WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, March 31, 2014

DK.SHEIN AKUTANA NA MABALOZI WA ULAYA


IMG_9076
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Kiongozi wa Ujumbe wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini Filiberto CERIANI SEBREGONDI,walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi kwa mazungumzo ,[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
IMG_9092
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Ujumbe wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini ukiongozwa na Filiberto CERIANI SEBREGONDI,(wa pili kulia)walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi kwa mazungumzo.
IMG_9097
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Kiongozi wa Ujumbe wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini Filiberto CERIANI SEBREGONDI,baada ya mazungumzo yao Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi kwa mazungumzo.
IMG_9102
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Mabalozi wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi baada ya mazungumzo yao.
 
 Chanzo, networkbloggers

Friday, March 28, 2014

Askofu wa Anglikana Dodoma afariki

Dodoma. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, Godfrey Mdimi Mhogolo amefariki dunia akiwa kwenye matibabu nchini Afrika ya Kusini.

Katibu wa Dayosisi ya Dodoma, Luteni Mstaafu Daudi Kandila alithibitisha jana kutokea kwa kifo hicho na kusema kimeacha pengo kwa dayosisi na Kanisa la Anglikana kwa jumla.

Kandila alisema Askofu Mhogolo alifikwa na umauti katika Hospitali ya Mil Park iliyoko Afrika Kusini ambako alipelekwa Machi 19.

“Ni kweli Baba Askofu amefariki jana saa 6:00 mchana. Siwezi kuzungumzia suala hili zaidi kwani katibu mkuu wa jimbo ndiye atakayetoa taarifa kwa undani,” alisema Kandila.

Alisema mtumishi huyo alianza kuugua mapema mwezi Februari na ilipofika Machi Mosi, alipelekwa Hospitali ya African Medical ya Dar es Salaam ambako alitibiwa kwa siku 18 kabla ya kupelekwa Afrika Kusini.
Ugonjwa uliosababisha kifo chake Mhogolo haujajulikana kutokana na maelezo kuwa hadi watakapopata ripoti za madaktari juu ya nini kilikuwa kikimsumbua marehemu kabla ya uhai wake.

Mhogolo amekuwa Askofu wa Dayosisi ya Kati ya Tanganyika tangu mwaka 1999 kipindi kifupi baada ya kifo cha aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Marehemu Yohana Madinda. Katika uchaguzi uliomwingiza madarakani, alimshinda aliyekuwa Askofu Msaidizi wa wakati huo, Donald Mtetemela na kufanya aende kuwa Askofu wa Ruaha (Iringa).

Mhogolo pia aliwahi kuwa katibu wa dayosisi hiyo kabla ya kushika wadhifa huo na alifanya kazi ya kufundisha katika Chuo cha Theolojia cha Kongwa.
Katika uongozi wake, alifanikiwa kuigawa dayosisi yake ambapo Dayosisi za Mpwapwa na Kondoa zilianzishwa. Mpwapwa akawekwa Simon Chiwanga kuwa Askofu na Kondoa akapewa Askofu Yohana Mkavu.

Hadi mauti yanamkuta, alibakiza miezi kadhaa astaafu kwani ratiba ya kanisa inaonyesha Desemba mwaka huu ingekuwa na uchaguzi.

source: mwananchi

Loga: Azam tishio Simba kuliko Yanga

Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Mcroatia,Zdravko Logarusic
Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Mcroatia, Zdravko Logarusic, amesema mechi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Azam itakayofanyika Jumapili ni ngumu na inampa mawazo kwa kuwa anaihofia timu hiyo kuliko hata Yanga.
Logarusic alisema Azam iko katika kiwango cha juu na ushindi mfululizo wanaoupata unawaongezea hali ya kujiamini tofauti na kikosi chake ambacho kimekuwa kikipoteza mara kwa mara.

Kocha huyo alisema pia umuhimu wa pointi tatu za kuamua hatma ya ubingwa kwa wapinzani wao ndicho kinampa wasiwasi zaidi wakati wachezaji wake wanatafuta heshima.

"Ni ukweli usiofichika kwamba mechi hii ni ngumu, ninawahofia zaidi Azam kuliko Yanga," alisema Logarusic.

Alieleza kwamba amekiandaa kikosi chake kukabiliana na ushindani wa kila aina katika mchezo huo na anaamini wapinzani wao pia wamejipanga.

Aliongeza kuwa bado Simba inahitaji kushinda licha ya kutokuwa na matumaini ya kumaliza kwenye nafasi mbili za juu msimu huu unaomalizika Aprili 19.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala, alisema kikosi chao kimejipanga kuendelea kufanya vizuri katika mechi za ligi zilizobakia ili waweze kutimiza malengo yao.

Ongala alisema wanaifahamu vyema timu ya Simba na wachezaji wake wanajua jinsi ya kuwakabili na hatimaye kupata ushindi katika mchezo wao wa Jumapili.

"Tumejipanga kufanya vizuri na kila siku tunaendelea kurekebisha makosa katika timu, lengo ni kuchukua ubingwa msimu huu," alisema kocha huyo msaidizi.

Simba itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha  bao 1-0 dhidi ya Coastal Union wakati Azam wenyewe walipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani kwa kuifunga JKT Mgambo.

Wekundu wa Msimbazi wana pointi 36 na Azam ndiyo vinara wa ligi wakiwa na pointi 50 wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga wenye pointi 46 na mechi moja mkononi huku Mbeya City ikishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 42.

Simba bado inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kinesi ulioko Sinza, jijini Dar es Salaam na Azam ilirejea jana ikitokea Tanga.
 
CHANZO: NIPASHE

Mwenendo huu Bunge la Katiba haufai,unawagawa Watanzania

Katuni
Hali  iliyopo sasa kwenye vikao vinavyoendelea vya Bunge Maalum la Katiba inatia shaka. Inawaogopesha Watanzania wengi, hasa wale waliojawa na shauku ya kuona kuwa taifa linapata katiba bora kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Sisi ni sehemu ya Watanzania tulioingiwa na hofu kubwa juu ya kile kinachoendelea kwenye vikao vya bunge hili.

Kauli zinazotolewa ndani na nje ya Bunge hilo haziashirii mwisho mzuri. Hakika, misukosuko ndani ya Bunge hilo inaonekana kuwa mingi kiasi cha kutoa ishara mbaya juu ya ufanisi wa chombo hicho ambacho kimsingi, kina wajibu wa kupitisha rasimu ya katiba mpya kabla ya kutoa nafasi ya kupigiwa kura na wananchi.

NIPASHE tunaona kuwa hivi sasa, badala ya kutumia muda mwingi wa kuijadili na kuipitisha rasimu ya katiba, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakipigana vijembe na kubishana kwa mambo yanayozidi kuwagawa wenyewe na taifa.

Tofauti kubwa za kimtazamo baina ya wajumbe zinapata nafasi kubwa zaidi. Ni dhahiri kuwa, kama hatua zisipochukuliwa mapema katika kumaliza mabishano ya mara kwa mara, ni wazi kwamba hakutakuwa na mafanikio. Katiba bora haitapatikana na badala yake, taifa litazidi kugawanyika kutokana na misimamo ya vyama.

Kwa bahati mbaya sana, badala ya wajumbe wa Bunge la katiba kujielekeza katika masuala yatakayoleta katiba bora, wengi wao wamekuwa wakionyesha waziwazi kuwa wanapigania zaidi maslahi ya vyama vyao.

Kwa mfano, kila uchao, wajumbe wa Bunge hili wamekuwa wakipeana vijembe baina yao, vingi vikionekana kujawa na mitazamo ya kisiasa. Upo ushahidi wa kutosha vilevile kuwa wajumbe wengi wamekuwa wazuri katika kuibuliana tuhuma.

Wengi miongoni mwa wale wanaopata nafasi ya kuzungumza wamekuwa wakimwaga tuhuma. Kiti pia kinaonekana kuyumba.
Nacho kimeanza kutuhumu. Hiyo ilidhihirika juzi baada ya Mwenyekiti wa Bunge kutoa yake ya moyoni, akisema kuwa wanaoyumbisha mwenendo wa bunge hilo ni baadhi ya watu waliodhamiria kuona kuwa mchakato wa kupitisha rasimu ya katiba mpya unakwama.
Na sasa, hali ya kutuhumiana huko imefika mbali zaidi.Ni baada ya Waziri Mkuu kueleza yake, akisema kuwa kutokana na mwenendo unaoonekana sasa, anafikiria kumuomba Rais aliyeunda Bunge hilo kuliahirisha hadi wakati mwingine ili kutoa fursa kwa masuala mengine ya Kiserikali kuendelea. Waziri Mkuu alikuwa akizungumzia mkutano wa Bunge la Bajeti ambao unapaswa kuanza baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba.

Sisi tunaona kuwa chanzo cha mkanganyiko unaoendelea sasa kwenye Bunge la Katiba ni kimoja tu, nacho ni hali ya kutoaminiana. Wajumbe wamekuwa hawaaminiani. Matokeo yake wanaishia kutuhumiana hata kwa mambo ya wazi na yasiyohitaji kubishana.

Ushauri wetu kwa wajumbe wa Bunge la Katiba ni kuwa, wajitahidi kutanguliza utaifa na wala siyo vyama vyao. Wakumbuke kuwa Watanzania waliwapa fursa ya kwenda kwenye Bunge hilo kwa nia ya kuwaandalia katiba bora na siyo kuimarisha vyama vyao.

Wajumbe wa Bunge la Katiba wakumbuke vilevile kuwa Watanzania wanawaangalia, teknolojia ya matangazo ya moja kwa moja ya televisheni inawaonyesha wote mbele ya umma ambao bila shaka, kuna siku utawahukumu kwa kuonyesdha mapenzi zaidi kwa vyama vyao kuliko taifa. Ni vyema wakaacha kufanya mambo yasiyokubalika.

Tunawasihi wajumbe wa Bunge la Katiba kuwa, mara zote wajitahidi kufanya kazi yao kwa umakini mkubwa ili mwisho wa siku waipatie Tanzania katiba bora. Kinyume chake, itakuwa ni janga kubwa kwa taifa.

Haipendezi hata kidogo kuona mchakato wa katiba ukiharibika baada ya taifa kutumia muda mwingi kuandaa rasimu na pia kupoteza mabilioni ya fedha kugharimia mchakato huo.

Tunawakumbusha wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwa ni vyema kwa kila mmoja kuwa na lengo la kuona kuwa katiba mpya yenye kukidhi matakwa ya Watanzania inapatikana. Na hii ni fursa ya kihistoria inayopaswa kutumiwa vyema kwa manufaa ya taifa.

Shime, Bunge Maalum la Katiba lilete katiba bora. Siyo kuwagwa Watanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

Kikwete: Tuwaache wabunge waamue serikali mbili au tatu


Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete amesema amemaliza  kazi ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba na sasa anawaachia wabunge wa bunge hilo kujadili na kuamua muundo wa Muungano unaofaa kama serikali mbili au tatu kwenye mapendekezo ya  Rasimu ya Katiba Mpya.
Rais Kikwete alielezea msimamo huo juzi wakati akizungumza na wazee  katika Ikulu ndogo ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara yake ya siku moja wilayani hapa, alitoa msimamo wake baada ya wazee hao kumweleza kwenye risala yao kuwa wao wanataka serikali mbili. Risala hiyo ilisomwa na   Mwenyekiti wa Wazee wa Wilaya ya Muheza, Hamisi Mzee.

Rais Kikwete alisema kwa sasa amewaachia wabunge kuamua muundo wa Muungano unaotakiwa na baadaye wananchi wataamua kama wanataka serikali tatu ama mbili wakati wa kupitisha Katiba.

Alisema kama watapendekeza serikali tatu ruksa kwani ndiyo mapendekezo yao, hivyo hayawezi kupingika kwa namna yoyote.

Hata hivyo, Rais Kikwetee alisisitiza kuwa lakini waelewe kuwa serikali tatu zina changamoto zake.
 
CHANZO: NIPASHE

Bunge machafuko

  Ni matumizi ya kura zote, wazi na siri
  Mwigulu achafua hali ya hewa
  Ezekiel Wenje awavuruga Mawaziri,Wajumbe

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuani na haki za Bunge Maalum la Katiba, Pandu ZAmeir Kificho (Kushoto), akiwasilisha mapendekezo ya kamati kuhusu butaratibu wa upigaji kura bungeni mjini Dodoma jana,kulia Mjumbe John Mnyika akichangia pia.(Picha na Khalfan Said)
Kitendawili cha kura ya wazi au ya siri limeemdelea kuliandama Bunge Maalum la Katiba kwa kuzua mvutano mkali jana jioni baada ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge kuwasilisha azimio la kupendekeza utaratibu wa kura ya siri na ya wazi kutumika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba.
Jana jioni yalizuka malumbano baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, kuwasilisha mapendekezo ya azimio la utaratibu wa wajumbe kupiga kura kwa kutumia njia mbili za kura ya wazi na siri kwa kadri kila mjumbe atakavyoona inafaa.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha mapendekezo yake, baadhi ya wajumbe walitoa maoni wengine wakipendekeza kutumika kwa kura ya kielektroniki na wengine wakipinga vikali kwa madai kuwa itakuwa na uchakachuaji.

MAKONDA

Paul Makonda alipendekeza kutumika kwa kura ya kielektroniki ambayo itaokoa muda wa upigaji kura na kila mmoja kufanya kwa uhuru zaidi.

Alisema mvutano uko baina ya wajumbe waliowafuasi wa vyama vya siasa huku 201 wakiwa njiapanda.

PAMELA
Mjumbe Pamela Maasai alisema kura ya elektroniki ni rahisi kuchakachuliwa hivyo siyo vyema Bunge hilo kukubali utaratibu huo na badala yake kura ya siri ambayo itatoa uhuru kwa kila mjumbe kufanya kwa uhuru.

NASSARI
Joshua Nassari aliwataka wajumbe kuacha unafiki na kila mmoja auzungumze kama haifahamu kesho, Katiba iwe neema kwa makundi yote kwa miaka ijayo.

“Bunge moja, taifa moja, katiba moja, nchi moja halafu upigaji kura uwe tofauti, wenzetu wanatengeneza ndege zinaruka bila rubani unasema tumebuni kupiga kura kwa kila kundi kupiga watakavyo…wengi wa wabunge wa CCM wanataka serikali tatu, ila wanashindwa kusema, njia pekee ya kuwasaidia ni kura ya siri,” alisema.

Alisema uchaguzi wa viongozi mbalimbali kura ni ya siri, wajumbe wa Bunge hilo nao wameteuliwa na Rais ambaye alijifungia na kuwateua kwa siri,” alisema na kuongeza kuwa siyo ajabu kwa Bunge hilo kupiga kura ya siri.

OLUOCH
Ezekiel Oluoch alisema kura ya siri ndiyo itasaidia kuiwafanya watu kuwa huru kwa kuwa ndani ya katiba hiyo kuna masuala ya kidini yanayopaswa kuamuliwa kwa usiri.

Alisema kura ya siri inatumika kuamua mambo yenye imani na utata mkubwa kwa kuwa inamsaidia mtu kuwa huru katika kuamua.

LAIZER
Mjumbe Michael Laizer alisema Kamati hiyo imepeleka pendekezo la kutoa suluhisho la utaratibu wa upigaji kura na kama haukubaliki ni wakati wa Mwenyekiti kuwuandikia Rais avunje Bunge ili wajumbe watawanyike na kuondoka Dodoma.

MBOWE

Freeman Mbowe, alisema ni lazima wafike hatua wafanye uamuzi kuliko kuendelea kujadili huku akisema Machi 11, mwaka huu walipitisha kanuni bila kifungu cha 37 na 38 vinavyozungumzia utaratibu wa kura ya wazi na siri.

Alisema utaalamu wa kurushiana maneno na vijembe hausaidii lolote na kwamba ni dhahiri kuwa kwa mazingira ya jana hakuna utaalamu wa kufikia mwafaha kwenye ukumbi kwa kila mmoja kuzungumza kwa kadri utaalamu wake unavyomruhusu.

“Pamoja na utaalamu wetu wa kufanya maamuzi hatuwezi kuliamua suala hili, itakuwa ni aibu tutajikuta kwenye mazingira ya kulazimisha na kuvunja Bunge, hakuna atakayetakoka mshindi si aliyesababisha na ambaye hakusababishiwa,” alisema

Alishauri viongozi wenye busara kukutana na kuzungumza na kuja na uamuzi sahihi kwa kuwa jambo la Katiba ni jambo la maridhiano, hivyo ni lazima kuwe na makubaliano ya kusonga mbele.

MWANGUNGA
Shamsha Mwangunga, alisema wanaotaka kura ya siri ni wanafiki, hawajiamini na wawajui walifanyalo na kwamba ni vyema likafanyika kwa uwazi.

“Tunashindwa kupiga hatua ya mbele kwa kuvutana, hivyo ni vyema kukubali ushauri wa kamati wa kila mmoja kupiga kura anayoona inafaa,” alisema.

RAZA
Mohamed Raza, alisema kura ya wazi ndiyo inayofaa na kwamba kuendelea kulumbana ni kutumia vibaya fedha za Watanzania.

MAKAIDI
Dk. Emmanuel Makaidi alisema kura ya siri itatoa nafasi kwa kila mjumbe kuonyeshana dhamira yake pasipo woga.

“Kura ya elektroniki haifai kuamua, tukubali kura ya siri kama ndiyo msingi wa maamuzi yetu,” alisema.

LEMA
Godbless Lema alisema kura ya siri itawaingiza baadhi ya wajumbe kwenye matatizo kwa kuwa kwa sasa kuna matamko mbalimbali yamesambaa kwenye mitanda ya jamii, vitisho vingi, ikiwamo Zanzibar inasema atakayerudi bila Zanzibar huru kichwa chake kitakuwa halali yao.

Alisema Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya wabunge wa CCM akiamua kupiga kura ya siria haamini kama yupo anayeweza kwenda kinyume cha kiongozi wake ambaye amepinga kura ya wazi.

BULAYA
Esther Bulaya alisema msimamo wake ni kura ya siri, lakini amefurahia mapendekezo ya kamati ya kila mmoja kupiga kura kwa nutaratibu anaupenda, hivyo ni vyema wajumbe hao wakakubaliana na kamati.

MWIGULU
Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu Freeman Mbowe na Ismail Jussa Ladhu kuwa wanataka kura ya siri kwa kuwa wanalengo la kuingiza ushoga.

Baada ya kauli ya Nchemba, Profesa Ibrahim Lipumba aliomba mwongozo wa Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan, akisema Bunge linaangaliwa na watu wa rika tofauti wakiwamo watoto na kwamba Nchemba ametumia lugha isiyo na staha.

Samia alimtaka Nchemba kufuta kauli yake na kuwaomba radhi Mbowe na Jussa, lakini aliendelea kutetea hoja yake akidai kuwa baadhi ya vyama (bila kuvitaja) vinafadhiliwa na nchi zinazokubali ushoga na kwamba ataondoa majina ya Mbowe na Jussa, lakini neno ushoga litabaki pale pale.

Kufuatia kauli za Nchemba, wajumbe waliendelea kupiga kelele na kutaka afute kauli na kuomba radhi, huku Samia akitumia dakika kadhaa kuwatuliza wajumbe na kumtaka Nchemba kufuta kauli na kuomba radhi.

Hata hivyo, baadaye Nchemba alifuta kauli hiyo na kuwaomba radhi Mbowe na Jussa.

MAPENDEKEZO YA KIFICHO

Akiwasilisha Azimio la kufanya marekebisho ya Kanuni za Bunge la Maalum jana, Kificho alisema kuwa marekebisho yanayofanywa ni kanuni za Bunge Maalumu kwenye kanuni ya 37 kwa kuongeza mwishoni mwa fasiri ya (3) maneno “ya siri kwa mjumbe anayetaka kupiga kura ya siri au kura ya wazi kwa mjumbe anayetaka kupiga kura ya wazi kwa kuzingatia utaratibu ulioanishwa katika kanuni ya 38.

WENJE AWASHA MOTO
Kauli ya Ezekiel Wenje kuwa baadhi ya mawaziri wamewahonga baadhi ya wabunge wa makundi ya wabunge 201 ilisababisha vurugu kubwa kwa mawaziri tajwa kutaka waombwe radhi, akiwamo, Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).

Mbali na mawaziri hao pia wajumbe kutoka kundi hilo walitaka kuombwa radhi.

Awali Makamu Mwenyekiti aliyekuwa anaongoza kikao, Samia Suluhu Hassan,  alimtaka Wenje kuomba radhi, lakini alisema mawaziri hao wamethibitisha wenyewe kuwaalika watu hao na kuongeza orodha ya mawaziri kuwa ni pamoja na Gaudensia Kabaka (Kazi na Ajira) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba walihusika kuwakirimu wajumbe hao na kuwapa msimamo wa serikali mbili.

Wakati vurugu za kelele na kurushiana maneno zikielendelea, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta, alirejea kwenye kiti chake na kumtaka Wenje amjibu kama kweli haoni kuwa kauli yake imewaudhi wajumbe wengine.

Wenje alisema kuwa inawezekana kuwa kuna watu wameudhika, lakini kwa kuwa alichosema ni ukweli na kwa kuwa anaomba radhi tu, lakini ukweli anausimamia.

Kwa kauli hiyo, Sitta alisema kwa kuwa Wenje amekataa kuomba radhi, basi suala hilo ameamua kulipeleka kwenye kamati ya Kanuni na Haki za Bunge la Bunge Maalum.

Baada ya uamuzi wa Sitta wajumbe walishangilia na Wenje alionekana alishangilia uamuzi huo.
 
CHANZO: NIPASHE

Saturday, March 22, 2014

Kikwete ‘avuruga’ mjadala


Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Michael Jamson 

Rais Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete alisema  suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.
Huku akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa  za kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar.  Sababu ya pili muundo huo unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”
Aliongeza, “Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo yangu.” Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu wanasema Watanzania waliotoa  maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”
Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.
“Watu wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7” alisema. Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
“Watu wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.”

Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kutafuta majibu mwafaka kuhusu changamoto za muundo wa Serikali tatu kwa sababu maelezo ya tume kuhusu muundo huo hayana majibu.
Aliongeza, “Kupanga ni kuchagua. Wanaounga mkono Serikali mbili wanasema mlolongo wa changamoto ulioanishwa na tume kuhusu Serikali tatu hautapunguza matatizo bali utayaongeza kuliko ilivyo sasa na wanasema changamoto hizo zinatatulika bila kuwepo Serikali ya tatu.”
Alisema kama mfumo wa Serikali tatu ukipita ni lazima Serikali ya tatu ijengewe msingi imara kwa sababu haitakuwa na chanzo cha uhakika cha mapato yake yatakayoiwezesha kusimama yenyewe na haitakuwa na chombo cha kukusanya mapato zaidi ya kutegemea kukusanyiwa mapato na nchi washirika.
“Kama tunataka Serikali ya tatu lazima tuitengenezee misingi ya uhakika. Hivi nani atakudhamini kwa virungu, pingu, magari ya kuwasha, majeshi au bunduki. Serikali hii ya tatu haidhaminiki wala kukopesheka,” alisema huku akitolea mfano jinsi mataifa kama Urusi yalivyoanguka baada ya kujitenga.
Huku akifafanua jinsi kero za muungano zilivyotatuliwa na kamati na tume mbalimbali mpaka kubaki kero sita, Rais Kikwete alisema Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zimeamua kutumia mchakato wa Katiba  kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana kulikuwa na mambo 11 ya muungano, baadaye kuongezeka hadi mambo 22 na kusisitiza kuwa mambo mengi yaliibuka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Alisema jambo ambalo  Serikali hizo mbili walikubaliana kuliondoa katika mambo ya Muungano ni suala la gesi asilia na mafuta.
Ammwagia sifa Warioba
Alisema Jaji Warioba wa wajumbe wenzake wa Tume ya Katiba wameandika Rasimu ya Katiba vizuri na kwa weledi wa hali ya juu, na kwamba wametoa maoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba tuliyonayo sasa.
“Katiba inayopendekezwa imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tuliokuwa nao na kuweka misingi mizuri kwa huko mbele tuendako,” alisema.
Alisema Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi kina kurasa 106, sura 17, hivyo wajumbe wa Bunge la Katiba wanapaswa kusoma kila kitu na kuelewa na kuamua kwa utashi wao.
“Uamuzi wako siyo uamuzi wa kuambiwa na mwenzako, unaulizwa na wenzako kwenye hilo tusemeje unasema na mimi nimeambiwa, ebo! Umeambiwa, umefundishwa na mimi nasema akili za kuambiwa…” alisema Rais Kikwete.

Mambo mengine
Pia Rais Kikwete aligusia suala la mbunge kupoteza ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi kwa miezi sita mfululizo, kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.

Alisema anaungana na wote wanasema jambo hilo liangaliwe vizuri na kwamba anashauri kama akiwa kizuizi amepatikana na makosa apelekwe mahakamani.

“Kwa mazoea ya duania ukomo unawekwa kwa wakuu wa nchi, hawaweki ukomo kwa wabunge, Tanzania wanataka kuwa wa kwanza,” alisema Kikwete.

Kuhusu suala la ugonjwa alisema mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wake, hivyo siyo sahihi kumwekea mgonjwa muda maalumu wa kuugua kwake.
Huku akicheka, Rais Kikwete alisema kitendo hicho kitawafanya wabunge kuanza kutembea na dripu katika majimbo yao kabla hawajapona vizuri.

source: Mwananchi