SATURDAY, OCTOBER 6, 2012
Siku za hivi karibuni kumekuwa na
zogo kubwa Tanzania kutokana na wanafunzi kushindwa mtihani wa dini yao.
Sikufuatilia vizuri undani wa kisa hicho na siwezi kukiongelea. Badala yake, napenda
tu kuongelea suala la kinadharia la mtu kushindwa mtihani kuhusu dini yake.
Tunapokuwa kanisani au msikitini,
kwenye mihadhara ya dini au madrassa ya dini, tunafundishwa dini yetu kwa maana
ya kwamba tunaelekezwa tuelewe dini inasema nini ili tuwe waumini bora. Suala
ni kutujenga kiimani na kimaisha kwa mujibu wa dini yetu, kutokana na yale
anayofundisha padri, imam au sheikh.
Mambo ni tofauti tunapokuwa shuleni au chuoni.
Mimi ni mwalimu, na ingawa sifundishi dini, napenda kusema kuwa darasani hatufundishi
kwa lengo la kujenga imani ya watu kwenye dini yao. Labda kabla sijaenda mbali,
nifafanue kuwa naongelea kiwango cha chuo. Kwenye madarasa ya mwanzo, ambako
tunawafundisha watoto, naamini tunategemewa kuwafundisha dini kwa lengo la
kuwafanya wawe waumini bora.
Lakini, lengo langu hapa ni kuongelea
ufundishaji wa dini vyuoni. Kwenye chuo, kazi yetu ni kutafakari na kuchambua
dini, kuhoji na kudadisi. Tunawajibika kutafakari historia ya dini husika,
mafundisho yake, mwelekeo wake, athari zake katika jamii na kadhalika.
Chuoni tunapaswa sio tu kusoma na
kuongelea yaliyomo katika misahafu na yaliyosemwa na watetezi wa dini husika,
bali tunapaswa pia kusoma na kutafakari yaliyosemwa na wapinzani wa dini. Kwa
mfano, ni wajibu kutafakari kauli kama zile za Karl Marx kwamba dini ni kama
bangi ya jamii yenye matatizo. Darasani tunapaswa kujadili kauli za aina hiyo
kwa makini, na kila mwanafunzi anawajibika kutumia akili yake ili kujenga hoja
zake.
Kwa hivyo, hata kama mtu ni muumini
bora wa dini yako, mtu ambaye umeelewa na kukubali kila kinachosemwa kanisani
au msikitini, ukija kwenye mtihani unaweza kufeli. Kwa msingi huo huo, kwa vile
darasani ni mahali pa kuchambua na kutafakari masuala, kama mtihani ni wa dini
ya u-Islam, muislam anaweza kufeli na m-Kristu akafaulu. Vile vile, kwenye
mtihani wa dini ya u-Kristu, mu-Islam anaweza akafaulu na m-Kristu akafeli.
Napenda kutoa mfano ambao unaweza
kufafanua hoja yangu. Nakumbuka tulipokuwa shuleni, mkoani Ruvuma, mbali kabisa
na pwani, tulikuwa tunajiamini kwamba pamoja na kuwa ki-Swahili si lugha yetu
ya kwanza, tuna uwezo wa kufaulu mitihani ya ki-Swahili kuliko vijana wa pwani
ambako ki-Swahili ni lugha yao ya kwanza. Kama nakumbuka vizuri, matokeo ya
mitihani yalidhihirisha jambo hilo, nasi tukawa tunawacheka vijana wa pwani.
Basi, katika mitihani ya dini mambo
ni hayo hayo. Watu tusijiaminishe kuwa kwa vile sisi ni waumini wa dini fulani,
basi ni lazima tufaulu mtihani wa dini hiyo. Ukweli ni kuwa kwa vile shuleni au
chuoni somo la dini linakuwa katika mkabala wa ki-taaluma, hata mtu asiye na
dini anaweza kufaulu mtihani wa dini na sisi waumini tukafeli.
source: Prof Joseph Mbele hapa kwetu blog
Lo, kumbe ulivutiwa kwa namna moja au nyingine na hiki kijimakala changu. Shukrani kwa kukisambaza.
ReplyDeleteni kazi nzuri ambayo inatufundisha na kutukumbusha hali halisi ambayo wakati mwingine tunajaribu kuikataa kwa nguvu zote asante kwa kazi nzuri.
ReplyDeleteni kazi nzuri ambayo inatufundisha na kutukumbusha hali halisi ambayo wakati mwingine tunajaribu kuikataa kwa nguvu zote asante kwa kazi nzuri.
ReplyDelete