WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 4, 2015

Buriani Kapteni Komba: Nakupigia makofi, nikifuta machozi




HAKUNA ubishi kwamba kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kapteni John Damiano Komba ni cha kuhuzunisha.

Ilikuwa ni mshtuko mkubwa kila mahali ziliposikika habari kwamba amefariki ghafla siku hiyo ya Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ mjini Dar es Salaam kutokana na ugonjwa wa kisukari na presha.

Ni kama mshumaa uliozimika ghafla katika giza nene. Mshumaa uliotarajiwa kutoa mwanga mkubwa katika kampeni za CCM za Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tayari katika sherehe za miaka 38 ya CCM mwezi uliopita, Komba aliwaonjesha wapinzani wa CCM aina ya vigongo ambavyo walikuwa watarajie kwenye kampeni za uchaguzi huo.
“Hatunywi sumu, hatujinyongi, CCM mbele kwa mbele…., tumeipenda wenyewe…chaguo letu milele na wavimbe wapasuke watajijua wenyewe….. waache waisome namba, CCM mbele kwa mbele, waacheni waandamane CCM mbele kwa mbele…,” wameambiwa hivyo wapinzani baada ya ‘kugaragazwa’ kwenye uchaguzi wa mitaa na vijiji uliofanyika mwaka huu.
Je, Komba alikuwa mtu wa aina gani? Kama tunavyomjua hakuwa malaika. Alikuwa ni binadamu wa kawaida tu mwenye msimamo wake, mtazamo wake, uamuzi wake, dini yake na chama cha siasa ambacho ni CCM.

Na kama binadamu hakukosa kasoro. Katika usanii Komba hakutaka kushindwa katika jambo lake lolote. Kama unabisha mwulize aliyekuwa mpinzani wake wa jadi, Norbert Chenga wa kikundi cha Muungano, Dar es Salaam ambacho sasa kimetoweka katika ulimwengu wa sanaa.

Yeye na Chenga waliendeshana kweli kweli hasa katika muziki wa taarab. Ilikuwa ni vita ya kunyang’anyana wasanii mahiri na mwenye kisu kikali ndiye mara zote aliyekuwa akishinda na mtu huyo alikuwa ni marehemu.

Mbali ya nguvu ya chama na kipaji cha Komba kuongoza sanaa, umahiri wa TOT dhidi ya Muungano katika taarab ulitokana pia na mkusanyiko wa vipaji vya muziki huo kutoka Zanzibar na kikundi cha JKT na Bima. Kwa mfano, Khadija Kopa na Fatma Dogodogo walikuwa wamechomolewa kutoka katika kikundi mahiri cha taifa cha Culture cha Zanzibar.

Kutoka JKT walitoka wasanii mahiri kama marehemu Mzee Bia Hassan na mtunzi asiye na makeke lakini mkali kweli kweli kwa kutunga, marehemu Ali Mtoto Seif.

Katika vita hiyo ya kukwapua wasanii, kitendo ambacho bila shaka hakitasahaulika ni kile ambacho mwimbaji na mtunzi mahiri wa Muungano, Ally Star ‘alipokiasi’ kikundi cha Muungano kwenda kutamba kwenye jukwaa la TOT siku ya onyesho lenye upinzani mkali kati ya vikundi hivyo viwili kwenye Ukumbi wa Vijana, Dar es Salaam.

Ilikuwa hatari kweli kweli. Fikiria katika upinzani wa kweli wa soka wa enzi za 1960 na 1970 mchezaji tegemeo wa Yanga aibuke ghafla katika benchi la Simba siku ya mechi ya watani hao iliyokuwa na gumzo kubwa. Lakini ilitokea hivyo katika mvutano wa taarab wa TOT na Muungano na sasa imebaki ni historia.

Lakini zaidi ya yote Komba alikuwa ni Mtanzania aliyeipenda nchi yake jinsi inavyoongozwa na CCM na alijitahidi kutumia kipaji chake cha usanii na ushawishi kwenye majukwaa ya siasa kukiongezea chama chake thamani kwa njia ya burudani na majukwaa ya kwao Mbambabay na maeneo mengine.

Tanzania sasa si tena nchi ya chama kimoja. Mzalendo wa kweli unatakiwa uwe shabiki wa chama tawala au upinzani ili kutoa mchango wako katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Komba alichagua kuendelea kuwa shabiki wa CCM mwaka 1992 wakati Tanzania ilipoamua kuwa nchi ya vyama vingi. Kwa sababu hiyo basi, huwezi kumlaumu kwa kutumia kipaji kukisifia CCM na kuvinanga vyama vya upinzani pale alipoona kwa mtazamo wake vinapotoka.
Kapteni Komba amefariki dunia akiwa kipenzi kikubwa cha wanaCCM waliokuwa wanafurahishwa na kipaji chake cha sanaa. Lakini siyo siri kwamba kwenye siasa alijitengenezea maadui kutokana na kauli na misimamo yake mbalimbali.

Yaliyojitokeza katika mitandao ya kijamii baada ya kifo chake yanathibitisha ukweli huo kuwa kuna watu ambao walikuwa hawampendi kabisa kutokana na kauli alizowahi kuzitoa kama mwanaCCM au mwanasiasa.

“.....Kupitia msiba wa Kapteni John Komba ndio nimeanza kuthibitisha chuki kati ya watawala na watawaliwa, hasira kati ya 'wao na sisi', roho mbaya kati ya daraja la chini na daraja la juu.....watu hawana huzuni tena...na kuna watu wanaongea maneno machafu......Nchi haipo salama sana....hasira za matabaka zinaongezeka..,” aliandika mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kila siku nchini katika hali ya utani wenye umakini mtandaoni.

“Chuki kati ya watawala na watawaliwa?” “Hasira kati ya wao na sisi?” “Roho mbaya kati ya daraja chini na daraja la juu?” Anachomaanisha mchambuzi huyo hapa kinafikirisha lakini ukweli ni kwamba mambo hayako sawa kisiasa nchini kutokana na kauli za watu baada ya kifo hicho.

Lakini hebu turudi nyuma. Ni mambo gani ambayo marehemu aliwatibua watu wa upande wa pili wa chama chake au wa vyama vya upinzani?

Yanaweza yakawepo mambo kadhaa lakini makubwa yanayojitokeza waziwazi kutokana na jinsi watu wanavyojadili mitandaoni ni matatu.

La kwanza katika orodha ni kauli yake aliyoitoa alipokuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Akichangia kwenye Bunge hilo Kapteni Komba alidai kwamba mfumo wa Serikali Tatu ukipitishwa ataingia msituni kudai Serikali mbili.

Hakufafanua lakini kimsingi wengi walivyomuelewa ni kwamba alikuwa anazungumzia kwenda kuanzisha vita katika kudai hizo Serikali mbili alizokuwa anashabikia ambazo ndizo hatimaye zilipitishwa katika mapendekezo ya katiba yaliyopitishwa baada ya wabunge wengi wa upinzani kulisusia bunge hilo.

Wapo waliojitokeza kudai kwamba kauli yake ya kuingia msituni ilikuwa ya hatari ya kuiingiza nchi vitani hivyo kustahili kukemewa.
Je, ilistahili kweli kukemewa? Chama chake, viongozi wa Serikiali wakiwemo wanasheria wake na hata viongozi wa dini zote hawakuiona athari waliokuwa wanaiona wanasiasa wengi wa upinzani ambao walilivalia njuga suala hilo bila mafanikio ya kutaka marehemu kuchukuliwa hatua.

Wapo wanaoamini hadi leo kwamba kauli hiyo ingetolewa na mjumbe wa upinzani angesakamwa.

Suala la pili la marehemu ambalo lilileta ukakasi lilitokea pia kwenye bunge hilo hilo maalum la Katiba alipomwandama aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba. Ilikuwa baada ya kutokea sintofahamu kati ya wajumbe wa CCM na wale wa vyama vya upinzani kupelekea wale wa upinzani kususia vikao.

Kapteni Komba hakumung’unya maneno kueleza jinsi alivyofadhaishwa na Jaji Warioba katika mchakato wake mzima wa kukusanya maoni na mapendekezo yake ya rasimu ya katiba.
Komba alisema kuhusu Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Tanzania: “Mimi nasema wazee nyinyi mkistaafu pumzikeni na kama tunawapeni vyeo au nyadhifa mtusaidie kazi, fanya kwa heshima uliojenga huko nyuma. Lakini leo hizi zote vurugu hizi ni warioba. Nashindwa kuvumilia kutosema, mtanisamehe….. vurugu zote hata tungezungumza namna gani , mzee huyu ni chanzo cha vurugu zote….”

Nao uamuzi wa Kapteni Komba wa kumshabikia waziwazi Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa katika mbio za kuwania urais 2015, ulimtenganisha na baadhi ya wanachama wenzake wa CCM waliopo katika kambi za wagombea wengine wa urais.

“Mimi hapa nilipo leo ukiniuliza nani atakuwa rais, mimi nasema Lowasa anafaa kuwa rais. ….Mimi nasema Edward Lowassa anafaa kuwa rais kabisa. Kama chama changu kitampendekeza mimi 100 kwa 1000 kabisa…..” alisema Komba alipohojiwa katika kipindi kimoja cha runinga kuhusu nani anayefaa kuwa Rais 2015.

Jimboni kwake, Komba alikuwa mtetezi mkubwa wa wananchi wake walioko katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Mara baada ya kuuvaa ubunge alilalamika sana kuhusu ukosefu wa usafiri wa uhakika wa meli.

Alifikia hata hatua ya kumsifu aliyekuwa Rais wa Kwanza wa nchi jirani ya Malawi, Hayati Kamuzu Banda kwamba ndiye aliyekuwa mbunge wao kwa kuruhusu meli ya nchi hiyo M.V Ilala kufanya shughuli zake pia katika mwambao wa Tanzania wa ziwa hilo kusafirisha abiria na mazao.

Mbali ya kulalamikia usafiri wa meli ambao sasa umeahidiwa utapatiwa ufumbuzi na serikali, Komba amefariki akilalamikia pia tatizo la mawasiliano ya matangazo ya redio za Malawi kuwa na nguvu kuliko matangazo ya redio za Tanzania katika jimbo lake.

Katika mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi, Komba alilalamikia uamuzi wa Malawi kusitisha safari za meli ya M.v Ilala katika mwambao wa Tanzania uliokuwa umefanywa na Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda.

Alimshutumu kwa kuibua upya mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kuwachanganya wananchi wa Mbinga kwa matangazo ya redio za Malawi zinazosikika jimboni mwake.

Komba alisema Rais Joyce Banda alikuwa anazitumia redio zake kupotosha umma kuwa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake na wananchi wanaamini hivyo.

Je, Komba alitokea wapi? Ni mwalimu wa shule ya msingi ambaye kipaji chake cha usanii kilivumbuliwa na aliyekuwa kada na CCM na mwenye kipaji cha aina yake ya usanii, hayati Brigedia Jenerali Moses Nnauye. Ndiye aliyemwingiza jeshini na Komba kuanza makeke. ‘CCM Nambari One’ kilikuwa kibao cha kwanza kilichomtoa.

Mwaka 1992 Tanzania ilipoamua kuwa na mfumo wa vyama vingi, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alimshawishi aache jeshi kuunda kikosi cha sanaa ndani ya CCM kilichoitwa Tanzania One Theatre (TOT).

Taifa halitomsahau Komba kwa nyimbo zake za simanzi za maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999.

Aliwahi kuniambia kwamba nyimbo zile alizotunga baada ya kujifungia chumbani aliposikia tu kwamba m Mwalimu amefariki, tofauti na wengi walivyokuwa wakifikiria kwamba zilitungwa wakati Mwalimu bado anauguzwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, Uingereza.

Hakika kifo chake kitawagusa Wamalawi walio wengi na hasa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi. Komba alikuwa kivutio kikubwa wakati alipopata nafasi ya kumfanyia kampeni Muluzi ili ashinde awamu ya pili ya uongozi wake.

Simulizi za Komba na kundi zima la TOT zilikuwa kubwa hasa vijijini ambako watu walikuwa hawaelewi ni vipi lori kubwa la wasanii hao lilikuwa linatoa muziki mkubwa katika maeneo yao yasiyokuwa na umeme. Ilikuwa kama wanaona uchawi fulani hivi.

Muluzi anakifahamu vyema kipaji cha usanii cha Komba na uzoefu wake wa kushiriki siasa za Tanzania kwani aliweza kummegea mawili matatu yaliyoweza kumuongezea sifa kufanya yeye na chama chake cha UDF kushinda uchaguzi wake wa awamu ya pili kwa kishindo.

Komba aliwahi kuniambia kuwa alifanikiwa kumbadilisha Muluzli kuwa kiongozi wa watu kwa ushauri wake wa kumtaka ajichanganye na watu wa kawaida katika mikutano yake na kuachana na staili iliyokuwapo ya viongozi kuonekana kama ni wafalme wa aina fulani kwa matendo na kauli zao.

Aliniambia kuwa alikuwa ameshibana sana na Muluzi hivyo haikuwa ajabu basi aliporudi nyumbani kuanzisha shule, jina la shule kuitwa Sekondari ya Bakili Muluzi.

Katika juhudi za kutaka muziki wa Tanzania uwe na aina moja ya upigaji, Komba alijaribu kuutangaza mtindo wa Achimenengule ili ufuatwe na bendi zote nchini uwe ni alama ya Tanzania.
Kwa bahati mbaya jambo hilo hakufanikiwa kwani ni bendi chache zilizoitikia hazikufanya hivyo kwa moyo na baadaye kuachna na suala hilo.

Hata hivyo Komba alistahili sifa kwa kujaribu jambo ambalo pengine huko mbele umuhimu wake utaonekana.
Komba alizaliwa Machi 18, 1954. Alisoma shule ya Msingi Lituhi baadaye kujiunga na Sekondari ya Songea kuanzia mwaka 1971 hadi 1974.

Mwaka uliofuata hadi 1976 alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kleruu Iringa na kuhitimu cheti cha ualimu.

Baada hya kujiunga na jeshi, alipata mafunzo ya uafisa wa Jeshi katika chuo cha Maafisa wa Jeshi cha Monduli mwaka 1977 hadi 1978. Ndipo kuanzia mwaka 1992 alipojikita kwenye sanaa na siasa hadi mauti yanamkuta.


Source:www.raiamwema.co.tz

No comments:

Post a Comment