WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, October 12, 2012

RPC Iringa azigeuka kamati


Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda
Waandishi Wetu
SIKU moja  baada ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wa mauaji ya Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi aliyeuawa katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa, Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda amebeza ripoti hiyo na kusema ni maoni yanayoweza kutolewa na mtu yeyote.
Ripoti ya tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Kiongozi Mstaafu Amiri Manento, ilimtuhumu moja kwa moja Kamuhanda kuwa alikiuka sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho huku ikiisafisha Chadema kuwa haikukosea kufanya mkutano.
Kamanda Kamuhanda alisema hakukiuka maadili ya kazi kama ripoti hiyo iliyowasilishwa juzi  inavyosema, bali alichukua madaraka kama ambavyo sheria za kazi zinavyomruhusu.


“Ninapofika eneo ambalo kuna Inspekta,  kwa kawaida mimi huchukua madaraka. Hata hivyo, aliyezuia mkutano ni OCD wa Mufindi Ambwene Mwakinyaki ,mimi nilifuata maagizo yangu ya kazi yanavyoniruhusu,” alisema Kamuhanda.
Kuhusu matumizi ya mabomu ya machozi, Kamuhanda alisema  Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kilitumia mabango kuwaonya Chadema wasitishe mkutano, lakini walikaidi amri hiyo na wakaanza kuwapiga polisi kwa mawe ndipo walipoamua kutumia mabomu ya machozi.
“Mawe yalirushwa mengi na makubwa kiasi kwamba baadhi ya polisi walijeruhiwa hadi kofia ngumu za polisi walizovaa zikapasuka, na polisi wawili walijeruhiwa, mmoja mguu na mwingine mkono,”alisema.
Kamanda Kamuhanda alikana na kusema kuwa hakuna mwandishi yeyote aliyemfuata kumwambia kuwa Mwangosi anauawa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo  vya habari.
“Gari langu lilikuwa mita 150 au 200 kutoka eneo ambalo ghasia zilikuwa zinafanyika, hakuna mtu yeyote aliyekuja kuniambia kuhusu kupigwa kwa Mwangosi,” alisema.

Pia ripoti ya Kamati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) inaonyesha kwamba Mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Said alimkimbilia Kamanda Kamuhanda ambaye alikuwa katika gari lake la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser kumwomba awaamuru askari waache kumpiga Mwangosi, lakini hakuchukua hatua yoyote.
Hata hivyo, mara ya kwanza alipohojiwa na Kamati ya Dk Nchimbi, Kamuhanda alikiri kuwapo karibu ya tukio kabla ya jana kukanusha.
Kamuhanda hakutaka kuzungumza zaidi kuhusu ripoti hiyo ya Jaji Manento akidai kuwa anahofia kuingilia uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
“Kazi yetu ni kutekeleza majukumu na maagizo tu na mimi niliyafanya hayo yote.”
Katika hatua nyingine Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi ambayo iliongozwa na Jaji Mstaafu Steven Ihema imezidi kupingwa na watu wa kada mbalimbali wakidai kuwa haikukidhi  haja kwa kuweka wazi tukio la kuuawa kwa Mwangosi.
Jaji Ihema alipotakiwa kuzungumzia shutuma hizo alisema watu wana uhuru wa kutoa maoni yao, hivyo wana uwezo wa kusema chochote wanachojisikia.
Alisema tume yake imeshatoa ripoti na ipo hewani  wanaozungumza wana haki ya kuzungumza kwa kuwa ni haki yao.
“Sijaisoma hiyo taarifa ya Jaji Manento, lakini hata kama watu wanaiponda, hayo ni mawazo yao wako huru kuzungumza kile wanachojisikia,” alisema Jaji Ihema.

Chadema wataka Dk Nchimbi afukuzwe kazi
Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Vincent Nyerere amemwomba Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Nchimbi kwa kile alichoeleza kutumia vibaya madaraka yake kwa kuruhusu  ufujaji wa fedha za umma  kwa kufanya uchunguzi wa kifo Mwangosi  usiokidhi mahitaji na kuficha ukweli.
Akizungumzia ripoti hiyo alisema: “Ripoti imelenga kuficha ukweli na kulisafisha Jeshi la Polisi.”
Florence Majani, Hadija Jumanne na Tausi Ally

Mwananchi

No comments:

Post a Comment