WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 26, 2014

RAIS KIKWETE ATUNUKU NISHANI NA TUZO ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO

Mama Maria Nyerere akipokea nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano(Order) kwa niaba ya Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku Mama Maria Nyerere Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungnao Daraja nne.
Mama Fatma Karume akipokea Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano(Order) kwa niaba ya Marehemu Abeid Aman Karume Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku Mama Fatma Karume nishani ya kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja Nne wakati wa hafla ya kutunuku nishani na tuzo za miaka 50 Muungano zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano ikulu jijini Dar es Salaam jana usiku.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku Rais mstaafu wa Awamu ya tatu Mh.Benjamin William Mkapa Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano(Order) wakati wa sherehe ya kutunuku nishani na tuzo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ikulu jijini Dar es Salaam jana usiku.(picha na Freddy Maro)
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Kwanza Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia alikuwa Mwenyekiti Tume ya kurekebisha Katiba  Mhe. JajiJoseph Sinde Warioba wakati wa Sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa kuamkia leo ametunuku nishani na Tuzo kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa na watumishi wa umma wapatao 86 waliotoa mchango wao katika kuulinda na kuudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka Hamsini 50.
Picha zote na Freddy Maro

JK: Sitaki tena kusikia dawa za kulevya zinapita


Rais Jakaya Kikwete akifurahi muundo wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana alipokwenda kuweka jiwe la Msingi. 


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameagiza kuimarishwa kwa udhibiti katika viwanja vya Ndege vya Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (Kia), kutumiwa kupitisha dawa za kulevya kwenda nje na kuingia nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la tatu la abiria JNIA, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema hajaridhishwa na kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya katika viwanja hivyo.

Alisema inashangaza dawa za kulevya zinapita katika viwanja hivyo na watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatiwa Afrika Kusini.

“Sijaridhishwa, unasikia kila siku mtu amekamatwa Afrika Kusini na dawa za kulevya, sijui mwanamuziki gani, siridhishwi hata kidogo,” alisema.

Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman kuhakikisha mianya hiyo inazibwa vinginevyo ataanza kumwadabisha yeye kisha wengine watafuata... “Nitaanza na wewe mkurugenzi na mwenyekiti wako wa bodi. Mtu anakuja hapa, sijui mwanamuziki gani, mara yoo...yoo... kwa kuwa mnamfahamu anapita, hatuwezi kuwa namna hiyo.”

Aliagiza apewe orodha ya majina ya maofisa wanaodhaniwa kujishughulisha na biashara hiyo naye atawaondoa kwa kuwa sheria inamruhusu... “Rais hashtakiwi, nitawaondoa, nipeni majina kwa kuwa kinachotokea hivi sasa kinaonyesha wote tunafanya biashara ya dawa za kulevya, wengine inatuumiza sana tunaonekana wote ndicho tunachofanya.”

Alibainisha kuwa haingii akilini kusikia kuna kitu kinakwamisha udhibiti wa dawa hizo katika viwanja hivyo ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma... “Miaka miwili hiyo sheria gani kwa kitu cha Sh2.5 milioni... je, ingekuwa Sh600 milioni si ndiyo kungegeuzwa gulio?” alihoji.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alifafanua baadaye kuwa Rais alikuwa anazungumzia kuchelewa kufungwa kwa mfumo wa kubaini dawa za kulevya uwanjani hapo, kutokana na mchakato mrefu wa sheria hiyo.
Jengo la abiria

Rais Kikwete alisema atahakikisha Hazina inatoa fedha zinazotakiwa kuharakisha ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na maegesho ya ndege 18 kwa wakati mmoja, litakalohudumia abiria milioni sita kwa mwaka badala ya milioni 2.5 wa sasa.

Mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya BAM ya Uholanzi, utagharimu Sh518 bilioni na Serikali iliahidi kutoa asilimia 50 ya fedha hizo sawa na Sh89 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na Serikali ya Uholanzi.

Hata hivyo, hadi sasa fedha hizo hazijatolewa jambo ambalo liliwahi kulalamikiwa na Mkurugenzi wa TAA kwamba linakwamisha ujenzi huo.

Jengo hilo litakuwa na mifumo yote ya mawasiliano, usalama na uendeshaji na maegesho yenye uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote, zikiwamo Airbus 380.
Awali, Suleiman alisema uwanja huo utakamilika kwa wakati kutegemeana na upatikanaji wa fedha na hivyo kuondoa msongamano wa abiria katika uwanja wa sasa (Terminal II) ambao licha ya kuhudumia milioni 2.5, uwezo wake ni kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.

Kabla ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi huo, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili katika eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza katika eneo hilo, Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inatayarisha haraka iwezekavyo ramani ya ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo kwa madaktari kinachotarajiwa kuwa kikubwa zaidi kwa Afrika Mashariki na Kati.

source: mwananchi

MAONI: Tuuenzi Muungano kwa vitendo

 
Waasisi wa Muungano Hayati baba wa Taifa Nyerere(kushoto) na Sheikh Abeid Aman Karume(kulia).PICHA|MAKTABA 

Leo ni miaka 50 tangu waasisi wetu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume   (kwa sasa wote ni marehemu), walipoziunganisha nchi zetu mbili za Jamhuri ya Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mojawapo ya sifa kuu katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano ni kuendelea kuwapo, licha ya changamoto mbalimbali tangu kuasisiwa kwake Aprili 26, 1964 lakini bado umeendelea kuwa imara na hakuna dalili za kuuvunja wala mwenye nia ya kuuvunja Muungano.
Hadi Karume anauawa Aprili 7, 1972 mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba yalikuwa 11, lakini yalifanyika marekebisho baadaye na hadi Mwalimu Nyerere anaondoka madarakani mwaka 1985, yalikuwa  yamefika 21 kwa mujibu wa Katiba.

Mwaka 1994 kulipozuka kundi la G-55 ndani ya Bunge la Muungano likidai Serikali ya Tanganyika, baada ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), Rais Ali Hassan Mwinyi (kwa wakati huo) aliunda tume iliyoongozwa na William Shelukindo kuchunguza kero za Muungano.

Tume ya Shelukindo ilibaini kero 31 ambazo zilishughulikiwa. Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani zilikuwa zimebaki kero 13 na ameshughulikia tisa, zimebaki nne na tatu kati ya hizo zinahitaji marekebisho ya Katiba.

Sisi Mwananchi tunasema Serikali imefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka 50, kwanza kuhakikisha Muungano unadumishwa, kushughulikia kero zinazojitokeza na sasa tuna mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea nchini.

Ni suala lisilopingika kwamba kila jambo lina changamoto zake na sisi tunaamini mjadala unaondelea kuhusu upi ni muundo sahihi wa Muungano ni changamoto ambazo utafika wakati zitakwisha na hatimaye Watanzania watapa kile walichokikusudia.

Siyo nia yetu kuhoji misimamo ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuhusu upi muundo sahihi wa Muungano, lakini hoja yetu kuu ni kuweka dhamira ya pamoja ya kuendelea kudumisha Muungano ambao una umri wa mtu mzima.

Kwa mantiki hiyo wazo lolote la kuvunja Muungano ni kutowatendea haki Watanzania.

Tunapenda kuwasihi wanasiasa kuwa malumbano yanayoendelea sasa ndani ya Bunge la Katiba na nje yasiwe hoja ya kutupeleka kuvunja Muungano, tupambane kwa hoja, lakini tusitupe hoja za wananchi kwa manufaa ya wachache.

Kama waasisi wa Muungano waliendelea kuuboresha ili uwe na tija zaidi kwa wananchi, hakuna sababu ya watu kutoa macho pale maboresho yanapotaka kufanyika kwa lengo la kuimarisha Muungano. 

Sisi wa Mwananchi Communications Limited tunaungana na Watanzania wenzetu katika kusherehekea nusu karne ya umoja wetu kwa kuweka msimamo wetu wazi.

Tunaamini katika kuulinda na kuuimarisha muungano wetu. Tunaamini katika ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda (regional economic integration).

Pia tunaamini katika kuwapa nafasi na sauti wasio na sauti, wanyonge na makundi madogo katika jamii (minorities). Tunaahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu wa kutoa nafasi ya mijadala mbalimbali ya kitaifa yenye lengo la kuindeleza nchi yetu, muungano wetu na watu wake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Huu ndiyo mchango wetu na ahadi yetu kwa taifa.

source: mwananchi

Hamad Rashid aikosoa Tume ya Jaji Warioba

Mjumbe wa Bunge la Katiba,Hamad Rashid Mohammed
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imevunja sheria kwa kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu kwani haikupata theluthi mbili za Wazanzibari na Watanzania Bara.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad  Rashid Mohammed, aliyasema hayo jana na kuikosoa Tume kuwa  Wazanzibari walitaka serikali ya mkataba siyo  serikali tatu kama ilivyoeleza.

“Tume ilipata wapi mamlaka ya kusema Zanzibar inataka serikali tatu, walikaa nao wapi wakazungumza?," Alihoji.

“Ukichukua katiba na sheria ya mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge inasema ili kufanya  badiliko la katiba ni lazima ipatikane theluthi mbili ya kura kwa   Zanzibar na Tanzania Bara.”

Mohammed ambaye  alivuliwa wadhifa na kufukuzwa uanachama wa CUF, alisisitiza kuwa kama Tume ya Warioba, haikupata theluthi mbili hizo imevunja sheria.

Alisema Tume ilitakiwa baada ya kupata theluthi mbili ya Bara  irudi Zanzibar na kuwashauri kuangalia matatizo ya kurekebisha kwenye mfumo ulioko badala ya kupendekeza serikali tatu.

“Kwa kuwa  Tume yenyewe ndiyo iliyoanza kuvunja sheria hiyo kwa sasa haina uhalali wowote hivyo wajumbe kutoka Tanzania Bara waliopo wakae wapate theluthi mbili na sisi kutoka Zanzibar tukae na kutengeneza theluthi mbili ili tupate Katiba mpya,” alishauri.

Akizungumzia serikali mbili, alisema ndizo mwafaka kwani tatu zitaongeza gharama zaidi.

Alisema Tume  ya Warioba haikukokotoa namna ya kuwatunza viongozi wakuu wakiwa madarakani na wanapostaafu.

“Leo Rais akisafiri anatumia  si chini ya Shilingi milioni 500, wakati mwingine hata bilioni moja,” alisema na kuongeza kuwa hizo ni gharama wakiwa madarakani na wakistaafu itakuwaje?

Alisema viongozi hao wakistaafu zaidi ya watatu kwa wakati mmoja utakuwa mzigo mkubwa wanabebeshwa wananchi.

“Tume haikuangalia gharama za miaka mingi ijayo,itakuwa gharama kubwa na kuhoji ni nani atazibeba?”
 
CHANZO: NIPASHE

JK: Muungano uko salama

Watakaochezea Muungano kukiona cha mtemakuni
Awashangaa Ukawa kususa…Awashauri warudi bungeni

Rais Dk.Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein jana, baada ya kupokea picha za waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,hayati Mwl.Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kwenye viwanja vya Saba Saba kupitia wananchi wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano huo. (Picha Tryphon Mweji).
Rais Jakaya Kikwete amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uko salama na watakaouchezea watakiona cha mtemakuni.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.

“Nimeamua kuzungumzia jambo hili leo ili kesho watu wapate kujimwaya kwenye sherehe za Muungano… Muungano uko salama na atakaye uchezea ataona cha mtema makuni”.

Alisema katika historia ya Jamhuri ya Muungano hakuna budi kukumbuka kitendo cha historia na cha kijasiri kilichofanyika Ikulu ya Zanzibar kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika  kwa kutia saini hati ya Muungano.

Alisema hati hiyo ndiyo makubaliano na mkataba rasmi wa Muungano. Rais Kikwete alisema hati hiyo imefafanua kuhusu muundo wa Muungano, mambo ya Muungano na mfumo mzima wa utawala.

Akielezea historia ya Muungano huo, alisema Desemba 10, 1964 jina rasmi la Tanzania liliidhinishwa baada ya kubuniwa na kijana wa miaka 18 mwenye asili ya kihindi aliyekuwa akisoma shule ya Aga khan Morogoro, baada yakufanyika mashindano ya kubuni jina.

“Watanzania tuna kila sababu ya kusheherekea jubilee ya zahabu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Miaka 50 ni mafanikio makubwa sana. Wapo wenzetu walioungana Afrika lakini hawakufanikiwa. Wapo wengine mpaka leo wanaendelea kujadiliana muungano lakini hawajafanikiwa,” alisema.

Alisema wengi wanamjua Kambarage Nyerere hakuwa mtu wa kujigamba, lakini katika Muungano alisema Tanzania ni lulu ya pekee iliyoundwa kwa juhudi za wananchi wenyewe.

Aliongeza kuwa hata Umoja wa nchi za Afrika Mashariki  na Umoja wa Nchi za Afrika unaweza kuwepo ikiwepo nia thabiti. “Sisi tumeweza na wenzetu pia wanaweza.

Alisema wapo wanaojiuliza Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika umewezekanaje na umewezaje kudumu kwa muda mrefu kiasi hiki. Alisema majibu ya maswali haya ni muhimu  kwa Watanzania kwa kuwa  unaendelea kudumu na kustawi.

Rais Kikwete alisema asilimia 91 ya Watanzania walizaliwa baada ya Muungano, na wale waliokuwepo baada ya Muungano wamebakia  kuwa asilimia 9 tu na kwamba majibu ya swali hilo yana umuhimu wa pekee na yatawasaidia wale waliozaliwa baada ya Muungano, kuelewa.

MIONGO MITANO YA MUUNGANO

Alisema  waasisi,  Nyerere na Karume walikuwa waumini wa dhati wa Muungano wa nchi zao kuungana. Walikuwa washiriki wa vuguvugu la ukombozi la Afrika ili kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano. Pia kuunganisha nchi zao baada ya uhuru.

Uamuzi wa waasisi hao haukuwa jambo la ghafla ulianza tangu harakati za kupata uhuru Alisema  waasisi hao, walitanguliza maslahi ya taifa mbele kabla ya mambo yao binafsi.
Waliunganisha nchi hizo zikiwa na muda mfupi tu baada ya uhuru na ukombozi kwa sababu ya imani yao na ujasiri mkubwa wa kuunganisha nchi zao. Ni uamuzi mkubwa ulioweza kufanywa na viongozi hao.
Alisema watu wa Tanganyika ni watu wamoja, lakini kwa bahati mbaya  wakoloni ndio waliowatenganisha na kujiona waishi katika nchi mbili.

WANAOTAKA MUUNGANO UVUNJIKE WANA LAO JAMBO

Alisema wako watu wachache wenye roho mbaya wanaochukia Muungano, lakini ni kidogo sana. Alisema Watanzania wengi wanataka kuona changamoto za Muungano zinatatuliwa.  “Wanaopenda Muungano uvunjike wana lao jambo si wenzetu.”

Aliongeza kuwa katika miaka 50 ya Muungano kumekuwa na muingiliano wa watu kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine na kuwa kwao na kwao  kwa asili wanakwenda kusalimia.

Alisema watu wapatao 600,000 wenye asili ya Zanzibar wanaishi Bara na Watu wapatao 100,000 wenye asili ya Bara wanaishi Zanzibar na kwamba wakati wa Muungano Zanzibar ilikuwa na watu 300,000 tu. Uhusiano wa kiuchumi, kibiashara na kijamii umekuwa wa kawaida na kufanya safari nyingi kwa siku kati ya Zanzibar na Bara.

Mwaka 2013 abiria waliosafiri kwa meli kati ya Zanzibar na Dar es Salaam ni  1,492,571, Usafiri wa ndege abiria mwaka 2012 ni 386,048.

“Tutakuwa tumetenda dhambi kubwa sisi viongozi kwa wananchi hawa kama tutakuwa  chanzo cha chokochoko ya kudhoofisha muungano huu na kuvunjika,” alisema na kuongeza  wananchi ndiyo watakaoumia na kusumbuka.

Viongozi watafanya mambo yao raha mstarehe kwa kupokelewa uwanja wa ndege kwa watu maalum ( VIP)  kwa kupigiwa mizinga. Alisema Muungano ndio ulioleta uhusiano wa karibu wa viongozi wa siasa na vyama vya siasa wa Tanganyika na Zanzibar.

Wakoloni waliwalazimisha wananchi kuwa katika makundi kutokana na rangi zao. Ndiyo maana kuna maeneo yanaitwa  uzunguni, uhindini na usawahilini.

 Waarabu na Wahindi walikuwa daraja la kwanza,  wwa ajili hiyo watu wakalazimishwa kuunda vyama vya kutetea maslahi yao ya kijamii. Vyama hivyo viliundwa kwa misingi ya rangi ndio maana kulikuwa na Pan African Association (PAA) na Tanganyika African Association (TAA).

Baadaye kukawana Afro Shiraz Part (ASP) ambayo ilifanya mapinduzi kuondoa dhuluma kwa upande wa Zanzibar na Tanganyika African National Union (TANU) ambavyo viliungana Februari 5, 1977 na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema katika vikao vya vyama hivyo, masuala ya Muungano yalikuwa yakizungumzwa na kufanya kuwa sehemu kubwa ya kudumisha Muungano huo.Alisema katika miaka 50 ya Muungano pia kumekuwa na matatizo ya ustawi wa Muungano huo lakini hatua mbalimbali zimekuwa zikuchukuliwa na kufanikiwa kupata ufumbuzi.

Mwaka 1993 wakati mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Rais, aliunda Tume ya Shelukindo kushughulikia mambo ya Muungano. Mwaka 2006 kati ya kero 31 za Muungano zilibaki 13 na katika vikao vya pamoja vya serikali mbili yamebaki mambo sita.

Alisema suala la ajira ya watumishi kutoka Zanzibar limeshapatiwa ufumbuzi. Serikali mbili zimekubaliana fomula  na kwamba kero iliyobaki ni mgawanyo wa mapato na mgao wa Zanzibar katika benki na masuala ya vyombo vya moto ambalo linazungumzwa kiutawala na kuahidi kuwa baada ya muda mfupi litapatiwa ufumbuzi.

HATI YA MUUNGANO
Amewashangaa wanaosema sahihi ya Nyerere ni sawa lakini ya Karume imeghushiwa. Alisema kama kughushiwa basi atakuwa ameghushi Nyerere.

“Unaposema sahihi ya Karume imeghushiwa, basi aliyegushi ni Nyerere, hivi watu walipokuwa wanashuhudia ni kwamba mzee Karume alikuwa asaini chochote pale,” alihoji. Alisema hati ile ni suala muhimu sana ndiyo maana  Nyerere alipostaafu alimuachia Mwinyi,  na Mwinyi alipostaafu alimuachia Mkapa na Mkapa alipostaafu alimuache yeye (Kikwete). Hati hiyo inahifadhiwa na Rais na ndiye mwenye dhamana nayo.

MCHAKATO WA KATIBA
Alisema dhamira yakuanzisha mchakato wa Katiba mpya ni kuwapa Watanzania fursa yakujadili kwa uwazi , kwa kina na kuyatambua matatizo ili yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba yaingizwe.

Alisema ni matumaini yake kuwa Wajumbe wa Bunge la Katiba watatumia vyema fursa hiyp kutunga Katiba iliyo nzuri.

Akizungumzia kitendo cha Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA) kususia bunge hilo kwa madai ya kwenda kushtaki kwa wananchi aliusihi urudi bungeni kujadili Rasimu ya Katiba na kuwataka wajumbe kutumia lugha ya staha na kuacha kukejeli waasisi wa Muungano

Amesema hatua ya Ukawa kususa vikao vya bunge na  kwenda kwa wananchi, wakati wake haujafika kwani  kazi ya kujadili Rasimu inafanywa bungeni na sio kwenye mikutano ya hadhara.

 “Nimekitika kusikia wanazunguka nchi nzima kwenda kushitaki kwa wananchi, sijui wanakwenda kushataki jambo gani,” alihoji na kuongeza “napenda kujumuika na watu wengi kuwahisi warudi bungeni.”

Alisema hivi  sasa ni wakati wa kujadili Rasimu na kutunga Katiba mpya ,kazi ambayo inafanyiwa bungeni na sio kwenye mihadhara ya wananchi wasiokuwepo bungeni. “Hawawatendei  haki wananchi waliowachagua na wale wa kundi 201 hawatutendei haki sisi wawili tuliowateua na kuwapendekeza.”

Aliwasisi kuwa wasipoteze fursa hiyo muhimu na kuwaeleza kuwa baada ya bunge kumaliza kazi yake wajumbe wa bunge hilo watatakiwa kwenda kwa wananchi kuwashawishi waunge mkono maamuzi  yao.

“Huko nje waendako siko, na siku yake sio sasa ipo siku watakwenda kwa wananchi ila wakati wake bado.  Hivi sasa ni kwakati wa kujadili Rasimu na kutunga Katiba mpya. Kazi hiyo inayofanywa bungeni na sio kwenye mikutano.” Alisema.

Alisema watu wanajua kuwa Wajumbe wa Bunge la Maalumu wana matatizo na tatizo lao kubwa ni uhusiano miongoni mwao na kwamba ufumbuzi wake wanao wenyewe.

“Kambi hii na kambi hii wakienda kwa wananchi hakuna jawabu,  wananchi hawahusiki na hawana la kuwasaidia…Majawabu ya matatizo yao yako bungeni kupitia mfumo wa bunge walioutengeneza wao wenyewe kupitia kamati zao za uongozi na maridhiano,” alisisitiza.

Alisema wananchi wanajua nani ni nani, nani kasema nini na nani kafanya nini kwa sababu mkutano wao unaonyeshwa moja kwa moja na televisheni. Alisema lugha za matusi  alishawasihi wasiache wakati alipokuwa akilizindua bunge hilo. “Maana hata wakati wanatunga kanuni nanga zinapaa… Tatizo kubwa la wajumbe ni lugha zisizokuwa na staha kwa pande zote mbili.”

Aidha, alisema inahuzunisha na kukasirisha kuona na kusikia wajumbe wanapotukana  waasisi waliounda Muungano wa Tanzania ambapo alisema hali hiyo haikubaliki na kwamba huo sioo uhuru wa kutoa mawazo.

Imeandikiwa na Beatrice Bandawe, Romana Mallya na Beatrice Shayo
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna Katiba bila UKAWA

kingunge c2ea5
Na Hudugu Ng'amilo
MWANASIASA mkongwe na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale – Mwiru, amesema makada wenzake wanaomshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wanakitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kumtukana au kumshambulia Jaji Warioba, au wajumbe wengine wa tume hiyo ni sawa na kukitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali.
Kingunge alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba, ambapo alisema wanaomshambulia Jaji Warioba wanaonyesha utovu wa adabu, kwa kuwa chama kina maadili na adabu katika kushughulikia masuala mbalimbali.
"Mimi sitakubali hata kidogo wajumbe watumie msimamo wa chama kumshambulia Warioba au wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, si halali kumshambulia Warioba au mjumbe yeyote yule binafsi.
"Mimi ni Mwana CCM niliyeondoka madarakani siku nyingi lakini naamini kuwa kumtukana mwenzetu ni sawa na kukitukana chama na sisi tuliopo hapa, wanaomshambulia Warioba wanakosea sana, hapa tuna rasimu ya Katiba ambayo ina mawazo tu, hakuna watu ndani ya rasimu hiyo, hatupaswi kukiuka maadili kwa kuwatukana au kuwakashifu watu," alisema.
Alisema kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho, hivyo wajumbe hawana sababu ya kumsema, kumtukana au kumkejeli mtu yeyote aliyekuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kingunge pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na kejeli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala mbalimbali.
"Hatuwezi kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana, wale waliokuwa wakitumia lugha hizo walikuwa wanatudhalilisha wote. Wengine walitumia lugha hizo kwa waasisi wetu...Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye ametumia fedha za Watanzania kupata elimu yake," alisema.
Alisema wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzeo Katiba mpya, iliyo bora na lazima izingatie miaka 50 ya muungano ambao umekuwa na mafanikio makubwa.
"Katiba bora lazima iimarishe yale mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hicho ikiwemo muungano, umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na kuunda mazingira ya amani na utulivu, kama haiimarishi, haifai hata kidogo. Haya mafanikio yote yametokana na muundo wa serikali mbili ulioasisiwa na wazee wetu," alisema.
Hakuna Katiba bila UKAWA
Kingunge alisema kuwa ili Tanzania ipate Katiba mpya iliyo bora, lazima kuwepo maelewano ya kuwashirikisha wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema kitendo cha wajumbe wa UKAWA kususia vikao vya Bunge, kinaonyesha upungufu mkubwa walionao lakini Katiba mpya haitaweza kupatikana bila ya wao.
Kingunge aliwaomba wajumbe wa UKAWA warejee bungeni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wananchi.
Alisema hata UKAWA wakirejea bungeni ni vema wajumbe wakatambua kuwa kupatikana kwa Katiba mpya kunahitaji maridhiano ya pande hizo mbili.
"Hatuwezi kupata theluthi mbili ya kura hasa kwa wajumbe wa kutoka Zanzibar watakaohalalisha maamuzi yetu bila kushirikiana na wenzetu, lazima tuzungumze, theluthi mbili ni takwa la kisheria, hatuwezi kulikwepa," alisema.
Kingunge alisema kwa muda mrefu Zanzibar kulikuwa na mfarakano mkubwa kati ya CCM na CUF lakini yalifanyika mazungumzo yaliyodumu kwa takriban miaka 13.
"Tumezungumza kwa muda mrefu tangu 1998 lakini hatimaye tulibuni suala la kugawana madaraka...katika hali ya Zanzibar tulisema haiwezekani lazima tukubaliane, sasa Zanzibar imetulia. Ni kutokana na mazungumzo hayo.
"Suala la Katiba mpya si utani ni lazima tukubali tuzungumze mpaka tuelewane....humu ndani sisi wajumbe tuzungumze lakini na wakubwa huko nje nao ni lazima wazungumze," alisema.
UKAWA waliteka Bunge
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd, wamewataka wajumbe wa UKAWA wabatilishe uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalumu.
Kauli hizo walizitoa jana walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya Katiba, ambapo walisema Katiba inayotungwa ni ya Watanzania wote, hivyo ni vema UKAWA wakarejea bungeni.
Balozi Iddi alisema taifa limetumia fedha nyingi kugharimia ujenzi wa Bunge Maalumu pamoja na kuwagharimia posho wajumbe wake ambapo mpaka jana lilitumia zaidi ya sh bilioni 20, hivyo si busara kwa UKAWA kususia vikao.
Alisema UKAWA ni sehemu muhimu katika utungaji wa Katiba na wajumbe wake wametumwa na wananchi ambao wanataka matatizo yao yawekewe utaratibu wa kushughulikiwa kwenye Katiba.
Alisema kutokana na umuhimu wa kutunga Katiba, Rais Jakaya Kikwete, amekubali kuliongezea muda wa siku 60 zaidi Bunge hilo ambalo jana limeahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu.
Alisema kuongezewa siku huko kumetokana na kutokamilisha kazi yake kwa siku 70 zilizopangwa awali ambazo zimemalizika jana hivyo UKAWA wanapaswa kutambua unyeti wa vikao vya bunge na umuhimu wao.
"Pamoja na serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza ukumbi na kulipana posho UKAWA wameamua kususia vikao vya Bunge. Nawasihi warudi tuendelee na kazi hii tuliyopewa na wananchi. Katiba haitungwi barabarani au kwenye mikutano ya hadhara bali bungeni.
"Nawasihi warejee bungeni tuifanye kazi hii tuliyotumwa na wananchi, tumetumia fedha nyingi na tutaendelea kutumia, kila mmoja wetu analipwa sh 300,000 kwa siku na serikali inatumia sh milioni 188 kwa siku kulipa posho."
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema anaamini katika umoja, hivyo kukosekana kwa wajumbe wa UKAWA ndani ya Bunge kumemsikitisha lakini ataendeleza jitihada za mazungumzo nao.
Pinda ametoa rai hiyo wakati ni takriban wiki moja imepita tangu alipokaririwa akitamba kuwa wanawafuata UKAWA huko huko kwa wananchi kwenda kusema ukweli.
Pinda aliwasihi wajumbe wa UKAWA warejee bungeni huku akiwasihi wajumbe wengine wajiepushe na lugha za kejeli na vijembe ambazo alidai zimechangia mijadala kuwa katika mazingira magumu.
'Mimi kila siku huwa nasema kuwa yaliyopita si ndwele...tugange yajayo, naomba wenzetu UKAWA warejee bungeni, Katiba mpya inahitaji ushirikiano wetu sote," alisema.
Pinda pia alisema Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri kwa kuwa yapo mambo mengi ambayo hayamo kwenye Katiba ya sasa lakini yameorodhoshwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Alibainisha kuwa anapingana na rasimu hiyo katika eneo moja la muundo wa serikali tatu kwa kuwa anaamini ni mzigo mkubwa kwa taifa na litachangia kuvunja muungano.
Alisema kuwa wanaosema kuwa kutofuata mapendekezo ya tume ya Warioba kwa kuwa imetumia fedha nyingi, wanakosea kwani wajumbe wa Bunge Maalumu wamepewa fursa ya kuondoa, kuboresha na kuingiza mawazo wanayoona yanafaa kuwemo kwenye Katiba mpya.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema kiti chake kiliamua kuwaacha wajumbe wajadili kwa uhuru zaidi na wananchi waamue kipi kinafaa.
'Huko mitaani tunalaumiwa kwa kuwaachia wajumbe, sisi tulifanya hivyo pasipo kutumia nguvu, kanuni au askari ili wananchi wajue tabia za wajumbe wao na kuamua, tungebanana sana najua lazima tungepigana na kutoana ngeu," alisema:{chanzo Tanzania Daima} - mjengwa blog.


Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar


IMG-20140426-WA0034_af1cd.jpg
IMG-20140426-WA0035_686a4.jpg
Umati wa watu waliohudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanayoendelea hivi sasa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, maonyesho haya yanajumuisha shughuli mbalimbali zikiwemo maonyesho. Maadhimisho haya yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoaka mataifa mbalimbali (Picha na Awadhi Ibrahim)........ Sag