MCHANGO WA WAPINZANI
KATIKA MAENDELEO YA TAIFA;
BADO TUNAHITAJI MCHANGO WA
UPINZANI KATIKA KUBORESHA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA NA WA HAKI TUKIZINGATIA
KUWA:
- “Siasa si mchezo mchafu, ila wachezaji wake ndiyo wachafu.”
- Litakuwa ni jambo la kuheshimiwa ka viongozi wetu wetu watakuwa wakweli na wenye Uzalendo wa kweli ndani ya mioyo kwa faida ya wananchi wao.
- Confucius aliwahi sema kuwa ‘Utajiri na vyeo ndivyo vitu ambavyo kila bianadamu anavitamani; lakini ikiwa njia ya kuvipata ni kwa kwenda kinyume na misingi yake, anapaswa ajiepushe navyo.’
- Rudolph Giuliani aliwahi sema kuwa ‘Kiongozi huchaguliwa kwa kuwa yeyote anayemuweka pale huwa anaamini maamuzi, tabia na uwezo wa maarifa yake – siyo ujuzi wa kufuata maoni. Ni wajibu wa kiongozi kuchukua hatua kufuatana na sifa hizo.’
- “kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu za kuwafurahisha viongozi wengine”
Demokrasia kama falsafa ya
Plato ambayo inahusiana na uendeshaji wa shughuli za kisiasa inalenga zaidi
katika utumishi kwa umma na uendeshaji
wa jamii na taifa. Wananchi wote hawawezi ongoza nchi kwa mara moja; Katika
msingi huu wananchi kutokana na wingi wao waliridhika itakuwa sio rahisi kwa
wao wote kukutana, kufanya maamuzi na kuyasimamia moja kwa moja maamuzi hayo
yanayowahusu wao kama jamii; dhana ya kuwachagua viongozi wachache huzaliwa kwa
chimbuko hili na kuruhusiwa kuunda serikali.
Tatizo kubwa tulilonalo
kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio
katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Kwani inatupasa kutambua
kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu. Lakini ridhaa hiyo
haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana, kwamba waongozi watatekeleza
dhamana na wajibu wao kwa makubaliano na maelewano ya kufuata
barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na maadili fulani yanayoitambulisha
na kuiongoza jamii husika.
Hapa ndipo chimbuko la
demokrasia linapochimbuka na dhana ya Upinzani kwa masilahi ya wananchi
linapoanzia. Lengo la vyama nya upinzani ni kuleta ushindani wa kisiasa dhidi
ya chama kinachotawala katika nchi husika. Upinzani unasimama kama mbaadala wa
wananchi katika kukosoa shughuli za serikali ambazo huzitenda kinyume na utaratibu
ambao unafaida kwa taifa husika.
Pamoja na hamu kubwa ya
upinzani kushika hatamu lakini husaidia kuleta uwajibikaji na uadilifu kwa
viongozi ambao wameshika hatamu ya uongozi. ikumbukwe kuwa kiongozi muadilifu
hakubali kufuata au kutoa maamuzi bila
kufanya ukadirifu wa hoja na hali husika. Uongozi ni kujitolea na kuweka
matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na
kujinufaisha.
Marehemu John Kennedy rais
wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa. Tuchague viongozi si kwa
kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na
kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi. Hii ndio
dhana ya upinzani inapoingia kwani hutupa sisi wananchi nafasi zaidi ya kupima
uwezo wa viongozi kupitia vyama vyao nani unafaa kuongoza nchi kwa kipindi Fulani
kulingana na mahitaji ya Taifa.
Tukumbuke kuwa, Serikali ni watu, inaundwa na
watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya
kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa
kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa
matakwa na utashi wa Wananchi wake.
Upinzani tunahitaji ni ule
ambao unatija kwa taifa, kwani taifa letu linahitaji utulivu, amani na upendo
miongoni mwa wananchi wake na kudumisha umoja wa kitaifa kupitia viongozi wake;
kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli
katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa
kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye
magomvi na huhasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na
haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya
maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi
wala upinzani wa kweli ambao haujejaa uroho wa madaraka kwa nia binafsi.
Uadilifu wa uongozi unadai
kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi
inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa
kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na
utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara
misingi ya kidemokrasia.
Bado binadamu si mkamilifu
na kwa vyovyote vile hufikia mahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama
yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati
maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa
kuyakubali na kuliomba radhi Taifa. Hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha
uadilifu wa uongozi katika siasa. Kukubali kubeba dhamana kwa madhara
yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako.
Maamuzi ya kiongozi wa
kisiasa huathiri taifa zima, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na
tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya
muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila
hatua anayochukua. Kama viongozi wetu wa bunge wakikiri kuwa walikurupuka
katika kufanya maamuzi hayo bila kuyafanyia kazi vizuri heshima na uwajibikaji
wa kuliendesha bunge letu itarudi. Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni
kukubali kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja.
Kama taifa bado tunahitaji
upinzani katika uendeshaji wa taifa letu ili kuweza kuikumbusha na kuibana
serikali pale ambapo hukiuka utekelezaji wa majukumu yake ya maendeleo kwa
wananchi wake; na pale inapokiuka utaratibu wa demokrasia na kukiuka haki za
binadamu na matumizi mabaya ya selikali.
Mungu ibarika Tanzania na
watu wake.
AMEN
No comments:
Post a Comment