WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 2, 2013

Mei Mosi: Wafanyakazi walia na kodi


Mgaya 

Wakati leo Watanzania wakiungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), wadau wa sekta mbalimbali nchini wameitaka Serikali iwapunguzie kiwango cha kodi wanachokatwa (Paye).
Kwa kipindi kirefu sasa, wafanyakazi nchini wamekuwa wakilalamikia kodi kubwa inayotozwa kwenye mishahara na kiwango kidogo cha mshahara wenyewe. Kwa sasa kima cha chini cha mshahara ni Sh180,000 kwa mwezi.
 

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeitaka Serikali kupunguza makato makubwa ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia wafanyakazi kupata kiasi kidogo cha fedha katika mishahara yao na kuishi katika mazingira magumu.
 

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema jana kuwa madai hayo ni ya muda mrefu, lakini hayajawahi kufanyiwa kazi, jambo ambalo limewafanya wafanyakazi wengi kukosa matumaini.
 

Alisema, awali walitoa mapendekezo ya kima cha chini cha mshahara kuwa Sh315,000 lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika na badala yake wamekuwa wakiongezewa kiasi kidogo kisichokidhi mahitaji.Mgaya alisema nyongeza ya mishahara imekuwa ndogo wakati makato ya kodi ni makubwa.

“Bado tunaendelea na malalamiko yetu ya nyongeza ya mishahara na kupunguzwa kwa makato ya kodi kwa sababu Serikali imeshindwa kutekeleza. Tutayawasilisha tena kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kesho (leo),” alisema Mgaya.
 

Alisema nauli zimepanda, lakini wafanyakazi bado wanalipwa mishahara duni, jambo ambalo linawafanya waendelee kuishi kwenye mazingira duni. Mbali na nauli, pia kuna tatizo la kupanda kwa mahitaji ya muhimu kama vyakula na malipo ya huduma za umeme na maji.
 

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally amevitaka vyama vya wafanyakazi nchini kupambana na mfumo badala ya kudai nyongeza ya mishahara pekee.
“Tanzania kuna mfumo wa unyonyaji, ili kuuondoa, vyama vya wafanyakazi vinatakiwa kuungana pamoja na kuwaunganisha wavuja jasho wengine kama mamalishe, madereva wa mabasi na wengineo ili wadai mfumo wa haki,” alisema Bashiru na kuongeza:
 

“Mfumo wetu ni wa kuwaongezea walionacho na kuwapunja wasionacho, wanatakiwa kuwa na mapambano ya muda mrefu ambayo yatawakomboa moja kwa moja, waige vyama vya wafanyakazi vya nchi jirani.”

Alisema hata kama mishahara itaongezwa, haitaweza kuwasaidia kwa sababu ya mfumo mbovu wa sasa uliokosa usimamizi ambao unashindwa kuzuia kupanda kwa gharama nyingine za maisha na hivyo kufanya kila jambo zuri kugeuka msiba kwa Watanzania.
 

Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Gaudance Mpangala alisema tatizo lipo katika mfumo wa uchumi, kwamba pato la Taifa lipo kwa ajili ya watu fulani na si kwa Watanzania wote... “Mfumo wetu ni wa ubepari uchwara na bado unatawaliwa na mabepari. Hata mawazo ya kutawala uchumi wetu yanatoka nje, hapa kwetu tuna tatizo kubwa tumeushindwa ubepari.”
Alisema ili kujinusuru, wafanyakazi wanatakiwa kudai masilahi yao kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho linapungua.
 

“Ufisadi umekuwa kikwazo karibu katika kila sekta, nadhani haya ndiyo mambo ya kupambana nayo na mapambano hayo yatafanikiwa iwapo wafanyakazi watakuwa kitu kimoja,” alisema Profesa Mpangala.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Frank Tily alisema kikwazo kikubwa kwa wafanyakazi nchini kinatokana na uongozi kushindwa kusimamia mambo muhimu hasa uchumi.
 

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hatma ya wafanyakazi ipo mikononi mwao wenyewe na kuwataka kuchukua hatua kama Serikali imeshindwa kutekeleza madai yao.
“Mwaka 2010 wafanyakazi walifanya sherehe zao wao wenyewe bila kuihusisha Serikali kwa sababu ya ahadi hewa, mwaka 2011 na mwaka jana Serikali imetoa ahadi nyingi kwa wafanyakazi, imetekeleza? Wafanyakazi wanatakiwa kuanzia hapo,” alisema.
 

Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema tambo za Serikali kwamba imepiga hatua kiuchumi hazisaidii kwa kuwa maendeleo hayo yameshindwa kusaidia kuondoa umaskini na kuzalisha ajira mpya kama inavyoelezwa.
 

Katika ripoti yake ya Haki za Binadamu ya mwaka 2012 iliyotolewa jana, kituo hicho kimesema kati ya watu milioni 24 wanaochangia nguvukazi ya taifa, asilimia 8.8 hawajaajiriwa huku wengi wao wakiwa ni vijana wa umri wa kati ya miaka 15-24.
 

Ripoti hiyo imesema idadi kubwa ya Watanzania, wasomi na wasiosoma hawana kazi, huku wengi wao wakihangaika kupambana na changamoto za kuhama vijijini kwenda mijini kutafuta kazi.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Patricia Kimelemeta na Goodluck Eliona


source: mwananchi

WOSIA WANGU KAMA IKITOKEA NIMETANGULIA KUFA KABLA YA RUGE AU JOE KUSAGA



Picture

Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, Utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja, Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi
Na bado naendelea ku experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa.

Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha , ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari.

Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki.

Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa.
Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anaeweza ku survive bila wao.

Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria.

Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu.

Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia.
Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, Naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa.

Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao.
Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu.

Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige wame
Enyi mtakaokuwa hai baada yangu.

Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai
Hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu.
Sina haja wanipende pia kwakuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.

Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge.
Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha lakini naona moto ndio unazidi kuwaka.

Na hii ni kwasababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha, Hamuwezi kumiliki dunia..
Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani??. kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba basi beba jiwe liimbe liwe star..

Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie??.
Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu.

Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili.
Mnadhani je! nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi?? nyimbo hazitakuwa nzuri.

Basi sawa ngoja tuone MUNGU ni nani, Binadamu nani??
Kwahiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi??

Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili.

Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu.
Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma??
Roho gani hiyo??

Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu

JIDE




Wednesday, May 1, 2013

Majibu ya Dk Kigwangalla (Mb) kuhusu tuhuma za ufisadi kupitia misamaha ya kodi

 
Taarifa iliyopachikwa hapo chini ni majibu ya habari iliyochapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei Mosi, 2013 ambayo imenukuliwa hapa kwa kichwa cha habari, “Dkt Kigwangallah (Mb) atuhumiwa kufuja misamaha ya kodi,” bofya hapa kuirejea ikiwa hukuisoma.

Mbunge wa Jimbo la Nzega,

Taarifa kwa vyombo vya habari

Bungeni, Dodoma, Mei 1, 2013.

Nawasalimu kwa heshima na taadhima.

Napenda kutumia fursa hii kutoa taarifa kwa wanahabari na umma kwa ujumla kufuatia habari iliyotoka leo mapema asubuhi kwenye gazeti la Sauti ya watu Tanzania Daima, toleo Na.3071 na kuzua mjadala mkubwa na mzito kwenye jamii pamoja na kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na hadhi, heshima na uadilifu wangu kwenye jamii nikiwa kama kiongozi wa umma. Niwape pole wale wote walioguswa na kushughulishwa na jambo hili, haswa familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi wa Nzega; ambao siku zote wanaamini sana katika uadilifu wangu na namna ninavyosimamia misingi ya haki, sheria na uzalendo.

Nimesikitishwa sana na habari  hii hususan kwa kuwa ilichapishwa bila kunipa fursa ya kueleza kwa mapana uhusika wangu. Niwapongeze gazeti la Nipashe kwa kupuuza uzushi huu mara baada ya kunipigia na kueleza upande wangu wa hadithi.

Kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya watu kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari za uongo kwa maslahi maovu ya kuwachafua wanasiasa na watu wengine. Watanzania sote tubadilike na tukatae tabia za kutumika vibaya namna hii, maana ni hatari kwa ustawi wa weledi, na kwa umoja na mshkamano wa kitaifa. Ukishaandika jambo ambalo litamchafua mwenziyo, hata kama utamsafisha kiasi gani ni wazi hautokuwa na uhakika kuwa utawafikia wale wale waliosoma zile za jana za kumchafua – hivyo ni jambo la kawaida kabisa kuanza kwanza kwa kuwa na uhakika kabisa na habari kabla ya kuiandika.

Mfano mwaka 2010 tu mara baada ya kuteuliwa nilizushiwa kashfa ya uongo kabisa inayohusiana na Uraia wangu na gazeti moja maarufu la kila siku na mengine yakaweka kwenye ukurasa wa mbele kabisa kwamba Kigwangalla ni Mrundi; hawakusema ni mrundi wa wapi, toka lini ama kivipi, walisema ni mrundi tu! Basi hata kusema shaka yao inaanzia wapi hawakusema. Kwa kuwa vyombo vya dola vilinisafisha na kupelekea kushinda mapingamizi yote yaliyowekwa na washindani wangu kisiasa, niliamua kudharau na kusema yatapita tu na yatasahaulika.

Pia gazeti lingine likaandika kwamba kampuni ya Kigwangalla ni miongoni mwa makampuni yaliyowahi kufaidika na ‘stimulus package’ baada ya mdororo wa uchumi mwaka 2008. Gazeti hata halikutaja kampuni ya Kigwangalla ni ipi, inaitwaje, Kigwangalla ana hisa kiasi gani, anaendesha kampuni hiyo ama la, na kampuni hiyo imepewa sh ngapi kutoka benki kuu, na je imepewa pesa hizo kwa nyaraka zipi na zenye namba gani? Na je pesa hizo imepewa kihalali ama imepitia mlango wa nyuma? Kama imezipata pesa hizo kinyume na utaratibu, basi kuna ushahidi gani! Kwa kuwa yalikuwa mambo ya uongo na uzushi niliamua kudharau na kuacha kama ilivyo.

Gazeti lingine la kila siku liliwahi tena kuandika ‘Kigwangalla atajwa kufadhili mgomo wa madaktari’ na liliweka hadithi hii kwenye ukurasa wake wa mbele kabisa. Halikusema amefadhili sh ngapi? Amempa nani? Zimeenda kufanya nini fedha hizo? Kwa kuwa lilikuwa ni jambo la uongo, pia nilidharau na kuacha lipite. Mwaka jana Novemba pia gazeti lingine liliandika habari na kuweka picha yangu na ya Ndg. Hussein Bashe, na katikati yetu picha ya bastola, na kusema ‘Kigwangalla na Bashe na vita ya bastola Nzega’, na humo ndani kueleza kuwa Kigwangalla na Bashe wanyoosheana bastola wakati wakirudisha fomu za kugombea ujumbe wa NEC. Na kuna mengine mengi: yale ya rushwa ya vitumbua n.k.

Yote haya kwa ujumla wake yalikuwa ni mambo ya uongo na yasiyo na chembe ya ukweli hata kidogo. Mara zote nimekuwa nikiyadharau na kuongea na wahariri wa vyombo husika vya habari kwa namna inayoashiria urafiki na weledi wa kushirikiana na kufanya kazi pamoja na si vinginevyo; ushauri ambao niliupata mwaka 2009 kutoka kwa moja ya wanasheria wa kampuni yangu (wa kampuni ya Marando, Mnyele & Co. Advocates), wakili nguli Mzee Mabere Nyaucho Marando, ambaye alisema ‘wasamehe tu hawa gazeti la Sauti Huru maana ni vema kujenga marafiki wengi zaidi na media kwa kuwa wewe ni kijana, kuliko kujenga maadui – na niliwasamehe bila gharama yoyote ile’. Mzee Marando hakukosea, ila ukweli ni kwamba ukifanya hivyo utaona patatulia kwa muda na baada ya hapo pataibuka tena jambo lingine la ukurasa wa mbele linaloandikwa bila ukweli wowote ule! Imekuwa wimbo wa kawaida kwenye baadhi ya media houses! Kufanya kazi kwa maslahi ya watu fulani ama chama fulani, misingi ya weledi ya uandishi haipo! Cha muhimu ni maelekezo ama utashi wa anayetoa chochote.

Jambo moja kubwa nililojifunza kutokana na yote haya ni kwamba, jambo likiishaandikwa kwenye media halifutiki kwenye bongo za watu, hata muda ukipita namna gani! Leo hii kila siku haya mambo yamekuwa yakirudiwa rudiwa kwenye mitandao ya kijamii hata baada ya kuyatolea ufafanuzi wa kina. Nimefika mahali nimeona niachane na passive ways za kushughulika na media ili kuweka sawa kumbukumbu zangu mbele ya umma wa watanzania.

Ya ukweli: ni kweli kwamba ninamiliki hisa kwenye kampuni ya Emergent Africa Ltd. Nina hisa 40% na mke wangu Dr. Bayoum Kigwangalla anamiliki hisa 11%. Sijihusishi na kuendesha biashara hii kama mtendaji wa kila siku – kampuni ina watumishi wake sehemu mbalimbali. Ni kweli kwamba kampuni ina mradi wa kujenga chuo cha afya Nzega (International Institute for Health Tabora), eneo la uchama, na ni kweli imepewa orodha ndefu ya vitu ilivyosamehewa kodi na serikali kwa kuwa ni vitu/vifaa vya mtaji (deemed capital goods). Ni kweli kwamba kampuni imewahi kuingiza nchini kontena moja lenye vifaa vichache sana katika vinavyotajwa kwenye habari ile, na vingi kati ya hivyo vipo aidha kwenye stoo ya kampuni iliyopo Nzega ama ya Dar es salaam, Kigamboni. Kwa kuwa vipo, wanahabari wanakaribishwa kwenda kuvitazama vitu hivi kama wanapenda.

Ya uongo: Si kweli kwamba nina hisa 78% na mke wangu Dr. Bayoum Kigwangalla ana hisa 22% - ni uongo. Si kweli kwamba kampuni imeagiza vitu na kuvipitisha bandarini na forodhani kwa msamaha kwa nia ya kuuza na hivyo kuiibia serikali kwa njia ya kukwepa kodi. Si kweli kwamba kampuni ya Emergent Africa Ltd imeingiza vifaa vyote ambavyo imepewa msamaha, kama habari inavyotaka kuwaaminisha waTanzania. Sijawahi kuuza bidhaa zozote zile za kampuni hii zilizoingizwa nchini kwa njia ya msamaha wa kodi. Kampuni ya Emergent Africa Ltd haina mradi wa kuuza tiles na hivyo haijawahi kufanya biashara hiyo.

Ingekuwa ni dhambi kubwa kama kweli ningekuwa naviuza vifaa hivi bila kuvilipia kodi. Na kama ningekuwa sina mradi genuine wa ujenzi wa chuo na labda nimetumia vibaya nafasi yangu ya ubunge kujipatia msamaha ili kurahisisha biashara zangu basi ningeanza kwa kuuza cement (ambayo ni bidhaa inayokimbia sana sokoni na kampuni yangu imepewa msamaha wa karibu tani 5000 – lakini sijawahi kuutumia msamaha huu kununua hata mfuko mmoja wa cement!). Ama ningeingiza mabati/vigae vya kuezekea (ambavyo pia vinakimbia sana sokoni kwa kuwa watu wengi wanajenga – lakini sijaingiza hata kigae kimoja!), ama ningeingiza malori 4, Nissan Navara pick up 4, Mitsubishi Canter 2, Landcruiser Hardtop 4( ambazo zinatumika sana kwenye utalii na hata kwenye barabara za vumbi) kwa msamaha – lakini sijaingiza hata gari moja kati ya haya, kinyume na habari hii ya Tanzania Daima inavyotaka kuuaminisha umma! Kuonesha uadilifu nitaeleza hapa mfano mmoja kwamba mnamo Novemba mwaka jana nilinunua gari moja SUV aina ya Nissan Patrol (T934 CDB) na nimeilipia kodi zote bila msamaha japokuwa ningeweza kutumia msamaha wa kodi kununua na kuingiza moja ya magari yaliyopo kwenye msamaha huu wa kampuni ambayo mimi ni major shareholder. Pia nina ujenzi wa nyumba ya kuishi Nzega, Tabora na Dar es salaam katika hatua mbalimbali: ningeweza kutumia msamaha huu wa kodi wa kampuni yangu ili kujipatia unafuu kwenye manunuzi ya vifaa mbalimbali vya ujenzi kama cement, vigae ama mabati, lakini sijawahi kufanya hivyo hata siku moja!

Kuwa na hisa kwenye kampuni inayofanya biashara halali siyo dhambi. Kupata msamaha wa kodi siyo dhambi. Dhambi ingekuwa kuviuza baada ya kupata msamaha. Kama kuna mtu anaamini kuwa kuna vifaa vimeuzwa na kampuni yangu, kati ya hivi vilivyoingizwa nchini kwa msamaha, anakaribishwa kuleta uthibitisho wa nyaraka za mauzo (cash sale receipts, tax invoice ya mauzo, pay-in slip ya benki ya malipo, delivery note, ama receipt yoyote ile ya kampuni hii inayoashiria kuwa mauzo yamefanyika) ili niweze kufuatilia kujua ni nani aliyeuza na kwa nini alifanya hivyo ili niweze kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumpeleka mbele ya vyombo vya sheria.

Msamaha wa vifaa hivi ni kwa ajili ya Ujenzi wa Chuo Cha Afya Nzega (kitakachoitwa International Institute for Health Tabora), ambacho nilikianza kwa fedha zangu mpaka pale kilipofikia na sasa tunasubiria majibu ya benki ya maombi yetu ya mkopo ndipo tuendelee. Na msamaha huo upo na hautotumika kwa mambo mengine ya binafsi kama nilivyoeleza hapo juu kwenye ununuzi wa gari langu binafsi la kutembelea na ujenzi wa nyumba yangu binafsi ya kuishi Nzega, Tabora ama Dar es salaam (ambako ninajenga).

Watanzania tuache kushabikia uongo. Kufanya hivyo kunaziba mianya ya ukweli kutamalaki. Tuache kutazama mambo kwa macho ya wivu, husda na majungu. Tusimame kwenye misingi ya ukweli daima. Nchi hii itaendelezwa na watu wenye kuchukua maamuzi thabiti na hatua za maksudi za kuleta mabadiliko – kama miradi ya namna hii (ya chuo cha afya Nzega kule!). Nchi yetu bado ina watu waaminifu na waadilifu na tunaamini tutafanikiwa kuwadhibiti walio waovu. Hata siku moja kweli haijawahi kushindwa vita na uongo. Si kila mtu aliyeko kwenye uongozi ndani ya CCM basi ni fisadi, watu wazuri na wasafi wapo pia. Tusimuangalie kila mtu kwa sura ya ‘ufisadi’ na ‘ubadhirifu’ tu! Tuaminiane jamani. Tusifedheheshane na kukatishana tamaa. Safari kuelekea mapinduzi ya maisha ya watanzania kiuchumi na kijamii bado ni ndefu lakini tutafika. Tufanyeni kazi.

Taarifa hii nimeiandika na kuitoa mimi mwenyewe, Hamisi Andrea Kigwangalla, M.D., Mbunge, Jimbo la Nzega. (simu yangu ya kiganjani ni 0782636963 na email yangu ni hkigwangalla@gmail.com, website: www.hamisikigwangalla.com)

MEI MOSI UWANJA WA AMANI ZANZIBAR

Seif-Ali-Iddi 3ce7f
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewataka vijana wa Zanzibar wabadilike na kujenga Utamaduni wa Ujasiriamali na wawe tayari kujiajiri kupitia vyama vya ushirika vya uzalishaji mali pamoja na kuanzishsa SACCOS ili kupata mitaji yenye unafuu.

Balozi Seif ameeleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei mosi) zilizofanyika katika Kiwanja cha Amaan na kuwashirikisha Wafanyakazi wa Mawizara, Maidara na Mashirika ya Serikali pamoja na taasisi binafsi baada ya kuyapokea maadamano ya wafanyakazi hao.

Amesema pamoja na Serikali kuchukua juhudi kubwa ya kupunguza tatizao la ukosefu wa ajira kutoka asilimia saba mwaka 2007 hadi asilimia nne mwaka 2010 bado tatizo la ajira ni changamoto kubwa Zanzibar kama lilivyo nchi nyingi Duniani.

Hata hivyo Makamu wa pili wa Rais ameahidi kwamba Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kupunguza ukosefu wa ajira nchini ili vijana waweze kuishi kwa amani.

"La muhimu vijana wetu waache tabia ya kuchagua kazi. Kazi ni kazi mradi inakupatia riziki yako kwa njia ya halali, " amesisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Ameviagiza Vyama vya Wafanyakazi kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa njia ya kutoa elimu itakayowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira la sekta binafsi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Amesema uzoefu unaonyesha kwamba vijana wengi wamekosa Utamaduni wa kufanyakazi katika sekta binafsi, matokeo yake huacha kazi baada ya kipindi kifupi cha kuajiriwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana kutoka nchi jirani.

Makamu wa pili wa Rais pia amevitaka vyuo vikuu nchini kuangalia mahitaji ya ajira yaliyokuwepo nchini kwa kuandaa mitaala na mafunzo yatakayowasaidia vijana kuajiriwa kwa urahisi.

"Vyuo vyetu vikuu nchini navyo vinanafasi kubwa ya kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuandaa mitaala yao ya kufundishia na mafunzo mengine kwa mujibu wa mahitaji yaliyopo kama vinavyofanya vvyuo vikuu vyengine vingi Duniani, " alifahamisha Makamu wa pili wa Rais.
Blozi Seif amewahakikishia wafanyakazi kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuboresha maslahi yao ili kuhakikisha yanalingana na kazi wanazofanya na kwa upande wao amewataka kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kukuza tija huku wakijua kwamba haki na wajibu ni watoto pacha.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwakilishi wa Shirika la kazi duniani (ILO) Bibi Hopholang Phororo ameishauri Serikali kuendelea kuwajengea wafanyakazi mazingira bora ya kazi ikiwemo kulinda afya na haki zao.

Ameahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kuendelea kuunga mkono katika kusaidia juhudi za Serikali ili kuhakikisha wafanyakazi wako salama wakiwa kazini.
Katibu Mkuu wa ZATUC Maalim Khamis Mwinyi Muhammed ameelezea kuridhishwa na mafanikio makubwa katika awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa karibu sana na Shirikisho hilo na kutekeleza kanuni na sheria za kazi.
Hata hivyo Maalim Khamis ameeleza masikitiko ya wafanyakazi wa Zanzibar kwa kutopandishwa viwango vya mishahara yao mwaka uliopita licha ya uchumi kuelezwa kuwa umekua.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBARMakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewataka vijana wa Zanzibar wabadilike na kujenga Utamaduni wa Ujasiriamali na wawe tayari kujiajiri kupitia vyama vya ushirika vya uzalishaji mali pamoja na kuanzishsa SACCOS ili kupata mitaji yenye unafuu.

Balozi Seif ameeleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei mosi) zilizofanyika katika Kiwanja cha Amaan na kuwashirikisha Wafanyakazi wa Mawizara, Maidara na Mashirika ya Serikali pamoja na taasisi binafsi baada ya kuyapokea maadamano ya wafanyakazi hao.

Amesema pamoja na Serikali kuchukua juhudi kubwa ya kupunguza tatizao la ukosefu wa ajira kutoka asilimia saba mwaka 2007 hadi asilimia nne mwaka 2010 bado tatizo la ajira ni changamoto kubwa Zanzibar kama lilivyo nchi nyingi Duniani.

Hata hivyo Makamu wa pili wa Rais ameahidi kwamba Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kupunguza ukosefu wa ajira nchini ili vijana waweze kuishi kwa amani.

"La muhimu vijana wetu waache tabia ya kuchagua kazi. Kazi ni kazi mradi inakupatia riziki yako kwa njia ya halali, " amesisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Ameviagiza Vyama vya Wafanyakazi kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa njia ya kutoa elimu itakayowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira la sekta binafsi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Amesema uzoefu unaonyesha kwamba vijana wengi wamekosa Utamaduni wa kufanyakazi katika sekta binafsi, matokeo yake huacha kazi baada ya kipindi kifupi cha kuajiriwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana kutoka nchi jirani.

Makamu wa pili wa Rais pia amevitaka vyuo vikuu nchini kuangalia mahitaji ya ajira yaliyokuwepo nchini kwa kuandaa mitaala na mafunzo yatakayowasaidia vijana kuajiriwa kwa urahisi.

"Vyuo vyetu vikuu nchini navyo vinanafasi kubwa ya kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuandaa mitaala yao ya kufundishia na mafunzo mengine kwa mujibu wa mahitaji yaliyopo kama vinavyofanya vvyuo vikuu vyengine vingi Duniani, " alifahamisha Makamu wa pili wa Rais.

Blozi Seif amewahakikishia wafanyakazi kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuboresha maslahi yao ili kuhakikisha yanalingana na kazi wanazofanya na kwa upande wao amewataka kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kukuza tija huku wakijua kwamba haki na wajibu ni watoto pacha.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwakilishi wa Shirika la kazi duniani (ILO) Bibi Hopholang Phororo ameishauri Serikali kuendelea kuwajengea wafanyakazi mazingira bora ya kazi ikiwemo kulinda afya na haki zao.

Ameahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kuendelea kuunga mkono katika kusaidia juhudi za Serikali ili kuhakikisha wafanyakazi wako salama wakiwa kazini.
Katibu Mkuu wa ZATUC Maalim Khamis Mwinyi Muhammed ameelezea kuridhishwa na mafanikio makubwa katika awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa karibu sana na Shirikisho hilo na kutekeleza kanuni na sheria za kazi.
Hata hivyo Maalim Khamis ameeleza masikitiko ya wafanyakazi wa Zanzibar kwa kutopandishwa viwango vya mishahara yao mwaka uliopita licha ya uchumi kuelezwa kuwa umekua.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

