WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, April 6, 2015

UJUMBE WA PASAKA 2015: AMANI YETU ITALINDWAJE TUNAVYOELEKEA KATIKA UCHAGUZI WA TAIFA LETU 2015?




"Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake.  Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa.  Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu."`

 "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?  Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu”.

Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi? Akawajibu, Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo. Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini?  Naye akawaambia, Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.  Nao askari wakamwuliza, "Na sisi tufanye nini?  Naye akawajibu, Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu."

Leo tunavyosherekea siku hii ya Pasaka ujumbe mzito kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa na viongozi wa dini tudumishieni amani yetu; na hii itawezekana kwa kutekeleza kauli ya Yohana Mbatizaji  Toshekeni na masilahi” na kwa viongozi wa dini “Hubirini ukweli na muwe wa kweli; hivi vikitekelezwa vitalijengeeni Taifa letu Amani ya kweli”:

Neno  hili ni zito japo lilizungumzwa kipindi kirefu nyuma lakini tunaendelea kulishuhudia leo tunapowaangalia watendaji wetu katika serikali zetu, ndani ya vyama vya siasa na sasa hata miongoni mwa viongozi wa dini ambao nao wameanza kupenyeza masilahi yao binafsi, na kuanza kuzoofisha amani ya Taifa letu.

Neno hili linatufundisha uadilifu, uwajibikaji kulingana na maadali  na kanuni za kazi ambazo zinatulazimu sisi kama watendaji wa Taifa kuweka mbele matakwa ya Taifa na sio masihahi binafsi;

Najiuliza tena  leo hii hata viongozi wa dini mbona wamekuwa mbele katika kutanguliza masilahi binafsi mbele kuliko mwongozo wa Vitabu vikatifu kwa katika kujenga amani; Je wanafanya hivyo kwa kivuli cha nani? Na  hili linamaana gani kwa taifa letu? 

wananchi wa Taifa hili wanahitajii uhuru wa kiuchumi ambao unatokana na viongozi wetu watangulize mbele masilahi ya Taifa, warizike kidogo wananchokipata; kinyume chake kama hawatarizika na hicho kidogo hawataweza  kuweka mbele masilahi ya taifa na bali watatanguliza mbele vitendo vya  rushwa na ufisadi ambao unarudisha maendeleo ya Taifa nyuma sana na kudhoofisha amani yetu.

Ujumbe wa  Pasaka ya mwaka 2015  itukumbushe sisi  Kama Taifa na kama Raia na watendaji ambao tumekula kiapo cha utii na maadili bora ya uwajibikaji kwa Taifa letu kuwapa wananchi wanyonge zawadi kubwa ya  uhuru  wa kiuchumi,  ili kila mmoja wetu aweze kuyafurahia  zawadi pekee ya rasilimali  ambayo Mungu amelijalia Taifa letu. Hakuna atayepingana nami kuwa  nchi yetu imefurika kwa  asali na maziwa tatizo ni wachache tu ambao wanafaidi kwa kutoridhika na mishahara yao. 

kwa kipindi kirefu tumeona kuwa nchi yetu  Tanzania iliyokuwa ikifurika neema  ya rasilimali sasa imegeuka; kuwa nchi inayofurika machungu; matendo yaleyale ya kifisadi, ya ukandamizaji, ya unyanyasaji ambao  Farao aliwatendea wana wa Israeli huko misri miaka hiyo; lakini kwa kuangalia falsafa hiyo ya matendo ya Farao ndio tunaishuhudia sasa namna watendaji wetu walikokabidhiwa dhamana ndani ya Taifa letu  ambao sio waadilifu wananyo haribu nchi, na kuacha machingu kwa wananchi ambao bado wako kwenye dimbwi la umasikini.

je viongozi wetu wa dini leo hii wanahubiri amani ambayo Yohane Mbatizaji aliifafafanua kulingana na makundi yaliyokusanyika?
Je viongozi wa dini wanahubiri amani au wanaendeleza chuki moingoni mwa wananchi wa Taifa letu?

Kulingana na Yohane matajiri wanaotakiwa kuangalia haki ya maskini, "Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo."(Lk 3,11), kwa watoza ushuru waepuke rushwa na matendo ya kifisadi "Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa."(Lk 3,13) na kwa maaskari wazingatie haki "Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu."(Lk 3,14).

Leo hii ndani ya Taifa vitendo hivi vimeshamiri tena kwa kiasi kikubwa; na pengine kila mmoja ameshiriki kwa namna moja au nyingine katika uovu huu. Hii inaweza kuwa moja kwa moja au kwa kutokuwajibika ipasavyo katika eneo lake la kazi na hivyo kusababisha mianya katika kukua kwa matendo haya maovu. Wito wakati tunasherekea Pasaka 2015 sisi kama Taifa inatupasa tubadilike na kuhakikisha haki na upendo vinashamiri katika jamii yetu.

Kama tutafanikiwa kuishi kwa ujumbe huu wa Yohani Mbatizaji kuwa tutosheke ni mishahara yetu mimi naamini kuwa tukiweka mbele maslahi ya nchi, nchi itasonga mbele. TUKUMBUKE KAULI YA YOHANA MBATIZAJI KWA WALE ASKARI kuhusu dhuluma:
TOSHEKENI NA MISHAHARA YENU, watu wana madaraka makubwa mishahara mikubwa na masurufu manono lakini bado wanaiibia nchi. Kwa nini lakini? Hii choyo ulafi kwa nini?

Nafikiri Tatizo la wanasiasa na Viongozi wa dini wakishafanikiwa kujikwamua kimasilahi wanasahau kuwa wananchi bado ni masikini na wanahitaji masaada ili nao waweze kufarahia zawadi ya maisha ambayo wamezawadiwa na Mwenyezi Mungu.

Amani kwao sio wimbo ulio bora tena kwao, maisha bora ya wananchi wao inabaki katika slogan tu.

Wanatumia muda mwingi kutukanana na kuonyeshana ufahari wao, ambao wamepata kwa kuendelea kuwakamua hawa wanachi masikini.

Je watendaji wetu wako tayari kutoa hesabu za utendaji wao siku watakapotakiwa na Mwenyezi Mungu tukiamini kuwa kazi zote hutoka kwa Mungu?

Nafiki Pasaka hii kujifunze kitu kingine kipya kuwa “Jihadharini na tabia ya kupenda fedha, na “toshekeni na mlivyonavyo” kwa sababu Mungu mwenyewe alisema,

“Kwa vyo vyote sitakupungukia kabisa, wala sitakutelekeza na kukuacha bila msaada. Kamwe, kamwe, sitakuacha hata kwa kiwango kidogo, kukuacha bila msaada, au kukuacha, au kukuangusha, au kulegeza mkono wangu kwako. Hakika sitafanya hivyo! Kwahiyo tunafarijika na kutiwa moyo, na kwa uhakika na ujasiri twathubutu kusema, ‘Bwana ndiye anisaidiaye” (Ebr 13:5, 6)

Kwa kutosheka na mishahara yetu na kwa kuamini kuwa sisi ni wachache ambao tumechaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa saidia wengine ili waweze kupata ridhiki zao; au kufurahia asali na maziwa kwa vipaji vyetu kwa kutimiza wajibu wetu tutakuwa tunatekeleza ujumbe huu wa “Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na hivi vitu vingine vyote mtapewa kwa maelefu.

Tukitenda kila kitu kwa haki kamwe hatutakosa chochote unachohitaji kitakuwa ziada. Mwenyezi Mungu atakupa namna ya kupata kila uchokihitaji zaidi.

Imani yangu ni kama ile ya Paulo kama tutatosheka ni mishahara yetu,na kuwajali wanyonge katika Kupata Riziki
zao, “Na Mungu wangu atawajazeni na kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu wake …”. Lakini hili litawezekana kama viongozi wetu wa serikali, vyama vya siasa na wale wa dini watafanya kazi zao kulingana na na viapo vya kazi zao.

"Mungu hatakosa KUWAONGEZEA wale wote wanaoifanya kazi yake sawasawa na mapenzi yake" huu ndio ujumbe wa Pasaka 2015

Sunday, April 5, 2015

Neno La Leo: Naye Yesu Akasema; " Simoni, Acha Kuvua Samaki.."

2_7ea4d.jpg

Ndugu Zangu,
Bwana Yesu alipotembelea mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, Simoni alikuwa ni miongoni mwa wavuvi hao. Yesu akasema; " Simoni, acha kuvua samaki,nifuate ukawe mvuvi wa watu.

Naam, watu wengi wanaangamia kwa kukosa uelewa. Kwa kutojitambua. Wanahitaji ukombozi wa kifikra. Na siku zote, haki uinua taifa, vivyo hivyo, dhulma huangamiza taifa. Na mahala pasipo na haki, basi, hapo hapatukuwa na amani.

Oneni, maovu yametamalaki katika dunia tunamoishi. Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu.
Siku zote, hamu inakuwa ni jambo jema, endapo binadamu ataweza kuitawala hamu/tamaa yake.Wanadamu tusipoitawala hamu yetu, tukaanza kujipendelea, kuwasahau wengine, basi, hilo huwa ndio chimbuko la maovu.
 

Hupelekea kutoelewana baina ya wanandugu, na hata kwa marafiki walioshibana. Hupelekea vurugu na machafuko katika jamii. Tunazungumzia uwepo wa upendo, haki na usawa.

Dini za kweli hapa duniani zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo.
 

" Naapa kwa zama . Hakika binadamu wote wamo katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya matendo mema. Wakahusiana na haki na wakahusiana na subira" (Koran tukufu, Surat ASWR)
Biblia nayo inasema; kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno, akamwua nduguye. Mfalme Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda alijipendelea mno, akakubali kumsaliti Yesu kwa Vipande Thelathini vya Fedha. Hatimaye, akamsaliti Yesu.
 

Na ufufuko wa Bwana Yesu utukumbushe jukumu letu la kupambana na maovu katika jamii. Utukumbushe jukumu la kusaidia kazi ya kuwakomboa kifikra wanadamu wenzetu.

Kama vile Bwana Yesu alivyomkumbusha Simoni kwa kumwambia; " Simoni, acha kuvua samaki. E nenda ukawe mvuvi wa watu.
Ni Neno la Leo.
Pasaka Njema.
 

Maggid,
Iringa.


source: mjengwa blog

Tukitafakari Ya Garissa, Hii Ndio Tanzania Tunayoitaka..


1_f67c8.jpg

Ndugu zangu,
Kwenye moja ya picha za magazetini leo, kuna hii inayomwonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi akimpa pole Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mazishi ya baba mzazi wa mkewe, Marehemu Mzee Abdallah Rehani yaliyofanyika kwenye makaburi ya Segerea jijini Dar es salaam,Aprili4, 2015.
Kwa hakika, hii ndio Tanzania tunayoijua. Kwamba Watanzania ni ndugu na tumechanganyika. Hata hivyo, Wahenga walisema; " Kamba hukatikia pabovu.
Siku zote, uzoefu ni mwalimu mzuri sana. Mathalan, uzoefu unatufundisha, kuwa kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana.
Ona, moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.
Jumapili hii ya leo ningependa sana tuyakumbuke maneno ya busara na hekima nyingi kutoka kwa Bi. Joy Mukanyange. Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa Rwanda nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka maneno haya miaka 16 iliyopita, takribani miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa Taifa. Bi. Joy Mukanyange ( Pichani juu) alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. Ni kama vile alikuwa mtabiri, maana, alichokisema mama yule leo ndio tunaanza kukiona. Siku ile ya Aprili 6, 1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro Hotel, Bi Joy Mukanyanga aliyatamka haya;
" Naogopa, kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha maauji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994." Alisema Balozi yule wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha mauaji yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao. Ndio, Bi Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona.
Na tutafanya makosa makubwa, kama hata sasa, tutajifanya kuwa hatukioni kile ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona . Kwamba hatukioni pia kile kilichotokea westgate na garissa.
Watanzania tukubali sasa kuwa tumepatwa na bahati mbaya sana ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini. Tunayashuhudia yakifanywa na baadhi ya viongozi wa kidini, makanisani na misikitini. Ni hao, ambao sasa wameamua kuchanganya dini na siasa huku waumini wao wakiwa ni wafuasi wa vyama tofauti tofauti vya kisiasa.
Hili ni jambo la hatari sana.
Ni hulka ya mwanadamu, anapokuwa matatizoni kumtafuta kondoo wa kafara. Mtu mwingine wa kummyooshea kidole kwa matatizo yake. Hali duni ya uchumi wa nchi, hali duni za maisha na umasikini wa watu wetu isiwe chachu ya kuanzisha vurugu za kijamii kwa kuegemea kwenye mitazamo ya kidini.
Maana, taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao, kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwapo na WAO.
Hatari kubwa ninayoiona ni tatizo la wengi wetu kuwa na ufahamu mdogo juu ya dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi, ufahamu mdogo wa historia yetu. Hivyo basi, kupelekea hali ya kutojitambua kama taifa. Ndio, uelewa wa historia ya jamii husika ni jambo muhimu sana. Kiumbe huwezi kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama huelewi ya jana. Kuielewa historia yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda. Historia ni kama maji ya mto, kamwe haijirudii. Historia ni wakati, ni muda. Kihistoria jana ni sawa na zamani.
Karne nyingi zilizopita wahenga wetu walitafsiri muda kama mkusanyiko wa matukio ya zamani na sasa. Waliamini kuwa yaliyotokea zamani na yanayotokea sasa ndiyo yenye kusaidia kubashiri yatakayotea kesho, yataamua mustakabali wetu.
Dalili tunazoziona sasa za kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini na maeneo tunakotoka si dalili njema. Haya yatatupelekea kwenye maafa. Tuliopata bahati ya kutumia kalamu zetu hatuna budi kuliweka hili hadharani.
Hii ni nchi yetu. Ni Nchi yetu sote. Katika ulimwengu tunamoishi kuna mamilioni ya watu ambao hawana nchi. Wahenga wetu walishiriki katika kuijenga nchi hii, wametutarajia sisi tuendelee kuijenga na kuilinda heshima na hadhi ya nchi yetu.
Mengine yanayofanyika sasa sio tu yanaitia doa nchi yetu, bali, yanaiaibisha nchi yetu. Hatukupata kufikiri, kuwa atatokea anayejiita kiongozi kwa kiimani, akasimama hadharani na kumtukana kiongozi mwingine wa kiimani. yanatokea sasa, na tusiyaone ni ya kawaida. Tuyakemee kwa nguvu zote.
Watanzania hatuna haja wala sababu za kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini na rangi. Sisi wote ni Watanzania. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe. Kinyume na baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri, historia yetu haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza. Historia yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz.
Na dini hizi za kimapokeo zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta dini zetu za asili, na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii matambiko. Afrika kila ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia Waafrika wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za matambiko yao.
Na sisi ni Waafrika. Hii leo mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo.
Naam; kamba hukatikia pabovu, wanasema wahenga.Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania. Tusifike mahali tukagombana kutokana na tofauti za imani ama dini ambazo wala si za asili yetu. Imani au dini ambazo, kama ilivyo dini zetu za asili, nazo zinatutaka wanadamu tuishi kwa amani, upendo na maelewano.
 
Maggid Mjengwa,
Iringa
 
source: mjengwa blog