SIFA YA MCHEZAJI MAHIRI
ANAYETAKIWA IKULU:
- RAFIKI NA MTETEZI WA WANYONGE
- AWE TAYARI KUTUVUSHA KAMA TAIFA KUTOKA KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI
- ANAYEWEZA WAKEMEA RAFIKI ZAKE MAFISADI
Taifa
letu linaelekea katika uchaguzi wa viongozi ambao kupitia vyama vyao vya siasa
wataunda serikali ya kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya
uchaguzi wa October 2015.
Mimi
jicho langu kubwa ni kwa kiongozi Yule ambaye atashika hatamu ya kuongoza Taifa
letu na ambaye atahamishia makazi yake IKULU.
Kama
taifa ni wakati mzuri umewadia sasa tuweze kumchagua mtu makini, mbunifu, mwaminifu,
mwadilifu na mzalendo wa kweli kwa wananchi wanyonge na masikini wa Taifa letu.Kiongozi
ambaye tunamwitaji lazima atambue kuwa kuwa wananchi wana haki ya kupata
chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora.
Akumbuke
kuwa wanaompeleka Ikulu ni wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na sio
marafiki wachache wenye pesa. Na ajue kuwa anapochaguliwa kuongoza, ajuwe
anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri awe tayari kuongoza kwa kuonyesha
njia awe ni mfano wa uwajibikaji.
Kiongozi
tutakaye mchagua lazima awe na tabia ya kuongoza kwa kutofikiria zaidi maslahi
binafsi wazo hili liwe mwiko. Tutataka atumie ustadi wa uongozi ambao utasimamia
haki za waoongozwa; wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua
ahadi ya kutenda kwa haki.
Hatuki
kumchagua kiongozi ambaye baada ya kuchaguliwa ataigeuza ikulu kuwa Ni pango la
wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji wa rasilimali za watanzania kwa masilahi
binafsi pamoja na marafiki wachache. Tunahitaji
kiongozi ambaye uadilifu kwake utakuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku
bila kujali au kupendelea mtu au kikundi cha watu au vile vile awe na uwezo wa
kuwajibisha viongozi watakao kuwa chini yake wanapotenda kinyume na taratibu na
sheria zilizowekwa.
Mwalimu
Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili
tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua
mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kiongozi wetu
tunataka aongoze katika misingi hiyo.
Kiongozi lazima ajue kuwa hakuna
mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani ataongoza
watu wake wateule. Tukiangalia katika historia ya dunia sehemu nyingi, Viongozi
wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na
kubarikiwa katika njia njia nyingi. Walipomsahau Mungu kupitia rushwa na
ufisadi na dhuluma shida na dhiki zilianza.
Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana
ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Kiongozi
anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake
unapatana na Neno la Mungu.
Itakuwa jambo bora tuweze kupata viongozi ambao kwa kweli nao watakuwa
bora katika kuongoza Taifa letu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila mtanzania.
kiongozi kuongoza kwa uwajibikaji;
kuonyesha uzalendo na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.Pengine katika
msingi huu tutahitaji kiongozi ambaye anauelewa mpana wa kuelewa shida za
wananchi mwenye UWEZO wa kufikiri kwa usahihi, kuamua kwa usahihi na kutenda
kwa usahihi wakitambua dhamana ya uongozi ambao taifa linampa. Kwa hivyo
tutahitaji RAIS pamoja na mambo mengine
awe na UWEZO kuongoza kwa usahihi.
Vile vile tunahitaji viongozi wajao katika
serikali zetu mbili wawe ni watu wa WATU; viongozi ambao wataweza kuona
matatizo ya wananchi wao ni yao na yanawakera wanawanyima usingizi, yana
wafanya waongeze nguvu ya uwajibikaji wa kusimamia rasilimali za Taifa. Nasi
kama wananchi tuwe na uwezo wa kuwapima kwa watakacho kifanya wakiwa
madarakani.
Pengine tutahitaji kidogo aina ya viongozi wetu wawe wakali japo sio
sahihi kutumia msemo huu lakini wakati mwingine ile tuweze kupiga hatua ya
maendeleo tutahitaji viongozi wenye mawazo ya
uwajibikaji chanja; ili tuweze kubadilisha
kidogo maadili ya utendaji kwa
Watanzania; Tunahitaji Maraisi katika
serikali zetu mbili ambao wanaweza
kuwawajibisha mara moja watendaji wake ambao wanashindwa kuwajibika,
tuwapate viongozi ambao wanaweka pembeni huruma ambazo hazina msingi kwa Taifa;
Nafikiri itakuwa ni jambo la busara kama sisi kama watanzania na wapiga
kura tukiweza kuepuka tabia ya kuwachagua viongozi wetu kwa Mazoea, Mkumbo na kwa kutumia Hisia na mapenzi binafsi juu ya wagombea.
