WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, September 1, 2014

Uraia pacha utahatarisha usalama wa taifa

 
Maoni ya Katuni
Moja ya mijadala ambayo imevuta hisia za wajumbe wengi wa Bunge la Katiba wiki hii ilikuwa namna ya kuridhia au kukataa suala la uraia pacha kuingizwa ndani ya Katiba.

Wananchi wengi waliangalia faida na hasara za kuruhusu aina ya uraia huo, ambapo wajumbe wengi walionyesha kuwa na hofu katika maeneo mawili ambayo ni usalama wa taifa na uzalendo.

Katika semina iliyoandaliwa kwa wajumbe wa bunge hilo, na mada kutolewa na Kamishna wa Udhibiti na Mipaka wa Idara ya Uhamiaji, Abdallah Khamis Abdallah, imedhirisha kuwa hasara ni nyingi zaidi kuliko faida endapo uraia pacha utaruhusiwa katika mfumo wa nchi yetu.

Wajumbe hao walieleza kuwa Watanzania wengi waliondoka nchini kwa sababu ya kufuata elimu, biashara pamoja na ajira, wakasema viapo vilivyowafanya wawe watiifu kwa nchi walizopata uraia ni pamoja na kuikana nchi yao na baadhi kuikashifu kwa matusi mbalimbali. Kwa mantiki hiyo, watu wa aina hiyo hawafai tena kurejea na kuishi Tanzania.

Moja ya faida iliyotajwa na Idara ya Uhamiaji kuhusiana na Uraia pacha ni za kiuchumi pekee.

Zilizobaki nyingi ni hasara, ikiwamo kushuka kwa kiwango cha uzalendo pamoja na kuhatarisha usalama wa taifa, jambo ambalo pia linaweza kuhatarisha mahusiano ya kidiplomasia ya Tanzania na nchi iliyotoa uraia.

Kwa mwananchi yeyote anayeamua kula kiapo cha kuwa raia wa nchi yoyote, tafsiri yake ni kuikana nchi yake na kushawishi nchi husika ili iamini sababu za mwananchi huyo kupewa uraia wa nchi nyingine. Wakati mwingine sababu za maombi ya uraia huambatana na maelezo binafsi ya kashfa na kejeli kwa nchi ya uzawa.

Tunaamini kuwa serikali iko makini sana katika suala hili la Uraia pacha maarufu kama 'Diaspora', na kwamba itaangalia zaidi masuala ya kiusalama, na ndiyo maana imekiriwazi kuwa endapo azma ya kuwa na uraia pacha itaruhusiwa nchini, athari zake kubwa zitahusu usalama wa taifa.

Suala hilo, ambalo lipo katika Sura ya tano ya Rasimu ya Katiba inayohusu Uraia katika Jamhuri ya Muungano, lilileta mvutano mkubwa na kusababisha Bunge hilo kualika viongozi wa Idara ya Uhamiaji ili kulitolea ufafanuzi wa kitaalam kuhusu faida na hasara zake kwa nchi endapo Diaspora itaruhusiwa.

Viongozi wa Uhamiaji walitaja sababu kubwa mbili za kukataa uraia pacha kuwa ni Usalama wa Taifa pamoja na Uzalendo, ambapo kwa upande wa Usalama walisema mtu anapokuwa na uraia wa nchi mbili, anaweza kufanya tukio linaloweza kuhatarisha usalama wa nchi na kukimbilia nchi ambako ana uraia mwingine.

Kuhusu kumomonyoka kwa Uzalendo, wasemaji wa Uhamiaji walisema uraia pacha unaweza kuwahamasisha wananchi wengi wakaamua kwenda kuomba uraia wa nchi nyingine na kuukana u-tanzania.

Ni kweli kuwa athari zilizotajwa kama uraia pacha utakubalika, zitawagusa wananchi ambao kwa nyakati mbalimbali waliamua kuondoka nchini kutokana na kuchukizwa na matukio mbalimbali yakiwamo ya upinzani wa serikali.

Huko Zanzibar wananchi waliokuwa wakipinga serikali wakati wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 walikimbilia nje, na kwa upande wa Tanzania Bara watu wengi walikimbia wakati wa sera za uhujumu uchumi.

Ikitokea kuwaruhusu hao kurudi nchini, waliohusika na moja kati ya masuala hayo, watajenga vitu vitatakavyoleta chokochoko nchini, kwani ni dhahiri kuwa kama kuna watu walitaifishiwa mali zao, wakirejeshewa uraia wa Tanzania watakuja kudai mali zao na wengine wakiwa na dhamira ya kulipiza kisasi.

Zipo sababu za msingi za kuingia hofu ya kulikubali suala la uraia pacha, hasara zake zimeonekana kugusa taifa zima, na kwa namna mazingira ya usalama katika kanda hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yanavyoathirika kutokana na wimbi la makundi ya ugaidi, ni sahihi kwa serikali kuwa na kigugumizi cha kuruhusu Uraia pacha.

Tunaamini mazingira yaliyopo ni salama, tunaona hatari kubwa mbele yetu kama tusipodhibiti uingiaji nchini na utokaji wa makundi ya watu kwa kigezo cha Uraia pacha, tunaweza tukajitengenezea maadui wakubwa watakaoathiri usalama na ustawi wa wananchi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment