Marais Dkt. Jakaya Kikwete na Dkt Ali Shein mara baada ya kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa Oktoba mwaka jana.
WAKATI
siku za kupiga Kura ya Maoni zikikaribia, imebainika kuwa zaidi ya nusu
ya Watanzania wataipigia kura ya Ndiyo Katiba Inayopendekezwa.
Aidha,
imeelezwa mwito wa vyama vinavyounda umoja wa Ukawa wa kususa kura ya
maoni haujawavutia wananchi wengi, hivyo wengi hawauungi mkono.
Hayo yamo
katika taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza
kati ya Januari 27 na Februari 17 mwaka huu na kutolewa jana kupitia
muhtasari wenye jina la “Kuelekea Kura ya Maoni ya Watanzania kuhusu
Katiba Inayopendekezwa.”
Kwa
mujibu wa taarifa ya utafiti huo uliosambazwa kwa vyombo vya habari na
Mshauri wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande, muhtasari huu umetokana
na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye
uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi.
Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa Tanzania Bara pekee juu ya Katiba Inayopendekezwa.
“Jumla ya
wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya Januari 27 na Februari 17, 2015.
Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la Sauti za Wananchi
(iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013) na duru la
14 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12 na
Machi 4, 2014).“Takwimu hizi zimetumika kufuatilia mwenendo wa muda
mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa mahojiano haya yalihusisha makundi yote
ya wananchi wa Tanzania Bara.
Hata
hivyo, maoni ya wananchi yanaonesha wazi mashaka yaliyopo katika
mchakato mzima wa kuibadili Katiba, kwani mwezi mmoja tu kabla ya siku
ya kupiga kura, uandikishaji wa wapiga kura haujakamilika.
Kutokana
na hali hiyo, nusu ya wananchi (asilimia 47) wanafikiri uchaguzi mkuu
ujao utafanyika chini ya Katiba mpya, lakini idadi ndogo (asilimia 30)
inafikiri kuwa uchaguzi huo utafanyika chini ya Katiba ya sasa.
Kuhusu
Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba na ushawishi wake kwa wananchi
kususa kura ya maoni, utafiti huo umeonesha: “Kati ya wananchi
waliosikia minong’ono juu ya Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba,
asilimia 66 wanapinga hatua hiyo.
Asilimia
68 wanapinga ushawishi kwa wananchi kususa kura ya maoni na robo tatu
(asilimia 75) ya wananchi wanasema hawatasusa kura ya maoni.” Aidan
Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema kuna “Kuna mambo matatu
yanayojitokeza kutokana na maoni haya ya wananchi.
Jambo la
kwanza ni kwamba kura ya ‘Ndiyo’ kwa Katiba Inayopendekezwa haina
uhakika. Tofauti iliyopo ni finyu na wananchi wameonesha kwamba kura hii
inaweza kubadilika wakati wote katika mchakato huu.
“Pili,
kuna kilio kilicho wazi kuhusu umuhimu wa Katiba kusisitiza masuala ya
uwazi na uwajibikaji. Wananchi wameunga mkono kwa nguvu zote vifungu
vinavyoimarisha uwajibikaji. Changamoto kubwa zilizopo katika
upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwepo kwa tatizo kubwa la rushwa
vyote vimekuwa na athari kubwa na wananchi wanatafuta njia za
kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao.
“Tatu,
wananchi hawajashawishika kuchukua hatua za nguvu za kuleta mabadiliko.
Mwito wa UKAWA wa kususa kura ya maoni haujawavutia na wananchi wengi
hawauungi mkono. Mambo haya matatu yatakuwa changamoto kubwa kwa
viongozi wa ngazi zote kuamini kwamba mawazo yao yanawakilisha maoni ya
wananchi.”
Elvis
Mushi, Mratibu wa Sauti za Wananchi alitoa maoni yake kuhusu matokeo
hayo alisema: “Mashaka yaliyopo juu ya kukamilika kwa mchakato wa
mabadiliko ya katiba na kubadilika kwa mwenendo wa mchakato huo
kumesababisha mashaka kwa wananchi. Hali hii ndio inayosababisha maoni
ya wananchi kugawanyika katikati kuhusu masuala yote muhimu.”
Askofu afunda viongozi wa dini
Viongozi
wa dini wametakiwa kufundisha amani na upendo kwawaumini wao na si
kuwahamasisha wananchi wasiipigie kura ya ndio Katiba ijayo, kwani hali
hiyo imeelezwa itasababisha nchi kutokea mitafaruku ya wenyewe kwa
wenyewe ikiwa hata viongozi wa dini nao watashiriki mambo ambayo
hayawahusu.
Hayo
alisema Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania, Erasto Ikongo na
ambaye ni Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste Tanzania
(PPT) alipokuwa anatoa tamko la kupinga kauli ya Jukwaa la Wakristo
Tanzania (TCF), kuhusu kushikilia msimamo wao wa kushinikiza waumini
kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa kwa kudai kuwa katiba
hiyo imefika hapo ilipofika kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.
Alisema
viongozi wa dini wanatakiwa wabebe vitu vya Mungu na kuongelea masuala
ya Mungu na si kuzungumzia yale ambayo hayawahusu.
“Viongozi
wa dini waendelee kuhamasisha dini ili nchi yetu ibaki kuwa na amani na
utulivu kama ilivyo sasa na si kuingilia masuala ya Katiba ambayo
hayawahusu,” alisema na kuongeza kuwa, kama wao walikuwa na nia na Taifa
hili wangebeba hoja moja tu ya inayohusu Mahakama ya Kadhi kwa vile ni
suala la kidini na si kubeba hoja za Ukawa.
Pia,
aliwataka viongozi wa dini wote waliokwenda bungeni Dodoma warudi kwani
wanahamasisha waumini ambao ni wabunge vitu ambavyo vinaweza kupoteza
amani nchini kwetu.
Awali,
tamko la umoja huo lilitolewa juzi na kusainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maskofu wa KipentekosteTanzania
(CPTC), Askofu Daniel Awet na kusema wao hawana hasira kama ambavyo
watu wengine walivyotafsiri.
CHANZO: HABARI LEO (Muro)
No comments:
Post a Comment