WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, June 3, 2013

WanaCCM Zanzibar wamshukia Maalim



Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad 


Msuguano huo unatokea katika kipindi ambacho nchi iko katika mchakato wa kupata Katiba na rasimu yake.
Zanzibar. Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Zanzibar imemshutumu Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kumchonganisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na viongozi wastaafu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alisema kauli za Seif zinaweza kusababisha mitafaruku isiyokuwa ya lazima.
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alikaririwa jana Jumapili akieleza kuwa marais wa zamani, Dk Aman Karume na Dk Salmin Amour walikuwa wanaunga mkono haja ya Zanzibar kuwa na mamlaka ya doka kamili ndani ya Muungano.
Akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Kamati ya Maridhiano huko Zanzibar juzi, Maalim Seif alikwenda mbali zaidi na kumsifia Dk Karume kuwa alikuwa Rais bora wa Zanzibar.
Hata hivyo, kitendo cha Maalim Seif kumsifia Karume ni cha kushangaza kwani aliwahi kutomtambua baada ya kushindwa na Rais huyo wa zamani kwenye chaguzi za urais za miaka ya 2000 na 2005.
Vuai alisema jambo hilo linakwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya Zanzibar na linaonyesha dharau kwa Serikali iliyokuwa madarakani.
“CCM kinalaani kwa nguvu zote kauli za uchochezi, kejeli, fitna na dharau zilizotolewa na Katibu Mkuu huyo wa CUF dhidi ya Dk Shein.
“Maalim Seif ametoa kauli zinazoweza kuleta mtafaruku wa maelewano kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alionya Vuai.
Vuai pia ameipinga Kamati ya Maridhiano, ambayo ilihusika kuandaa maandamano huko Zanzibar juzi. Alistaajabu kuwepo kwa kamati hiyo yenye wajumbe sawa kutoka vyama vya CCM na CUF.
“Chama cha CCM hakijawahi kufanya kikao cha pamoja kwa kukubaliana kuunda kamati kama hiyo ya maridhiano wala hakuna kikao chochote cha CCM cha kikatiba kilichowahi kujadili na kuwateua baadhi ya wanachama wake kuwa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano,” alisema Vuai.
Vuai alishauri wananchi wa Zanzibar kutumia fursa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kutoa ushauri kuhusu Katiba Mpya.
“Kama kuna mtu ana mawazo yake kuhusu katiba basi aheshimu mchakato wa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya,” aliongeza Vuai.
Malumbano haya ya CCM na CUF yanaashiria mpasuko wa ndoa ya vyama hivyo vinavyounda Serikali ya Umoja wa Taifa huko Zanzibar.

source: mwananchi

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AZINDUA RASIMU YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KARIMJEE DAR LEO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiinua juu na kunyesha Kitabu cha Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa rasimu hiyo uliofanyika leo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, (kushoto) ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Joseph Sinde Warioba.
Meza kuu ikiwa na baadhi ya Viongozi wakuu wa Serikali na Jukwaa la Tume ya Katiba mpya.

 Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe (kulia) akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake katika hafla ya uzinduzi wa rasimu ya Katiba hiyo.

 Baadhi ya wazee waasisi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo leo.

  Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa bize kunakili kila kinachozungumza mahala hapo.


 Sehemu ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, waliohudhuria hafla hiyo, wakiwajibika.Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
 
source:haki ngowi

Mwili marehemu Albert Mangwear kuwasili Kesho Jijini Dar es Salaam

Wadau wa Sauzi wakiwa katika harakati za kuusafirisha mwili wa msanii wa kizazi kipya aliyefariki majuzi marehemu  Albert  Mangwear jioni hii huko  Johannesburg, Afrika Kusini. Ratiba zinaonesha mwili huo utawasili kesho jijini Dar es salaam. Muda na ratiba kamili zitafuata punde.
 
source:haki Ngowi

Sunday, June 2, 2013

Maalim Seif, Karume waungana kupinga mfumo wa Muungano


Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza kushirikiana na Rais mstaafu wa Awamu ya Sita Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka yake kamili.

