Wapanda nafasi ya tatu, MO aimwagia Sh. milioni 500
Yanga imeendelea kuwa mteja wa Simba baada ya jana kukubali kichapo cha bao 1-0 katika mechi ya raundi ya pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Ushindi huo wa Simba ni wa pili mfululizo baada ya Desemba mwaka jana Wekundu wa Msimbazi hao kuibamiza mabao 2-0 timu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyoandaliwa na wadhamini wao wakuu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro.
Katika mechi ya raundi ya kwanza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyochezwa Oktoba 18, mwaka jana katika uwanja huo, timu hizo zilitoka sare tasa.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 26 tano nyuma ya vinara Yanga na nne nyuma ya mabingwa watetezi wa VPL, Azam FC ambao wanashika nafasi ya pili.
Bao la Okwi
Emmanuel Okwi ndiye aliyepeleka kilio Jangwani katika dakika ya 51 baada ya kutupia bao hilo pekee kwa shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 27 ambalo lilimshinda kipa wa Yanga, Ali Mustafa 'Barthez'. Okwi alifunga bao hilo kutokana na kupenyezewa pasi murua na Ibrahim Ajibu.
Bao hilo ni la tano kwa Okwi msimu huu na ni pili kwa kipa wa Yanga Ali Mustafa 'Barthez' kufungwa VPL msimu huu, pia kipa huyo alifungwa mengine mawili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ugenini nchini Botswana.
Kabla ya mechi kuanza
Awali katika mechi ya utangulizi iliyozikutanisha Timu B za miamba hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kuingia uwanjani kupasha misuli majira ya saa 9:14 alasiri wakiongozwa na kipa wao, Ivo Mapunda, hata hivyo dakika nne baadaye (saa 9:18) Yanga nao walitinga uwanjani kupasha wakiongozwa na mfungaji bora wa VPL msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe.
Robo saa kabla ya mechi kuanza mashabiki wa Yanga waliokuwa wamekaa sehemu ya chini ya jukwaa la VIP C, walianza kuzichapa kavukavu baada ya kutofautiana kuhusu utabiri wa matokeo.
Kipa Ivo Mapunda wa Simba alitakiwa na marefa wa mchezo huo kuondoa taulo lake langoni kabla ya mechi kuanza. Taulo hilo limempatia umaarufu mkubwa nchini Kenya wakati akiidakia Gor Mahia.
Katika mechi hiyo, timu zote zilivaa jezi za kampeni maalum ya kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) ambazo zilikuwa zimeandikwa mbele "imetosha". Kadhalika mechi ilisimama kwa dakika moja kwa kuwakumbuka albino waliokufa kwa mauaji ya ukatili.
Kipindi cha kwanza
Pambano hilo lililoanza kwa timu kusomana, Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kufika langoni mwa Yanga katika dakika ya pili, lakini shuti la Ajibu lilikosa macho baada ya kwenda pembeni kabla ya dakika moja baadaye Ivo kudaka shuti kali la Simon Msuva.
Dakika ya 18, beki wa Simba Juuko Murshid alifanya kazi ya ziada kwa kuruka juu na kuokoa kwa kichwa krosi ya Msuva iliyokuwa ikielekea kimyani.
Nafasi nzuri zaidi kwa Yanga ilikuwa katika dakika ya 28, Mrwanda alipopewa pasi murua ndani ya 18 na Mrisho Ngasa lakini akapata kigugumizi katika kupiga shuti jambo lililoonekana kumkera Kocha Mkuu Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye aliamua kumtoa dakika mbili baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
Dakika ya 36, Javu alitoa pasi murua kwa Ngasa ambaye aliachia shuti kali lakini Ivo akawa makini kulicheza.
Nafasi nzuri kwa Simba zilikuwa dakika ya pili, tatu, 27, 42 na 44, lakini mashuti ya washambuliaji Emmanuel Okwi na Ajibu hayakuwa na macho huku Ramadhani Singano 'Messi' akishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata dakika ya 43 baada ya kukwatuliwa kwa nyuma na Haruna Niyonzima jambo lililomsabishia kadi ya njano.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake huku Yanga ikipata faulo 9-8, kona 1-1, kuotea 3-1, mashuti 4-4 na njano 3-4 dhidi ya Simba.
Kipindi cha pili
Hapakuwa na mabadiliko zaidi ya yale ya Yanga ya kipindi cha kwanza, hata hivyo kasi ya Simba ilionekana dakika ya 51 baada ya Okwi kutupia bao la kwanza kwa shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 27 ambalo lilimshinda kipa wa Yanga, Ali Mustafa 'Barthez'. Okwi alifunga bao hilo baada ya kupenyezewa pasi murua na Ajibu.
Bao hilo lilipandisha mzuka kwa Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic baada ya kucharuka akihamasisha mashabiki wa Simba wasimame kushangilia.
Kama Ajibu angeongeza umakini, basi mambo yangezidi kuiendea vibaya Yanga kwani dakika ya 60 akiwa ndani ya 18 alikosa bao la wazi huku dakika tisa baadaye Ivo akifanya kazi ya ziada kwa kucheza shuti la Javu.
Dharau za Niyonzima kupiga mpira na kufunga wakati refa Martin Saanya kutoka Morogoro akiwa ameshapuliza kipenga ziliigharimu Yanga na kuifanya icheze pungufu kuanzia dakika ya 73 baada ya Mnyarwanda huyo kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje, huku pia akienda na kupiga meza ya mwamuzi wa akiba wakati akitoka uwanjani.
Dakika ya 75 Ajibu alimpisha Elius Maguri huku Yanga nayo ikifanya mabadiliko katika dakika ya 76 kwa kumtoa Ngasa na kumuingiza Mliberia Sherman Kpah wakati dakika 12 baadaye Simba ikimtoa Abdi Banda na kumuingiza Simon Sserunkuma.
Kipenga cha mwisho
Baadhi ya mashabiki wa Jukwaa la VIP C walishindwa kujizuia baada ya kuonekana wakimwaga machozi mara baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Saanya. Kadhalika shabiki mmoja wa kike wa Yanga alidondoka na kuzirai kabla ya kukimbizwa hospitali mara baada ya mechi kumalizika.
Nyimbo kuu ya mashabiki wa Simba mara baada ya kipenga cha mwisho, walikuwa wakiimba Jerry Muro, Jerry Muro, Jerry Muro..., ingawa haikufahamika sababu ya kuimba hivyo lakini huenda ni kutokana na tambo alizozitoa msemaji huyo wa Yanga siku moja kabla ya mchezo akisema "Simba si mpinzani tena wa Yanga bali ni mtani tu".
Kauli za makocha
Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Pluijm alisema walitengeneza nafasi chache lakini walishindwa kuzitumia, huku pia akifafanua kuwa hata Simba walitengeneza nafasi mbili tu za uhakika kipindi cha pili na kwamba anadhani bahati ya kushinda mechi hiyo ndiyo iliyowabeba.
Akizungumzia kitendo cha kumtoa Mrwanda, alisema "Ninamjua Danny (Mrwanda) kitabia, niliamua kumtoa mapema ili asionyeshwe kadi ya pili ya njano.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Kopunovic alisema: "Ninawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo niliyowapa. Hivi ndivyo Simba inavyopaswa kucheza siku zote.
"Bao la Okwi ni gumu, ni mchezaji bora mwenye uwezo wa kufunga mabao ya aina ile, kwa kweli anastahili pongezi."
Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro', alisema tumepambana sana, lakini tumefungwa bao la kushangaza, hatujui limeingiaje.
Naye Niyonzima alisema "ninafikiri ilipangwa na Mungu nitolewe kwa kadi nyekundu".
Kwa ujumla Simba ilipata faulo 12-5 dhidi ya Yanga, kona 0-5, kuotea 0-0, mashuti, 4-3, njano 1-2, nyekundu 0-1 na kunawa mpira 0-1. Simba: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Abdi Banda, Ramadhani Singano, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na Emmanuel Okwi.
Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngasa na Danny Mrwanda.
Katika hatua nyingne inadaiwa Mohamed Dewji (Mo) amemwaga kitita Sh. milioni 500 katika klabu hiyo.
Kwingineko
Mtibwa Sugar ikiwa Manungu Turiani ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City. Bao la Mtibwa lilifingwa na Musa Mgosi dakika ya sita huku la City likifungwa na Themi Felix dakika ya 64. Nayo Mgambo Shooting ilishinda 3-1 dhidi Ndanda FC
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment