Kauli ya Spika wa Bunge Anne Makinda: Wabunge wanafanya mambo ya KIJINGA ina maana gani kwa jamii
· “Tufunge mlango tupigane”
· "Mmezowea kutuburuza"
· "Naomba mjiheshimu hapa si sokoni, Watanzania wengi wanawaangalia mnavyofanya mambo ya kijinga na kupiga kelele,"
Tusiwalaumu tuu wabunge, tujiulize wameingiaje bungeni? Tatizo la ujinga kama uko ambao unatokea Bungeni kama alivyosema mheshimiwa Spika linatoka na sisi tunaowachagua; je tunatumia vigezo gani kujua kweli kama WABUNGE TUNAOWACHAGUA wanaweza kujenga hoja za kweli na sio itikadi tu ya chama atokacho mbunge? Kama bunge halifanyi kazi yake vizuri lawama ni kwetu wananchi tuliowachagua.
Kwa watanzania wengi ambao walibahatika kufuatilia nini kilikuwa kinajili bungeni Dodoma wiki chache zilizopita watakubaliana nami kuwa tuliweza kupata kioja cha kuhitimisha mijadala ya bunge katika kikao chake cha 10.
Ilimlazimu Mheshimiwa Spika kutamka maneno ambayo nafikiri yalikuwa hayastahili kutamkwa bungeni kwa heshima na majukumu makubwa ya kazi ya bunge kama chombo muhimu sana katika kusaidia kuendesha shughuli za serikali; katika majukumu ya Kiuwakilishi (representational),utungaji wa sheria (legislative), upitishaji wa bajeti, mapato na matumizi ya nchi (budgetary and resource approval) pamoja na uwajibishaji wa serikali iliyoko madarakani (accountability). Bunge pia ni chombo cha kutathmini mwenendo wa jumla wa kisera unaopendekezwa na serikali ili kubaini kama mwelekeo wake unasawiri matakwa ya wananchi walio wengi nchini. Aidha ni kazi ya Bunge katika mfumo wa kidemokrasia kuhakikisha kuwa matendo ya serikali iliyopo yanakidhi matakwa ya jamii wanayoiwakilisha, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hoja nzuri na kupinga zile zinazoonekana kukinzana na maslahi ya jumla ya kitaifa.
Je Bunge letu linatekeleza kwa umakini majukumu haya au bunge kwa sasa limekuwa ni chombo kikuu cha ushauri tu kwa serikali bila kuwa na meno ya kuiwajibisha serikali pale ambapo inakosea?
Kwa maneno mengine wabunge wamechaguliwa na wananchi ili wawakilishe katika kuisimamia serikali. Hivyo wabunge hawatakiwi kabisa kupeleka mawazo na mitazamo yao wenyewe. Wanatakiwa wanapozungumza Bungeni au kupiga kura ni lazima wafikirie wapiga kura wao wamewatuma kufanya nini.
Je tuliwatuma waende kupigana bungeni? Au kugeuza bunge kuwa ni soko kama mheshimmiwa makinda alivyowakemea wabunge wenzake;
Je wabunge wetu ambao tumewachagua wanao uwezo wa kutawala katika kuchangia hoja bila kupigana na kutishana? Au ni wale ambao wanapenda sana kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala.”
Je wabunge wanafahamu kuwa Bunge letu la sasa bado lina nguvu kubwa ambayo halijaweza kuitumia vyema.
Nafikiri tatizo la wabunge wengi wanatumia muda wao mwingi kulalamika na kushangaa mapungufu. Wanatakiwa wawe na uwezo wa kupangua na kupanga upya mambo wanavyoona wao inafaa bila kujali maneno na minong’ono ya wanafiki wachache na wasio jali maslai ya wengi au kuwa na muono wa mbali.
Je wabunge wetu wengi ni kundi gani?
Je tunao wabunge wenye uwezo wa uongozi na wito wa uongozi kwa kuweka maslahi ya taifa mbele kwa manufaa ya watu.
Wabunge wetu wameingia bungeni kama moja ya njia sahihi za kujipatia neema, ubinafsi na maslahi binafsi;
Je abunge wetu ni wale wenye uwezo mkubwa wa kushawishi kutokana na uwezo wao wa kiuchumi, haautegemei mshahara wala marupurupu ya ubunge; Hawana muda wa kuchangia mijadala ya bungeni, wala hawana maswali, ila kwa sababu wana nguvu kubwa kiuchumi na jeuri ya pesa, wanao uwezo wa kuwabuluza wabunge wengine na kuhakikisha kuwa wanalolitaka liwe, ndilo linakuwa. Kwa maneno mengine aina hii ya wabunge ndio viongozi wenye nchi.
No comments:
Post a Comment