WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, June 10, 2011

SERIKALI VS VIONGOZI WA DINI -

JE KAULI YA MHESHIMIWA RAIS KIKWETE IKO SAHII DHIDI YA VIONGOZI WA DINI NA BIASHARA YA MADAWAYA KULEVYA?


‘RAIS Jakaya Kikwete, amewaonya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini kuacha tabia ya kushiriki biashara ya kuuza dawa za kulevya na badala yake washirikiane na viongozi wa serikali kuidhibiti biashara hiyo haramu’.

Mheshimiwa Rais alisema ‘Inasikitisha sana na kutisha, biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili kwani baadhi yenu tumewakamata. Kwa kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususan vijana waweze kuepuka na matumizi ya dawa hizi,’ mmmmm

Je kuna utata gani katika taarifa hii ya mheshimiwa Rais ambayo , imewapandisha mumkari maskofu (CCT) na kumpa kiongozi wa nchi masaa 48 ya kuwataja wahusika?
Je Maaskofu wamekurupuka katika kumpa kiongozi wa Nchi amri ya kutekeleza matakwa yao?

Je kama Mheshimiwa Rais asipotekeleza matakwa yao jamii ya watanzania inajifuanza nini katika swala hili nzima?

Je wale ambao serikali imesema imewakamata tayari  wameshafikishwa katika vyombo vya sheria kama bado kwa nini?

Je sheria na haki ya kushitakiwa kwa kosa la kujihusishwa na madawa ya kulevya “ambalo ni kosa la  jinai” inatekelezwa tofauti kulingana na hadhi na heshima, cheo cha mtu?

Tunafahamu kuwa serikali sio mtu ni taasisi ambayo kiongozi wake mkuu ni Rais wa nchi; na kiongozi huyo ili atekeleze majukumu yake hafanyi kazi peke yake ana timu nzima abayo inamsaidia ili aweze kufanikisha adhima yake ya kuongoza nchi na watu wake ili kufikia maendeleo ambayo jamii ina tegemea kufikia;

Katika siku za karibuni kumekuwako na vitendo ambavyo hufanywa na baadhi ya watu au kikundi cha watu au mtu mmoja moja ili kudhoufisha nguvu za maendeleo au hata kuharibu nguvu kazi ya jamii yetu; kwa kujihusisha na mambo kama;

·        Rushwa,
·        Uingizaji wa madawa ya kulevya,
·        Ufisadi wa rasilimali za umma na kadhalika


Mshangao wa watanzania wengi kwa nini Mheshimiwa Rais Kikwete pamoja na timu yake ya usalama wasiwafikishe kwenye vyombo vya sheria wahusika ili wachukuliwe hatua baada ya kuendelea kuyaeleza haya katika majukwao ya mikutano na makongamano? Inafahamika wazi kuwa Biashara ya madawa ya kulevya ni kosa, na kama hivyo sheria zipo? Sasa kama wamekamatwa kwa nini serikali inaendelea kuwabembeleza bembeleza waache hiyo biashara?

Nafikiri ni vyema kuikumbusha serikali kuwa kama washauri wa usalama hawana uhakika na taarifa sio vyema kumshauri mshemihwa Rais kutozisema kwani swala la madawa ya kulevya sio la kuendelea kulikemea kama wahusika wanajulikana; serikali itaendelea kuwakemea mpaka lini na ni nini? Hivi kisheria mtu ukiwa na taarifa za uhalifu lakini mwenye taarifa au uthibitisho akaendelea kukaa kimya bila kuzichukulia hatua ni kosa kisheria kwani ni namna ya kuendelea kuruhusu uhalifu huo, kuendelea na kama ni uhalifu wa   madawa ya kulevya taifa linazidi kuangamia kwa faida ya wachache.

nakubalia na kauli ya Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyosema ”Katika kupambana na tatizo hili la madawa ya kulevya, hatuna budi kutofumba macho ili kutowaonea haya watakaobainika kuwa chanzo cha usambazaji madawa ya kulevya, kwa sababu hili ni janga la kitaifa na tayari limeshawaathiri vijana wetu wengi sana” matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa Taifa, kiuchumi, kiafya na kijamii. Alisema kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa ni vyema kushirikiana na jamii na kuwa waaminifu katika utekelezaji wake kwani wasambazaji kutokana na ushawishi na uwezo mkubwa wa kifedha walionao wamiliki na waingizaji madawa ya kulevya bado ni tishio kwa usalama wa jamii.

Lakini pamoja na  utata wa serikali katika kulikabili jambo hili sio busara kwa baraza la maaskofu  kumpa mheshimiwa Rais masaa ili kuwataja wahusika;  ni vyema Baraza hilo lingetumia njia mbadala yenye hekima katika kuiomba Serikali kuwafichua wahusika na sio kutoa muda wa kumshinikiza rais katika utendaji wake; kwa kumweleza rais kuwa asipofanya hivyo yeye atakuwa Mwongo na Mzushi; Ni kweli kuwa maneno haya yamesemwa na   watu wenye heshima kabwa ndani ya jamii. 

“Tunampa saa 48 rais awataje kwa majina viongozi hao ambao yeye anadai wanajihusisha na kuuza dawa na kama atashindwa kufanya hivyo tunamtafsiri ni mwongo na mzushi... Tunasikitishwa na kushangazwa kwa kauli hiyo na tunamheshimu kama kiongozi wa nchi, hivyo tunampa masaa hayo awataje kwa majina” 

Nafikiri umefika wakati kwa viongozi wa dini nchini Tanzania kukaa pamoja na Serikali kupembua kwa dhati mambo yanayopelekea uwepo wa mkanganyiko huu wa kutofautiana na kutokukubaliana 


Ni kweli  kuna tatizo ambalo linahitaji kulitafutiwa suluhu ya haraka; ama sivyo linaweza hatarisha misingi ya haki, amani na utulivu. Lazima tukubali kuwa sheria inapovunjwa haiangalii huyu ni kiongozi wa dini au la, inatakiwa chukua mkondo wake dhidi ya watu hao

Serikali ikiwaogopa vigogo na viongozi wa dini katika biashara hii, serikali itakuwa inakimbia jukumu lake la msingi la kulinda raia wake; hivyo jukumu la serikali kulinda maisha ya watanzania  hasa vijana dhidi ya madawa ya kulevya itakuwa ni ndoto tu.


Kwa hiyo serikali lazima isimamie kwa dhati kabisa  katika kulinda heshima ya Tanzania kama nchi isiyovumilia siyo tu biashara bali pia matumizi haramu ya dawa za kulevyawa. Kwa msingi huu hata watu wa Mungu kama wamo katika biashara hii ni busara kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria na kukamata mali zao na pasi zao za kusafiria ili haki itendeke. 

No comments:

Post a Comment