Nafikiri umefika wakati tuwachagua viongozi wetu kwa upeo wao wa kuona mambo
mbalimbali nauwezo wao wa uongozi hapa nazungumzia uzoefu wa kiongozi kabla ya
kuchaguliwa kuwa rais je amefanikiwa kwa kiasi gani katika idara ambayo amewahi
kuongoza?
kama taifa tunafahamu kuwa taifa letu bado linaogelea sana katika tope nzito la
matumizi mabaya ya rasilimali ya Taifa Rushwa na Ufisadi basi tunahitaji Rais
ambaye analiona hili kuwa ni tatizo na linahitaji utatuzi wa haraka. Lazima
tukubali kuwa mabadiliko yoyote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yenye kulenga
kuletea faida wananchi walio wengi hayawezi kufanikiwa bila ya kutokomeza
rushwa na ufisadi. Kiongozi wetu aweze kuliona hili na kuwa tayari kupambana
nalo akiamini kuwa Tanzania rushwa imeshaota mizizi, umepelekea mamilioni ya
watanzania kupoteza matumaini na hali zao za maisha lakini kupitia yeye ataweza
kulitatua tatizo hili na kuwachukulia sheria wale wote ambao wamehusika katika
uchafu huu,
Tunahitaji
kiongozi ambaye ataweza kuyatekeleza kwa vitendo manemo haya ya Mheshimiwa Yusuph Makamba “maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao
wenyewe, kwa kufanya kazi. Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba
kila kitu wanategemea kitafanywa na serikali … Watanzania wataendelea kulia
umaskini kwa kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,”. Kauli hii ni nzito kiongozi wetu anayetaka kuongoza taifa hili
lazima awe tayari kuwaeleza wananchi bila kuogopa kukosa kura katika kipindi
kingine cha uchaguzi.
Daima tunapofikiria kuwachagua viongozi wa juu
wa Taifa letu tunayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi sema kuwa kazi ya urais ni ngumu na inahitaji busara na kuchukua maamuzi
magumu, ili kuweza kutimiza haki wananchi wanyonge “ walala hoi ”; aliendelea
kushauri kuwa “Ole wale wanaokimbilia Ikulu, wanakimbilia nini, Ikulu hakuna
biashara ya kufanya, Ikulu ni mahali patakatifu na kama kuna mtu anadhani kuwa
kukaa Ikulu ni raha basi angeniuliza mimi katika kipindi cha miaka 21 niliyokaa
Ikulu nimefanya biashara gani,Ikulu ni mzigo mzito”
Mwandishi
Nyenyembe aliwahi andika kuwa “Kwa maana hiyo mtu
anapoamua kuulilia urais,urais sio pambo la nchi,urais ni jalala, urais ni
chumba cha kuhifadhia maiti,urais ni njaa,urais ni magonjwa,urais ni bakuli la
kukingia machozi ya watu wanyonge wanaolia kila siku wakihitaji msaada na kama
hawapati anayetazamwa hapo ni rais”
Katika demokrasia wananchi
ndio wenye dhamana na uwezo wa mwisho wa kumrejesha mwanasiasa kuendelea kuhozi
madaraka; pamoja na umaarufu wake, uadilifu na utaalam katika kushughulikia
maswala ya siasa bila ridhaa ya mwananchi sio rahisi kurejea madarakani;
Hebu tuanagalie historia
ya vyama vingi na chaguzi za Zambia zinaainisha kwa ukomavu wa demokrasia ndani
ya Zambia wananchi ndio wenye sauti ya mwisho wananchi wa Zambia wanapima na
kuamua kulingana na utendaji wa viongozi wao na sio ushabiki wa vyama vyao;wamejitahidi
sana kuweka nchi mbele vyama baadae.
Tatizo la kushabikia sana
vyama ndilo linaloponza sana maendeleo ya nchi nyingi za kiafrika; wananchi
wanakumbatia zaidi chama na sio utendaji wa viongozi wa vyama vyao;
Kama wananchi tunatakiwa
kuanza kuangalia upya maamuzi yetu dhidi ya viongozi wetu; tunahitaji viongozi
waadilifu na viongozi wa namna hii
wataweza kuchukua hatua kwa maslahi ya jamii kwa manufaa ya wote, na
wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo kulingana na utaratibu
wa nchi husika na kukendelea kukubalika kwako kwa masilahi ya wengi; Katika
mfumo wa kidemokrasia wa serikali, ambapo nguvu ya utawala ina inapatika upya
kila baada ya miaka mitano na wananchi ndio wenye dhamana ya kuwarejesha
madarakani.
Nchi ya Zambia
imetufundisha kuwa hakuna kiongozi anayemiliki watu, hakuna chama chenye
hatimiliki ya kuwa na kundi la wananchi kama itakuwa hivyo basi kuna tatizo na
wananchi katika nchi hiyo; wananchi mara zote wanategemea na wanataka mabadiliko makubwa ya kiuchumi hawahitaji
propaganda za chuki, wanahitaji kufaidi raslimali zao wazambia walikuwa wanashangaa utajiri wote
unaotokana na shaba unakwenda wapi? Pale ambapo hawakuridhika hawakuwa na
papara walisubiri tu wakati ulipofika walimweka pembeni kiongozi na kumpa
dhamana kiongozi mwingine. Lazima tukubali kuwa katika nchi zilizopo kusini mwa
Afrika Zambia ni moja ya changamoto za
mabadiliko ya kisiasa:
Maamuzi ya wananchi katika
awamu tofauti Zambia umeendelea kuwashangaza viongozi walioko madarakani
kuanzaia enzi Kaunda, pamoja na ukongwe
wake wa kutawala kwa miaka 27 hadi awamu ya Banda; Kiini cha msukumo huu nini?
Wananchi wanatamani kupata maisha bora; na kuwa viongozi wenye kiwango cha juu
kabisa cha uadilifu kuweza kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo sio kwa
nadharia bali vitendo;
Viongozi wetu wa vyama vya
siasa wamesahau kuwa, Kimsingi, raia huzaliwa wakiwa huru dhidi ya mikingamo ya
kijamii, kwa lugha ya kitaalamu tabula rasa. Lakini mikingamo hii ya kijamii
huingizwa katika fikra za wananchi kupitia itikadi na elimu ya siasa katika
vyama ambavyo wanafuata; na wakati mwingine hata kupitia shule na sehemu za
ibada.
Cha ajabu haitoshi
kuivuruga jamii peke yake tumeona na tunaendelea kuona kuwa viongozi wetu wa
kisiasa hapa nchini wamekuwa wakigombana kila mara katika mambo ya msingi na
yasiyo na msingi. Kugombana si kubaya kama kunaleta tija, lakini kule kugombana
kunakofanywa kwa misingi ya kujitafutia umaarufu kunasabaisha viongozi
kushindwa kutekeleza majukumu yao ambayo yanatokana na ahadi wakati wakiomba
ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, ni dhambi ambayo haiwezi kuvumilika hata
kidogo.
Wakati tunaelekea katika
kipindi cha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi ya uraisi kupitia vyama
mbalimbali; sisi kama wananchi tuanze kujipima na kujua ni kiongozi wa namna gani
tuna mwitaji; tuziangalie khali zetu za uduni wa maisha sisi bado ni masikini, tunahitaji barabara
bora; huduma za afya nzuri, elimu bora kwa vijana wetu; ajira za kutosha kwa
wenye sifa za kuajiriwa;
Kama Rais Kenedy wa
Marekani alivyowahi kusema ‘Wewe UMELIFANYIA NINI TAIFA LA TANZANIA’ ni wajibu
wa msingi kwetu kama wapiga kura kujiuliza swali hili je tumelitendea haki Taifa
kwa kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya serikali zetu mbili? Yatupasa kutimize
wajibu wetu kwa maisha bora kwa kila mtu kwa kuchagua viongozi bora na sio bora
kiongozi. Miaka mitano ni mingi sana tukichagua kiongozi mbovu.
Wananchi
tujiulize je kama taifa tumaini letu ni lipi dhidi ya viongozi wetu wa
siasa ambao tunatarajia kuwachagua; tunahitaji viongozi wakuu wa nchi ambao
wataweza kutupeleka kwenye nchi yenye
neema na amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa,
kidini .
Niliwahi andika huko nyuma
kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya tusiendelee;tukumbuke
kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe, juhudi zetu na misimamo
yetu; tukiangalia kwa ujumla wanasiasa wanpoteza muda mwingi katika propaganda na sio
kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana
na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.
Wanasiasa wetu ndio wapiga
majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia sisi
wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya utamaduni
wa siasa za Tanzania kwa kuwachagua viongozi watakao endeleza umasikini wa
Taifa letu kwa faida ya wachache.
Kiongozi tunaemtaka
tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake
basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya
kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda sisi kama Taifa.
Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani,
kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia
kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?
Taifa letu katika kipindi
cha miaka ya karibuni kiliingia katika vurugu za Mtwara, Dar es salaam Zanzibar
Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika; Je kiini cha vurugu hizi kimepata jibu? Kama jibu
ni hapana sasa tutahitaji viongozi wetu wakuu tutakao wachagua wawe wanaweza
kuona na kutumia muda wao katika kuleta majibu ya matatizo ya wananchi wao;
Wananchi tunatakiwa tuamke na tusiwape nafasi
wanasiasa kutufanya sisi kuwa daraja lao
la wao kuweza kutimiza malengo yao bila sisi kujitambua kwa haraka; matokeo
yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunauwawa na tunaendelea kuwa masikini.
Imefika wakati sasa hata
viongozi wengine tutakao wachagua tusirudie kosa la kuchagua viongozi ambao
wanasilka na tabia ya
kuzomeana,
kulaumiana, kutukanana;mwelekeo huu hautatusaidia sisi lengo letu la kuwa na maisha
bora
Nafikiri linalowezekana
leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi
tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina ya Muumba wetu tu;
Baba wa Taifa aliwahi
kusema kuwa “Kupanga
ni kuchagua”. Wananchi kwa kweli inatakiwa tujipange sasa kwa
maendeleo ya Taifa letu na kwa masilahi yetu binafsi ili kupata viongozi wetu
wakuu walio bora na makini. Tunataka tupate viongozi waadilifu kweli kweli.
Tukumbuke kuwa Uadilifu ni karama,
ya utambuzi wa kujifahamu kwa mtu binafsi hususa kiongozi wa serikali, ambaye
anatakiwa kufanya kazi zake kulingana na sheria na taratibu ambazo hujenga,
utamaduni, wa kuwajibika kulingana na
sheria husika. Kwa kufuata taratibu nzuri za utendaji kazi Uadilifu katika kazi husaidia uimarishaji wa misingi
ya utawala bora.
Kwa kujumuisha kabisa
uadilifu na utimilifu kwa uhusiano wa biashara yetu inayoendelea na kufanya
uamuzi, tunaonyesha kujitolea kwa utamaduni ambao unakuza kiwango cha uadilifu
wa hali ya juu kabisa; ni kweli kuwa uadilifu inahitaji uaminifu binafsi wa
kiongozi husika; uadilifu unahitaji uaminifu
wa kupinga ubinafsi kwa kiongozi ambaye amepewa dhamana. Uadilifu unaendana na Kuwa
mkweli katika utendaji na kuishi kulingana na maadili ya kazi na kuheshimu
rasilimali kwa faida ya wengine.
Wajibu wa kutenda ukweli ni
wajibu wa juu kabisa wa uadilifu kwa viongozi wa umma; kiongozi wa umma lazima atambue hali halisi ambayo inaendana na wajibu
kwa kufuata maadili hivyo kusambaza cheche ili hata jamii nzima nayo iweze
kuishi kulingana na maadili ya Taifa.
Kiongozi mwadilifu daima hutakiwa kuonyesha uhusiano kati ya maadili yake
ya utendaji na kwa urahisi kabisa aweze kusema na nafsi yake ili isitawaliwe na tama ya rushwa ambayo
itapingana na dhana nzima ya maadili kulingana na kiapo chake. Hapa ni jukumu
la serikali kuweka mipaka bayana wa uhusiano kati ya maadili binafsi na sheria
za utendaji wake kwa manufaa ya umma. Uadilifu daiama huashiria haki, ikiwa na
maana kuwa kiongozi wa umma lazima aweka maslahi binafsi pembeni;
Uadilifu hujenga amani, huleta ufanisi, kwani Watumishi wa umma watakuwa
wanauwezo wa kuhakikisha matumizi sahihi, ufanisi wapesa za umma. dhana na
misingi ya uwajibikaji anatarajiwa kufanya ya viongozi wa umma kuwajibika kwa
matendo yao au kutotenda
Ni zinatakiwa kuongeza uwazi wa serikali, kusisitiza na kuimarisha
mwitikio wa kiserikali na uhalali na kuboresha utekelezaji wa sera. Mwalimu
Nyerere katika hija ya maisha yake, alijitahidi kutanguliza masilhai ya watu wake,
bila ya kujikita katika ubinafsi, uroho na uchu wa madaraka; uchoyo na
ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa viongozi wengi ndani ya Taifa letu.
Maadili ni muhimu zaidi na
katika siasa na kwa maendeleo ya wananchi. Maadili ya kweli yatapunguza
wanasiasa kujishughulisha na rushwa.
MUNGU IBARIKI JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA UTUVUSHE SALAMA ILI TUWEZE KUWAPATA VIONGOZI BORA KWA MANUFAA YA WATU WAKO katika uchaguzi wa mwaka huu 2015.