Utajiri wetu ni mkubwa lakini?
Siasa ni sayansi ya utengenezaji wa maneno matamu matamu ambayo yanatumika katika kuibadili akili ya wananchi ili waweze kukubaliana na kikundi Fulani ambacho kimejipanga kisera ili kiweze kupata nafasi ya k utawala, ambacho mara nyingi huwa na mipango mitamu ya kinadharia zaidi ya maendeleo kwa wananchi.
Kutokana na sera zao wakati mwingine upangaji wa hoja na utamu wa maneno yao hupelekea kuaamini kuwa wanasiasa ni watu wanaojua kila kitu. Na kila mtu anadhani hakuna mtu anayeweza kufanya kitu kwa maslahi ya nchi bila kuhusisha siasa. Kinachoendele hapa ni dhana tunayoijenga kuwa mwanasiasa umekuwa bingwa wa kujenga hoja, wanataka kuona umekuwa bingwa wa kutatua matatizo na kuwaletea wananchi asali na maziwa.
Siasa ili inafinikwe lazima ijengwe chini ya msingi wa sera, na sera hizo lazima ziwalenge kwa watu Sera zote zinapotungwa ni kwa ajili ya watu, lakini tatizo ni kubwa wanasiasa wanawarubuni watu, hivyo kuvurugu mipango ya maendeleo; Ni wazi kwamba mhemko wa kisiasa, umeikumba nchi yetu; Kila kitu tumekifanya ndani ya siasa, hili ni tatizo kubwa. Siasa uchwara tunazipa nafasi na kujikosesha maendeleo. Kutokana na kushindwa kuwaelimisha watu kuhusu tabianchi, ufahamu wa maisha, mbinu za kukabiliana na majanga na mengineyo, moja kwa moja vinasaliti jamii
Tanzania ni nchi maskini ni lazima tuwe na viongozi ambao kweli wanasaidia wananchi. Muda wa kukubali kuendelea kudanganywa umekwisha, ni lazima sasa sisi kama wananchi tuwahukumu wanansiasa kutokana na namna wanavyotufanyia mambo, wanavyotufanya sisi masikini kana kuwa hatujui nini kinaendelea. Kauli mbiu yetu iwe kama hawatujali kwa maendeleo na kutuzidishia umasikini, inatunapasa kuachana nao tumechoka kuendelea kudanganywa..
Leo hii kigezo chetu cha maendeleo ni nini? Tunayaangaliaje maendeleo ya wananchi? Kwa nini kuna tofauti kubwa kati ya mtu na mtu? Je tukisema wananchi hawajitumi kwa maendeleo yao je tumewawezesha?
Kipimo chetu cha maendeleo ni kuangalia maisha ya jumla au ya mwananchi mmoja mmoja? Je tunayalinganisha maendeleo ya wananchi wetu kwa kuangalia uwezo wao wa kuzalisha mali na wanatumia vifaa gani, na vinahusiana vipi na kuimarisha afya zao? je thamani ya fedha yetu, kiwango cha elimu na uimara wa sekta za viwanda tunaviangaliaje katika kumletea maisha bora huyu mwananchi? Au tunaridhika na Msongamano wa magari na watu katika miji yetu mikuu ikianzia darn a miji mingine na tunaridhika kuwa hii ishara tosha ya maendeleo na maisha bora?
Je kuna uwiano kati ya uimarishaji wa bidhaa za ndani na zile zinazokuja toka nje ya nchi? Au tunaridhika na kilimo cha duni cha wananchi serikali kupitia wanasiasa hatuoni sababu ya kuwasaidia wananchi kuwajengea uwezo wa kupata masoko; Uwezo wetu wa kuwatafuti masoko yenye tija umefia wapi? Bila dhana bora na elimu nzuri ya kilimo tunaelewa kuwa tumepania kuwamaliza kabisa wananchi kwa kuwaletea ushindani wa kupambana na biashara kutoka nje na hivyo kuwanjima uwezo wa ushindani katika midhani sawa.
Je Tanzania ya leo ni chama tawala pekee ndicho kinachoongoza kutoa ahadi ambazo baada ya uchaguzi zinakuwa mzigo ndani ya chama? Je vipi vyama vya upinzani vimefanikiwa kukibana chama tawala katika kuhakikisha kuwa wanatekeleza ahadi zake kwa wananchi? Ni ukweli ambao haufichiki kuwa wanaotawala ndio wenye meno ya kutafuna, basi la msingi wabanwe watekeleze ahadi zao; kwa msingi huu watawala kupitia vyama vyao wasipobanwa kitakachoendelea na tunakiona kikiendelea kutokea ni kuwa taifa letu litaendelea kuzalisha wafanyabiashara feki na bidhaa feki. Elimu na walimu feki, mitihani feki, wahitimu feki, na vyeti feki. Hospitali zitaendelea kutikiswa na dawa feki. Mwisho wa siku wimbo wetu utakuwa kila kitu ni feki
Hivi sasa tunaona vyama ushindani vikipita sehemu mbali mbali kwa kauli ya kuhamasisha ubovu wa serikali inayotawala; swali la msingi hapa ni kweli wanachokisema ndicho wanachokiamini na kuwa tayari kuwaletea wananchi maendeleo punde wakipata nafasi ya kuongoza?
Au tuendelee kuamini kuwa hii ni siasa kila mtu anatafuta ulaji kwa staili ya kuonyesha mabaya ya mwenzake? Je hakuna jema ambalo serikali inayopingwa sasa hivi imewafanyia wananchi? Nikifikiri haya yote ninaishia kwa kusema kuwa TUWAFANYE NINI WANASIASA KWANI HAWAAMINIKI HATA KIDOGO; wanaendelea kuwafanya wananchi kama watoto wa kuku watanyonya kesho wakati hakuna uwezekano wa kuwatoa katika umasikini uliopindukia;
Utajiri huu wote tulio nao kwa nini tunaendelea kuwa masikini inauma sana wanasiasa mnatutesa jamani;
No comments:
Post a Comment