WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, April 10, 2013

Uchambuzi Wa Habari; Viboko Mashuleni Au La, Ni Mjadala Wa Aibu!

3 05e57


Ndugu zangu ,

Moja ya habari kubwa leo ni hii;

“Serikali imesema itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua tovuti ya www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa njia ya mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji.

“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa na wageni waalikwa.” ( Mwananchi, Aprili 9, 2013)

Nionavyo;

Tunarudi nyuma miaka 50 badala ya kwenda mbele. Kuna wengi kama mimi tusioamini, kuwa, kumchapa mwanafunzi bakora ni kumsaidia kujenga nidhamu na kujituma.

Kinyume chake, kama ni nidhamu, utamjengea nidhamu ya woga na kufanya yale ambayo anadhani unataka ayafanye na si kuwa ayafanye kwa faida yake na jamii hapo baadae.

Viboko vinamfanya mwanafunzi asijiamini na hata akose uwezo wa kudadisi. Bado nakumbuka, kuwa nikiwa Darasa la Tano ilinitokea nikachapwa bakora darasani kwa kosa la ‘ kumdadisi sana mwalimu’. Mimi nilitaka kupata ufahamu zaidi lakini mwalimu aliniona nimekosa nidhamu.

Habari hiyo ya kwenye Mwananchi inazungumzia mpango wa kurudisha sheria ya adhabu ya viboko wakati kimsingi watoto wetu wanachapwa viboko mashuleni kila kukicha.

Wanafunzi kukosa nidhamu na kutokufanya vizuri kwenye masomo inachangiwa na mambo mengi. Tuanze kuyaangalia hayo kwanza kabla hatujawahamasisha walimu wakate bakora za miti ya mipera kuwachapa watoto wetu.

Na kwa Waziri mwenye dhamana kuonyesha kushabikia watoto kuchapwa bakora si kitu kingine bali ni jambo la kusikitisha sana. Na mjadala wa kama watoto tuwachape bakora au la, katika wakati tulio nao, ni mjadala wa aibu- A shameful debate!

Maggid Mjengwa,

Iringa.

Neno La Leo: ' Jogoo Mwembamba' Kaapishwa Urais- Ni Uhuru Kenyatta


2 4f64f

Ndugu zangu,
SIASA za Afrika zina yasiyolingana na siasa za wenzetu wa mataifa mengine. Afrika aliyechafuliwa sana anaweza kuibuka akawa msafi kama aliyesafishwa na sabuni ya punda. Na hasa, kama katika kuchafuliwa huko kutakuwa na shaka ya wanyonge kuhisi aliyechafuliwa  kaonewa.
Naam, wanyonge wengi Afrika wanauzoefu wa kuonewa.

Niliandika saa kadhaa tu baada ya matokeo ya uchaguzi wa Kenya kuanza kutangazwa; Kuwa kuna kila dalili kuwa Uhuru Kenyatta anaelekea kwenye ushindi.

Hiki ndicho nilichoandika;

"Afrika ukikuta jogoo wawili wanagombana, basi, hapo hapakosi mashabiki. Na kila shabiki aliyesimama kutazama mpambano wa majogoo hao, ujue, kuwa ana jogoo wake anayemshabikia.

Na jogoo anayemshabikia akishindwa pambano, shabiki ataondoka akisononeka. Kuna ambao watakosa hata hamu ya chakula siku hiyo. Kisa? Jogoo wake kagalagazwa!

Na kama jogoo mmoja ni mnene na mwingine ni mwembamba, ujue, kuwa jogoo mwembamba ana mashabiki wengi.

Ukifuatilia mwenendo wa Uchaguzi wa Kenya kuna dalili kuwa Uhuru Kenyatta ambaye pia anatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai anaelekea kwenye kupata ushindi.
Moja ya tafsiri ya jambo hili ni ilivyo kwenye fikra za wapiga kura ambao ni wengi ni watu wa kawaida- kuwa Uhuru anaonewa, hata na mataifa ya nje. Kwamba mambo ya Kenya yao yanaingiliwa pia na wasio Wakenya, tena Wazungu.

Wakenya wana historia ya mapambano magumu ya kudai uhuru kutoka kwa ' Wazungu'- ni tangu enzi za Mau Mau.

Pamoja na utajiri wake, bado Wakenya wengi wa kawaida wanamwona Uhuru kama mtu wanayefanana naye. Ni mwanadamu kama wengine. Huko nyuma Uhuru amekuwa na historia ya matatizo binafsi pia ya kimaisha, ikiwamo matatizo ya pombe, hivyo ya kifamilia pia. Wakenya wengi wanaishi wakijisikia kuwa wananyanyaswa na kuonewa. Wanamwona Uhuru Kenyatta kuwa ni mtu anayeonewa pia.

Hivyo, yawezekana kuna kura za ' kuonewa huruma' ambazo Uhuru Kenyatta anaweza kuzipata, hata kutoka kwa watu wa kabila la Wajaluo. Wanaojiona ' wanafanana naye'.

Na lingine ambalo laweza kutokea ni ukweli, kuwa katika matatizo mengi wanayoyakabili Wakenya kwa sasa, kuna ambao wanaikumbuka ' Bora ya jana' ya Mzee Jommo Kenyatta. Wanaikumbuka historia. hivyo, kuna Wakenya waliopiga kura za ' nostalgie'- Kura za ' Zilipendwa'.

Kuna Wakenya wengi walimpenda Mzee Jommo Kenyatta. Bado wanakumbukumbu za ' Fuata Nyayo'. Na Uhuru naye anaitwa ' Kenyatta'- Jina lake la pili. Ni mwana wa Mzee wa ' Fuata Nyayo.

Naam, Nyayo zilishapotea. Kuna wenye hamu ya kuzitafuta. Wanaamini Uhuru atawasaidia kuziona. Na tusubiri tuone.”
Na liwe Neno La Leo.
Maggid,
Iringa

Monday, April 8, 2013

Mkapa atema cheche; ataka viongozi wafuate misingi ya Nyerere

 
Na Phinias Bashaya,

 Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa amesifia utawala wake kwa kuongoza taifa bila ya kubaguana na amesikitishwa na matukio ya udini, ambayo yanaashiria kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania katika siku za karibuni.

Akitoa salamu zake baada ya kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Desdelius Rwoma, Mkapa alisema anachojivunia ni kuheshimiwa na waumini wa madhehebu yote.

“Katika kipindi cha uongozi wangu, viongozi wa madhehebu yote walikuwa wakinisisitizia kuwa sisi sote ni ndugu pamoja na tofauti zetu za kiimani. Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,” alisema Mkapa, ambaye aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995-2005.

Mkapa alionya kuwa taifa limeacha misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara zote alisimamia umoja wa taifa.

“Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,” alisema.
Mkapa ambaye hakupanga kuongea lolote katika tukio hilo, alitaka taifa lijenge utamaduni wa kupendana, huku akilaumu kuwa kizazi kipya cha uongozi kimeanzisha mambo ya ajabu ya kukosa upendo na kudhalilishana.

Pia alitahadharisha kuwa zama hizi kumeibuka mitafaruku mbalimbali na kuwakumbusha Watanzania kuwa ni wakati wa kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mkapa alisema mara nyingi alishauriana na viongozi wa dini katika masuala ya kijamii na kiroho na kumtaja askofu mpya wa Bukoba, Rwoma na Mtangulizi wake aliyestaafu Nestory Timanywa kuwa alishirikiana nao katika masuala ya wananchi. Onyo la Mkapa limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukemea mambo ya kidini na kutetea Serikali yake haiongozi kwa misingi ya ubaguzi.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alikwenda mbali zaidi na kudai amekuwa akilalamikiwa na viongozi wa madhehebu ya Kikristo na yale ya Kiislamu.

Maneno ya Mkapa na Kikwete yamekuwa katika kipindi hiki taifa likiwa limetikiswa na matukio yenye mwelekeo wa chuki za kidini. Matukio makubwa yakiwa yale ya kuuawa wa Padri Evarist Mushi huko Zanzibar na Mchungaji Mathayo Kachila wa Geita.
Pia kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Sheikh Fadhil Soraga na vurugu za mambo ya kuchinja huko Geita na Tunduma.

Askofu Mpya wa Bukoba Rwoma alimshukuru Mkapa kwa kuzungumzia umuhimu wa amani ya nchi, huku akisisitiza suala la upendo miongoni mwa wananchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye jana alitaja vyanzo vya vurugu zinazoendelea nchini kuwa unatokana na tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua santuri ya nyimbo za dini kwa Kwaya ya Mt Joseph, Mfanyakazi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Sumaye alionya kuwa kama hali ya utajiri kwa baadhi ya watu itaachwa na kuendelea hivyo, ni wazi kuwa nchi haitatawalika kwa amani.
 
“Binadamu mwenye njaa na aliyekata tamaa kamwe hawezi kutawalika kwani kila wakati anahisi kutengwa na kundi jingine,” alisisitiza Sumaye.
 
source: Mwananchi

Dk Salim ataka Serikali kukomesha vurugu

 
Na Nuzulack Dausen, Mwananchi

 Dar es Salaam. Mwanadiplomasia mkongwe nchini, Dk Salim Ahmed Salim amesema amesikitishwa na vitendo vya vurugu za dini zinazoendelea na kuzitaka mamlaka husika kudhibiti hali hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, baada ya kumalizika Kumbukumbu za mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda miaka 19 iliyopita, Dk Salim alisema hali hiyo inatakiwa kudhibitiwa mapema kabla amani haijatoweka.

Dk Salim ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), alisema kila Mtanzania ana wajibu kuhakikisha anadhibiti uchochezi na vurugu za kidini, ili kulinda amani ya nchi ambayo imedumu kwa muda mrefu.

“Vurugu za dini ni jambo la kusikitisha na hatari sana, nchi hii ni ya Watanzania wote bila kujali itikadi za imani, hivyo tunatakiwa kulitatua tatizo hili mara moja,” alisisitiza Dk Salim.

Alisema Serikali, viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za dini, taasisi za kiraia na wananchi hawana budi kukaa pamoja kuhakikisha wanalitatua tatizo la migogoro ya dini linalotaka kuvuruga amani ya nchi.
Alisema kuna haja ya kuendeleza jitihada za kulitatua tatizo hilo mara nyingi zaidi ya hatua iliyofikiwa, ili kulinda mustakabali wa nchi.

Wakati huohuo, Dk Salim alizitaka nchi za bara la Afrika kuwa chachu ya kutatua matatizo ya ndani ya bara lao, badala ya kutegemea watu kutoka nje.
Dk Salim alisema nchi za Afrika zinatakiwa kuwajibika ipasavyo kwa matendo yao, kwa kutafuta suluhu haraka iwezekanavyo siyo kutegemea taasisi kutoka nje ya bara.

“Lazima watafute suluhu za matatizo ambabyo yanawakabili, wahakikishe wanayadhibiti haraka ipasavyo kabla hayajafikia mahali pabaya” alisisitiza.
Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda nchini, Dk Benjamin Rugangazi alisema maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ni salamu kwa ulimwengu mzima katika harakati za kudumisha amani na upendo, ili kuzuia mauaji kama hayo yasitokee tena. 
 
source: mwananchi

Sunday, April 7, 2013

Kumbukumbu ya Sheikh Abeid Aman Karume;Fatma asimulia siri yake na Mzee Karume



Mama Fatma Karume akisalimiana na Rais Jakaya Kikwete katika moja ya sherehe za kitaifa.  Picha na Maktaba yetu. 
Na Masoud Sanani,

Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku
hiyo mwaka 1972
Leo Aprili 7 Watanzania wanakumbuka kifo cha aliyekuwa Rais waKwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku hiyo mwaka 1972. Mwandishi Wetu, MASOUD SANANI anazungumza na aliyekuwa mke wa Mzee Karume, Fatma Karume juu ya Mzee Karume na masuala mengine kadhaa. Mwanamke huyo mcheshi na mwenye bashasha anajibu maswali ya mwandishi kama ifuatavyo.
Swali: Mama Fatma mlikutana wapina Mzee Karume na ilikuwaje hadi mkawa mume na mke?
Jibu: Mzee Karume alikuwa mtu wa kusafiri kwenda Ulaya mara nyingi. Aliporudi hapa akaunda kikundi cha kupiga muziki wa dansi kilichoitwa African Dancing Club pale Michezani. Wakati huo kulikuwa hakuna bendi wakawa wanapiga santuri, vijana wakawa wanacheza.
Siku zinakwenda, mambo yanafunguka mtu mmoja akiitwa Salum Beni akajitokeza kupiga muziki wakawa wanamkodi. Mara nyingi akawa anawapigia hasa wakati wa kuvunja jungu na sikukuu.
Akawa maarufu.Akawa anatakiwa kupiga sehemu zingine, sasa huyu Beni akawa anawapiga chenga.Wakamchukua mtu mwingine akiitwa Rashid Kigogo, sasa huyo akawa anawapigia muziki. Huyu Kigogo alikuwa mume wa mama yangu mkubwa alikuwa akiiishi pale Mwembeladu Mbuyupacha. Wakati wa siku za sikukuu nilikuwa nikienda kwa mama mkubwa. Siku moja Mzee Karume alikuja hapo kuongea na Mzee Kigogo akaniona wakati huo nikiwa kijakazi mzima. Akamuuliza mwenyeji wake huyo ni mtoto wa nani? Mzee Kigogo akamjibu ni mwanangu lakini Mzee Karume hakutaka kuamini.
Akamsisitizia ni mwanangu. Karume akasema anataka kuja kuniposa. Mzee Kigogo akamwambia ili uamini kuwa ni mwanangu nitakuja naye kwenye dansi. Siku hiyo Mzee Kigogo akanichukua kwenye dansi namikwa mara ya kwanza nikawaona watu wakicheza dansi.Mzee Karume akawafuata wazee akaposa na akakubaliwa na baada ya muda akanioa.
Swali: Arusi yenu ilikuwaje?
Jibu: Haikuwa arusi kubwa. Shughuli ilifanyika kwetu, Bumbwini. Aliporudi mjini akatuma gari, nakumbuka lilikuwa jeusi, wakati huo si rahisi kwa gari kwenda shamba. Nikachukuliwa nikafikia kwa mama mkubwa nikashinda hapo na usiku nikapelekwa kwangu, Kisimamajongoo. Kikundi chake cha African Dancing Club wakafanya sherehe wakapiga dansi hapo nyumbani na wakacheza sana.
Swali: Maisha mapya yalianza vipi?
Jibu: Nilikuwa mke wa nyumbani nikatawishwa. Nikapata mimba lakini haikuwa riziki, badaye nikapata mimba ya Amani na baadaye Ali ambao ndiyo watoto wangu pekee wa kuwazaa.
Mzee Karume alishaoa kabla yangu, lakini bahati mbaya hakujaaliwa kupata watoto. Lakini nilipoolewa mimi hakuwa na mke kwa hiyo sikuwa na mke mwenza.
Lakini, alipokuja kuwa Rais alioa wake wengine, wakati ule ziliingia zile ndoa sijui zinaitwaje, viongozi wengi walioa na yeye akaoa na ana watoto wengine watatu, wanajuana na kaka zao na mimi wananijali.
Awali wakati wa maisha yetu, Mzee Karume alikuwa anafanyakazi bandarini. Walikuwa na ushirika wao wa boti, walikuwa wanasafirisha watu na mizigo. Hiyo ndiyo iliyokuwa kazi yake.
Swali: Mzee Karume alikuwa ni mtu wa aina gani?
Jibu: Mzee Karume hakuwa mtu mwenye hasira. Alikuwa mtu wa kupenda watu. Alikuwa na kipaji, lakini zamani tulikuwa hatujui vipaji. Alikuwa mtu bashasha alikuwa akipenda kusaidia watu. Amenifunza mambo mengi na kunikataza mengi.
Swali: Hali ya sasa unaionaje tangu kifo cha Mzee Karume, malengo aliyoyapanga yamefikiwa?
Jibu: Kila mtu anapoingia madarakani anakuwa na malengo yake. Alikuwa na mipango ya kuwa na nyumba kama vile Michenzani na nyumba za vijiji. Akajenga sehemu mbalimbali.Sasa tujiulize zile nyumba alizojenga bado zipo?Zimeongezeka au vipi? Nilicho na hakika ni kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bado ipo.
Swali: Ndoto za Mzee Karume za maendeleo ni kuifanya Zanzibar iwe kama Ulaya, unadhani alifanikiwa?
Jibu: Alifanikiwa lakini hakupata nafasi ya kumaliza kutekeleza dhamira yake. Angepata nafasi,leo tungekuwa na mengi ya kujivunia. Aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa amekaa madarakani kwa miaka minane tu.
Swali: Mzee Karume alipenda umoja, mwanawe Amani Karume alikuwa injinia wa kuleta maridhiano Zanzibar akishirikiana na Maalim Seif Sharif Hamad. Lakini, hali inaonekana kuanza kujirudia kama zamani (kabla ya maridhiano) unadhani nini kifanyike?
Jibu: Kwa upandewa matokeo mabaya na vipeperushi vya matusi na vitisho yanatokea kwa sababu ya utashi wa watu. Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar sijaiona kasoro yake. Matokeo mengine ni kwa utashi wa watu, wengine hawana uvumilivu.
Swali: Katika kitabu chake kimoja Mzee Karume aliwahi kuandika “election (uchaguzi) ni ngazi ya kikoloni”. Unadhani alikuwa na maana gani?
Jibu: Uchaguzi ndiyo uliotufikisha mpaka tukafanya mapinduzi. Tulifanya uchaguzi lakini haukutoa matokeo sahihi. Mtu anaposhindwa kwenye uchaguzi hubaki na chuki. Ndiyo hivyo ilivyo na hata sasa baadhi wanapokosa nafasi hata za kuteuliwa hubaki na chuki na haya yapo hata katika vyama vya CCM na CUF.
Swali: Je, kwa mtazamo wako kuna umoja thabiti wa wanawake wa Zanzibar?
Jibu: Hakuna umoja wa wanawake wa Unguja na Pemba, kuna umoja wa wanawake wa Tanzania. Na huu umetokana na muungano wa vyama (ASP na TANU na kuzaliwa CCM). Mzee Karume aliunganisha serikali hakuunganisha vyama. Muungano wa vyama ukaleta umoja wa Watanzania.
Swali: Kuna madai kuwa Mkataba wa Muungano kati ya Mzee Karume na Mwalimu Nyerere ulikuwa wa miaka 10. Je, kuna ukweli wowote juu ya jambo hili?
Jibu: Mimi sijui.
Swali: Je, bado unafurahishwa na mwenendo wa muungano unavyokwenda sasa?
Jibu: Mzee Karume alipokubali Tanganyika na Zanzibar ziungane, watu hawakujua faida ya muungano. Lakini sasa wengi wamefaidika kwa vile una faida kwa watu. Kwa vile jambo lina faida kwa watu na mimi ni mtu silioni baya. Hata hivyo, kero za muungano zirekebishwe ili mambo yaende sawa.
Swali: Mchakato wa Katiba Mpya unaendelea, je, kwa mawazo yako ungependa Zanzibar iwe katika mfumo gani?
Jibu: Mimi sitaki kujiingiza mahala ambapo pameingia sheria. Ukiingia utakuja kukosea sheria uone vibaya.Waache wanaohusika wafanye tuone masilahi yako wapi.Marekebisho ya kero za muungano yakishafanywa haya yote yatakwisha.Sasa tufuate sheria.
Swali: Je, wakati wa utawala wa Mzee Karume na sasa hali ya ushirikiano kati ya Waunguja na Wapemba ikoje?
Jibu: Mzee Karume hakuwabagua Wapemba aliwapa uwaziri na ukuu wa chama. Tulikuwa tunakwenda Pemba kwa meli tunakaa siku mbili tatu na watu wa Pemba. Katikati kukaja siasa baada ya vyama vingi vya siasa, kukawa na CCM na CUF viongozi wakawa wanatukanana kwenye majukwaa. Nani hakushuhudia? Ukakosekana ushirikiano angalau sasa imekuja Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Amani na Maalim Seif walifanya kazi kubwa na walijitoa ili kuleta maridhiano haya ambayo yanafaa yaendelezwe.
Swali: Wakati wa mapinduzi inasemekana Mzee Karume hakushiriki moja kwa moja. Ni kwa sababu gani na alikuwa wapi?
Jibu: (Anacheka kidogo). Mimi ndiyo mke wake Mzee Karume. Najua baadhi ya mambo. Mapinduzi walijua watu wachache sana.
Yeye alikuwa na mipango yake na yeye ndiye aliyekuwa mkuu. Alikuwapo hapa Zanzibar. Lakini hakuniambia hata mimi kuwa kuna mapinduzi siku hiyo. Ililia risasi ya kwanza na ya pili nikamwambia unasikia risasi hizo, ndiyo akanieleza kuwa kuna mapinduzi wameyaandaa na amewatuma vijana.
Akanieleza kuhusu mpango mzima wa mapinduzi na akanipa wosia akanieleza mambo kadhaa, akasema;“Tukifanikiwa itakuwa vyema lakini tukishindwa mimi nitakuja kuchukuliwa na kufungwa.”
Usiku wa saa 10:30 gari ikaja ina alama yetu ya Kisima kwa hiyo nikawa sina wasiwasi. Yule mtu akashuka akaenda kwa nyuma akagonga mlango na akaondoka na Mzee Karume. Kamanda anapeleka jeshi lake haendi mwenyewe vitani.
Source: Mwananchi

Saturday, April 6, 2013

Philip Mangula na Mkewe Yolanda Kaberege Wameremeta

 Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Philip Mangula na Mkewe Yolanda Kaberege leo wakiingia kanisani 
Akifungisha Ndoa Hiyo Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kusini Njombe Isaya Mengele Amekumbusha Maneno ya Mungu na Kuwataka Wanandoa Kuishi Kwa Misingi ya Dini Kama Ilivyoelekezwa Kwenye Vitabu Vya Dini.
 Kushoto ni msemaji wa familia ya mzee Philip Mangula Dr.Lechion Kimilike ambaye ni Mhadhiri wa chuo kikuu huria cha Tanzania Tawi la Njombe[NJOMBE OPEN UNIVERSITY].
 Kulia ni mkuu wa wilaya ya Njombe Bi.Sarah Dumba akiwa na waziri mkuu Mizengo pinda katikati akifuatiwa na Katibu mkuu wa CCM.
 Waziri mkuu Mizengo pinda akisalimiana na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa wilaya ya Njombe bwana Lupyana Fute[Jacky's]ambaye ni diwani wa kata ya Njombe mjini leo wakati wa Harusi ya Mzee Philip Mangula.
 Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana Katika harusi ya mzee Mangula leo Njombe.
 Hapa ni ndani ya kanisa la KKKT Dayosisi ya kusini Njombe Mjini ambako pingu za maisha kwa mzee wetu Mangula zimefungwa.
Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Philip Mangula na Mkewe Yolanda Kaberege leo wakifunga pingu za maisha. Picha na Gabriel Kilamya.Picha Zote na Picha na Gabriel Kilamya
 
source: Haki Ngowi 

Taswira Za Mtuhumiwa wa Mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili mjini Zanzibar,

 Mtuhumiwa wa Mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili mjini Zanzibar, Omar Mussa Makame (35) akiongozwa na Askari polisi kuingia katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kusikiliza kesi inayomkabili.
 
   
Mtuhumiwa wa Mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili mjini Zanzibar, Omar Mussa Makame (35) akiwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kesi yake kutajwa mahakamani hapo.
 
  Mtuhumiwa wa Mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili mjini Zanzibar, Omar Mussa Makame (35) akiwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kesi yake kutajwa mahakamani hapo.
 
 
Mawakili wanaomtetea Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri , Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki parokia ya minara miwili mjini Zanzibar, Omar Mussa Makame (35) wakili Abdalla Juma (kulia) na Rajab Abdalla wakipitia majalada kabla ya kutajwa kwa kesi ya mteja wao katika mahakama Kuu Vuga mjini Zanzibar.Picha zote na Haroub Hussein
source: haki ngowi