Ninaandika ujumbe huu kwa wa-Tanzania wenzangu. Ninatoa hoja kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tuachane na utaratibu wa sasa wa serikali kuvipa ruzuku vyama vya siasa.
Fedha inayotolewa na serikali KAMA ruzuku kwa vyama vya siasa ni kodi ya walipa kodi wote, na wengi wao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ruzuku hii ni hujuma dhidi ya hao walipa kodi ambao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ni hujuma, ingawa imehalalishwa kisheria. Sheria na haki si kitu kile kile. Ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini ulikuwa ni hujuma dhidi ya haki.
Fedha inayotolewa kwa vyama hivi ni nyingi sana, mamilioni mengi ya shilingi kila mwezi. Ni fedha ambazo zingeweza kununulia madawati na vitabu mashuleni, kulipia mishahara ya walimu au madaktari, kukarabati barabara, kuwanunulia baiskeli walemavu wanaotambaa chini, kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi ambayo yanaoza katika mikoa KAMA vile Ruvuma, na kadhalika.
Kutoa ruzuku kwa chama kimoja tu, KAMA kingekuwepo kimoja tu, tayari ni hasara na hujuma. Sasa tunavyo vingi, na hasara ni kubwa mno. Utitiri wa vyama unavyoongezeka, hali itazidi kuwa mbaya. Huduma za jamii zitaendelea kuzorota, na hata kutoweka, kwa fedha kutumika kama ruzuku kwa vyama vya siasa.
Kama kweli vyama hivi vina maana kwa wanachama wao, wanaweza kuvichangia vikastawi bila tatizo. Vyama kama Simba, Yanga, Maji Maji, na Tukuyu Stars havitegemei ruzuku. Wanachama, kwa mapenzi waliyo nayo kwa vyama vyao, wanaviwezesha kuwepo na kustawi, na hawako tayari vitetereke. Wako tayari kuvichangia wakati wowote ikihitajika. Nini kitawazuia wanachama wa vyama vya siasa kufanya vile vile, kama kweli vyama hivi vina maana kwao?
Sisi raia ambao si wanachama wa vyama vya siasa TUNA wajibu wa kuanza kampeni ya kushinikiza itungwe sheria ya kufuta ruzuku kwa vyama vya siasa, ili kuokoa fedha, ziweze kutumika kwa huduma muhimu kwa jamii yetu.
Kama umevutiwa na makala hii na ungependa kufuatilia zaidi mawazo yangu ya kichokozi na kichochezi, utayapata kwa wingi katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.
- Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Prof. Mbele: Hapa Kwetu
No comments:
Post a Comment