Mbunge ‘mpumbavu’ hatapigiwa kura 2015

BAADHI ya raia wa Ethiopia wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia msemo mashuhuri ambao kwa namna fulani umebeba mantiki ya kifalsafa ndani yake.
Wanasema; “When spider webs unite they can entangle a lion.” Kwamba  utando wa buibui unapounganishwa basi huweza kumnasa hata Simba.”
Buibui ni mdudu mdogo na kimsingi, utando wake si imara ikilinganishwa na nguvu za mnyama Simba, lakini bado Waethiopia wanasema utando huo unapotanda vizuri, basi huweza kumnasa huyo Simba. Kwa maana nyingine, unaweza kusema jambo dogo linaweza kusababisha maafa makubwa.
Ni katika muktadha huo huo, tunaweza kuanza kulitazama Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama chombo kinachoashiria au kuthibitisha kupungua kwa kiwango cha kuvumiliana miongoni mwa Watanzania na hata kupungua kwa ustaarabu na staha, miongoni mwa Watanzania. Kwa mfano, tumemsikia bungeni, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi akitamka kuwa Baraza la Mawaziri limejaa wapumbavu!
Si kwamba Mbilinyi ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki wa bongoflava alitamka hayo maneno wakati akiimba mashairi au mistari ya bongo flava la hasha, alizungumza akiwa bungeni katika mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Sugu anajitetea ya kwamba maneno upumbavu si matusi lakini hata kama si matusi, ni lazima kila mahali kuna hadhi ya lugha au matamshi yake. Kwa mfano, lugha inayotumika katika vijiwe vya watumiaji wa dawa za kulevya na mihadarati mingine hata kama si matusi, haiwezi kutumika ndani ya Bunge.
Lugha inayotumika kwenye vijiwe mbalimbali vya mitaani (hata kama si lugha za matusi) nazo zina nafasi yake katika maeneo hayo husika.
Lugha ya kuitana wapumbavu, kwa watu walioko katika ngazi ya uongozi wa kitaifa ni sawa na lugha ya kihuni, na pengine inaakisi kiwango cha hadhi ya mtamkaji wa maneno hayo.
Kwa viongozi wa kitaifa kuitana au kutambulishana mbele ya umma (tena kupitia Bunge linalorushwa hewani moja kwa moja nchi nzima), kama ni wapumbavu (hata kama upumbavu si tusi) ni kuashiria shari. Ni kuashiria kutoweka kwa ustaarabu kati ya viongozi husika.
Katika mfumo wa demokrasia ambao bila shaka vyama vyote vya siasa nchini vinautumikia hata kama si kwa dhati, kura za wananchi ndizo, kwa kawaida, huamua nani aongoze nchi. Na waliopewa mamlaka ya kuongoza nchi, ni lazima waunde serikali. Na kwa hiyo basi, mfumo wa dekomrasia kwa wanaouamini kwa dhati katika mfumo huo hawana budi, hasa katika vyombo vya uwakilishi kama Bunge, kushindanisha hoja zao kwa kuzingatia nguvu za hoja husika na si nguvu ya misamiati ya kukera wengine, misamiati au maneno yanayoashiria shari na kimsingi, yanayoweza kusababisha wadogo wakapuuza kuheshimu wakubwa.
Kwa bahati mbaya, Mbunge Mbilinyi hakuwa tayari kuomba radhi bungeni na hata kufuta kauli yake kwa kuwa tu, neno pumbavu au mpumbavu lipo katika biblia.
Kwa kawaida, madhara ya matumizi ya maneno fulani hutegemea sana mazingira maneno hayo yanapotamkwa na msukumo wa utamkaji wa maneno husika.
Inawezekana, tunao mawaziri ambao hawafanyi kazi yao vizuri na kwa kweli nami nakubaliana na hali hii ya kwamba kuna mawaziri ni mzigo tu kwa nchi, ni kama hawapo na hata ukitathmini utendaji wao wa kazi, huoni mabadiliko yoyote katika sekta wanazosimamia.
Lakini hata kama kuna viongozi wa namna hii, haikuwa sahihi kwa mbunge kuwaita wapumbavu, kwa kuzingatia mazingira ya kibunge.  Pengine, kuwaita hivyo inawezekana katika vijiwe vya kuvutia bangi na kwingineko, lakini kwenye chombo rasmi cha uwakilishi wa umma ni kuvuka mipaka.
Tutafakari, inawezekana kabisa katika maisha yake Joseph Mbilinyi amewahi kushuhudia wazazi wake wakiwa wametenda makosa ya hapa na pale, makubwa au madogo kwa sababu mbalimbali, za msingi au zisizo za msingi. Je, mbunge huyo atakuwa tayari kuwatamkia wazazi wake kuwa ni wapumbavu? Je, anaweza kutamka hivyo kuwa wazazi wake au mzazi wake ni mpumbavu kwa sababu tu neno pumbavu si tusi?
Bila shaka, jibu ni rahisi tu kwamba hawezi kuwatamkia hivyo licha ya udhaifu fulani ambao anaweza akawa ameubaini. Kwa nini hawezi? Hawezi kwa sababu neno hilo ingawa si tusi, lakini halibebi ustaarabu kati ya mwana na wazazi wake.
Tutambue ya kuwa, mawaziri ambao wameitwa wapumbavu ni watu wenye familia zao na miongoni mwao ni wachapakazi ingawa pia wapo ambao ni butu katika utendaji kazi.
Lakini si Joseph Mbilinyi pekee, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia naye alitamka bungeni akimweleza mbunge mwenzake kuwa; yeye (Nkamia) hazungumzi na mbwa bali anazungumza na mwenye mbwa.
Bahati nzuri, Nkamia alitambua makosa yake katika kutamka maneno hayo ndani ya ukumbi wa Bunge, akaomba radhi. Inawezekana kwa mfano, kama mtu fulani akatamka maneno hayo kwenye vijiwe vya kuvuta bangi au maeneo mengine yasiyo ya kistaarabu, asingelazimika kuomba radhi na tena kila mmoja katika eneo hilo asingebaini kama ni tatizo kutamka hivyo.Sasa kwa kuzingatia msemo wa Waethiopia, utando wa buibui unaweza kumnasa Simba na kwa hiyo, kauli zenu hizi wabunge wetu zinaweza kuashiria machungu mbele ya safari zenu za kisiasa na hasa katika majukwaa ya kuomba kura siku zijazo.
Tunaweza kutamka maneno ambayo yanaweza kufurahisha baadhi ya mashabiki wetu lakini gharama zake zinaweza kuwa kubwa zaidi ya furaha hiyo ya muda mfupi kutoka kwa mashabiki.
Tusiitane wapumbavu wala mbwa bungeni, jiulizeni, watoto wenu wanaweza kujifunza nini kutokana na kauli zenu hizo?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

source: Raia Mwema:  Godfrey Dilunga

Dkt Kigwangallah (Mb) atuhumiwa kufuja misamaha ya kodi

 
Picture
Screen-shot kutoka kwenye ukurasa wa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Habari iliyonukuliwa hapo chini kutoka kwenye gazeti la Tanzania Daima imeandikwa na Josephat Isango. Dkt Hamisi Kigwangallah anapatikana Twitter kwa @hkigwangalla

MBUNGE wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla (CCM), anadaiwa kuliibia taifa kwa kutumia vibaya misamaha ya kodi ya mamilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha afya eneo la Uchama, wilaya ya Nzega.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, Dk. Kigwangallah amejipatia misamaha ya kodi ya ongezeko la thamani na ushuru wake kupitia kampuni ya Emergent Africa Limited, anayoimiliki kwa asilimia 78 na Bayoun Kigwangallah ana asilimia 22.

Kupitia kampuni hiyo, mbunge huyo ameingiza nchini bidhaa mbalimbali ambazo badala ya kuzielekeza katika ujenzi, amefungua duka la kuuza vifaa vya ujenzi eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam na nyingine anaziuza kwa wafanyabiashara wengine.

Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa kampuni ya Emergent Africa Ltd, ilisajiliwa katika Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) Septemba 27, 2011 na iliruhusiwa kupata misamaha hiyo kuanzia Septemba 2011 hadi Agosti 2014.

Kwa mujibu wa makubaliano kati ya kampuni ya Emergent Afica Ltd na TIC, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliombwa kuisamehe kodi kampuni hiyo ya Dk. Kigwangallah vitu mbalimbali vyenye orodha toka namba 1 hadi 390.

Bidhaa hizo kwa uchache ni kompyuta 1042, mashine za kutolea kopi 12, printa 12, ‘binding machines’ 12, vikokotozi (calculator) 640, projekta 12, video kamera 12, feni 30, vifaa vya simu masanduku 28, jenereta moja, magari aina ya Toyota 13, lori 3, Nissan Navarra Pik up 4, Mitsubishi Canter 2 na mabasi madogo manane.

Pamoja na msahama huo, Dk. Kigwangallah kupitia kampuni hiyo, aliingiza nchini vitu bidhaa mbalimbali vikiwemo vigae vya sakafuni 2500 vyenye ukubwa wa 600X600 na 1000 vyenye ukubwa wa 400 X 400 pamoja na vigae vya ukutani.

Katika orodha hiyo viko viti na meza za kulia, hema la bustanini, sofa, kabati za kuwekea nguo, mazulia, vitanda na magodoro, televisheni na vingine.

Aidha nyaraka hizo zinaonyesha baada ya kupokea bidhaa hizo kutoka nchini China, ziliuzwa katika maduka mbalimbali ya Kariakoo na vigae vingine kuuzwa kwa mkuu wa wilaya moja mkoani Tanga (hatukumtaja) kwa kuwa hakupatikana kujitetea.

Hata hivyo, kumeonekana utata katika nyakara hizo kwani kampuni ya Delmas iliyosafirisha kontena la bidhaa hizo kuja kwa Dk. Kigwangallah, ziko tofauti na ankara za malipo.

Ankara hizo zinaonyesha kuwa zilitolewa na makampuni ya Louis Valentino Investment and Development Co. Ltd iliyopo Na. 19 Ji Hua 3 Road Foshan na Sharpeye Furniture.

Wakati manunuzi yakionekana kufanyika China Oktoba mosi, 2012, nyaraka nyingine zinaonyesha kuwa mali zilishaingizwa nchini tangu Aprili 14 mwaka huo, kupitia kampuni ya Innovative Freight yenye TIN 100-145-596, risiti namba 2012/0000002986.

Na nyaraka za mamlaka ya mapato zinaonyesha bidhaa hizo ziliingia nchini Aprili 3 mwaka jana, hali inayoonyesha kupishana katika tarehe za kununua na kuingiza bidhaa hizo.

Pia utata huohuo unaonekana katika taarifa za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambazo zinaonyesha bidhaa hizo zilikaguliwa Machi 28, 2012.

Huku kukiwa na orodha zinazotofautiana za makampuni mawili ya kibiashara wakati ankara ya malipo ilikuwa moja.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa kontena hilo lilipofika nchini lilionekana kuwa na vitu tofauti na vile vilivyoorodheshwa, hivyo kusababisha kontena hilo kufanyiwa uchunguzi usio wa kawaida kwa kupekua mzigo mmoja mmoja.

Dk. Kigwangallah alipotafutwa kwa simu kufafanua tuhuma hizo, alisema amebanwa na kazi. Na alipoambiwa ametumiwa maswali kwenye barua pepe yake, aliahadi kujibu lakini hakufanya hivyo.

Alipopigiwa tena jioni, alisema, “Sema haraka unataka nini?” Alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alikata simu.

Lakini baadaye aliandika ujumbe kwa simu: “Nitakupigia jioni nikitoka bungeni.”

Alipoambiwa inaandikwa habari gazetini, alijibu kwa ujumbe mfupi kuwa tuhuma zilikuwa za uongo bila kufafanua.

NITAGOMBEA URAIS MWAKA 2015 IWAPO WANANCHI WENGI WATANIOMBA ---WAZIRI MEMBE

 

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bw ,Benard Membe akiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu mkoa wa Iringa wanaotoka mkoa wa Mtwara na Lindi jana
Waziri Membe

Na Francis Godwin,Iringa
HUKU hali ya mambo ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) kuwa si shwari kutokana na makada wake kuendelea kupigana vikumbo ikiwa ni sehemu ya harakati mbio za urais mwaka 2015 , waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe ameibuka na kutoa ya moyoni kuwa atakuwa tayari kuwania urais mwaka 2015 iwapo wananchi wataona anafaa na watamtaka agombee nafasi hiyo.
Pia waziri Membe alisema kuwa hali ya nchi inavyokwenda kwa sasa si shwari kutokana na baadhi ya wabunge wa CCM na vyama vya upinzani kuendelea kuzungumza ovyo ovyo juu ya chama na serikali jambo ambalo ni hatari zaidi kwa Taifa.
Waziri Membe aliyasema hayo jana wakati akijibu maswali ya mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kuhusu mbio hizo za Urais .
mtandao huu ulifanya mahojiano hayo mjini Iringa baada ya kumalizika kwa kongamano la wana vyuo vya elimu ya juu mkoani Iringa kongamano lililofanyika katika ukumbi wa St. Dominic ambako alikuwa mgeni rasmi waziri Membe alisema kuwa pamoja na kauli yake ya kwanza kwa Taifa kuwa muda bado kufika wa kufanya hivyo .
Waziri huyo alisema kuwa mbali ya kuwa muda wa kutangaza kuwania nafasi hiyo bado haujafika na chama chake kina utaratibu wa kutangaza mara baada ya muda kufika ila kwa mtazamo wake kama alivyopata kuueleza umma awali alipozungumza na vyombo vya habari juu ya mbio hizo za urais ,alisema kuwa anaheshimu sana taratibu za chama .
" Naomba kurudia tena mimi nilishapata kuueleza umma kuwa muda bado haujafika wa kutangaza kugombea Urais ....ila nasema hivi natagemea sana ushauri wa watanzania iwapo wataniona nafaa na kunitaka nigombee nitapima mawazo yao na iwapo ni wananchi wengi watakaoniunga mkono kutaka nigombee basi nitachukua fom na kuijaza ili nigombee nafasi hiyo kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu " alisema waziri Membe
kuwa kama wananchi watasema jaza fom na nikaona ni sauti ya wengi nitajaza fomu ya kuwania kiti cha urais
Pia alisema kuwa hadi sasa hali ya nchi inazidi kwenda vibaya kutokana na kila mtu kuzungumza mambo bila kuthathimini na kuwa mbaya zaidi hata baadhi ya wabunge wa CCM nao wamekuwa si msaada kwa chama kutokana na mambo wanayozungumza dhidi ya serikali na chama.
Kuhusu mwenendo wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sasa waziri Membe alisema kuwa kwa upande wake amepata kukaa bungeni zaidi ya miaka 15 toka bunge la spika Pius Msekwa hadi sasa chini ya spika Anne Makinda ila anachokiona ni baadhi ya wabunge kukosa maadili na kuzungumza mambo bila kuzingatia kanuni za bunge jambo ambalo ni hatari zaidi.
Alisema kuwa bunge linalotazamwa na watanzania ni lazima liwe bunge lenye mfano wa kuigwa na lenye kuzingatia maadili katika kuzungumza ila kwa sasa ndio maana bunge linaendelea kupoteza mwelekeo wake .
"Bunge linapoteza mwelekeo kutokana na mawazo ya baadhi ya wabunge wakifikiri wakisema ovyo na kutumia lugha kali katika kuzungumza basi wao ndio wanaonekana ni wabunge bora kitu ambacho hakipo ....kwani kuwa mbunge ni pamoja na kujiheshimu na kutumia lugha nzuri katika kuwakilisha wapiga kura wako bungeni"
Waziri Membe alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge kutotumia busara katika kujadili mambo bungeni si ubunge mzuri na watambue wazi kuwa wananchi wao wanawatazama na hukumu yao itatolewa mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu kama hivyo wanachokifanya ni kuwawakilisha wananchi ama kujiwakilisha wao.
"Nawaomba wabunge kuwa wazalendo na kuwawakilisha wananchi waliowatuma badala ya kuligeuza bunge kama sehemu ya kuonyesha ujuzi wa kuzungumza ovyo ....nasema tuwaogope wananchi mwaka 2015 watatoa adhabu kwa kila mbunge kwa sasa wananchi wanakusikiliza na kunakutazama ila muda ukifika watakuacha"
Alisema kuwa wabunge wengi ni vijana na wanafikiri kusema vibaya juu ya CCM ndio ubunge bora ila watu watafanya uchunguzi wa kutembelea jimbo la mbunge husika na kuangalia kuwa amefanya nini katika jimbo lake na watakupima kwa kazi uliofanya na sio ukali wako bungeni.
Aidha waziri Membe alisema kuwa baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi katika majimbo yao na pia wamekuwa msaada kwa chama na serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa msaada mkubwa wa kusukuma mbele maendeleo ya Taifa ila baadhi yao wapo kwa ajili ya kuonyesha uwezo wao wa kusema ovyo.