Tamko hilo amelitoa wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliokuwa umebeba agenda ya kujadili mabadiliko ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika kwenye uwanja wa Kibandamaiti na kuhudhuriwa na wanachama wa CUF toka mikoa mitatu ya Unguja.

Maalim Seif alisema mbali na Dk Karume kazi hiyo pia itaendelea kufanywa na kamati ya maridhiano inayoongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hassan Nassor Moyo na Makamu wake Abubakari Khamis Bakari wakiwemo wajumbe wanne.

Wajumbe hao ni pamoja na mjasiriamali Eddy Riyami, mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu, Aliyekuwa Waziri wa SMZ Mansour YusuF Himid, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF Salum Bimani.

Maalim Seif aliwaeleza wanachi kuwa Dk Karume na Kamati hiyo hawatarudi nyuma hadi pale Taifa la Zanzibar litakapopata uwakiklishi katika Umoja wa Mataifa na kuwa dola yenye mamlaka kamili kama lilivyokuwa kabla ya Aprili 26,1964.

“Madai haya si ya Seif, Karume, Jussa, Moyo au Eddy, ni sauti ya Wazanzibari wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, kwanini tusiwe na mamlaka yetu kamili, kudai haki ni wajibu uliohimizwa na Mungu hivyo hatutakatishwa tamaa,”alisema Maalim Seif.

Alisema kwa upande wake yuko imara katika kuitetea nchi yake na kwamba dola ya Zanzibar ni kongwe kuliko Tanganyika, Malawi, Kongo, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi iliokuwa na mabalozi wake katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Alisema kabla ya kukatwa kwa mipaka na wakoloni mwaka 1884/1885 huko Berlin, Zanzibar ilikuwa ni Taifa kamili lakini baada ya kukatwa kwa mipaka hiyo ikabakishiwa visiwa vya Pemba na Unguja pamoja na maili kumi katika masafa ya usawa wa mwambao wa Pwani.

“Nitaendelea kushirikiana na Dk Karume, Wazanzibari na kamati ya maridhiano hadi pale mamlaka kamili yatakapopatikana, mimi ndiye Maalim Seif, nishazoea kufungwa, kutukanwa, kunyanyaswa hivyo hakuna ninalolihofia katika kuipigania Zanzibar,”alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Akiizungumzia Tume ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba alisema ni muhimu kwa rasimu ijayo ya katiba mpya mambo kadhaa aliyoyataja yakazingatiwa ili kuipa haki Zanzibar ya kuwa na madaraka yake kamili ambayo yataisaidia kujijenga kiuchumi na kimataifa.

Akionekana kutia shaka ya wananchi wengi kutopewa vitambulisho vya ukaazi na kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, alimtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwa mkweli na kutimiza ahadi yake ya kumpa kila Mzanzibari kupata haki yake.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Mwelekeo wa Tanzania mpya kujulikana leo



Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Picha ya Maktaba 
 
Na Boniface Meena na Aidan Mhando,

Dar es Salaam. Mwelekeo wa Taifa la Tanzania utaanza kujulikana leo mchana Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapozindua rasimu ya Katiba Mpya kwenye tukio la kihistoria litakalofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama rasimu hiyo itakuja na majibu ya maswali magumu, makubwa ya muundo wa Muungano, madaraka ya Rais, uteuzi wa mawaziri kutokana na wabunge, muundo wa wakuu wa mikoa/wilaya na muundo wa mihimili mingine miwili ya dola; Mahakama na Bunge.

Uzinduzi wa rasimu hiyo unafanyika baada ya Tume hiyo kufanyia kazi ya uchambuzi wa maoni ya wananchi. Maoni hayo yalitolewa na wananchi wapatao 1,015,564 kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na waliohudhuria mikutano ya moja kwa moja, waliotuma ujumbe mfupi wa simu (sms), barua pepe na kutumia mitandao ya kijamii.

Idadi ya makundi yaliyotoa maoni ni 170 zikiwamo asasi 22 za dini, kiraia 72, taasisi za Serikali 71, vyama vya siasa 19, viongozi na watu mashuhuri 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Rasimu hiyo ndiyo itakayopelekwa kwenye Mabaraza ya Katiba na itajadiliwa miezi mitatu ili kuona kama mapendekezo ya Tume hiyo baada ya kuchambua maoni hayo ya wananchi yanafaa au yanahitaji marekebisho.

Huo ni mwendelezo wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulioanza mwaka jana baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanza kukusanya maoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid uzinduzi huo utaonyeshwa moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) kuanzia saa nane mchana.

Taarifa hiyo iliwaomba wananchi kufuatilia uzinduzi huo kwa umakini ili waweze kujua kinachoendelea. Kuzinduliwa kwa rasimu hiyo kutaanzisha upya mjadala wa Katiba ambayo inatungwa kwa mara ya sita.

Katiba iliwahi kutengenezwa mwaka 1961 wakati Tanganyika ilipopata Uhuru, mwaka 1962 baada ya nchi kuwa Jamhuri, mwaka 1964 ilipoundwa Katiba ya Muda baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na mwaka 1965 ilitungwa Katika Mpya iliyodumu hadi mwaka 1977 baada ya vyama vya Tanu na ASP kuungana na kuifanya nchi kuwa chini ya utawala wa chama kimoja cha siasa.

Kwa upande wa Zanzibar kumekuwapo Katiba Tatu. Kwanza ni ile ya Uhuru iliyotungwa mwaka 1963, Mwaka 1979 ikatungwa Katiba nyingine na ya mwisho ni ile ya mwaka 1984.
Muundo wa Muungano

Kwa muda mrefu, suala la muundo wa Serikali mbili katika Muungano limekuwa mwiba katika siasa za Tanzania Bara na Zanzibar.

Wakati wa kutoa maoni yao, wananchi na wadau wengi wametofautiana kuhusu ni aina gani ya Muungano unaokidhi mahitaji ya sasa ya Watanzania. Kundi ambalo limeonekana kuwa kubwa likitaka Muungano wa Serikali Tatu ikiwa na maana ya Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, kuna kundi lingine ambalo linapendelea muundo uliopo sasa wa Serikali mbili, ya Muungano na SMZ uendelee na lingine linataka Serikali moja. Rasimu itakayotolewa leo inatarajiwa kutoa mwelekeo wa muundo huo.

Mwaka 1984, suala la muundo wa Muungano liliwahi kumlazimu aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais, Aboud Jumbe kujiuzulu kwa kile kilichoitwa kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa huko Zanzibar.
Pia mwaka 1993, Muungano huo ulitikiswa baada ya kuibuka kwa kundi la Wabunge wa CCM lililokuwa linaitwa G-55 waliotaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano lakini hoja yao ilizimwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Pia suala la mgawanyo wa rasilimali nalo limekuwa likisababisha matatizo makubwa katika Muungano.
Madaraka ya Rais

Mbali na suala la Muungano ambalo lilikuwa ni moto katika maoni hayo, suala la madaraka ya Rais nalo ni eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa ambalo rasimu inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu madaraka hayo hasa katika uteuzi wa mawaziri na idadi ya wizara kama ilivyo katika Katiba ya Kenya ya sasa.
Mawaziri kutokana na wabunge

Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba wametaka mfumo wa sasa wa uteuzi wa mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge ubadilishwe. Wanataka wateuliwe kwa kuzingatia sifa na weledi badala ya utashi wa kisiasa.

Mmoja wa watu maarufu waliowahi kutoa maoni wakitaka mawaziri wasitokane na wabunge ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Bunge na Mahakama

Spika wa Bunge, Anne Makinda alipotoa maoni yake alipendekeza kwenye tume hiyo kwamba kuwe na mabunge mawili; la seneti na la kawaida.
Hoja hii nayo imekuwa ikizungumzwa na wadau mbalimbali hasa wakihoji chombo kinachodhibiti Bunge kwa sasa.

Pia wadau wengi hasa wanasheria wanaona kwamba mfumo wa sasa wa uteuzi, hasa wa majaji una kasoro na kwamba mhimili huo wa Dola uachwe ujiendeshe na kuteua viongozi wake kama ilivyo Bunge.
Nafasi za wakuu wa mikoa/wilaya
 
Moja ya hoja ambayo imejadiliwa pia katika mchakato huo wa Katiba Mpya ni nafasi ya wakuu wa mikoa na wilaya. Baadhi ya wananchi wanataka vyeo hivyo vya kisiasa viondolewe na madala yake wawepo magavana ambao watachaguliwa na wananchi katika mikoa husika.

source: mwananchi

Tumetoka Mbali; Je, Unaijua Historia Ya Daladala?

4 e8c83

Ndugu zangu,
Jana nikiwa viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa niliweza pia kuongea na baadhi ya wasomi wa Chuo hicho wakati tukiangalia mpira.

Mmoja wao alikuwa Mwalimu Mgaya aliyeniambia kuwa anakwenda kuwa mwalimu wa historia.Hapo tukaingia kwenye mada ya Daladala. Nikamwuliza kama anaijua historia ya Daladala. Hapana, hajawahi kuisoma au kusikia mahali popote. Kwake yeye Daladala ni Daladala.

Basi, akashangaa sana nilipomsimulia, kuwa asili ya Daladala ni jina tulilolitohoa kutoka sarafu ya Marekani, yaani, Dola. Nakumbuka kwenye miaka ya 80 mwanzoni , na katikati ya shida kubwa ya usafiri Dar, nauli za usafiri wa vibasi vidogo vidogo ikaongezeka na kufikia shilingi tano kwa safari. Ndipo hapo tuliweza kumsikia konda akiita; " Kariakoo Dala ..dala..dala... dala!"

Maana, shilingi tano yetu iliyokuwa nzito kidogo hata kuishika na yenye pembe sita ilikuwa na thamani sawa na dola moja ya Marekani. Ndipo hapo, shilingi tano yetu ikabatizwa jina la ' Dala'.
Jana jioni niliongea kwa simu na ndugu yangu  Mrisho Mpoto, nikamwuuzia wazo, kuwa siku moja tukutane tulijenge wazo la kuwa na kitu kwa jamii  kitakachotufanya tuzungumzie tulikotoka kwa nia njema ya kukumbushana historia yetu. Jambo hilo lingeenda sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Usafiri wa Mabasi yaendayo kwa Kasi jijini Dar.

Maana, kuna mengi ya kutafakari kuhusiana na uchumi na jamii yetu. Tujiulize; wakati wasafiri wa daladala enzi hizo walikuwa ni watu wa kipato cha chini na hata cha kati, je , wasafiri wa daladala wa leo ni watu wa aina gani?Je, anayepanda daladala leo anatazamwa vipi; ni mtu asiye na uwezo kifedha au anaweza kuwa ni mtu  anayeona kuliacha gari lake nyumbani na kupanda dala dala amefanya mawili; amebana matumizi na kuelekeza fedha zake kwingine na hata kutunza mazingira. Maana, magari mengi mijini yanachafua mazingira.Je, ni kwa nini uchumi wetu wakati huo ulikuwa na nguvu kutuwezesha kubatiza sarafu zetu kwa fedha za kigeni kama dala kwa shilingi tano. Wengine waliita gwala.

