WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, April 27, 2014

Rais Kikwete aongoza Sherehe za miaka 50 ya Muungano


joyce_075c0.jpg 

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Rais Joyce Banda wa Malawi katika sherehe za miaka 50 ya Muungano.Rais Banda kwa sasa ndiye mwenyekiti wa jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika SADC. 

(PICHA:FREDDY MARO)

source: mjengwa blog

Warioba: Matusi, uongo vinaniumiza

warioba2 d63d1

Na Hudugu Ng'amilo
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia na kumsingizia mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa dhidi yake yanamuumiza.

Aidha, Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa kuwapatia Katiba wanayoitaka.

Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na viongozi wa CCM wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwa maneno makali,huku wakimshutumu na kumkejeli yeye na baadhi ya wajumbe wa tume aliyoiongoza.

Akizungumza kwa mifano katika mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa anawashashangaa wajumbe hao na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili Rasimu ya Katiba, badala yake wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno yasiyo ya kweli.

"Bulembo (Abdallah Bulembo mjumbe wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM) amenitukana, amenitukana... amesema niliwahi kupokea rushwa huku akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM, anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi simjui wala sijawahi kumwona huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara," alisema Jaji Warioba kwa sauti ya upole iliyoashiria kuumizwa.

Aliongeza kwamba siyo mara ya kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za matusi, kwani aliwahi kufanya hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM mkoani Tanga.

"Alifanya hivyo Tanga, anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea," alisema.
Akizungumzia kauli aliyoitoa Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana na kazi yake ya kuwasilisha Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema: "Wao wanataka waseme uongo, mtu mwingine asiseme kitu."

Warioba alieleza kuwa tangu lugha za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi yake, baadhi ya watu walimshauri kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu Bunge.
Alisema Bunge ndiyo lenye mamlaka ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa bungeni, kama wahusika hawafanyi hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.

"Kama kinga ya Bunge inatumika vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia ya kuchukua hatua, watu walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria walisema hata nisipokwenda, wao watakwenda mahakamani nikawazuia," alisema Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu.

Akisimulia kuhusu uchaguzi wa ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa kupokea rushwa na kufungiwa kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen Wassira ambaye sasa yuko CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu."Uchaguzi ule ulikuwa umejaa sana rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa asigombee," alisema.

Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Warioba alisema: "Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50 taifa limekaa kwa amani, mshikamano na umoja. Ni kweli tumekuwa na matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuz
 
CHANZO MWANANCHI

MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR YAFANA


1
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete akiingia kwenye uwanja wa Uhuru kuwaongoza watanzania katika maadhinimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania yanayofanyika kila mwaka Aprili 26 kusherehekea muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili mwaka 1964 watanzania wengi wamejitokeza katika maadhimisho hayo wakiwemo viongozi mbalimbali na marais wa nchi mbalimbali za Afrika na wawakilishi wa nchi mbalimbali pia katika mataifa mbalimbali ya Ulaya,  
8
Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Rais Yoweri Mseveni wa Uganda katikati nI King Mswati wa Swaziland na kushoto ni Rais Piere Nkurunzinza wa Burundi.
raaaaaaaa_b1d05.jpg
Kikosi cha Makomandoo kikionyesha ukakamavu na kuonyesha uwezo wake katika mapambano ya Karatee na  mbele ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Kikwete


0L7C0297 5e5bb
Na Hudugu Ng'amilo.
Sherehe za kuhadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyozaa nchi ya Tanzania zimefanyika leo mjini Dar es Salaam na kupambwa kwa maonyesho mbali mbali ya kijeshi pamoja na halaiki zilizoandaliwa na watoto.
Marais wanne wa nchi za Afrika Afrika Mashariki akiwemo Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi ni miongoni mwa marais waliohudhuria sherehe hizo.
Wengine ni Rais Joyce Banda wa Malawi, Mfalme Mswati III wa Swaziland, mfalme Letsie III wa Lesoto Makamu wa Rais wa Nigeria Mohammed Sambo, Makamu wa Rais wa Zambia Guy Scott, Waziri Mkuu wa Rwanda Piere Habumurenyi, Waziri Mkuu wa Misri Ibrahim Mahlab na Rais Mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki.
 
Katika maadhimisho yao pia kulikuwa na maonyesho ya silaha mbali mbali za kivita zikiwemo ndege za kivita pamoja na za kiraia.
 
Hata hivyo kilichovutia  ni kikosi cha makomandoo wa jeshi la Tanzania ambao walionyesha umahiri wao kupambana na adui bila kutumia silaha na kuvunja vitu vigumu kwa kutumia kichwa  na mikono.
 
Onyesho jingine lililotia fora zaidi ni askari wa miamvuli ambao waliruka kutoka kwenye ndege umbali wa futi elfu arobaini  kutoka usawa wa bahari kwa kutumia miavuli na kutua katikati ya uwanja wa sherehe.
0L7C0250 888b4


source: mjengwa blog

UKAWA wamjibu Kikwete

ukawa5 eeb08
Na Hudugu Ng'amilo
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) warudi bungeni akidai hawana sababu ya kwenda kushitaki kwa wananchi kwa sababu watawacheka na kuwasikitikia, umoja huo umemjibu wakisema wapo tayari kuchekwa.
Akihutubia vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, siku moja kabla ya sherehe za miaka 50 ya muungano, Rais Kikwete alisema kuwa huko nje wanakotaka kwenda UKAWA siko na siku yake sio sasa, hivyo akawaomba wasipoteze fursa hiyo muhimu ya kutoa mawazo yao bungeni ili yafanyiwe kazi.
Alisema wananchi hawahusiki wala hawana namna ya kuwasaidia kwani mengi ya hayo yanayowakasirisha ni matatizo waliyoyazusha wao.
Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa
kama Kikwete anafikiri kwamba watarudi bungeni kwenye mijadala ya dharau, ubaguzi na matusi inayofanywa na wajumbe wa CCM, basi hajui chimbuko la tatizo.
"Kadiri anavyoendelea kuliacha Bunge liendelee na mijadala ya kibaguzi na matusi, taifa linazidi kupasuka na washauri wake hawamwelezi tatizo hilo," alisema.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atalitumbukiza taifa kwenye machafuko ingawa yeye anafanya utani kwa kuipasua nchi na kushangilia kauli za kibaguzi, kejeli na matusi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa CCM.
"Rais na wasaidizi wake inaelekea hawajasikiliza hata kauli zinazotolewa na viongozi wa dini kuhusu rasimu ya Warioba, atuache twende kwa wananchi, wao ndio wataamua. Tumevumilia kwa kiwango fulani, lakini itafika mahali uvumilivu utaisha, kwani hatuwezi kuendelea kuzuiliwa kufanya mikutano na jeshi la polisi wakati mikutano ya CCM inafanyika kote nchini kutuchafua," alisema Mbowe. 
CHANZO: TANZANIA DAIMA/ mjengwa blog

Wastaafu wamteka JK

wastaafu 13cf0
Na Hudugu Ng'amilo
RAIS Jakaya Kikwete amehujumiwa na viongozi wakuu wastaafu waliomlazimisha kuachana na msimamo wa muundo wa muungano wa serikali tatu na kukumbatia serikali mbili zilizopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa kutoka kwa baadhi ya vyanzo vya habari vilivyo karibu na rais, Ikulu na makao makuu ya CCM, zimelithibitishia  kwamba hadi Bunge Maalumu la Katiba linaanza, Rais Kikwete alikuwa na msimamo ule ule wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Baadhi ya viongozi wastaafu, wakiwamo marais na viongozi waandamizi wa CCM, walishinikiza rais aachane na serikali tatu, kwa vitisho kwamba zitaua muungano.
Baadhi ya wastaafu hao walimficha Rais Kikwete kwamba kwa kuwa yeye aliingia madarakani akiwa rais wa muungano wa serikali mbili, halikuwa jambo la busara kwake kujiingiza kwenye historia ya kuwa rais aliyevunja muungano.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, shinikizo hilo liliambatana na jingine la kumtaka asizindue Bunge kabla ya rasimu ya pili ya katiba mpya kuwasilishwa bungeni, ili apate fursa ya kudhoofisha hoja ya serikali tatu.
Mara baada ya Rais Kikwete kukubaliana na "washauri wake", serikali ililazimika kuingilia kati ili Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta atengue kanuni, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba awasilishe rasimu kabla ya rais kuzindua Bunge, jambo ambalo limesababisha mvurugano unaotishia kuvuruga kabisa mchakato wa katiba mpya.
Hata hivyo, hali hiyo inasemekana kumnyima amani Rais Kikwete ambaye ndiye aliyepokea na kusaini rasimu hiyo, kwa maana kwamba aliridhia.
Uamuzi huo umefanya rais aonekane kiongozi asiye na msimamo thabiti katika masuala muhimu.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai hatua hii imemfanya ashindwe kuacha urithi makini na muhimu katika utawala wake wa miaka 10, kama ambavyo alikuwa amedhamiria.
Wadadisi wanasema wastaafu walimzuia rais kutekeleza azima yake kwa sababu ya hofu tu, wakidhani kwamba katiba mpya yenye mfumo mpya inaweza kufumua mambo yaliyofichika na kuwaingiza matatani.
Wanadai kwamba muungano wenye mfumo mpya una kila dalili za kuiondoa CCM madarakani, na kuhatarisha maslahi ya watawala waliopo na waliopita.
Hoja hii, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, ndiyo ilimkuna Rais Kikwete hata akabadili msimamo.
Kwa hali halisi ilivyo, na mchakato unavyoendelea, ahadi ya Rais Kikwete kuwapa Watanzania katiba mpya mwezi huu imeshindikana.
Alipohutubia taifa na kutangaza kuanzisha mchakato wa katiba mpya miaka mitatu iliyopita, alisema kwamba lengo lake lilikuwa kuzindua katiba mpya katika maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya muungano iliyofanyika jana.
Hadi Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa juzi, zilikuwa zimepita siku 68 kati ya 70 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, huku kukiwapo mgawanyiko mkubwa wa wajumbe na kutishia uhai wa muungano, hasa baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia Bunge baada ya kukerwa na hujuma na matusi kutoka kwa wajumbe wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hadi sasa Bunge la Katiba limefanikiwa kujadili sura mbili za rasimu bila ya kuzipigia kura. CCM imekataa maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanayopendekeza mfumo wa muungano wa serikali tatu, wakatetea mfumo wa serikali mbili.
Mapendekezo hayo ni kinyume kabisa cha yaliyomo kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa ili ijadiliwe na wajumbe hao na kisha kutunga katiba mpya.
UKAWA wanadai kuchoshwa na vitisho na matusi kutoka kwa wajumbe wa CCM na viongozi wa serikali, wakisema kuwa kwa hali ilivyo katiba bora ya wananchi haiwezi kupatikana kwa shinikizo la muundo wa serikali mbili.
Katika hili, Rais Kikwete analalamikiwa kuwa ndiye mvurugaji wa kwanza wa mchakato ambao aliuasisi na kuahidi kuwapatia wananchi katiba bora kabla ya kuondoka madarakani.
Wakati akilihutubia Bunge la Katiba na kulizindua rasmi Machi mwaka huu, Rais Kikwete aliibeza rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, akisema takwimu zao kuhusu watu waliotoa maoni ya muundo wa muungano zinatiliwa shaka.
Alisema kuwa muundo wa serikali tatu unaopendekezwa hautekelezeki kwani rais wa dola hiyo hatakuwa na mamlaka kwa vile hana ardhi, rasilimali na hivyo hataweza kukopa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, katika hali kama hiyo, jeshi linaweza kupindua serikali na hivyo ukawa mwanzo wa kuvunjika kwa muungano, huku akisisitiza kwamba wao kama CCM muundo ambao unaweza kutatua kero zilizopo ni ule wa sasa wa serikali mbili.
Kauli hiyo ya rais iliibua mjadala mkubwa, na hivyo kufifisha ndoto za kupatikana kwa katiba bora kwani ilionyesha wazi kwamba mapendekezo ya wananchi ya serikali tatu yaliyomo kwenye rasimu hayatazingatiwa.
Hali hiyo imeendelea kujitokeza kwenye Bunge Maalumu la Katiba baada ya wajumbe wote wa CCM kuendeleza msimamo wa rais wa serikali mbili na kumshambulia Jaji Warioba binafsi kwa matusi mazito wakidai ana ajenda ya kuvunja muungano kwa kupendekeza serikali tatu.
Hatua ya Rais Kikwete kubadilika na kuvuruga mchakato aliyouasisi na kuusimamia kwa mafanikio makubwa, imeelezwa kusababishwa na mambo makubwa mawili, likiwemo hilo la kuburuzwa na viongozi wastaafu.
Duru nyingine za kisiasa katika suala hilo la kukwama kwa mchakato wa katiba, zinahusisha na rasilimali ya gesi na mafuta zilizopatikana nchini, ambapo inadaiwa mataifa makubwa yanayotaka kuwekeza ndiyo yanaishinikiza serikali isibadili muundo wa muungano uliopo.
Vyanzo vyetu vya habari vinaeleza kwamba mataifa hayo tayari yameweka msimamo wa kuisaidia CCM kifedha ili kuhakikisha inapigana kufa au kupona kutobadili muundo wa muungano katika katiba mpya.
Inaelezwa kuwa muundo wa shirikisho la serikali tatu unaopendekezwa kwenye rasimu ya katiba mpya, unatoa fursa ya wazi kwa wananchi wa serikali washirika kusimamia rasilimali zao tofauti na ilivyo katika muundo wa sasa ambapo mambo mengi yamefanywa siri na serikali.
Hadi sasa majaliwa ya kupatikana kwa katiba mpya yametoweka baada ya UKAWA kujiondoa, na hivyo kulifanya Bunge la Katiba kushindwa kufanya maamuzi ya kupitisha ibara na sura za rasimu kutokana na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar kushindikana.
Chanzo Tanzania Daima./ mjengwa blog

Tsvangirai asimamishwa uongozi MDC



Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change MDC kimesema kimemsimamisha kiongozi wake Morgan Tsvangirai kwa kukiuka kanuni za kidemokrasia.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa MDC Tendai Biti kufuatia mkutano wa chama hicho uliofanyika katika mji Mkuu Harare.

Tangu mwaka 2009 hadi 2013 Bwana Tsvangirai alitumikia taifa la Zimbabwe katika nafasi ya Waziri Mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa kwa pamoja na Rais wa sasa Robert Mugabe.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilifikia kikomo mwezi julai mwaka 2013 baada ya Rais Mugabe kushinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi wa rais na Tsvangirai kususia uchaguzi kwa madai ya udanganyifu. (J M)
Kushindwa kwake kulipunguza nguvu yake kama kiongozi ambaye alikuwa mshindani mkuu wa Rais Mugabe.

Waangalizi wanasema ndani ya MDC kumekuwa na mgogoro wa kiuongozi kwa miezi kadhaa.

Viongozi wengine wa ngazi za juu wameripotiwa kusimamishwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya jumamosi na wanachama wengine wa chama hicho watachukua nafasi zao.

source: mjengwa

Papa wawili watangazwa watakatifu


Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani
Umati mkubwa wa watu wamekusanyika mjini Vatican kushuhudia tukio la kihistoria ambapo viongozi wawili wa zamani wa Kanisa Katoliki, Papa John Paul II na Papa John XXIII wametangazwa watakatifu.

Ibada iliyoendeshwa kwa pamoja kati ya Papa Francis na mtangulizi wake Papa Benedict XVI imeangaliwa na karibu mahujaji milioni moja na wengine mamilioni ya watu kupitia matangazo ya televisheni na redio.

Karibu ujumbe wa wageni 100 wamehudhuria sherehe hiyo, wakiwemo kutoka koo za kifalme na wakuu wa nchi na serikali.

Hii ni mara ya kwanza kwa papa wawili kutangazwa kwa wakati mmoja kuwa watakatifu.

Waandishi wa habari wanasema hatua hii inachukuliwa kama njia ya kuziunganisha kambi mbili za wapenda mageuzi na wasiotaka mabadiliko ya sheria katika Kanisa Katoliki.(P.T)

source: mjengwa blog