Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza vikao vyake nyeti wiki hii mjini Dodoma vitakavyochambua, kujadili na mwishowe kumteua mgombea wake atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Vikao hivyo ambavyo vilitarajiwa kuanza jana kwa kuhusisha Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Taifa (CC) vinatarajiwa kuhitimishwa Jumapili wakati umma wa Watanzania utakapotangaziwa rasmi jina la mshindi wa kinyang'anyiro hicho cha uteuzi ndani ya CCM, ambaye hatimaye atakuwa kinara wa kuinadi sera ya chama hicho katika kampeni zinazotarajiwa kuwa kali dhidi ya vyama vya upinzani, vikiwamo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Taarifa zilizoripotiwa jana kuhusiana na vikao hivyo zilionyesha kuwa leo kutakuwa na kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili na baada ya hapo, utaendelea mfululizo wa vikao vingine vikiwamo vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kitakachoteua majina matatu kutoka matano miongoni mwa wale watakaoteuliwa kutoka katika orodha ya makada 38 waliorejesha fomu kuwania kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais na pia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wenye wajumbe 2,400, ambao nao utapiga kura na kumtoa mshindi atakayejulikana Jumapili kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu Oktoba.
Sisi tunaitakia kheri CCM katika kila hatua ya vikao vyake hivi muhimu kwa mustakabali wa chama hicho na taifa.
Tunaamini kuwa mafanikio katika mfululizo wa vikao hivyo ndiyo yatakayoendelea kuihakikishia nchi amani na utulivu.
Kwa sababu hiyo, ni wajibu wa wajumbe wote wa vikao vya CCM kutumia busara na hekima katika maamuzi yao, huku wapambe wa wagombea wanaochuana kuteuliwa kuzingatia kwa vitendo ile kauli ya wahenga isemayo 'asiyekubali kushindwa si mshindani'.
Tunasisitiza hili la kuwapo kwa mafanikio ya kila kilichopangwa katika mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kutokana na ukweli kuwa kasoro zozote zitakazojitokeza kupitia mchakato huu zinaweza pia kuathiri taifa zima. Zitawagusa wafuasi wa CCM yenyewe, wa upinzani na hata wananchi wasiokuwa wafuasi wa chama chochote cha siasa.
Siyo nia yetu kutaka kujadili undani wa mchakato unaoendelea katika kumpata mgombea wa nafasi ya urais ndani ya CCM, ambaye mwishowe atakuwa mwenyekiti wa chama hicho na pia kuwania kuwa rais wa awamu ya tano nchini.
Bali tunaamini kwamba kuna kila sababu ya kuombea mafanikio mema ya CCM katika mchakato huu kutokana na ukweli kuwa chama hiki ndicho kinachotawala. Kimekuwa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru wa taifa hili mwaka 1961, lakini wakati huo kikiitwa TANU kabla baadaye kuungana na ASP na kuzaliwa CCM mwaka 1977.
Kina mizizi mirefu na hivyo, ni wazi kwamba athari zozote hasi zitakazotokana na kasoro zozote kubwa za mchakato wa uteuzi wa mgombea urais zitawagusa wengi.
Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo nasi tunapolazimika kuwaombea kheri na fanaka wana CCM katika vikao vyao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Kadhalika, NIPASHE tunaamini kuwa demokrasia itatwaa nafasi kwenye mchakato wa chama hicho. Wagombea wote watapata fursa sawa na mwishowe kutangazwa mshindi kwa kuzingatia kanuni na taratibu walizojiwekea. Kamwe mizengwe haitakuwa na nafasi katika mchakato wao na mwisho wa siku, atapatikana mgombea atakayetokana na uungwaji mkono na wengi miongoni mwao.
Ni imani yetu vilevile kuwa wapambe wa wagombea wote hawatakuwa chanzo cha kuhasimiana miongoni mwao na kuhatarisha amani na utulivu katika kipindi chote cha mchakato wa uteuzi mjini Dodoma na hata nje ya mji huo wenye makao makuu ya chama chao.
Aidha, ni vizuri pia kwa wageni wote wanaofika Dodoma kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa minajili ya kuhudhuria vikao vya CCM kuchukua tahadhari za kiusalama kwani ni busara kuzingatia jambo hilo kila palipo na mkusanyiko wa watu wengi kama ilivyo sasa.
Wakumbuke vilevile rai ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, aliyeonya tangu juzi kuwa kamwe hawatavumilia kuona vitendo vya uvunjifu wa amani vikifanywa na makundi ya wapambe wa watangaza nia ya urais. Hili ni muhimu kuzingatiwa kwani haitapendeza kuona watu wasio na hatia wakiathiriwa kwa namna yoyote ile kutokana na visa vya kisiasa katika kipindi hiki muhimu kwa CCM na taifa kwa ujumla.
Kila la kheri vikao vya uteuzi wa mgombea urais CCM.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment