Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema atawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotoa maneno ya kashfa dhidi yake.
Alitoa kauli hiyo jana katika kongamano liloandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika maadhimisho ya miaka minne tangu alipoingia madarakani.
Alisema amekuwa akisikiliza hotuba nyingi zinazotolewa katika majukwaa na nje ya majukwaa zinazotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani zenye maneno ya kashfa, matusi na kejeli dhidi yake.
“Tuheshimiane, tusitukanane, tusipeane majina yaliokuwa hayana maana na nawaambia viongozi wa vyama vya siasa na serikali na nawajua viongozi wote wanaofanya hivyo na nitawachukulia hatua za kisheria,” alisema.
Alisema haendeshi nchi kiubabe kama wanavyoeleza Chama cha Wananchi (CUF) wakati Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, anapokuw kwenye majukwaa ya kisiasa.
Alisema kila mmoja ana haki ya kuzungumz kwa mujibu wa katiba ya nchi, lakini lazima kuwepo na heshima na kuwataka viongozi kuacha kutukanana na kupeana majina ya kashfa.
Kuhusu mafanikio katika uongozi wake, alisema jambo ambalo anajivunia ni kuimarisha hali ya amani na utulivu wa nchi.
Alisema atahakikisha Zanzibar inabaki salama na suala la amani na maendeleo halina mbadala, hivyo atahakikisha amani inadumu kwani bila ya amani hata ibada hazitafanyika.
Alisema wengi walidhani atakwazwa na hataweza kuiongoza Zanzibar, lakini ameweza na kwa mafanikio makubwa na kuleta maendeleo, hivyo anajivunia hilo.
“Wapo walotubeza kusema kuwa mipango yetu haitekelezeki ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi na wapo walopiga kelele kuwa nimeunda serikali kubwa kwa sababu ya wingi wa wizara, niwaambie kuwa wingi wa wizara siyo serikali, ” alisema Dk. Shein.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment