanajadili masuala ya Bunda na kwingine kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, kwa sasa tutenganishe yale ya Muungano ndiyo tuyazungimze kwenye Bunge la Muungano," alibainisha.

Mwenyekiti wa kamati ndogo inayoshughulikia masuala hayo, Suluhu anasema wamemaliza kujadili na kuandika mapendekezo ya masuala ya Mahakama ya Kadhi na uraia pacha ambayo yamewasilishwa kwenye kamati kwa ajili ya kufanya maamuzi ngazi ya kamati.

Kwa upande wake Dk. Michael anasema kamati yake imependekeza kuwa iwapo mgombea urais atatoka Bara, mgombea mwenza atoke Zanzibar na Rais wa Zanzibar awe Makamu wa pili wa Rais.

Tofauti na kamati nyingine, kamati ya Mwalimu na Masauni imependekeza Rais wa Zanzibar awe Makamu wa kwanza wa Rais ili anapokwenda nje ya nchi apate hadhi kama Rais wa Tanzania na Makamu wa pili awe Waziri Mkuu.

Agosti 22, mwaka huu, kamati zilipokea maoni mapya kutoka kwa makundi, taasisi, wananchi na serikali ambayo yatajadiliwa na kuangalia kama wanaweza kuunda sura mpya.

Mapendekezo yaliyoletwa na serikali kupitia kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro yanahusu masuala ya ardhi, maliasili, mazingira na serikali za mitaa.

Yaliyoletwa na wananchi na taasisi ni nchi kuwa na uchumi imara, haki za wanunuzi wa bidhaa mbalimbali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), kutaka iruhusiwe kushughulikia wahujumu uchumi.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo kamati itapiga kura kuamua masuala mbalimbali ingawa hazina mamlaka ya kutoa maamuzi ya mwisho na badala yake maamuzi hayo yatatolewa na Bunge zima kwa kupiga kura ili kupata theluthi mbili ya Zanzibar na Bara.

Makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi nayo yaliwasilisha maoni yao kwa uongozi wa Bunge yakitaka matatizo yao yaingizwe kwenye Katiba mpya.
CHANZO CHA HABARI: Na Salome Kitomary: NIPASHE

EMMANUEL OKWI AREJEA SIMBA SC



Msimbazi ni nyumbani; Okwi akiwa na jezi ya Simba SC baada ya kurejea timu yake ya zamani leo

NA BIN ZUBERY
 
STAILI ile ile waliyotumia Yanga SC kumpata mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi ndiyo ambayo klabu yake ya zamani, Simba SC inaitumia kumrejesha kundini Mganda huyo.
 
 
 
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari jioni hii mjini Dar es Salaam, Okwi amesema kwamba amesaini Simba SC mkataba huru wa muda, baada ya Yanga SC kumpa barua ya kusitisha mkataba naye jana pamoja na kumshitaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
 
Okwi amesema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki
ambacho ana matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA haitaki mchezaji akae bila kucheza.
 
“Sasa wakati Yanga wanaendelea na kesi yao, mimi ninaomba nichezee Simba SC ili kulinda kipaji changu. Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina matumaini usajili wangu utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika hili,”amesema.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.
 
“Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC,”amesema Poppe. 
 
Yanga mtanikoma; Okwi akiwa ameshika jezi yake nbamba 25 kwa pamoja na Hans Poppe

Tayari Simba SC imetuma jina la mchezaji huyo katika usajili wake TFF na ataungana na Mganda mwenzake, Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe na Mkenya, Paul Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni.
 
“Tumewaandikia barua TFF kuomba kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi yake na Yanga inaendelea, tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba kucheza kwetu kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.
 
Okwi aliichezea Simba SC tangu mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia.
 
Etoile haikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi, aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu.
 
Okwi akawafungulia Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.
 
Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani.
Okwi aliichezea Yanga SC mechi 11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo.
 
Okwi alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi minne tu baadaye tangu asajiliwe.
 
Vikao kadhaa vimekwishafanyika baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta suluhu ya suala hilo na kikao cha mwisho leo baina ya mchezo huyo na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.
 
Kuhusu deni lao la dola 300,000 kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema haihusiani kabisa na usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha zetu kule FIFA ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa hukumu tu,” amesema.
 
source: matukiotz.com

Wednesday, August 20, 2014

JK AHANI MSIBA WA MAREHEMU JAJI MAKAME

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweha saini katika kitabu cha maombolezo alipokwenda kutoa pole nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame Masaki jijini Dar es salaam aliyefariki  katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe Agosti 19, 2014.
 Mama Salma Kikwete akiweha saini katika kitabu cha maombolezo alipokwenda kutoa pole nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame,  Masaki jijini Dar es salaam aliyefariki  katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe  Agosti 19, 2014.
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiwafariji wafiwa walipokwenda kutoa pole nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame,  Masaki jijini Dar es salaam aliyefariki  katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam  Agosti 19, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na watoto wa marehemu pamoja na Jaji Mstaafu Mark Bomani alipokwenda kutoa pole nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame Masaki,  jijini Dar es salaam aliyefariki  katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe Agosti 19, 2014.(P.T)

source: mjengwa blog

Tuesday, August 19, 2014

KWA NINI TUNASHINDWA KUTEKELEZA SHERIA




Kwa nini sheria hazifuatwi katika maisha ya kila siku ya mtanzania  tatizo liko wapi? Sheria hazieleweki au sheria zimejaa mianya mingi inayoruhusu kutofuatwa katika utekeleji wake?

Tunapaswa kufanya nini ili kuhakikisha kuwa harakati za kutetea na kuona kuwa sheria zinafuatwa, zinafanikiwa bila kuvunja misingi ya utawala bora na wa sheria?

Je "Watu wote ni sawa mbele ya sheria, au wengine wanayo haki zaidi kutokana na umaarufu wao?.

Je utekelezaji wa sheria unafanyika bila ubaguzi wowote, na kumwezesha kila raia keheshimiwa na kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria"?



Ni kwa namna gani tunaweza kujenga mfumo wa utawala wa sheria usioipa nafasi dola kutumia kiujanja mianya ya kisheria na kupata nafasi ya kutotekeleza kanuni za sheria na kama itatekelezwa kuchukua muda mrefu ili kupunguza nguvu ya kosa katika kuleta haki inayotakiwa kwa jamii?

Je Migomo, maandamano, pamoja na uharibifu mkubwa wa mali unaofanywa kutoka na matukio haya ni sababu ya kwisha kwa uvumilivu kutoka na uzembeaji katika kutekeleza sheria au ni mazoea tu yaliyojengeka mbele ya raia au jamii?


Ni ukweli ambao haufichiki kuwa miaka takribani 50 ya uhuru wa  nchi hii wananchi wameweza kuona ni kwa jinsi gani matatizo yanayoikumba nchi Tanzania yanazidi kuongeza licha ya kuwepo utawala wa sheria. Na wakati huo huo kuna vyombo na taasisi mbalimbali za kisheria zenye nguvu na mamlaka ya kushughulikia zikiwa zimepewa nyenzo na nguvu za kisheria katika kutekeleza majukumu yao, cha kushangaza ni kuwa taasisi au idara hizo zipo na pengine zinaangalia tu bila kuwajibika. 


  • Je zinaogopa au hazioni umuhimu wa kuwajibika kwa sababu za masilahi zaidi?



Je hii inatokana na ukweli kuwa pengine sheria pamoja na kupitishwa na vyombo husika lakini utekelezaji wake lazima ubarikiwe na kikundi kidogo cha wenye mali Mafisadi ili itekelezwe kwa matakwa yao.


  • Kama ni hivyo basi sheria iko kwa ajili na kwa manufaa ya nani? 



  • Je sheria zinatungwa na matajiri kuwazuia maskini kuwasogelea matajiri na kuhakikisha matajiri wanaendelea kutumia utekelezaji wa sheria kuwakandamiza maskini; 



  • je sheria zinatungwa kuwafurahisha matajiri na kuwaridhisha maskini lakini wakati wote kuwanufaisha watawala!

Ni aibu kama vyombo vya dola vinaweza kumfunga Mmachinga katika siku mbili kwa kosa na kuuza vitu katika sehemu ambayo haijeruhusiwa na wakati huo huo inashindwa kumfunga Fisadi aliyethibitika kuliibia taifa mabilioni ya shilling kwa vile tu eti kwa sababu ya pesa zake anaweza kushinda kesi na kuisababishia serikali hasara zaidi; lo hii ni hatari.

Swali la msingi hapa sheria zetu ni kwa ajili na manufaa ya nani? Kwa nini utekelezaji wake unakuwa na kigugumizi. Nafikiri uzaifu huu wa sheria zetu ndio unaotuletea kila ambacho wananchi kuhukumu na kuchukua hatua ambazo wakati mwingine zinakiuka utaratibu wa utawala bora;



  • je ni busara haki hata kama iko ndani ya sheria haitatekelezwa mpaka kwa maandamano na migomo;

Haki ya ya matibabu bora haitapatikana mpaka kwa utoaji rushwa;
Haki yangu ya kosa lolote la barabarani haitaeleweka mbele ya askari wa usalama wa barabarani bila ya hongo;


Wananchi wanatakiwa kuelimisha kwa upole na upendo pale wanapokosea na ikibidi adhabu ifanywe kulingana na sheria; mkosa alipe faini yake kihalali ili iwe ni fundisho na pesa hiyo isadie maendeleo ya nchi;

Kwa kufanya hivyo taifa litaweza kuimarisha utawala bora, amabao ni utawala wa sheria, na hapo itakuwa rahisi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali ya umma. Mhalifu anaweza na anapaswa kuadhibiwa kwa sababu amehalifu sheria kwa matakwa/ridhaa yake.  

kwani inamaanisha kuwa mara mtu anapotiwa hatiani na kuonekana kuwa alitenda kwa ridhaa yake na akijua anachotenda hapo hapo uhuru wake unabadilishana na faini halali ambayo inampasa kulipa. tukiweza kujenga mazingira ya kulipa faini halali kwa makosa halali;tutafanikiwa vile vile kwashinda wale ambao wanatumia mamlaka au madaraka waliyopewa vibaya kwa lengo la kujipatia manufaa binafsi. 

Nafikiri itakuwa ni busara kama wasimamizi wa sheria watakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yao katika kupinga matumizi mabaya ya sheria hizo kwa mtu yeyote bila kujali cheo chake na pesa zake na anamfahamu nani;

Hilo likiwezekana tutaondoa dhana ya kukimbilia kuhukumu wakati hatuna vithibitisho “Prejudice” ni ukweli ambao haupingiki kuwa watu hawajezaliwa na hali ya kupinga kutotaka kutekeleza sheria bali tatizo na utaratibu mzima wa usimamiaji wa sheria ndio unaopelekea watu kuvunja sheria.

Wazo la leo nini kifanyike kuondoa hali hii ambayo imetawala vichwa vyetu kwa muda mrefu sasa?
·        Jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu haki zao za msingi za     sheria na wanatakiwa wasiinunue haki yao kwa rushwa.
·  Tunahitaji wasimamiaji wa sheria ambao watakuwa tayari kutekeleza majukumu yao bila kuogopa na vile vile kuwaelimisha jamii kuhusu haki yao ya msingi.
·        Inatupasa kujenga uhusiano mzuri kati ya raia na watekelezaji wote wa sheria mfano polisi wawe ni msaada mzuri kwa madereva pale madereva wanapokosea na wawaadhibu bila ya kuwaonea haya hata kidogo na hii itatusaidia kupunguza ajali nyingi;
·  Viongozi wetu wakuu waonyeshe mfano mzuri katika kutekeleza majukumu yao bila upendeleo wowote ule;

Tukifanya hivyo huu utakuwa mwanzo mzuri wa kuirudisha nchi yetu katika dira ya utawala bora na wa sheria.

Pamoja tukisimama hatutashindwa jambo lolote

AJALI HIZI MPAKA LINI?





TATIZO LA AJALI ZINAZOENDELEA NA KUPOTEZA MAISHA YA WATANZANIA WENGI;



  • NI UBUTU WA SHERIA?

  • UBOVU NA UFINYU WA BARABARA ZETU


  • KIBURI CHA MADEREVA?

  • UBOVU WA MAGARI NA UBABE WA WAMILIKI?

Taifa la Tanzania limeendelea kushuhudia  mwendelezo wa ajali nyingi za barabarani ambazo zimeendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa hili.  Kwa ujumla ajali hizi zimekuwa zikitokea kila kona wakati mamlaka za kisheria  zikiendelea kuhimiza kuwa zitahakikisha kuwa zitakomesha vifo vinavyoyokana na ajali hizo.husika kutekeleza yafuatayo;.

Kuimarisha doria katika njia kuu,

Askari wa Usalama Barabarani kuimarisha shughuli za ukaguzi wa magari mabovu,

Kuimarisha elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa kuisaidia Serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu madereva walezi, wanaoendesha mabasi yao kwa kasi, madereva wanaotiliwa mashaka kuhusu ujuzi wao wa kuendesha, na pia kukataa kupanda magari mabovu au yaliyojaa kupita kiwango kinachohitajika,

Kuendelea kuboresha sheria za Usalama Barabarani ili zichangie katika kudhibiti shughuli za usafiri na usafirishaji,. Kutoa elimu kwa madereva ili wazingatie sheria za kanuni za kazi zao,

Kukagua leseni za madereva ili kuhakikisha kuwa ni za halali,

 Kuwashirikisha wenye magari ili washiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanaajiri wadereva waaminifu na wenye kuwajibika. 

Pengine swali ambalo daima ninajiuliza pamoja na malengo mazuri yaliyoainishwa hapo juu, kwa nini serikali imeshindwa kabisa kisimamia utekelezaji wa sheria na sera zake za usalama barabarani kwa raia wake kwa muda mrefu?

  • Je serikali haina askari wa usalama barabarni wa kutosha kukabiliana na tatizo hili?

  • Je ni tatizo ni la wamiliki wa biashara hii wamefanikiwa kuiteka idara nzima ya usalama barabarani?

  • Je madereva wanaoendesha magari hayo wanafahamu fika maadili ambayo wanapaswa kuyafuata kulingana na sheria za usalama  barabarani wakati wa kuendesha magari hayo?



Tathimini ya muda mrefu kutoka  vyanzo mbalimbali inabaini kuwa licha askari hawa kuwapo na tunaambiwa kwa  kiasi kikubwa ajali zinazotokea zinasababishwa na madereva wazembe ambao wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za usalama barabarani.

Tunajua, kwamba madereva wengi wa mabasi ya abiria  wanaendesha wamelewa. 

  • Je hakuna sheria inayowabana kama katika nchi nyingine kuhusu kilevi? 


  • Je, dereva huyu aliyekunywa pombe kabla ya kuanza kuendesha nap engine wakati wa safari  ataweza kuendelea kuwa na maarifa yake ya kawaida na uwezo wake wa kawaida kumudu gari na mazingira ya barabara yanayomkabili?

Inafahamika wazi mara nyingi  askari wa usalama barabarani wanabariki mwendo kasi wa madereva  kwa kupokea rushwa; 

  • je taifa linakubaliana na tabia hii izidi kuendelea? Tunawaacha wakimbize magari wanavyotaka mpaka lini?. 


  • Je tumeshindwa kabisa kusimamia “Speed Limit” ni ukweli ambao huupingiki kuwa Madereva wa mabasi wengi wanakimbia kupita speed waliyopangiwa. 


  • Je ni kweli kuwa serikali kupitia wizara yake kweli imeshindwa kuwadhibiti hawa madereva ambao ambao tunaweza kuwaita  wahuni  na wenye viburi kwani wamekuwa wakiendesha vyombo hivi vya moto kwa mwendo kasi, usiofuata taratibu za usalama barabarani na matokeo yake kusababisha ajali mbaya ambazo matokeo yake ni vifo vingi vya watu.


Kama Taifa imefila wakati sasa serikali iamke na kusema basi inatosha kwa sasa hasa kwa kuanzaia na askari wake wa usalama barabarani wanaelezwa kuchangia uwepo wa ajali kwani wamekuwa wakiruhusu makosa kutendeka kwa sababu tu ya kuchukua rushwa ndogondogo.


Kwa nini serikali imeshindwa kusimamia sheria ya kutowaruhusu madereva matumizi ya simu za mikononi wanapokuwa wakiwaendesha raia;  ni vigumu sana kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja uwe makini barabarani na hapo hapo utumie simu kuongea na mtu mwingine;

Ni busara ya kawaida tu dhamana ambayo umebeba kama dereva ni zaidi ya Kuongea kwenye simu za mikononi kwa hiyo tabia hii  haifai kabisa kwa dereva wa gari la abiria aendeshapo gari. Hii ni hatari kwa abiria na watu wengine watembeao kwa miguu. Matokeo yake baada ya kujenga   madereva wanaleta kilio na hasara kubwa kwa taifa taifa letu na familia zetu kwa mambo tunayonaweza kuyazuia bila gharama yoyote

  • Je serikali kupitia wizara inakubali kuwaona askari wake wakikwepa maadili na kiapo chao cha kazi kwa kujihusisha na rushwa na kuhatarisha usalama wa watu wake; Tumke sasa kwa usalama wa watu wetu na kupinga kwa kauli moja mwendo kasi unaoendana na kutojali sheria na alama za barabarani

Ni ukweli ambao haufichiki kuwa hata sheria zetu zinatoa mwanya mkubwa kwa mahakama kuwatoza faini ndogo badala ya kifungo au adhabu kubwa ambayo itakuwa pigo kwa dereva mna mmiliki wa biashara hiyo. 

Wote ni mashahidi wa jinsi ambayo watu ambao wamesababisha ajali kwa uzembe wa kujitakia, tena ajali ambayo imesababisha vifo vingi , lakini wamekuwa wakipigwa faini ya Sh50,000 na kuachiwa huru.  

  • Je nchi nyingine wamefanikiwa namna gani kudhibiti ajali hizo za uzembe? Kwa nini tusijifunze kutoka huko?  


Pamoja na kwamba ajali haziwezi kuzuilika jumla,lakini tuzipunguze.Ajali ya gari inapotokea sio dereva tu ndiye wakulaumiwa,ang alia hali za barabara zetu zilivyo,hali ya hewa,abiria nao je wanaelewa sheria za barabarani ili kumkemea dereva anapovunja sheria hizo.Jambo la msingi ni kuelimisha watanzania wote wajue sheria za barabarani.

Tuangalie sheria Namba 30 ya Mwaka1973 na marekebisho yake ya mwaka 1996 inayohusu ni jinsi gani magari yanatakiwa yawe yakiwa barabarani.  Pamoja na tatizo la madereva  tuzinagatie vile vile tatizo la ubovu wa magari amabayo vile viel huwa ni chanzo cha ajali nyingi;

je wamiliki wanatoa kipaumbele gani katika kuhakikisha kuwa magari yao yako katika hali nzuri ya kusafirisha abiria kwa usalama?



Kwani nini gari bovu ambalo halina break nzuri linaruhusiwa kusafiri? Kama dereva ambaye anajali akatae kuendesha mpaka litengenezwe; uungwana wa wamiliki utaweza kuepusha ajali nyingi ambazo zinaweza kuzuilika kwa kutumia muda wa ziada kutengeneza gari na kuhakikisha kuwa liko salama kwa matumizi ya wananchi;  kama wamamiliki watalazimisha matumizi ya gari bovu  hatulidanganyi jeshi la polisi bali tunajidanganya sisi wenyewe na hatimaye kupoteza nguvu kazi ya taifa. 

Pamoja na tatizo kubwa la uchakavu wa miundombinu, ikizingatiwa kuwa   barabara nyingi haziko katika hali nzuri sana au nyingine pamoja na kutengenezwa hivi karibuni bado hazijeweza kusaidia kupunguza vifo kutokana na pengine kuwa chini ya kiwango  na kusababisha ajali haraka.  



Tunaomba serikali ikishauriana na wataalamu wake kuangalia  namna ya  kuepusha janga hili kwa kuwa na usimamizi ulio bora na kurekebisha mapungufu yatokanayo na:

Barabara mbovu; Magari mabovu; Mwendo wa kasi; Udereva mbaya; Usimamizi dhaifu wa sheria; na Watembea kwa miguu wasiojali. Rushwa katika utoaji leseni za udereva umetajwa katika orodha ya sababu za ajali chini ya kifungu cha Usimamizi dhaifu wa sheria. Kuruhusiwa kwa magari mabovu.


Safari bila ajali zinawezekana kabisa tunaomba serikali na watendaji wao watusaidie kuokoa maisha ya watanzania wanaendelea kupoteza maisha kwa uzembe tu wa utekelezaji wa sheria

Monday, August 18, 2014

LIPUMBA: MOYO WETU UKAWA NI WAJUMBE 14


Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.(Martha Magessa)

Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kuhudhuria vikao.

Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya serikali tatu.

Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.

Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.

"Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21," alisema.

"Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia kwa karibu."

Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.

"Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni Serikali," alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

"Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano."
Aitetea Tume ya Jaji Warioba

Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.

CHANZO:MWANANCHI

Friday, August 15, 2014

Si kila kiongozi ana akili ya kuongoza


Uongozi hauji na akili MOJA ya tunu kubwa ambayo Mwalimu Julius Nyerere alituachia kama taifa ni kuwaamini sana viongozi. Mwalimu tulimpenda na tulimwamini karibu kwa kila jambo alilosema na kutenda. Kilichofanya Watanzania tumwamini sana mwalimu sio kwamba alikuwa ni malaika.

 Mwalimu Nyerere aliaminika kwa sababu tatu kubwa kwa maoni yangu, ambazo ni ukweli, uhalisia na kujua mambo. Mwalimu kama kiongozi alikuwa ni mkweli, mhalisia na alijua kikamilifu alichokisema na kukitenda. Hizi ni bidhaa adimu kabisa katika uongozi uliofuata baada ya Mwalimu.

 Kwa kuwa tulimwamini sana Mwalimu Nyerere, na kwa kuwa alikuwa anajua mambo mengi na kwa upana wake, tulimsikiliza sana na kukubaliana na karibu kila kitu alichokizungumza na kukifanya. Hata pale tulipojua Mwalimu alikosea hatukumsuta kwa sababu tulijua hakukosea kwa kutaka au kwa makusudi. Tulimpa kile wazungu wanakiita ‘benefit of doubt’ kwa sababu ya ukweli na uhalisia uliokuwa dhahiri. Kwa imani yetu kwa Mwalimu ilifika mahala kama vile ‘tukajiuzulu’ kufikiri, kwa sababu tulikuwa na mtu anayefikiri kwa niaba yetu.

 Kwa hiyo nchi ikiwa katika msukosuko, tulisubiri kusikia Mwalimu anasemaje katika hili. Ndivyo ilivyotokea kwa vita ya Kagera. Kabla ya Mwalimu hajazungumza, taifa lilikuwa limezizima tusijue cha kufanya, lakini alipozungumza wote tulikubaliana naye. Ndivyo vile vile ilivyotokea wakati taifa lilikuwa kama halijui likubali mfumo wa vyama vingi au la. Viongozi wengi wa CCM walikuwa wamepinga vikali kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini mara baada ya hotuba ya Mwalimu kwa vijana huko Mwanza, wote tukageuka na kukubaliana na mfumo wa vyama vingi.

 Kwa hiyo Mwalimu alipandikiza mbegu ya uaminifu kwa viongozi. Tumeendelea kuwaamini viongozi hata baada ya Mwalimu kuondoka madarakani na duniani. Tumeendelea kuwaamini kwamba tuna viongozi wanaofikiri kwa niaba yetu na sisi hatuna sababu ya kuhangaisha bongo zetu zaidi ya kuchangamkia matamasha ya Fiesta ambayo nayo yanafunguliwa na viongozi wetu huko mikoani.

Tunadhani kwamba mtu akishapewa uongozi anapewa na akili! Kwa hiyo hatuwapimi viongozi wetu kwa uwezo na historia yao kabla na baada ya kupewa uongozi, bali kwa sababu ni viongozi wanajua na wanaaminika, kwa sababu moja tu - ni viongozi. Sisi tunaendelea kuamini kwamba kila aliye kiongozi ana akili za kuongoza! Ambacho hatujang’amua ni kwamba yale ambayo yalitufanya tumwamini Nyerere ni mambo adimu sana katika uongozi wa leo. Utakuwa na bahati kubwa ukikutana na kiongozi aliye mkweli, mhalisia na anayejua mambo katika nchi hii. Na hapa sizungumzii tu uongozi serikalini; ni kote –katika serikali, mashirika ya umma, vyama vya siasa na maeneo mengine mengi.

Viongozi wetu wengi wana akili za kuagizwa. Ukimuuliza kwa nini unafanya jambo hili la ovyo kabisa, jibu lake ni kwamba wakubwa wameamua. Mkubwa naye ukimuuliza anakwambia hivyo hivyo, kwamba wakubwa wameamua. Yote hii ni kwa sababu si wa kweli, si wahalisia na wala hawajui sawa sawa mambo wanayoyasimamia. Na hawajui kwa sababu hawajishughulishi kujua wakiamini kwamba kwa kuwa wao ni viongozi wanajua!

Ni kwa sababu ya kuwaamini sana viongozi wasio wa kweli, wasio na uhalisia na ambao hawajishughulishi kujua mambo tumeanza kushuhudia mambo ya ajabu katika nchi hii. Tumefika mahala watu wanauawa mbele ya viongozi kama ilivyotokea huko Iringa. Lakini kwa sababu ya kutokuwa wa kweli na kukosa uhalisia, viongozi wetu wanajaribu kusema uongo bila aibu kwamba kilichomuua marehemu ni kitu kizito kilichorushwa kutoka kwa raia. Kiongozi huyu anafanya hivyo kwa sababu anajua kwamba ataaminiwa kwa sababu Watanzania walipandikiziwa mbegu ya kuamini viongozi siku nyingi.

Kiongozi mwingine naye anakurupuka bila aibu na kutangaza kwamba nitakifuta chama fulani kwa sababu kinasababisha vurugu katika nchi. Kiongozi anajua anadanganya kwa sababu anajua fika kwamba vurugu zinasababishwa na vyombo vilivyopewa jukumu la kuzuia vurugu. Lakini kiongozi huyu anapata ujasiri wa kusema uongo kwa sababu si mkweli wala mhalisia, lakini muhimu zaidi ni kwa sababu anajua kwamba Watanzania watamwamini kwa sababu ni kiongozi.

 Utamaduni wetu wa kuwaamini sana viongozi ndio uliosababisha mashirika ya umma kufa kwa sababu viongozi walikuwa wanafanya mambo ya kipuuzi huku wafanyakazi wakiwaangalia kwa sababu ni viongozi. Na sasa wafanyakazi wa mashirika ya umma wanaendelea kushuhudia mashirika yakifa kwa sababu ya imani waliyonayo kwa viongozi wao wanaofanya upuuzi. Vinginevyo, tutaelezaje kitendo cha mashirika kama ATC, Bandari na TANESCO kufika hapo yalipofika huku wafanyakazi (wazalendo?) wakiwapo? Ni kipi kilichowafanya wafanyakazi wa mashirika haya kuvumilia upuuzi uliokuwa ukifanywa na viongozi hadi mawaziri walipoingilia kati kwa sababu za kisiasa?

 Hatua muhimu ya kuwafanya viongozi wetu kuamka ni kupunguza imani yetu kwao. Tukipunguza imani yetu kwao watafanya bidii ili waweze kuaminika. Na ili waweze kuaminika itabidi wajifunze ili kupanua uwezo wao wa kiakili na kiutendaji. Tatizo tulilonalo sasa ni kwamba viongozi wetu wengi hawana bidii ya kujifunza. Ni wachache wanaosoma vitabu. Hawaandiki, na kwa hivyo hatujui wanachokifikiria. Kibaya zaidi, hata mambo madogo kama kuhudhuria makongamano na mijadala mbalimbali hawapo, na hasa makongamano yasiyo na posho. Kwa hivyo, sisi kama wananchi hatuna njia ya kujua viongozi wetu wanafikiri nini na wanajua nini. Tumeendelea kuwaamini kwamba kwa sababu ya imani yetu ya muda mrefu kwamba viongozi wanajua.

Ukweli ni kwamba uongozi haumpi mtu akili, bali unaweza kumpatia fursa ya kujifunza kama anataka kujifunza. Ndio kusema kama mtu ni mjinga leo, ataendelea kuwa mjinga hata kama atapewa nafasi ya uongozi kesho kama hatafanya bidii ya kujielimisha. Uongozi hauondoi ujinga. Kwa hiyo tuache kuamini kila jambo linalosemwa na viongozi kwa sababu tu ni viongozi. Hii ni muhimu zaidi katika kipindi hiki ambacho taifa lina uhaba mkubwa wa ukweli na uhalisia miongoni mwa viongozi wa kizazi cha leo. Kwa maneno mengine, hakuna Nyerere wa kufikiri kwa niaba yetu na ni lazima sasa tuanze kujitegemea katika kufikiri. -