Tuliweza pia kuibatiza noti ya shilingi 20 kwa kuiita ' Paundi' ikiwa na maana, thamani ya paundi moja ya Uingereza wakati huo ilikuwa ni sawa na shilingi 20 za Tanzania.  Ni kwenye miaka ya 80.Je, rasilimali zetu ikiwamo gesi na mafuta vinaweza kuturudisha kwenda kuwa ' Taifa Kubwa' kama tulivyokuwa wakati fulani. Maana, nakumbuka nikiwa mdogo nilisikia redioni  taarifa ya habari ikisema kuwa  ' Tanzania imetoa msaada wa magunia ( Sikumbuki idadi) ya kunde na maharage kwa nchi ya India kutokana na mafuriko yaliyowakumba. Nilisikia pia Tanzania ikitoa msaada wa chakula kwa nchi ya Msumbiji na kwingineko zilizokumbwa na maafa.

Je, tunaweza kurudia kuwa ' Taifa Kubwa' kiuchumi kama tutaendelea kuruhusu karibu kila nchi kubwa kiuchumi kuwa na benki zao hapa kwetu? Maana siku hizi hapa kwetu kuna benki za Wahindi mpaka Wapakistani! Je, na sisi tuna mabenki kwao?

Na tafsiri ya benki hizo si ina maana  pia kuwa nchi hizo zimeamua kujenga ' Vihenge' vyao kwetu kuhifadhia wanavyovuna hapa kwetu na kusafirisha kwenda kula kwao.

Na tuendelee kujadili daladala na uchumi wetu...!
Picha hiyo juu niliilipiga mwaka 1988 pale Posta ya Zamani. Huo ulikuwa ni usafiri tulioutumia ennzi hizo, maarufu kama ' Chai- Maharage'. Ni moja ya picha zangu za zamani sana zilizo kwenye Maktaba yangu.
Maggid,
Iringa.
0754 678 252

Saturday, June 1, 2013

Wabunge DRC wampongeza JK

Na VOA
Kufuatia wito wa rais Jakaya Kikwete kwa marais wa mataifa ya maziwa Makuu marais Paul Kagame, wa Rwanda, Joseph Kabila wa jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Yoweri Museveni wa Uganda, kuzungumza na makundi ya waasi yanayopambana na nchi zao, wabunge wa Kongo Kwenye taarifa yao ya pamoja iliyosomwa na mbunge Benjamin Mukulungu , wabunge hao wa Kivu Kusini na Kaskazini wameomba kuwe na mtazamo wa jumla wa viongozi wa kanda ya maziwa makuu na umoja wa mataifa ili kumaliza vita nchini Congo.

Wabunge wa Kivu wamepongeza msimamo wa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wa kutaka kuwe na mazungumzo kati ya serikali za Congo Rwanda na Uganda na makundi ya waasi wanayopingana nayo.

Wabunge wa Kivu wametaka pendekezo la Rais Kikwete ni lazima lipewe kipaumbele na jumuiya ya kimataifa ili kuwe na amani ya kudumu kwenye eneo hilo.

Mbunge wa upinzani Emerio Kunji kutoka jimbo la Kasai amesema amepanga kutoa hoja rasmi bungeni ili kuweko na azimio la bunge kuhusu msimamo ambao serikali ya Congo inatakiwa kuchukua kwa ajili ya kutatua mzozo wa Kivu.

Akisema “Rais wa Tanzania alichukua msimamo wa kijasiri wa kuonyesha kwamba mzozo wa maziwa makuu hauwezi kutambuliwa kwa njia ya kinafiki bali kupitia mtizamo ulio thabiti. Bunge letu ni lazima litoe shinikizo kwa serikali ili kuweko na mtizamo mpya wa ufumbuzi wa mzozo huo”.

Kwa muda wa siku tano sasa pendekeo hilo la rais Kikwete limeendelea kuzusha maoni mengi kwenye vyombo vya habari ngazi ya kisiasa, na kwa watu wa kawaida huko mjini Kinshasa