Na Mwinyi Sadallah
Zanzibar.Kamati Kuu ya Halmashauri ya CCM Zanzibar imempendekeza Dk Ali Mohamed Shein kwa kauli moja kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar baada ya kuchukua fomu na kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo kupitia chama hicho, Zanzibar.
Kabla ya wajumbe wa kamati maalumu kuanza kujadili ajenda ya mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar jana, walimchagua kwa kauli moja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal kuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kikao hicho kilipokea na kujadili jina la Dk Shein baada ya kujitokeza kwa mara ya pili akiiomba CCM imchague kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar.
“Kikao cha Kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kwa kauli moja imempendekeza kwa Kamati Kuu ili ateuliwe kugombea tena kiti cha urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisema Vuai.
Alisema hatua inayofuata baada ya kupendekezwa, jina lake litawasilishwa na kujadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kabla ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Wakizungumza baada ya kikao, Wajumbe wa NEC akiwamo Dk Maua Daftari alisema DK Shein ameonyesha uadilifu katika kipindi cha uongozi wake pamoja na kufanikiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Alisema DK Shein amekuwa karibu na watendaji wakuu wa Serikali kwa kufanya vikao vya tathimini kila baada ya miezi mitatu ili kuangalia mafanikio na matatizo, utaratibu ambao umesaidia kuwapo kwa uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa kazi za Serikali.
Upande wake Rashid Ali Juma alisema Dk Shein katika kipindi cha miaka mitano ameonyesha uwezo mkubwa na amefanikiwa kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa umakini mkubwa licha ya kuwapo kwa changamoto zilizokuwa zikijitokeza.
Mjumbe wa NEC, Alex Simon Marangira alisema Dk Shein ameleta mabadiliko makubwa ya viwango vya mishahara kwa wafanyakazi na watendaji wakuu wa Serikali, hatua ambayo imewasadia kupunguza ukali wa maisha katika kipindi chote cha uongozi wake.
Marangira alisema wakulima wa zao la Karafuu kwa mara ya kwanza wameshuhudia bei ya zao hilo ikipanda kwa kiwango kikubwa kutoka Sh3,500 hadi Sh 14,000 kwa kilo hatua ambayo imesadia kuinua kipato cha wakulima wa Unguja na Pemba pamoja na kupunguza kwa kiwango kikubwa biashara ya magendo ya zao hilo.
Dk Shein ni miongoni mwa wagombea sita waliotangaza nia ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka huu wote wakitokea Kisiwani Pemba akiwamo mwanasiasa mkongwe, Seif Sharif Hamad, (CUF) Hamad Rashid Mohamed (ADC), Juma Ali Khatibu (Tadea) Ambary Khamis Haji (NCCR- Mageuzi) na Soud Said Soud wa (AFP) Zanzibar.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment