WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, February 24, 2013

Simba yaweka rehani ubingwa




JAHAZI la Simba limeendelea kuzama baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Beki Salvatory Ntebe aliifungia Mtibwa Sugar bao pekee katika dakika ya 18 akiunganisha vizuri pasi nzuri ya Vicent Barnabas katika mchezo huo ambao Simba walimaliza wakiwa 10 baada ya beki Juma Nyoso kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 86.

Kwa matokeo hayo Simba imebaki ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 31, huku Yanga wakiendelea kuongoza wakiwa na pointi 39, wakifuatiwa na Azam (36) katika mbio hizo za kusaka ubingwa.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alisema nafasi ya timu yake kutwaa ubingwa ni ndogo kwa sasa kutokana na matokeo hayo.
“Uchovu wa safari ndefu iliyoifanya timu yake hivi karibuni mikoani na kucheza mechi za mfululizo ni sababu ya kupoteza mchezo wa leo,” alijitetea kocha huyo.

Naye Mecky Mexime aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kufanikiwa kupata ushindi huo mzuri dhidi ya Simba.
Katika mechi hiyo dakika ya pili, beki Amir Maftah alipitisha krosi nzuri kwa Shomari Kapombe aliyepiga shuti kali lililopaa juu ya lango la Mtibwa Sugar.

Katika dakika ya 18, pasi ya Barnabas ilimkuta Ntebe aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja na kujaa wavuni hivyo kuipa Mtibwa Sugar bao la kuongoza.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari ya Mtibwa Sugar kwani katika dakika ya 23, shuti la mshambuliaji Hussein Javu lilipanguliwa kwa ustadi mkubwa na kipa Kaseja.

Simba ilijaribu kurudi mchezoni katika dakika ya 28, ambapo Felix Sunzu alipiga shuti kali, lakini lilipaa juu ya lango la Mtibwa.
Katika mchezo huo kocha wa Simba, Liewig hakuwaanzisha wachezaji wake mahiri, Amri Kiemba pamoja na Mrisho Ngassa, lakini baadaye alifanya mabadiliko kwani aliwatoa Ramadhani Chombo, Haruna Moshi na Haruna Chanongo na kuwaingiza Kigi Makasi, Kiemba na Ngassa.

Katika hali ya kushangaza wachezaji Chombo na Moshi baada ya kutolewa walikwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo badala ya kukaa katika benchi.

Pamoja na mabadiliko hayo, Simba ilishindwa kurudi mchezoni, ambapo zikiwa zimebaki dakika nne kabla ya mchezo kumalizika, mwamuzi Ibrahim Kidiwa ‘Mdudu’ alitoa kadi nyekundu kwa Nyoso kwa kumchezea vibaya Barnabas.
Vikosi

Simba: Juma Kaseja, Nasoro Masoud, Amir Maftah, Juma Nyoso, Komanbil Keita, Shomari Kapombe, Ramadhan Chombo/Kigi Makasi, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi/Amri Kiemba na Haruna Chanongo/Mrisho Ngassa.

Mtibwa Sugar: Hussein Shariff, Said Mkopi, Issa Rashid, Salvatory Ntebe, Salum Sued, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Shaaban Kisiga na Vicent Barnabas.

Source: Mwananchi

Matokeo ya kidato cha Nne: Wakuu wa shule wadai ilitungwa kwa mfumo tofauti



Na Fredy Azzah na Kelvin Matandiko  

MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka ya nyuma, ambapo

mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya kulazimika kuvielezea kwa undani.

Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na miaka ya nyuma wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.
Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa upo kama ule wa miaka yote.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.

Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu, Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya elimu.

“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.

Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”

source: Mjengwa Blog

Neno La Leo: Mtoto Wako Ni Mwalimu Wako!

Photo: Neno La Leo: Mtoto Wako Ni Mwalimu Wako!
Ndugu zangu,
Moja ya maamuzi mazuri niliyopata kuyafanya ni hili la kutojihusisha na siasa za majukwaani ili kuwa na muda zaidi na watoto wangu.
Hakika, miaka kumi ya mwanzo ya makuzi ya mtoto ni muda muhimu sana katika makuzi ya mtoto. Hapo ndipo unajengwa msingi wa mtoto maishani.
Mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto katika miaka yake kumi ya mwanzo, lakini, hata baada ya hapo, kabla mtoto hajatimiza miaka kumi na minane, bado mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto wako. Kujenga misingi ya mahusiano ya mtoto na mzazi, awe mzazi wa kike au kiume.
Mara nyingi tumefanya makosa kudhani kuwa mahusiano yanayopaswa kujengwa ni kati ya watu wazima. Kati ya mke na mume, na kati ya mzazi na wazazi wengine. Tunayasahau mahusiano kati ya mtoto na mzazi.
Tunafanya makosa kuwaachia mayaya wa nyumbani jukumu la kulea watoto wetu. Tunafanya makosa pia, kuwaachia walimu tu, jukumu la kufuatilia mienendo ya elimu ya watoto wetu.
Na wazazi wa kiume tumekuwa mfano mbaya sana wa kuliacha jukumu la kulea kwa mzazi wa kike.
Hakika, mtoto, awe wa kike au kiume, anahitaji sana kuwa karibu na mzazi wa kiume pia. Kuwa na mahusiano ya kirafiki pia. Kazi ya mzazi haipaswi kuwa ni ya kukaripia watoto tu, bali kuwa rafiki nao, kuwa na muda wa kucheka nao. Na kubwa zaidi, uwa tayari kujifunza kutoka kwa watoto.
Na mtoto anaweza kuwa Mwalimu mzuri kwa mzazi, kama mzazi atamwandalia mtoto mazingira ya kuifanya kazi ya ualimu kwa mzazi wake.
Niwe mkweli, kuwa nimejifunza mengi kutoka kwa watoto wangu kama wao wanavyojifunza kutoka kwangu.
Mathalan, leo asubuhi nilimkuta mwana wangu akisoma kitabu (hicho pichani). Nikamwomba anisimulie kidogo juu ya anachosoma. Alipoanza kunisimulia, basi, nilijikuta nataka kumsikiliza zaidi. Kinahusu mtoto ambaye wazazi wake walitengana.  Mzazi mmoja anaishi Marekani na mwingine Canada.
Mtoto huyu aliondoka kwa mama yake Marekani ili aende kumwona baba yake Canada. Alipanda ndege ndogo. Alikuwa yeye na rubani tu. 
Huko angani rubani akapatwa na mshtuko wa moyo. Mtoto huyu akalazamika kuongoza ndogo hiyo. Aliongoza huku ndege ikipotea angani. Mwisho ndege ikaishiwa mafuta, maana hakujua haswa namna ya kuongoza ndege.
Ndege ikaanguka ziwani.  Bahati njema mtoto aliweza kuogelea na  kunusurika. Akalikuta pango, hapo akaanza kutafuta mbinu za kuishi akisubiri msaada wa kuokolewa... Kisa kinaendelea...!
Tunajifunza nini?
Umuhimu wa wazazi kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kujisomea. Mimi niliwasomea vitabu watoto wangu tangu wangali wadogo sana. Hivyo, nikawajengea hamu ya kusoma.
Si ajabu, kuwa leo wanasoma vitabu kiasi cha hata kuweza kunisimulia ya kwenye vitabu ambavyo nisingeweza kuviona maishani mwangu. Na kuna ninayojifunza. Hivyo, watoto wangu wanakuwa walimu wangu pia.
Naam, mtoto wako ni mwalimu wako.
Na hilo ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Ndugu zangu,
Moja ya maamuzi mazuri niliyopata kuyafanya ni hili la kutojihusisha na siasa za majukwaani ili kuwa na muda zaidi na watoto wangu.

Hakika, miaka kumi ya mwanzo ya makuzi ya mtoto ni muda muhimu sana katika makuzi ya mtoto. Hapo ndipo unajengwa msingi wa mtoto maishani.

Mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto katika miaka yake kumi ya mwanzo, lakini, hata baada ya hapo, kabla mtoto hajatimiza miaka kumi na minane, bado mzazi unatakiwa kuwa karibu na mtoto wako. Kujenga misingi ya mahusiano ya mtoto na mzazi, awe mzazi wa kike au kiume.


Mara nyingi tumefanya makosa kudhani kuwa mahusiano yanayopaswa kujengwa ni kati ya watu wazima. Kati ya mke na mume, na kati ya mzazi na wazazi wengine. Tunayasahau mahusiano kati ya mtoto na mzazi.

Tunafanya makosa kuwaachia mayaya wa nyumbani jukumu la kulea watoto wetu. Tunafanya makosa pia, kuwaachia walimu tu, jukumu la kufuatilia mienendo ya elimu ya watoto wetu.

Na wazazi wa kiume tumekuwa mfano mbaya sana wa kuliacha jukumu la kulea kwa mzazi wa kike.

Hakika, mtoto, awe wa kike au kiume, anahitaji sana kuwa karibu na mzazi wa kiume pia. Kuwa na mahusiano ya kirafiki pia. Kazi ya mzazi haipaswi kuwa ni ya kukaripia watoto tu, bali kuwa rafiki nao, kuwa na muda wa kucheka nao. Na kubwa zaidi, uwa tayari kujifunza kutoka kwa watoto.

Na mtoto anaweza kuwa Mwalimu mzuri kwa mzazi, kama mzazi atamwandalia mtoto mazingira ya kuifanya kazi ya ualimu kwa mzazi wake.

Niwe mkweli, kuwa nimejifunza mengi kutoka kwa watoto wangu kama wao wanavyojifunza kutoka kwangu.

Mathalan, leo asubuhi nilimkuta mwana wangu akisoma kitabu (hicho pichani). Nikamwomba anisimulie kidogo juu ya anachosoma. Alipoanza kunisimulia, basi, nilijikuta nataka kumsikiliza zaidi. Kinahusu mtoto ambaye wazazi wake walitengana. Mzazi mmoja anaishi Marekani na mwingine Canada.

Mtoto huyu aliondoka kwa mama yake Marekani ili aende kumwona baba yake Canada. Alipanda ndege ndogo. Alikuwa yeye na rubani tu.

Huko angani rubani akapatwa na mshtuko wa moyo. Mtoto huyu akalazamika kuongoza ndogo hiyo. Aliongoza huku ndege ikipotea angani. Mwisho ndege ikaishiwa mafuta, maana hakujua haswa namna ya kuongoza ndege.

Ndege ikaanguka ziwani. Bahati njema mtoto aliweza kuogelea na kunusurika. Akalikuta pango, hapo akaanza kutafuta mbinu za kuishi akisubiri msaada wa kuokolewa... Kisa kinaendelea...!

Tunajifunza nini?

Umuhimu wa wazazi kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kujisomea. Mimi niliwasomea vitabu watoto wangu tangu wangali wadogo sana. Hivyo, nikawajengea hamu ya kusoma.

Si ajabu, kuwa leo wanasoma vitabu kiasi cha hata kuweza kunisimulia ya kwenye vitabu ambavyo nisingeweza kuviona maishani mwangu. Na kuna ninayojifunza. Hivyo, watoto wangu wanakuwa walimu wangu pia.

Naam, mtoto wako ni mwalimu wako.

Na hilo ni Neno la Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Tumesahau kujitawala, tujifunze upya kujitawala!




WIKI iliyopita niliandika kuhimiza uchapaji kazi nchini, na kusema kwamba maendeleo haya ambayo CCM na serikali yake wanayatambia hivi sasa yana walakini, kwa sababu, kwa kiasi kikubwa, hayatokani na uchapaji kazi wetu mkubwa; bali ukopaji wetu mkubwa.
Nataka kuuendeleza kidogo mjadala huu kwa sababu kiwewe hiki cha kukopa cha Serikali ya Rais Kikwete hadi kwenye mabenki ya biashara na mashirika ya hifadhi za jamii nchini, kisipodhibitiwa kitatuletea madhara makubwa huko mbele ya safari.
Wiki iliyopita nilipendekeza tuidhibiti hali hii kwa Bunge kuweka ukomo wa ukopaji (debt ceiling); yaani kiwango fulani kikishafikiwa hakuna tena kukopa mpaka madeni yaliyopo yapunguzwe kwanza hata kwa asilimia 50. Nadhani nilieleweka.
Msingi wa hoja yangu ni kwamba maendeleo yaliyokamilika na ya kujivunia ni yale yanayotokana na uchapaji kazi wetu katika kila sekta ya uzalishaji nchini kuanzia kilimo vijijini hadi kwenye viwanda, maofisini, sekta za utalii, madini nk.
Hatma ya uchapaji kazi huo ni kukua kwa uchumi wetu, hali ambayo inatuweka katika mazingira mazuri ya kujiletea wenyewe maendeleo tunayoyahitaji – iwe ni uboreshaji miundombinu, ujenzi wa viwanda, uboreshaji huduma za afya, elimu nk.
Japo mimi si mchumi, sihitaji kuwa mchumi kuelewa kwamba kama tutachapa kazi zaidi sekta ya utalii nk na kuzalisha zaidi katika kilimo na viwandani, na hapo hapo tukatoza kodi stahiki makampuni ya madini na mengine makubwa nchini, tukakomesha ufisadi, na pia tukapunguza matumizi ya serikali na hasa ukubwa wake, tunaweza kujiletea wenyewe maendeleo tunayoyahitaji bila Serikali kulazimika kukopa sana nje au kukopa sana mabenki ya kibiashara hapa nchini na hata kwenye asasi za hifadhi ya jamii.
Lakini kwa sababu tumeacha kuchapa kazi, na kwa sababu viongozi wetu wameacha kabisa kuzunguka nchini kuhimiza uchapaji kazi, kidogo kidogo tumegeuka taifa la wavivu - taifa linalotegemea misaada na pesa za kukopa kujiletea haya tunayoambiwa na CCM kuwa ni “maendeleo makubwa”.
Kwa sababu ya utamaduni huu wa uvivu tulioukumbatia, watawala wanalikimbia tatizo kwa kutegemea mikopo ya ndani na nje ya nchi kuendesha nchi. Na ndiyo maana ndani ya kipindi cha miaka mitano tu, Serikali ya Kikwete imeongeza deni la Taifa kutoka Sh. trilioni 6 hadi Sh. trilioni 21!
Ni hoja yangu kwamba kama tunataka maendeleo ya kweli na ya kujivunia, hatuna budi kuujenga upya utamaduni wa kuchapa kazi na kuuvunjilia mbali utamaduni wa uvivu ambao umeanza kutamalaki nchini.
Binafsi, sikumbuki mara ya mwisho kumsikia Rais Kikwete au Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakitoa hotuba za kuhimiza uchapaji kazi nchini kwa namna ile walivyofanya Nyerere na Sokoine. Ni nadra kuwasikia watawala wetu wa sasa wakihimza uchapaji kazi kwa wakulima vijijini au kwa wafanyakazi viwandani au hata maofisini!
Na ma-DC wao wengi huko wilayani ni hivyo hivyo. Wanaochapa kazi ni wachache mno. Wengi hawaonekani vijijini. Kutwa nzima wako maofisini wakipanga namna ya kutumia vyeo vyao vipya kujitajirisha. Kama wakienda vijijini ni pale tu wanapopokea taarifa za migogoro inayotishia amani.
Kwa hakika, tangu Mwalimu Nyerere anga’atuke madarakani na baadaye kufariki, suala la watawala wetu kuhimiza uchapaji kazi nchini ‘limefariki’ naye! 
Sasa niambieni:Ni taifa gani duniani ambalo linaendelea kwa kasi kwa sababu ya kukopa na kukopa zaidi na si kwa sababu ya uchapaji kazi uliotukuka? Si zile nchi za Mashariki ya Mbali zinazoitwa Asian Tigers na wala si India au Brazil.
Katika uvivu wetu huu ambao Watanzania tunaogelea nao, tunazungukwa na kuishi na matatizo; lakini hatuchukui hatua yo yote ya kujaribu kuyatatua mpaka aje mgeni (Mzungu) atuonyeshe namna ya kuyatatua, hata kama tulikuwa tunajua namna ya kuyatatua.
Saratani hii ya utegemezi wa mikopo na wafadhili (dependency syndrome) – kwa fikra, mawazo na hata kwa matendo, inaanzia serikalini. Zaidi ya asilimia 40 ya bajeti yetu ni pesa za wafadhili. Sehemu kubwa ya miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea nchini ni  mikopo ya vyombo vya fedha vya nje na vya ndani. Zaidi ya asilimia 50 ya mipango yetu ya maendeleo inaanzia kwanza kwenye fikra za kukopa nje na ndani ya nchi, na si kwenye pesa zetu wenyewe.
Tumefika mahali sasa tumeanza kuamini kuwa kazi ya rais kuongoza nchi sasa inarahisishwa na uhodari wake wa kukopa. Anayependwa na wafadhili ndiye tunayemtaka awe rais wetu kwa sababu tunajua kuwa itakuwa rahisi kwetu kukopeshwa na mataifa makubwa atakayoyafuata kuomba mikopo au misaada!
Ilivyo sasa, tumeaminishwa kuwa anayehitajiwa si rais mchapakazi na mbunifu, bali ni yule anayewasikiliza wafadhili na anayekubaliwa na wafadhili. Ni yule ambaye ni hodari wa kutembeza bakuli la omba omba Ughaibuni kabla ya kikao cha bajeti cha bunge letu!
Hatuna maadili yetu wenyewe. Hatuna dira yetu wenyewe. Hatuna mipango yetu wenyewe ya maendeleo isiyo na mkono wa wafadhili au wa mkopeshaji iwe ni IMF, World Bank, Exim Bank ya China au NSSF ya hapa nyumbani nk!
Hali hii ya kutegemea mikopo ya nje na ya ndani ya nchi kwa karibu kila mradi mkubwa wa maendeleo nchini imeua kabisa ule moyo wa kufikiri, kubuni, kuchacharika wa viongozi wetu. Imeua ule moyo wa kujitegemea uliojengwa katika kipindi cha utawala wa Mwalimu Nyerere.
Hali hii ya utegemezi kwa kila kitu imewalemaza na kuwabwetesha si tu viongozi wetu, lakini hata na sisi wananchi wa kawaida. Kule kwetu Upare kulikuwa na utaratibu wa kazi za kujiletea maendeleo ulioitwa Msaragambo ambao Wapare tuliurithi kutoka kwa mababu zetu. Zama hizo, kila tatizo la kijiji lililowagusa wanavijiji wote lilishughulikiwa kwa pamoja kwa njia ya Msaragambo.
Kama ni kuharibika kwa barabara au mfereji mkubwa unaotumika kwa kilimo cha umwagiliaji, basi, ilipigwa mbiu na wanavijiji walijitokeza kukalafati mfereji huo kwa njia ya Msaragambo. Asiyejitokeza alipigwa faini ya pesa kidogo au vitu kama vile kuku au mbuzi!
Lakini sasa Msaragambo na matumizi ya nguvukazi ya wanavijiji kutatua matatizo yao wenyewe, hakuna tena Upareni. Kinachosubiriwa ni pesa za Halmashauri au za wafadhili au pesa za mkopo!
Zamani utegemezi wa pesa za Wazungu au za Halmashauri kwa kazi ambazo wanavijiji wenyewe walimudu kuzifanya haukuwepo hata kidogo. Leo hii, hata kujenga choo tunasubiri pesa za wafadhili au za mkopo! Hata kufukia madimbwi ya maji ambayo ni mazalio ya mbu wanaosababisha malaria, tunasubiri tufanyiwe na wengine.
Miaka kadhaa iliyopita niliwahi kutembelea kijiji kimoja cha wilaya moja ya mkoa wa Tabora ambako nilitembezwa katika bwawa la mfano la kufugia samaki lililojengwa kijijini humo kwa pesa za wafadhili (Wazungu)!
Katika hali iliyonishangaza kabisa, wenyeji wetu waliona fahari kutuonyesha bwawa la kawaida kabisa lililojengwa kutokana na fedha za wafadhili! Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tumekuwa mazezeta tusiofanya lolote kujisaidia wenyewe mpaka waje Wazungu kutufanyia hata mambo tunayomudu kuyafanya sisi wenyewe.
Sasa, ungetaraji watawala wetu wangehaha kuuzima moto huu wa dependency syndrome usisambae kwa kasi nchini kwa kutembea kote nchini kuhimiza uchapaji kazi na kuhubiri juu ya manufaa ya dhana ya kujitegemea. Je; ndivyo wanavyofanya?
Jibu langu ni hapana. Na hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wao wenyewe ni waumini wakubwa wa maendeleo yanayotokana na fedha za mikopo, na ndiyo maana miaka mitano tu deni la Taifa limeruka kutoka Sh. trilionji 6 hadi Sh. trilioni 21!
Mtunzi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chinua Achebe, akizungumzia hali ya mambo ilivyo katika nchi yake na katika nchi nyingine za Afrika, alipata kunukuliwa akisema: “We have to begin to learn to rule ourselves again” ; yaani: tunapaswa kuanza kujifunza namna ya kujitawala wenyewe tena” (tafsiri ni yangu).
Naamini Achebe hakukosea kusema hivyo, na naamini pia kwamba nasi Tanzania tunapaswa kuanza kujifunza upya kujitawala; maana yaelekea baada ya Nyerere kufariki tumesahau namna ya kujitawala.
Vinginevyo tusingejivunia mno maendeleo yanayotokana na pesa za kukopa na kukopa zaidi hata kutoka katika asasi za hifadhi za jamii zinakotunzwa pesa za masikini wastaafu wetu!
Tafakari.
Source: Raia Mwema: Johnson Mbwambo

YANGA NUSU BINGWA



               
YANGA jana iliendelea kujiimarisha kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Azam bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salam.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 16 huku ikiwa na mechi moja mkononi wakati Azam ni ya pili ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 17. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 31.

Kiungo Haruna Niyonzima ndiye aliyepeleka majonzi kwa mashabiki wa Azam baada ya kuifungia Yanga bao pekee na la ushindi dakika ya 31. Alifunga bao hilo baada ya gonga safi kati yake na Hamisi Kiiza.

Pambano hilo lilikuwa na burudani ya aina yake kutokana na timu zote mbili kuonyesha soka ya ufundi, hasa katika safu ya kiungo na ulinzi. Katika safu ya ushambuliaji, ukosefu wa umakini ndio uliokuwa kikwazo kuzikosesha kupata mabao.

Mshambuliaji Jerry Tegete aliikosesha Yanga mabao mengi wakati alipobaki yeye na kipa Mwadini Ally wa Azam mara tatu. Kipa huyo ndiye aliyekuwa nyota ya mchezo kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari.

Mwamuzi Abdalla Hashim wa Dar es Salaam alijikuta akiingia kwenye matatizo na wachezaji wa Azam kutokana na maamuzi yake kuwa ya kutatanisha. Baada ya pambano hilo kumalizika, mwamuzi huyo alilazimika kuokolewa na askari wa kutuliza ghasia (FFU) baada ya wachezaji wa Azam kumvamia.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons ilishindwa kutambiana na Polisi Moro baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

JKT Mgambo iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kuichapa JKT Ruvu bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Bao pekee na la ushindi la Mgambo JKT lilifungwa na Fully Maganga dakika ya 25.

Source: Liwazo Zito Blog