Demokrasia ina miiko yake. Miongoni mwa miiko hiyo inayopaswa kuheshimiwa katika jamii yoyote inayojitambulisha kuwa ni ya kidemokrasia ni pamoja na uvumilivu wa kusikiliza hoja za wengine hata kama hazifurahishi.
Kwamba, kila mtu katika jamii anapewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusiana na jambo fulani huku wengine wakisikiliza na kuwa na uhuru wa kukubaliana na hoja husika au kuipinga kwa hoja nyingine madhubuti. Na imethibitika katika maeneo mengi kuwa jamii inayoheshimu mwiko huu hujikuta ikifanikiwa kwa kiwango cha juu.
Watu wake huendelea kuwa huru na maamuzi mengi hufanyika kutokana na uzito wa hoja. Wala si kichume chake.
Aidha, jamii yenye kuzingatia kigezo hiki cha demokrasia hufaidi pia matunda ya kushamiri kwa upendo. Chuki huwa ni msamiati mgumu kwa watu wa jamii hii. Matumizi ya nguvu au hila za namna yoyote ile hukosa nafasi.
Bali, watu hushindana katika kufikiri. Hoja zenye mashiko ndizo hupata uungwaji mkono zaidi. Kwa kiasi kikubwa, taifa letu limekuwa likijitahidi kufikia kiwango hiki cha demokrasia.
Watu huvumiliana katika kusikiliza na kutoa hoja. Hukubaliana katika kutofautiana kwao.Hata hivyo, kile kilichotokea juzi wakati wa kongamano la kujadili mambo ya msingi ya kuangaliwa katika katiba inayopendekezwa hakiashirii kuwapo kwa ustaarabu wa kuvumiliana miongoni mwa baadhi ya watu.
Hiyo ni baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba kufanyiwa vurugu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na wazungumzaji wakuu wakiwa ni waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Cha kusikitisha, katika kile kilichoonekana wazi kuwa bado kuna safari ndefu ya kuelekea kilele cha demokrasia, baadhi ya vijana walianza kufanya vurugu wakati Jaji Warioba alipokuwa akizungumza. Walionekana wakiwa na mabango yenye ujumbe uliokuwa na maudhui yanayofanana. Cha kushangaza, hati iliyotumika kuandikia mabango hayo ilionekana pia kufanana kwa kiasi kikubwa, kama ilivyokuwa kwa aina ya mabango yenyewe na hata wino mzito uliotumika.
Yote hayo yaliashiria kwamba vijana waliomfanyia fujo Warioba walikuwa na ajenda iliyofanana, wakitekeleza kazi waliyotumwa na mtu mmoja au kikundi fulani cha watu.
Hakika, watu hao walionekana wazi kwamba walitumwa kwa nia ya kumziba mdomo Warioba, wakiamini kuwa hiyo ndiyo njia nzuri ya kuhakikisha kuwa maoni ya Waziri Mkuu huyo mstaafu hayawafikii maelfu ya Watanzania waliokuwa wakifuatilia mdahalo huo kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.
Muda mfupi baada ya kuibuka kwa vurugu hizo, polisi walifika katika eneo la tukio na kufyatua mabomu kadhaa ya machozi. Waliotekeleza mpango huu wakahisi kuwa wamefanikiwa. Ni kwa sababu baada ya hapo hakukuwa tena na mdahalo. Vurugu zao zikafanikiwa kusitisha utoaji maoni zaidi kuhusu katiba mpya.
Sisi tunaona kuwa hili siyo jambo jema. Kamwe, haikubaliki hata kidogo kwa kikundi fulani cha watu kufanya vurugu kwa nia ya kuzuia maoni ya wengine kusikika.
Ikumbukwe kuwa, mbali na Warioba kutumia uhuru wake kidemokrasia katika kutoa maoni yake kuhusiana na masuala ya katiba inayopendekezwa, vilevile ana historia isiyofutika nchini. Amewahi kushika nafasi mbalimbali za juu za uongozi zikiwamo za kuwa Mwanasheria Mkuu na pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa kuzingatia ukweli huo, sisi tunaona kuna kila sababu kwa Watanzania wote kulaani matukio ya aina hii. Daima demokrasia idumishwe kwa kuruhusu kila mmjoja kutoa mawazo yake, alimradi hatukani wala kuvunja sheria za nchi.
Aidha, upo umuhimu pia wa kuhakikisha kwamba viongozi wastaafu kama Warioba wanapewa ulinzi madhubuti na yeyote anayejaribu kuwafanyia vurugu anafikiwa kirahisi na mkono wa sheria. Hili ni muhimu kwani litatoa fundisho kwa wengine wenye kufikiria mipango haramu kama huu wa juzi wa kumfanyia vurugu Warioba.
Vurugu ni ishara mbaya kwa demokrasia. Kwa sababu hiyo, hazipaswi kuachwa hivi hivi. Bali, Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake na kuwabaini wote waliopanga vurugu dhidi ya Warioba juzi na kisha kuwafikisha mahakamani ili wakapate wanachostahili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment