WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 9, 2012

MITAZAMO JUU YA - TANGANYIKA - TANZANIA NA ZANZIBAR



Picture
Picture
Habari via gazeti la HabariLeo --- WAKATI Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikianza awamu ya tatu ya kukusanya maoni katika mikoa mbalimbali nchini, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amefanya mkutano kuhamasisha muundo wa Muungano wa Mkataba, huku Makamu wa Pili, Balozi Seif Iddi, akihamasisha Serikali mbili.

Jana katika mkoa wa Pemba Kaskazini ambako Tume ilikuwa ikikusanya maoni, Maalim Seif naye alikuwa na mkutano wa hadhara ambapo alisema Muungano wa Mkataba ndio ‘mwarobaini’ wa matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Zanzibar na si vinginevyo.

Akiwa katika viwanja vya Mchanga mdogo, Wilaya ya Wete, Pemba, Maalim Seif alisema anahisi matatizo ya msingi ya uchumi ya Zanzibar hayawezi kutatuliwa na mfumo wa sasa wa Muungano wenye muundo wa kikatiba wa serikali mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka 48.

Badala yake alisema anaamini mfumo wa Muungano wa Mkataba ndio utakuwa ‘mwarobaini’ wa malalamiko hayo ya takriban nusu karne, hasa kwa upande wa Zanzibar unaolalamika kubanwa kiuchumi na kimaendeleo ndani ya Muungano.

Akieleza msimamo wake katika mkutano huo ulioandaliwa na CUF, Maalim Seif alikiri kuwa mwumini wa Muungano wa Mkataba, kwa sababu ni mawazo yake kwamba aina hiyo ya Muungano si tu ina maslahi kwa Wazanzibari, bali pia kwa Tanzania Bara. Maalim Seif alisema mfumo wa Muungano wa Mkataba utarejesha hadhi na heshima kubwa ya Zanzibar kimataifa, “Bendera hii ya Zanzibar ni mpaka Chumbe tu, tunataka bendera ya Zanzibar ipepee Umoja wa Mataifa ilivyokuwa zamani”.

Katibu Mkuu huyo wa CUF, alisema itakuwa ni heshima na hadhi kubwa kwa Wazanzibari kuona Rais wao, Dk Ali Mohammed Shein anapepea bendera ya Zanzibar hata anapokuwa nje ya nchi. Alidai, kwamba muundo huo ana imani utamaliza manung’uniko ya miaka mingi kati ya pande mbili hizo za Jamhuri kuhusu Muungano. Aidha pamoja na mambo mengine, alihimiza wananchi wa Kaskazini Pemba kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa Tume juu ya mabadiliko ya Katiba.

Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, jana ilianza awamu ya tatu ya kuchukua maoni hayo, na kwa Zanzibar awamu hiyo inahusisha mikoa ya Kaskazini Pemba na Kaskazini Unguja.

Akielezea maeneo ya uchumi ambayo Zanzibar hainufaiki na Muungano, Maalim Seif alisema ni katika suala la kufunga mikataba ya miradi ya maendeleo na Jumuiya pamoja na mashirika ya kimataifa. Alisema inapotokea Zanzibar kufanya kazi kubwa na nzuri ya kupata miradi ya maendeleo inayoweza kuimarisha uchumi na kuinua hali za wananchi wake, hulazimika kupata baraka kutoka kwa Waziri wa Muungano.

Alitaka kuwapo Zanzibar na Tanganyika zenye mamlaka kamili na baadaye nchi mbili hizo ziwe na Muungano wa mkataba ambao kila upande utakuwa huru akidai ni utaratibu unaofuatwa na mataifa mengine duniani.

Alisema hali hiyo itaiwezesha Zanzibar kuwa na mahakama zake hadi Mahakama ya Rufaa, Baraza la Wawakilishi litakalokuwa mwanachama wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) wa moja kwa moja bila kupitia sehemu nyingine, Benki Kuu yake na Waziri wa Mambo ya Nje. Alieleza kuwa chini ya utaratibu wa Muungano wa Mkataba, utaondoa shaka ya matumizi ya rasilimali za ndani zenye malalamiko, kama vile mafuta na gesi asilia, na kila upande utanufaika nazo.

Maalim Seif alisema hivi sasa Zanzibar mbali na kuamua masuala ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, upande wa Bara haujatoa baraka zake, wakati ambapo Bara wanaendelea kutafiti gesi asilia katika maeneo yao na kunufaika na maliasili hizo, “Wenzetu ni miaka zaidi ya 14 wanachimba gesi asilia, watwambie Zanzibar inapata kiasi gani, kila siku wanafanya utafiti sisi tumefungika, halafu tuseme hakuna matatizo chini ya utaratibu huu, zipo kasoro nyingi,” alisema Maalim Seif, huku mamia ya wananchi katika mkutano huo wakishangilia.

Alitaka kila mwananchi awe huru kusema kile anachotaka na asilazimishwe, kwa sababu mambo ya kujificha na kutishana yamepitwa na wakati. Balozi Seif Wakati Maalim Seif akisema hayo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi amedai msimamo wa CCM kuhusu muundo wa Muungano ni wa serikali mbili (Bara na Zanzibar).

Balozi Seif akiwa na viongozi wa UVCCM katika ukumbi wa Amaan mjini hapa, aliwataka wasikubali kutumika na wanasiasa katika uchaguzi mkuu ujao (2015) kwani kufanya hivyo watashusha hadhi na heshima ya umoja huo, “Vijana msikubali kuyumbishwa katika Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar...msimamo wa CCM katika Muungano ni wa serikali mbili,” alisema Balozi Seif.


Source: http://www.wavuti.com

No comments:

Post a Comment