MACHO YETU YANAWANGALIA
DR.MAGUFULI VS MHESHIMIWA LOWASA NA TANZANIA TUNAYOITAMANI BAADA YA UCHAGUZI
2015
JE KIONGOZI GANI KATI YA
HAWA WAWILI NI:
- MWADILIFU
- MWAJIBIKAJI
- MKWELI
- MTETEZI WA AMANI
- RAFIKI NA MTETEZI WA WANYONGE
- SHUPAVU KATIKA MAAMUZI
- AWE TAYARI KUTUVUSHA KAMA TAIFA
KUTOKA KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI
- MTU WA WATU
- MKUZAJI WA DEMOKRASIA
- MWOGOPA MUNGU
- ANAYEWEZA KUKEMEA MAFISADI BILA
WOGA
Taifa letu linaelekea
katika uchaguzi wa viongozi ambao kupitia vyama vyao vya siasa wataunda
serikali ya kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya uchaguzi
wa October 2015.
Mimi jicho langu kubwa
ni kwa kiongozi Yule ambaye atashika hatamu ya kuongoza Taifa letu na ambaye
atahamishia makazi yake IKULU.
Kama taifa ni wakati
mzuri umewadia sasa tuweze kumchagua mtu makini, mbunifu, mwaminifu, mwadilifu
na mzalendo wa kweli kwa wananchi wanyonge na masikini wa Taifa letu.Kiongozi
ambaye tunamwitaji lazima atambue kuwa kuwa wananchi wana haki ya kupata
chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora bora huduma bora ya afya
na usalama wa mali zao.
Akumbuke kuwa
wanaompeleka Ikulu ni wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na sio
marafiki wachache wenye pesa. Na ajue kuwa anapochaguliwa kuongoza, ajuwe
anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri awe tayari kuongoza kwa
kuonyesha njia awe ni mfano wa uwajibikaji.
Kiongozi tutakaye
mchagua lazima awe na tabia ya kuongoza kwa kutofikiria zaidi maslahi binafsi
wazo hili liwe mwiko. Tutataka atumie ustadi wa uongozi ambao utasimamia haki
za waongozwa; wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya
kutenda kwa haki.
Hatuki kumchagua
kiongozi ambaye baada ya kuchaguliwa ataigeuza ikulu kuwa Ni pango la wizi,
rushwa, uonevu, unyonyaji wa rasilimali za watanzania kwa masilahi binafsi
pamoja na marafiki wachache au chama chake. Tunahitaji kiongozi ambaye uadilifu kwake utakuwa ni sehemu
ya maisha yake ya kila siku bila kujali au kupendelea mtu au kikundi cha watu
au vile vile awe na uwezo wa kuwajibisha viongozi watakao kuwa chini yake
wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.
Mwalimu Nyerere
aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee
tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa
Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya
mwanadamu. Kiongozi wetu tunataka
aongoze katika misingi hiyo.
Kiongozi lazima ajue
kuwa hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani
ataongoza watu wake wateule. Tukiangalia katika historia ya dunia sehemu
nyingi, Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote
ilisitawi na kubarikiwa katika njia nyingi. Walipomsahau Mungu kupitia rushwa
na ufisadi na dhuluma shida na dhiki zilianza.
Kama Mungu ndiye
anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za
Mungu jinsi alivyoongoza. Kiongozi anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu
anahakikisha kwamba mwenendo wake unapatana na Neno la Mungu.
Itakuwa
jambo bora tuweze kupata kiongozi Mkuu Raisin a viongozi ambao kwa kweli nao
watakuwa bora katika kuongoza Taifa letu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila
mtanzania. Tanzania ya leo inahitaji kiongozi ambaye atawajibika; na kuonyesha uzalendo
na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.Pengine katika msingi huu tutahitaji
kiongozi ambaye anauelewa mpana wa kuelewa shida za wananchi mwenye UWEZO wa
kufikiri kwa usahihi, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa usahihi wakitambua
dhamana ya uongozi ambao taifa linampa. Kwa hivyo tutahitaji RAISI pamoja na mambo mengine
awe na UWEZO kuongoza kwa usahihi.
Vile
vile tunahitaji viongozi wajao katika serikali zetu mbili wawe ni watu wa WATU;
viongozi ambao wataweza kuona matatizo ya wananchi wao ni yao na yanawakera na
hata kuwanyima usingizi, hivyo itakuwa jukumu lao kuongeze nguvu ya uwajibikaji
wa kusimamia rasilimali za Taifa. Nasi kama wananchi tuwe na uwezo wa kuwapima
kwa watakacho kifanya wakiwa madarakani.
Pengine
tutahitaji kidogo aina ya viongozi wetu wawe wakali japo sio sahihi kutumia
msemo huu lakini wakati mwingine ile tuweze kupiga hatua ya maendeleo
tutahitaji viongozi wenye mawazo ya uwajibikaji chanja; ili tuweze kubadilisha kidogo maadili ya
utendaji wetu wa kazi kwa Watanzania;
Tunahitaji Maraisi katika serikali
zetu mbili ambao wanaweza kuwawajibisha mara moja
watendaji wake ambao wanashindwa kuwajibika, tuwapate viongozi ambao wanaweka
pembeni huruma ambazo hazina msingi kwa Taifa;
Nafikiri
itakuwa ni jambo la busara kama sisi kama watanzania na wapiga kura tukiweza
kuepuka tabia ya kuwachagua viongozi wetu kwa Mazoea, Mkumbo na kwa kutumia Hisia na mapenzi
binafsi juu ya wagombea au chama. Nafikiri umefika wakati tuwachagua viongozi
wetu kwa upeo wao wa kuona mambo mbalimbali nauwezo wao wa uongozi kama
kiongozi na sio kama chama, hapa nazungumzia uzoefu wa kiongozi kabla ya
kuchaguliwa kuwa raisi je amefanikiwa kwa kiasi gani katika idara ambayo
amewahi kuongoza? Ana mzigo gani wa hisani ambao anatakiwa arudishe baada ya
kuchaguliwa.
kama taifa tunafahamu kuwa taifa letu bado linaogelea sana katika tope nzito la matumizi mabaya ya rasilimali ya Taifa Rushwa na Ufisadi vimekuwa ni wimbo wa kila siku. Tumeendelea kuona jinsi pesa za walipa kodi zikipotea na tumeendelea kuona jinsi umasikini wa watanzania ukiendelea kuongezeka.
Basi tunahitaji Raisi
ambaye analiona hili kuwa ni tatizo na linahitaji utatuzi wa haraka. Lazima
tukubali kuwa mabadiliko yoyote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yenye kulenga
kuletea faida wananchi walio wengi hayawezi kufanikiwa bila ya kutokomeza rushwa
na ufisadi. Kiongozi wetu aweze kuliona hili na kuwa tayari kupambana nalo
akiamini kuwa Tanzania rushwa imeshaota mizizi, NA TANZANIA BILA RUSHWA
INAWEZEKANA.
Nafahamu mamilioni ya
watanzania wamepoteza matumaini na hali zao za maisha lakini kupitia yeye
ataweza kulitatua tatizo hili na kuwachukulia sheria wale wote ambao wamehusika
katika uchafu huu,
Tunahitaji kiongozi
ambaye ataweza kufanya kazi na watanzania na kuendelea kuwaelimisha kuwa ni
jukumu la mtanzania mmoja mmoja kuwajibika kwa vitendo na kupunguza kulalamika
kila siku kama Mheshimiwa Yusuph
Makamba alivyowahi sema kuwa “maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao wenyewe, kwa kufanya
kazi. Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba kila kitu
wanategemea kitafanywa na serikali … Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa
kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,”. Kauli hii ni nzito kiongozi wetu anayetaka
kuongoza taifa hili lazima awe tayari kuwaeleza wananchi bila kuogopa kukosa
kura katika kipindi kingine cha uchaguzi kuwa uvivu ni adui wa maendeleo.
Daima
tunapofikiria kuwachagua viongozi wa juu wa Taifa letu tunayakumbuka maneno ya
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi
sema kuwa kazi ya uraisi ni
ngumu na inahitaji busara na kuchukua maamuzi magumu, ili kuweza kutimiza haki
wananchi wanyonge “ walala hoi ”; aliendelea kushauri kuwa “Ole wale
wanaokimbilia Ikulu, wanakimbilia nini, Ikulu hakuna biashara ya kufanya, Ikulu
ni mahali patakatifu na kama kuna mtu anadhani kuwa kukaa Ikulu ni raha basi
angeniuliza mimi katika kipindi cha miaka 21 niliyokaa Ikulu nimefanya biashara
gani,Ikulu ni mzigo mzito”
Mwandishi Nyenyembe
aliwahi andika kuwa “Kwa maana hiyo mtu
anapoamua kuulilia uraisi;uraisi sio pambo la nchi,uraisi ni jalala, uraisi ni
chumba cha kuhifadhia maiti,uraisi ni njaa,uraisi ni magonjwa,uraisi ni bakuli
la kukingia machozi ya watu wanyonge wanaolia kila siku wakihitaji msaada na
kama hawapati anayetazamwa hapo ni raisi”
Katika demokrasia
wananchi ndio wenye dhamana na uwezo wa mwisho wa kumrejesha mwanasiasa
kuendelea kuhozi madaraka; pamoja na umaarufu wake, uadilifu na utaalam katika
kushughulikia maswala ya siasa bila ridhaa ya mwananchi sio rahisi kurejea
madarakani;
Hebu tuanagalie historia
ya vyama vingi na chaguzi za Zambia zinaainisha kwa ukomavu wa demokrasia ndani
ya Zambia wananchi ndio wenye sauti ya mwisho wananchi wa Zambia wanapima na
kuamua kulingana na utendaji wa viongozi wao na sio ushabiki wa vyama vyao;wamejitahidi
sana kuweka nchi mbele vyama baadae.
Tukiendekeza sana kushabikia
sana vyama ndilo linalotuponza sana na wakati mwingine kurudisha maendeleo yetu
nyuma katika nchi nyingi za kiafrika; wananchi wanakumbatia zaidi chama na sio
utendaji wa viongozi wa vyama vyao; pamoja na uganganianyi wa madaraka kwa
baadhi ya viongozi waliomaliza muda wao.
Kama wananchi tunatakiwa
kuanza kuangalia upya maamuzi yetu dhidi ya viongozi wetu; tunahitaji viongozi
waadilifu na viongozi wa namna hii wataweza kuchukua hatua kwa maslahi ya jamii kwa manufaa ya wote,
na wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo kulingana na
utaratibu wa nchi husika na kukendelea kukubalika kwako kwa masilahi ya wengi;
Katika mfumo wa kidemokrasia wa serikali, ambapo nguvu ya utawala ina inapatika
upya kila baada ya miaka mitano kama ilivyo katika nchi ya Tanzania ni wananchi
ndio wenye dhamana ya kuwarejesha madarakani viongozi wanaowapenda kufuatia
sera za vyama vyao na ubora wao.
Nchi ya Zambia
imetufundisha kuwa hakuna kiongozi anayemiliki watu, hakuna chama chenye
hatimiliki ya kuongoza nchi Milele; au kuwa kikundi cha wananchi ambao wao
matakwa yao lazima kila mwananchi akubaliane nayo;kama itakuwa hivyo basi kuna
tatizo na wananchi katika nchi hiyo; wananchi mara zote wanategemea na
wanataka mabadiliko makubwa ya
kiuchumi hawahitaji propaganda za chuki, wanahitaji kufaidi raslimali zao wazambia walikuwa wanashangaa utajiri wote unaotokana
na shaba unakwenda wapi? Pale ambapo hawakuridhika hawakuwa na papara
walisubiri tu wakati ulipofika walimweka pembeni kiongozi na kumpa dhamana
kiongozi mwingine. Lazima tukubali kuwa katika nchi zilizopo kusini mwa
Afrika Zambia imekuwa na
imeonyesha kwa vitendo kukabiliana na changamoto
za mabadiliko ya kisiasa kwa ustarabu mkubwa wenye tija kwa Taifa:
Maamuzi ya wananchi
katika awamu tofauti Zambia umeendelea kuwashangaza viongozi walioko madarakani
kuanzaia enzi Kaunda, pamoja na
ukongwe wake wa kutawala kwa miaka 27 hadi awamu ya Banda; Kiini cha msukumo
huu nini? Wananchi wanatamani kupata maisha bora na kuwa viongozi wenye kiwango
cha juu kabisa cha uadilifu kuweza kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo sio
kwa nadharia bali vitendo;
Viongozi wetu wa vyama
vya siasa wamesahau kuwa, Kimsingi, raia huzaliwa wakiwa huru dhidi ya
mikingamo ya kijamii, kwa lugha ya kitaalamu tabula rasa. Lakini mikingamo hii
ya kijamii huingizwa katika fikra za wananchi kupitia itikadi na elimu ya siasa
katika vyama ambavyo wanafuata; na wakati mwingine hata kupitia shule na sehemu
za ibada.
Cha ajabu haitoshi
kuivuruga jamii peke yake tumeona na tunaendelea kuona kuwa viongozi wetu wa
kisiasa hapa nchini wamekuwa wakigombana kila mara katika mambo ya msingi na
yasiyo na msingi. Kugombana si kubaya kama kunaleta tija, lakini kule kugombana
kunakofanywa kwa misingi ya kujitafutia umaarufu kunasabaisha viongozi
kushindwa kutekeleza majukumu yao ambayo yanatokana na ahadi wakati wakiomba
ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, ni dhambi ambayo haiwezi kuvumilika hata
kidogo.
Wakati tunaelekea katika
kipindi cha kuchagua viongozi wetu; sisi kama wananchi tuanze kujipima na kujua
ni kiongozi wa namna gani tuna mwitaji; tuziangalie khali zetu za uduni wa
maisha sisi bado ni masikini,
tunahitaji barabara bora; huduma za afya nzuri, elimu bora kwa vijana wetu;
ajira za kutosha kwa wenye sifa za kuajiriwa;
Kama Raisi John Kenedy
wa Marekani alivyowahi kusema ‘Wewe UMELIFANYIA NINI TAIFA LA LAKO’ ni wajibu
wa msingi kwetu kama wapiga kura kujiuliza swali hili je tumelitendea haki
Taifa kwa kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya serikali zetu mbili? Yatupasa
kutimizAa wajibu wetu kwa maisha bora kwa kila mtu kwa kuchagua viongozi bora
na sio bora kiongozi. Miaka mitano ni mingi sana tukichagua viongozi mbovu.
Wananchi tujiulize je
kama taifa tumaini letu ni lipi dhidi ya viongozi wetu wa siasa ambao
tunatarajia kuwachagua; tunahitaji viongozi wakuu wa nchi ambao wataweza kutupeleka kwenye nchi yenye neema na
amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa, kidini .
Niliwahi andika huko
nyuma kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya
tusiendelee;tukumbuke kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe,
juhudi zetu na misimamo yetu; tukiangalia kwa ujumla wanasiasa wanapoteza muda mwingi katika propaganda na sio
kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana
na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.
Wanasiasa wetu ndio
wapiga majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia
sisi wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya
utamaduni wa siasa za Tanzania kwa kuwachagua viongozi watakao endeleza
umasikini wa Taifa letu kwa faida ya wachache.
Kiongozi tunaemtaka
tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake
basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya
kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda sisi kama Taifa.
Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?
Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?
Taifa letu katika
kipindi cha miaka ya karibuni kiliingia katika vurugu za Mtwara, Dar es salaam
Zanzibar Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika; Je kiini cha vurugu hizi kimepata
jibu? Kama jibu ni hapana sasa tutahitaji viongozi wetu wakuu tutakao wachagua
wawe wanaweza kuona na kutumia muda wao katika kuleta majibu ya matatizo ya
wananchi wao;
Wananchi tunatakiwa
tuamke na tusiwape nafasi wanasiasa kutufanya sisi kuwa daraja la wao kuweza kutimiza malengo yao bila
sisi kujitambua kwa haraka; matokeo yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunaendelea
kuwa masikini.
Imefika wakati sasa hata
viongozi wengine tutakao wachagua tusirudie kosa la kuchagua viongozi ambao
wanasilka na tabia ya
kuzomeana,
kulaumiana, kutukanana;mwelekeo huu hautatusaidia sisi kufikia lengo letu la
kuwa na maisha bora
Nafikiri linalowezekana
leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi
tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina na mikono ya Muumba wetu
tu;
Baba wa Taifa aliwahi
kusema kuwa “Kupanga ni kuchagua”. Wananchi kwa kweli inatakiwa tujipange sasa kwa
maendeleo ya Taifa letu na kwa masilahi yetu binafsi ili kupata viongozi wetu
wakuu walio bora na makini. Tunataka tupate viongozi waadilifu kweli kweli.
Tukumbuke kuwa Uadilifu
ni karama, ya utambuzi wa kujifahamu kwa mtu binafsi hususa kiongozi wa
serikali, ambaye anatakiwa kufanya kazi zake kulingana na sheria na taratibu
ambazo hujenga, utamaduni, wa kuwajibika kulingana na sheria husika. Kwa kufuata taratibu nzuri za
utendaji kazi Uadilifu katika
kazi husaidia uimarishaji wa misingi ya utawala bora.
Kwa kujumuisha kabisa
uadilifu na utimilifu kwa uhusiano wa biashara yetu inayoendelea na kufanya
uamuzi, tunaonyesha kujitolea kwa utamaduni ambao unakuza kiwango cha uadilifu
wa hali ya juu kabisa; ni kweli kuwa uadilifu inahitaji uaminifu binafsi wa
kiongozi husika; uadilifu unahitaji uaminifu wa kupinga ubinafsi kwa kiongozi ambaye amepewa
dhamana. Uadilifu unaendana na Kuwa mkweli katika utendaji na kuishi kulingana
na maadili ya kazi na kuheshimu rasilimali kwa faida ya wengine.
Wajibu wa kutenda ukweli
ni wajibu wa juu kabisa wa uadilifu kwa viongozi wa umma; kiongozi wa umma
lazima atambue hali
halisi ambayo inaendana na wajibu kwa kufuata maadili hivyo kusambaza cheche
ili hata jamii nzima nayo iweze kuishi kulingana na maadili ya Taifa.
Kiongozi mwadilifu daima
hutakiwa kuonyesha uhusiano kati ya maadili yake ya utendaji na kwa urahisi
kabisa aweze kusema na nafsi yake ili isitawaliwe na tama ya rushwa ambayo itapingana na dhana
nzima ya maadili kulingana na kiapo chake. Hapa ni jukumu la serikali kuweka
mipaka bayana wa uhusiano kati ya maadili binafsi na sheria za utendaji wake
kwa manufaa ya umma. Uadilifu daiama huashiria haki, ikiwa na maana kuwa
kiongozi wa umma lazima aweka maslahi binafsi pembeni;
Uadilifu hujenga amani,
huleta ufanisi, kwani Watumishi wa umma watakuwa wanauwezo wa kuhakikisha
matumizi sahihi, ufanisi wapesa za umma. dhana na misingi ya uwajibikaji
anatarajiwa kufanya ya viongozi wa umma kuwajibika kwa matendo yao au kutotenda
Ni zinatakiwa kuongeza
uwazi wa serikali, kusisitiza na kuimarisha mwitikio wa kiserikali na uhalali
na kuboresha utekelezaji wa sera. Mwalimu Nyerere katika hija ya maisha yake,
alijitahidi kutanguliza masilhai ya watu wake, bila ya kujikita katika ubinafsi,
uroho na uchu wa madaraka; uchoyo na ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa
viongozi wengi ndani ya Taifa letu.
Maadili ni muhimu zaidi
na katika siasa na kwa maendeleo ya wananchi. Maadili ya kweli yatapunguza
wanasiasa kujishughulisha na rushwa.
MUNGU IBARIKI JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
NA UTUVUSHE SALAMA ILI TUWEZE KUWAPATA VIONGOZI BORA KWA MANUFAA YA WATU WAKO KATIKA UCHAGUZI WA MWAKA 2015.
No comments:
Post a Comment