WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, September 23, 2014

Maximo awaomba radhi Yanga

Kocha Mkuu wa Yanga,Mbrazil Marcio Maximo

Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo ameawaomba radhi wanachama na mashabiki wa Yanga baada ya timu yake kuanza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kikianza na wachezaji wanne wa kimataifa, Wanyaruanda Haruna Nyinzoma na Mbuyu Twite, Mganda Hamis Kizza na Mbrazil Genilson Santos Santana ‘Jaja’, Kikosi cha Yanga kilijikuta kikikubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya timu isiyo na mchezaji hata mmoja wa kimataifa, Mtibwa Sugar katika mechi yao ya kwanza ya VPL msimu huu iliyopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Maximo, kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars) amelazimika kuwaomba radhi Wanajangwani kutokana na kipigo hicho huku akiahidi kufanya vizuri katika mechi zinazofuata.

“Maximo anawaomba radhi wapenzi, mashabiki na wanachama wa Young Africans (Yanga) waliojitokeza kwa wingi mjini Morogoro kushangilia timu yao kwa matokeo mabaya ya kupoteza mchezo wa kwanza.

Ameahidi kuhakikisha kuwa timu inajipanga vizuri ili kupata pointi zote tatu katika mechi inayofuata,” inasomeka sehemu ya taarifa ya uongozi wa Yanga iliyowekwa kwenye mtandao wa klabu hiyo.

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa Maximo amesema amekubaliana na matokeo, lakini hakuridhishwa na maamuzi ya marefa wa mechi hiyo.

Lakini, Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haziruhusu makocha kutoa maoni kuhusu uchezeshaji wa marefa wa mechi husika.

Mabao ya Mtibwa katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa mshambuliaji mpya wa Yanga kutoka Brazil Jaja akikosa penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili, yalifungwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi na Ame Ali aliyekuwa mwiba mkali kwa Yanga siku hiyo.

Kipigo hicho ni mwendelezo wa ‘uteja wa Yanga kwa Mtibwa’ kwani Yanga haijawahi kuwafunga mabingwa hao wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara kwenye uwanja huo tangu Septemba 19, 2009 Wanajangwani waliposhinda 2-1, mabao yakifungwa na Mrisho Ngasa na Nurdin Bakari.

Kikosi cha Yanga, ambacho kinatiwa nguvu na kupona kwa kiungo mpya kutoka Brazil Andrey Coutinho, kinaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi inayofuata.

Mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara, watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili wakati Kagera Sugar watakuwa wageni wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam siku hiyo.

Jumamosi vinara wa msimamo wa ligi hiyo kwa sasa, Ndanda FC watavaana na wababe wa Yanga, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani, Kilometa 100 kutoka mjini Morogoro wakati Simba watashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa kuwakabili Polisi Morogoro walioanza kwa kipigo cha 3-1 dhidi ya Azam FC.

Mechi nyingine za Jumamosi zitawakutanisha mabingwa watetezi, Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam, Stand United walioanza kwa kipigo cha 4-1 dhidi ya Ndanda FC watasafiri kutoka mjini Shinyanga hadi jijini Tanga kuwavaa Mgambo Shooting walioanza kwa kuichapa Kagera Sugar 1-0.

Mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union ambao juzi waliishika Simba katika sare ya mabao mawili, watakuwa wageni wa kikosi cha kocha Juma Mwambusi cha Mbeya City kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment