WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 8, 2014

MISS TANZANIA MPYA LILIAN KAMAZIMA AFUNGUKA KUHUSU KUMRITHI SITTI MTEMVU!

Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kujiuzuru kwa Sitti Mtemvu aliyekua Miss Tanzania 2014 baada ya kuzuka Sintofahamu kuhusu Umri wake, Lundenga amesema Sitti Mtemvu aliandika barua ya kujivua taji na kuiwasilisha kwa kamati ya Miss Tanzania Novemba 5 2014 ambapo kamati hiyo imeridhia kujiuzulu kwake na kumvua taji.Hivyo taji hili na majukumu ya Miss Tanzania sasa yatachukuliwa na mshindi wa pili Lilian Kamazima aliyekaa kushoto katika picha ambaye taratibu za Miss Tanzania zinamruhusu kuchukua jukumu hilo, Hashim Lundenga ametangaza uamuzi huo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya JB Belmonte jijini Dar es salaam leo.

Miss Tanzania 2014 Lilian Kamazima akizungumza na waandishi wa habari kuelezea furaha yake baada ya kamati ya Miss Tanzania kumvisha taji hilo kutokana na kujiuzuru kwa Sitti Mtemvu aliyekuwa Miss Tanzania, Kulia ni Hashim Lundega Mkurugenzi wa kamati ya Miss Tanzania.Hashim Lundega Mkurugenzi wa kamati ya Miss Tanzania akionyesha barua iliyowasilishwa kwa kamati hiyo na Bi. Sitti Mtemvu mara baada ya kujiuzulu Umiss Tanzania na kujivua taji hilo.

source: matukiotz.com

Wednesday, November 5, 2014

Kumfanyia vurugu Warioba ni ishara mbaya kwa demokrasia


Katuni

Demokrasia ina miiko yake. Miongoni mwa miiko hiyo inayopaswa kuheshimiwa katika jamii yoyote inayojitambulisha kuwa ni ya kidemokrasia ni pamoja na uvumilivu wa kusikiliza hoja za wengine hata kama hazifurahishi.

Kwamba, kila mtu katika jamii anapewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusiana na jambo fulani huku wengine wakisikiliza na kuwa na uhuru wa kukubaliana na hoja husika au kuipinga kwa hoja nyingine madhubuti. Na imethibitika katika maeneo mengi kuwa jamii inayoheshimu mwiko huu hujikuta ikifanikiwa kwa kiwango cha juu.

Watu wake huendelea kuwa huru na maamuzi mengi hufanyika kutokana na uzito wa hoja. Wala si kichume chake. 

Aidha, jamii yenye kuzingatia kigezo hiki cha demokrasia hufaidi pia matunda ya kushamiri kwa upendo. Chuki huwa ni msamiati mgumu kwa watu wa jamii hii. Matumizi ya nguvu au hila za namna yoyote ile hukosa nafasi.

Bali, watu hushindana katika kufikiri. Hoja zenye mashiko ndizo hupata uungwaji mkono zaidi. Kwa kiasi kikubwa, taifa letu limekuwa likijitahidi kufikia kiwango hiki cha demokrasia.

Watu huvumiliana katika kusikiliza na kutoa hoja. Hukubaliana katika kutofautiana kwao.Hata hivyo, kile kilichotokea juzi wakati wa kongamano la kujadili mambo ya msingi ya kuangaliwa katika katiba inayopendekezwa hakiashirii kuwapo kwa ustaarabu wa kuvumiliana miongoni mwa baadhi ya watu.

Hiyo ni baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba kufanyiwa vurugu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na wazungumzaji wakuu wakiwa ni waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Cha kusikitisha, katika kile kilichoonekana wazi kuwa bado kuna safari ndefu ya kuelekea kilele cha demokrasia, baadhi ya vijana walianza kufanya vurugu wakati Jaji Warioba alipokuwa akizungumza. Walionekana wakiwa na mabango yenye ujumbe uliokuwa na maudhui yanayofanana. Cha kushangaza, hati iliyotumika kuandikia mabango hayo ilionekana pia kufanana kwa kiasi kikubwa, kama ilivyokuwa kwa aina ya mabango yenyewe na hata wino mzito uliotumika.

Yote hayo yaliashiria kwamba vijana waliomfanyia fujo Warioba walikuwa na ajenda iliyofanana, wakitekeleza kazi waliyotumwa na mtu mmoja au kikundi fulani cha watu. 

Hakika, watu hao walionekana wazi kwamba walitumwa kwa nia ya kumziba mdomo Warioba, wakiamini kuwa hiyo ndiyo njia nzuri ya kuhakikisha kuwa maoni ya Waziri Mkuu huyo mstaafu hayawafikii  maelfu ya Watanzania waliokuwa wakifuatilia mdahalo huo kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni. 

Muda mfupi baada ya kuibuka kwa vurugu hizo, polisi walifika katika eneo la tukio na kufyatua mabomu kadhaa ya machozi. Waliotekeleza mpango huu wakahisi kuwa wamefanikiwa. Ni kwa sababu baada ya hapo hakukuwa tena na mdahalo. Vurugu zao zikafanikiwa kusitisha utoaji maoni zaidi kuhusu katiba mpya.

Sisi tunaona kuwa hili siyo jambo jema. Kamwe,  haikubaliki hata kidogo kwa kikundi fulani cha watu kufanya vurugu kwa nia ya kuzuia maoni ya wengine kusikika. 

Ikumbukwe kuwa, mbali na Warioba kutumia uhuru wake kidemokrasia katika kutoa maoni yake kuhusiana na masuala ya katiba inayopendekezwa, vilevile ana historia isiyofutika nchini. Amewahi kushika nafasi mbalimbali za juu za uongozi zikiwamo za kuwa Mwanasheria Mkuu na pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kuzingatia ukweli huo, sisi tunaona kuna kila sababu kwa Watanzania wote kulaani matukio ya aina hii. Daima demokrasia idumishwe kwa kuruhusu kila mmjoja kutoa mawazo yake, alimradi hatukani wala kuvunja sheria za nchi.

Aidha, upo umuhimu pia wa kuhakikisha kwamba viongozi wastaafu kama Warioba wanapewa ulinzi madhubuti na yeyote anayejaribu kuwafanyia vurugu anafikiwa kirahisi na mkono wa sheria. Hili ni muhimu kwani litatoa fundisho kwa wengine wenye kufikiria mipango haramu kama huu wa juzi wa kumfanyia vurugu Warioba.

Vurugu ni ishara mbaya kwa demokrasia. Kwa sababu hiyo, hazipaswi kuachwa hivi hivi. Bali, Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake na kuwabaini wote waliopanga vurugu dhidi ya Warioba juzi na kisha kuwafikisha mahakamani ili wakapate wanachostahili.
 
CHANZO: NIPASHE

Tuesday, October 21, 2014

BREAKING NEWZ: MSANII WA BONGO FLEVA Y-P AFARIKI DUNIA

http://photos-a.ak.instagram.com/hphotos-ak-xaf1/10727233_709860805766368_1533290281_n.jpg
Tasnia ya Bongo Flava imepata pigo baada ya msanii wa kundi la Wanaume Family anaefahamika kwa jina la YP kufariki jana usiku baada ya kuugua muda mrefu ugonjwa wa kifua.

Meneja wa kundi la Wanaume Family amethibisha kifo cha msanii huyo na kueleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mrefu.



“Tatizo alikuwa anaumwa kifua muda tu, lakini alishaanza kunywa dozi lakini majuzi akazidiwa na tukampeleka hospitali. Jana ndo mwenyezi Mungu kampenda zaidi akamchukua. Wazazi wa marehemu wapo Keko pale, lakini wazazi wake baba na mama walifariki ila ndugu zake wapo, na kuna kibanda waliachiwa na wazazi wake, kwahiyo msiba utakuwa Keko.” Fella ameiambia Bongo5.
Kuhusu ratiba ya msiba huo, Fella amesema itafahamika leo majira ya saa saba mchana.
Mungu ailaze pema roho ya marehemu YP. Amen!

source: matukiotz.com

Monday, October 13, 2014

LEO NI SIKU YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE - 1922 - 1999


  • TUTAENDELEA KUENZI DAIMA MAZURI YOTE ALIYOTUACHIA;



"Inawezekana tatizo la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa kengele shingoni: taabu ni kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo. Na panya watakuwa wajinga sana wakidhani kuwa paka watajifunga au watafungana kengele shingoni"


"Hakuna umaskini mbaya kama umaskini wa mawazo, ni umaskini mbaya sana"

'Mtu mwenye akili akikuambia neno la kipumbavu -ukalikubali, anakudharau!'

Tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike mpaka nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale pasipo na matumaini, upendo pale palipojawa na chuki na heshima pale palipojaa dharau –


"tunataka kiongozi ambaye anachukia rushwa, na hata tukimwangalia usoni tunaamini anachukia rushwa, Sio ambaye hata ukimuangalia unajiuliza, mnh, huyuu????!" 


“TUNAPOZUNGUMZA habari za uhuru maana yetu nini hasa? Kwanza; kuna uhuru wa nchi,yaani uwezo wa wananchi wa Tanzania kujipangia maisha yao, wakijitawala wenyewe bila ya kuingiliwa kati na mtu yeyote asiyekuwa Mtanzania. Pili; kuna uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, maradhi na umasikini. Tatu, kuna uhuru wa mtu binafsi, yaani haki yake ya kuishi, akiheshimika sawa na wengine wote, uhuru wake wa kusema na uhuru wake wa kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayogusa maisha yake, na uhuru wa kutokamatwa ovyo na kutiwa ndani kwa kuwa tu kamuudhi mkubwa, japo kama hakuvunja sheria yoyote”.



“Lakini ni dhahiri kwamba mambo hayo yanategemea maendeleo ya uchumi, madhali nchi yetu bado masikini; na wananchi hawakupata elimu; na ni wajinga na wanyonge, basi uhuru wetu wa kujitawala unaweza kuhatarishwa na taifa lolote la kigeni lenye maendeleo na nguvu zaidi.”

...."Kiongozi anayetufaa Tanzania , ni yule anayejua kuwa nchi yetu ni masikini na watu wake ni masikini. Na ukimwangalia usoni ...uone anaguswa na umasikini wetu. Vinginevyo hatufai...."

“Kwa sasa uhuru wa taifa letu, mara nyingi ni uhuru wa maandishi tu; maana nchi yetu ni maskini mno, ni nyonge mno kulinganisha na nchi nyingine, hata hatuwezi kutimiza wajibu wetu kwa ukamilifu kwa binadamu wengine”.  

“Watu wenye mawazo tofauti, hata wakiwa wachache, lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika majadiliano bila ya hofu ya kusumbuliwa; mawazo yao na yashindwe katika hoja za majadiliano, siyo kwa vitisho au mabavu. Majadiliano yenyewe yatakayoleta uamuzi lazima yawape nafasi watu kusema kwa uhuru kabisa.  Hata baada ya kuamua jambo, watu wawe na uhuru kuendelea kulizungumza jambo hilo”




“Elimu inayotolewa ni lazima ijenge mambo matatu kwa kila mwananchi, akili ya kuuliza, uwezo wa kujifunza kutoka kwa wengine - na kuyakataa au kuyakubali kutokana na mahitaji yake - na uwezo wa kujiamini kama raia huru na sawa katika jamii, anayethamini wengine na kuthaminiwa kwa anayofanya na siyo kwa anachopata” 

Thursday, October 9, 2014

NINI HASARA YA DEMOKRASIA MATAYARISHO YA KATIBA MPYA JAMUHURI YA MUUNGANO TANZANIA?


Demokrasia imefafanuliwa katika namna mbalimbali; wengi wa wanazuoni wameeleza  kuwa “Demokrasia ni mfumo wa utawala ambao watu huwachagua  viongozi wa serikali yao wenyewe na kuainisha jinsi inavyopaswa kufanya kazi”. Wakaendelea kukufafanua kuwa “ Demokrasia hukuza ustawi wa watu wote kwani Kila raia ana haki ya kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za umma na katika mambo yote yanayoathiri maisha yake”.wengi wa wanazuoni wanakubalia kuwa Demokrasia inauwezo mkubwa wa kushugulikia  uwajibishaji serikali kupitia kura za maoni  na maamuzi yanayofanywa na wawakilishi wao katika vyombo mbalimbali vya maamuzi”.



Kwa maneno mengine Demokrasia ni  mkataba wa kijamii kati ya wananchi na watawala(serikali); mkataba huu ni wa pande mbili raia wana wajibu wa kutekeleza sehemu yao na serikali pia inawajibu wa kuwatendea raia matakwa yao. Kwa maneno mengine ni mkataba wa kijamii unadhihirisha uaminifu na matumaini ambayo raia  wanakuwa nayo kwa wawakilishi wao ili watende kwa niaba yao.na pale wanaposhindwa kufanya majukumu ambayo jamii iliyowachagua imewapa wananchi wanayo nafasi ya kuwachagua wawakilishi wengine.


Swali la msingi chimbuko la demokrasia ni nini?

Tunafahamu kuwa lengo kubwa la demokrasia ni kuleta mabadiliko kwa wananchi wake, ili kuwaletea maisha mazuri, kuwatoa  kwenye dimwi la umasikini na kuwaletea maisha bora kwa jamii nzima na sio kikundi kidogo cha watu; kwa msingi huu ukifuatwa vizuri na kutekeleza kwa ufanisi ni ukweli usiopingika kwamba mfumo wa utawala wa kidemokrasia una umuhimu wake katika  maendeleo ya jamii nzima.

Je demokrasia inatumika wakati wote?

Hili ni swali lenye changamoto kubwa; lakini ni lazima ieleweke na tujiulize kuwa  ni wakati gani demokrasia inapaswa kutumika na wakati gani siyo muhimu kuitumia; Nasema hivyo kwa sababu siyo wakati wote ni muhimu ama lazima kutumia mfumo wa demokrasia umaohusisha maamuzi ya wengi, ndani ya  uendeshaji wa serikali na maamuzi yake; mfano mzuri ni uamuzi ambao uliwahi tolewa Mheshimiwa Raisi Kikwete baada ya kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa na kukubaliana kuwa mchakato wa kupata katiba mpya utakao husisha maoni ya wananchi utaendelea baada ya uchaguzi ujao.  Uamuzi huu umekuwa tofauti na uamuzi wa awali kuwa Katiba mpya itapatikana kabla ya uchaguzi 2015.

Je msingi wa demokrasia ni nini?

Msingi wa demokrasia inawapendelea sana walio wengi kwa kukubali mawazo ya wengi. Usahihi wa hoja mara nyingi sio jambo muhimu kuliko wingi wa ufuasi. Walio wengi katika kufikia muafaka wa jambo kulingana na demokrasia ndio washindi wa demokrasia hata kama hawana hoja

Je hasara ya demokrasia ni nini?
Demokrasia inaangalia uwingi wa wawakilishi na sio lazima hoja zinazotolewa, hata kama hoja hazina mantiki lakini zina ungwa mkono na wengi zinafanyiwa maamuzi na hatimaye yanaonekana kuwa sahihi.

Hasara hii ya demokrasia tunaweza kulinganisha na mwenendo wa upatikanaji wa katiba mpya ambao umekamilika huko Dodoma hivi karibuni.
kinachoangaliwa katika kufikia upatikaji wa katiba mpya umekuwa ni wa wawakilishi ndani ya bunge la Katiba, kwa mfano katika nchi yetu ya Tanzania “Chama cha Mapinduzi (CCM) kina wajumbe wengi katika Bunge la Katiba kwa hiyo  Msingi wa wingi wao ni ushindi walioupata katika uchaguzi halali wa kisheria na kidemokrasia”

 
Kutokana na mazingira haya, mjadala wa upande mmoja uliokuwa unaendelea bungeni ulikuwa halali, hata kama UKAWA waliamua vikao vya bunge hilo. Walichofanya UKAWA ni mbembwe za siasa za kususia ili pengine kupata huruma ya wananchi lakini kimsingi walitakiwa kuendelee kujenga hoja ili kuwafanya walio wengi wabadilishe mawazo yao na wananchi weelewe msingi wao wa hapana ni nini.

Naamini kuwa UKAWA walikuwa na hoja walitakiwa kufa kiume katika ushindani wa hoja Bungeni;  kwa maneno menginehii ndio demokrasia ya ushindani iliyoletwa kwetu na warumi na tukaikubali na kuona ni chombo sahihi cha maamuzi. Ndio hasara ya demokrasia lakini kwa kuwaachia wenzao uwanja wamewanyima wananchi ushindani wa hoja za pande mbili.

Hata kama UKAWA watafanya mikutano ya kupinga katiba nje ya vikao halali vya Bunge inakuwa ni hadithi, ni simulizi ya upande mmoja ambao hauna usindani.

Ushindani wa hoja kati ya wanasiasa na kati ya vyama vya siasa inatakiwa ieleweke kama ustawi wa jamii husika. Kwa kuwa tofauti ya hoja haitakiwi ilete  utengano na hatimaye migongano, bali iwe ni sehemu ya kuleta maendeleo ndani ya jamii husika; kwani demokrasia ya ushindani itakayo ishia katika kuleta vurugu na ugomvi ndani ya jamii itaathiri maendeleo ya jamii na kuongeza maisha magumu kwa jamii husika hivyo kubadilisha mfumo huu na kuingia katika mfumo wa kikatili

 

Utawala wa demokrasia unatakiwa utufundishe namna ya kupanua fikra za wawakilishi wetu. Demokrasia inatakiwa iwe mkombozi wa fikra na kuwapa wananchi uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutenda na hata wa kwenda kinyume na fikra za kikale. Ili jamii iweze kuendelea na iwe na demokrasia iliyopevuka ni muhimu wananchi wawe na uhuru wa kuweza kuasi kisiasa na kuwa na fikra zisizofuata mkondo wa fikra za kawaida za wanajamii.

 

Tofauti za hoja baina ya wafuasi wa vyama tofauti  ndani ya mfumo wa demokrasia huzaa chuki ambayo inajengwa kati ya watawala na wapinzani dhidi ya wananchi kila upende ukijaribu kushinda  hisia za wananchi ambao ndio wenye nchi. Ni wajibu wa wananchi kuamka  na kuwa  imara na kukataa mbwebwe za wanasiasa.

 Tunatakiwa kuanza kuhoji mambo ambayo tunaona kuwa sio ya kweli. Inafurahisha kwa sasa ndani ya Tanzania  kuwa mwamko wa wananchi wetu kwa sasa umebadilika na wananchi wameanza kuonyesha dalili ya kuelewa Zaidi nini wanataka hasa kuhusiana na maendeleo yao.
 

Tukiweza kuepukana na itikadi za matukio  na polojo za matukio na udaku: Lazima tukubali kuwa kila chama cha siasa Tanzania tupende au tusipende kina uzuri wake na ubaya wake, lakini la msingi katika mantiki ya demokrasi lazima tukubali kuwa chama ambacho kimefanikiwa kuingia mkataba wa hiari na wananchi wa kuongoza nchi ndicho kimefanikiwa kupata ridhaa ya kuongoza ndipo tunapona hasara ya demokraisa pengine matendo yao hayakubaliki na wachache ambao wanafikiri kuwa nao wana mwelekeo tofauti na wenye tija kwa jamii. Kwa msingi huo ni kuwa  tofauti za siasa na wanasiasa katika jamii haziwezi kuepukika na wakati mwingine unyama wao unaotokana na tofauti zao za kutamani kuhodhi madaraka unapelekea kuiangamiza  jamii ambayo haina kosa kutokana tu na uelewa wao mdogo;


Napenda katika hitimisho la Makala yangu nimshukuru sana Mheshimiwa Raisi Kikwete na Mheshimiwa Ally Mohamed Shein wamekuwa wasikivu, wavumilivu  na walezi wa demokrasia ya kweli kwa  kuendelea kuvishirikisha vyama na asisi zote ambazo zimefika mahala na kukinzana na serikali zetu zote mbili ili kufikia muafaka kwa kusikiliza mawazo ya wachache bila  kinyongo na hata wakati mwingine kubadilisha  msimamo wa wengi na kufuata mawazo ya wachache.
 

Hapa tunaona  Sifa mojawapo ya demokrasia ya kweli ni kwamba: inawapatia wachache VILEVILE nafasi ya kisheria ya kuwashawishi wengi waone ubora wa maoni yao hata kama hawakubaliani nayo. Demokrasia ya namna hii ndiyo njia pekee ya kuleta mawazo mapya katika jamii kwa njia ya amani na utulivu. Hii ndio sifu kubwa ya viongozi wa serikali zetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Dr. Mohamed Ally Shein

Lazima tukubali kuwa demokrasia in faida na hasara yake na kamwe sio kila mtu ataridhika na maamuzi ambayo yataendelea kutolewa katika uwajibikaji wa pamoja.

 

Mungu Ibariki Tanzania

JK:CCM walinipinga Katiba Mpya

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, wakionyesha Katiba mpya ya Tanzania iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba, baada ya kukabidhiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana. PICHA: KHALFAN SAID
Rais Jakaya Kikwete amesema mchakato wa katiba mpya kabla ya kuanza mwaka 2011, ulipingwa vikali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).Alisema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi, viongozi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), baada ya zoezi la kukabidhiwa katiba inayopendekezwa na kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, mjini Dodoma jana.

Alisema alipata wakati mgumu, lakini alisimama imara kuhakikisha mchakato huo unaanza.“Jambo, ambalo wengi hawalifahamu, makundi pia yalikuwapo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, walikuwapo baadhi walionihoji kuwa jambo hili umelizua kutoka wapi, hii siyo ajenda ya CCM, bali ya watu wengine.

Nikasema ni ajenda ya Watanzania na mimi ndiye mwakilishi mkuu. Baada ya mjadala mkali, tulielewana, ingawa wapo walioondoka shingo upande,” alisema Rais Kikwete.

Alisema baadhi ya wana-CCM waliokuwa wakali kwenye Halmashauri Kuu (Nec) na Kamati Kuu (CC) aliwateua kuwa wajumbe wa BMK na kwamba, walitoa msaada mkubwa na mchango ambao umewezesha kutungwa kwa katiba inayopendekezwa.

Rais Kikwete alisema mchakato ulianza mwaka 2011 na kwamba, safari hiyo ilikuwa na changamoto nyingi.Alisema mjadala ulikuwa mkali bungeni na nje na baadhi ya wajumbe walitoka nje.

Rais Kikwete alisema wakati anafungua BMK, aliwakumbusha wajibu wa wajumbe kuwa Watanzania wanategemea wawatungie katiba inayokubalika na wengi, itakayoimarisha Muungano, inayotekelezeka, itakayoondoa changamoto kwenye Muungano, kuimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

“Katiba inayosimamia demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu katika jamii, itakayoweka mazingira mazuri ya uchumi wa nchi kukua na kunufaika sawia na maendeleo yanayopatikana,” alisema Rais Kikwete.

Aliwapongeza wajumbe wa BMK kwa kuyatendea haki matarajio ya Watanzania kwa kuwa katiba inayopendekezwa inajumuisha maslahi ya makundi yote, inajali anayotaka kila mtu katika nchi yake, utu unaheshimiwa na haki zinazingatiwa.

KURA YA MAONI
Kuhusu kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa Katiba mpya, alisema kumekuwa na maoni tofauti lakini wanaendelea kutafakari ikiwamo kupitia vikao vya wawakilishi wa vyama vya siasa, na endapo itakubalika kura ya uamuzi ifanyike baada ya uchaguzi mkuu kutakuwa na ulazima wa kufanya marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

DK. SHEIN
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema katika kila hatua hadi kupatikana kwa katiba inayopendekezwa, Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu.

“…wananchi kwa ujumla walikuwa wakifuatilia majadiliano bungeni, wakitutia moyo. Ustahamilivu mkubwa wa rais na serikali ya Zanzibar umewezesha kufika hapo.

Tulistahamili, kutumia busara na kuvumilia sana ili tupate katiba,” alisema Dk. Shein.

Alisema jambo linalohusu maendeleo ya Watanzania na hatma yao halitakiwi kufanyiwa mchezo na kwamba, katiba ndiyo uhai wa Taifa.

Dk. Shein alisema katiba inayopendekezwa itajenga mustakabali mzuri wa maendeleo ya Watanzania na taifa na pia inajenga matumaini kwao.

Alisema zipo ibara, ambazo zitaondoa kero za Muungano na kwamba, la kufurahisha ni kuandika katiba kwa kuhakisha Muungano unashamiri, ambao ni kinga kwa Bara na Zanzibar.

Dk. Shein alisema katiba hiyo ni msingi wa dhati wa kuendeleza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliwataka wananchi kutobabaishwa na wale wasiokubali malengo na misingi ya Muungano na hawaridhiki na jitihada za viongozi.

MWENYEKITI BMK
Mwenyekiti wa BMK alisema Bunge hilo limetumia siku 125 kati ya 130 zilizotengwa na kwamba kati yake, 67 ni za Februari hadi Aprili na 58 za Agosti hadi Oktoba, mwaka huu.

Alisema katiba inayopendekezwa imeambatana na taarifa za kamati moja hadi 12, taarifa ya kamati ya uandishi, bango kitita kuhusu kamati zote na taarifa fupi ya kuwasilisha katiba inayopendekezwa.

MWENYEKITI KAMATI YA UANDISHI
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema asilimia 81.8 ya ibara za katiba inayopendekezwa zime tokana na rasimu ya katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema ibara 42 hazikufanyiwa marekebisho, 200 zilifanyiwa marekebisho ya kiuandishi na maudhui, 29 ambayo ni sawa na asilimia 10.7 zimefutwa na 54 ambayo ni sawa na asilimia 18.2 za katiba inayopendekezwa ni mpya kutokana na mapendekezo ya wajumbe wa BMK.

ATETEA MUUNDO WA MUUNGANO
Chenge alisema muundo wa Muungano umedumu kwa zaidi ya miaka 50 na amani, mshikamano wa kitaifa umekuwapo na kwamba, katiba inatoa uhuru kwa Zanzibar kuanzisha uhusiano na taasisi, au jumuiya za nje, kuomba na kupata ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ili kufanikisha ushirikiano huo, ikiwa ni pamoja na kukopa.

HAKI NA WAJIBU WA MAKUNDI MBALIMBALI
Alisema katiba inayopendekezwa pia inatambua haki za wenye ulemavu, haki za vijana pamoja na kuundwa kwa baraza la vijana, haki za wanawake, uzazi salama na miliki, kusimamia na kutumia ardhi kwa masharti yaleyale kama ilivyo kwa mwanaume, haki ya mtoto, ambaye anatambuliwa ni mtu wenye umri chini ya miaka 18, mtoto na haki za wazee.

Haki nyingine ni za wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji madini na makundi madogo, kutumia kuendeleza na kuhifadhi ardhi, kupata taarifa na maarifa kwa lengo la kuboresha shughuli zao.

Alizitaja sura mpya zilizoongezwa kuwa ni ardhi raia wa Tanzania pekee ndiye mwenye haki ya kumiliki ardhi, mgeni kuendeleza na kutumia, maliasili na mazingira.

HAKI ZA HUDUMA ZA AFYA NA MAJISAFI NA SALAMA
Alisema katiba hiyo imenyambua haki ya wananchi kupata huduma bora ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.

Mengine ni uhuru wa kushirikiana katika mambo yanayoendeleza sanaa, ubunifu, utafiti na ugunduzi katika sanaa na sayansi na teknolojia na kwamba, italinda haki miliki.

MWAKILISHI WA WANAWAKE
Jesca Msambatavangu alisema wanawake wa Tanzania wameendelea kuteseka katika mila potofu, lakini wamepambana na kuendelea kulea familia na kwamba, hadi sasa wamefikia asilimia 50 kwa 50.

MWAKILISHI WA ZANZIBAR
Hamad Rashid Mohammed alisema Zanzibar kuvaa koti la Muungano limeshugulikiwa ipasavyo na mfumo wa serikali mbili katika ibara ya saba sura ya 75.

Alisema pia muundo wa Muungano na misaada kutoka nje vimeshughulikiwa na kwamba, Zanzibar sasa wana haki ya kujiunga na taasisi yoyote ya kimataifa baada ya kuwasiliana na Jamuhuri ya Muungano na kukopa bila idhini ya serikali ya Jamhuri na iwapo kutakuwa na masharti ndiyo lazima.

Hamad alisema masuala ya gesi na mafuta yatasimamiwa na serikali ya Zanzibar bila kuingiliwa na serikali ya Muungano na kwamba, hakuna mahali katiba inaweza kupatikana nje ya Bunge.

DK. FRANCIS MICHAEL
Alisema katiba imezungumzia masuala ya ardhi kwa upana na kwa undani, haki ya elimu na elimu bora ili kila Mtanzania apate elimu ya kushindana kwenye ushindani wa ajira na kujiajiri.

Dk. Francis alisema jambo jipya kwenye katiba hiyo ni uhuru wa taaluma, kufundisha, kufanya tafiti na gunduzi zao zipate haki na haki kumiliki ya mali isiyoshikika kama ubunifu.

Alisema tume ya ualimu imetambulika kwenye katiba na kutoa nafasi kwa walimu kujadili na kutolea uamuzi masuala mbalimbali yanayowahusu.

MWAKILISHI WA WAKULIMA
Dk. Nzigula Maselle alisema miaka 50 iliyopita wakulima hawakuwa na haki zao kwenye katiba na kwamba, katiba inayopendekezwa imewakumbatia wakulima kwa kuwawekea ibara mpya inayotaja haki ya wakulima kumiliki ardhi, kupata taarifa sahihi, masoko na sheria zinazogusa kundi hilo.

MWAKILISHI WA WAFUGAJI
Doreen Maro alisema haki za wafugaji zimetambuliwa, ambazo ni haki ya kumiliki, kuiendeleza na kuitumia na kwamba, ibara ya 13 imezungumzia malengo yanayoeleza viwanda mama kwa lengo la kuchakata na kusindika mazao yanayotokana na mifugo.

MWAKILISHI WA WAFANYAKAZI
Mbaraka Igangula alisema katiba hiyo imeainisha haki mbalimbali za wafanyakazi na waajiri, ikiwamo haki ya kugoma, ambayo imeingizwa kwenye katiba na kwamba, haitaruhusu walioko kwenye sekta nyeti kufanya majadiliano na waajiri.

MWAKILISHI WA WAVUVI
Issa Ameir Suleiman alisema katiba imezingatia mambo yote yaliyokuwa na changamoto kwa wavuvi, migogoro baina ya wavuvi na wawekezaji, lakini wamepewa umiliki wa maeneo ya fukwe, ambayo yatamilikiwa na wavuvi.

MWAKILISHI WA WAISLAMU
Sheikh Thabit Jongo alisema katiba hiyo ni ya Watanzania ina mchango ya jamii zote zilizo ndani na nje ya Bunge.

Alisema Mahakama ya Kadhi ilileta msuguano, lakini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alimaliza kwa kusema sheria za kadhi zitatungiwa sheria na Bunge ili zikubalike kwenye jamii na kwamba, kilio cha Waislamu ilikuwa ni hiyo, lakini ibara ya 41 imeleta faraja.

“Tuwe mbele kuitetea na kupiga kura ya ndiyo..tunajua wenzetu watatangulia mtaani, lakini nasi tusibaki nyuma, tutakwenda bega kwa bega kuhakikisha inapigiwa kura ya ndiyo,” alisema Sheikh Thabit.

MWAKILISHI WA WAKRISTO
Askofu Amos Muhagachi alisema katiba imetambua uchaguzi wa imani ya dini, imani au kutokuwa na imani, kutangaza dini, kufanya ibada itakuwa huru na jambo la hiari almradi muumini hakiuki sheria na ili hayo yatekelezwe, lazima kuwa na amani na utulivu.

Aliwaomba waumini wa dini zote kuisoma katiba na kuielewa na Watanzania kuipokea kwa kuwa imezingatia maslahi yao kwa kuwa imewapa uhuru wa kuabudu kwa amani na utulivu.

MWAKILISHI WA SEKTA BINAFSI
Godfrey Simbeye alisema wawekezaji wanapenda kuona nchi yenye amani na utulivu, katika malengo makuu, uwezeshaji na fursa za uwekezaji wa ndani na nje, umuhimu wa wawekezaji wa nje kushirikiana na wa ndani, umuhimu wa kupingana na rushwa kwa Takukuru kutajwa kwenye Katiba.

Alisema suala la manunuzi ya umma likitumika vizuri linaweza kuleta mabadiliko katika nchi.

MWAKILISHI WA WALEMAVU
Amon Mpanju alisema katiba ya mwaka 1977 imetaja walemavu mara moja katika hali ya kupewa msaada, lakini inayopendekezwa imetaja katika ibara zaidi ya nane, lugha ya alama na alama mguso, njia mbadala kwa watu wenye ulemavu katika sehemu za umma na vyombo vya habari vinavyotangaza kitaifa.

Sherehe hizo zilipambwa na shamrashamra mbalimbali, ikiwamo viongozi wa dini kutoa sala.

Viongozi mbalimbali, akiwamo Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, mabalozi, wakuu wa mikoa, wilaya, wadau na wananchi.

MCHAKATO ULIKOANZIA
Mchakato wa katiba mpya ulianza baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitaka kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Rais aliteua wajumbe wa tume hiyo Aprili 6, mwaka 2012, waliapishwa Aprili 13 na kuanza kazi Mei 2, mwaka huo huo, ikiwa na wajumbe 34 na hadi rasimu ya pili inakabidhiwa, walikuwa 32 baada ya Mjumbe Dk. Sengondo Mvungu, kufariki na John Nkolo, kupata matatizo ya kiafya.

Tume hiyo chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, ilikusanya maoni ya wananchi, kuyachambua na kuandaa rasimu ya kwanza iliyojadiliwa na mabaraza ya katiba.

Bunge lilianza Februari 18 na kukamilisha awamu ya kwanza Aprili 25 kwa kupisha Bunge la Bajeti na baadaye liliendelea Agosti 5, mwaka huu hadi katiba inayopendekezwa ilivyopitishwa.

Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitoka ndani ya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, baada ya kudai kuna uchakachuaji wa rasimu ya tume kwa kuingiza mambo mapya.

Bunge hilo liliundwa na wajumbe 629, wakiwamo kutoka kundi la 201 walioteuliwa na rais, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Baada ya katiba inayopendekezwa kukabidhiwa kwa Rais Kikwete na Rais Shein, hatua itakayofuata ni wananchi kupiga kura ya maoni ya ama kuikubali au kuikataa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Imeandikwa na Salome Kitomari, Dar; Augusta Njoji na Editha Majura, Dodoma.

 
CHANZO: NIPASHE

NENO LA LEO: NI LAZIMA TUPANDE MBEGU...!

Ndugu zangu,

Kwenye moja ya mashairi yake, Marcelino Dos Santos wa Msumbiji anasema; " We Must Plant". Kwa maana ya tuna lazima ya kupanda.
Dos Santos hazungumzii kupanda mbegu za mahindi au mtama, bali kupanda fikra za kimapinduzi kwa wanajamii.

Ni fikra zitakazowasaidia kutoka katika hali iliyopo na kwenda kwenye hali nyingine iliyo bora zaidi.
Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu;(P.T)

" Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!" Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani amgetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndiko njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite.

Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri?
Jibu: Anaanza kuamini kwa yasiyo na maana. Ni kama haya ya kuendekeza abrakadabra za Freemasons. Ni kielelezo cha udhaifu wetu Watanzania, Si tunakumbuka ilivyokuwa kwa Babu wa Loliondo, Tuliamua kuacha kufikiri. Ndiyo, kuna waliojifunika vilemba vya ujinga. Wako gizani. Wanahitaji mwanga.
Ni Neno La Leo.
.
Maggid Mjengwa,
Nairobi.

Tuesday, October 7, 2014

RAIS KENYATTA AKABIDHI MADARAKA KWA ROTO TAYARI KWENDA ICC

Kenyatta amemkabidhi mamlaka kwa muda naibu wake William Ruto kwa siku mbili atakazokuwa nje. Mahakama ya kimataifa ya ICC, inajianda kuwa mwenyeji wa mkutano maalum wa siku mbili kuhusu kesi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye atakuwa rais wa kwanza aliye mamlakani kufika mbele ya mahakama hiyo.
Kenyatta anakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu anazodaiwa kutenda baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.Mahakama hiyo inasama kuwa Kenyatta alihusia katika kupanga na kufadhili ghasia za kikabila baada ya uchaguzi uliozua utata mwaka 2007/08Zaidi ya wakenya 1,000 waliuawa kwenye gasia hizo.
Ruto ambaye ni rais kwa muda naye pia anakabiliwa na kesi katika mahakama hiyo ya ICC
Mawakili wa Kenyatta wanasema kuwa kesi hiyo inapaswa kufutiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.
Kenyatta ameombwa na mahakama hiyo kufika mbele yake ili kujadili malalamiko yaliyowasilishwa na kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda kwamba serikali ya Kenya imekataa kuwasilisha ushahidi unaohitajika katika kesi ya Kenyatta. 
Majaji wa mahakama hiyo hata hivyo watathmini kauli kutoka kwa pande zote mbili.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa pia kutangaza tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Kenyatta.
ICC imemtaka Kenyatta kujibu madai ya upande wa mashitaka kuwa Kenya inakataa kutoa ushahidi unaotakikana na mahakama hiyo.
Rais Kenyatta akikagua gwaride la heshima kabla ya kuondoka nchini kuelekea Hague
Mwezi Septemba, mahakama iliahirisha kesi dhidi ya Kenyatta baada ya upande wa mashitaka kusema kuwa Kenya imekosa kutoa ushahidi unaotakikana na mahakama hiyo.
Mashahidi wa upande wa mashitaka wamejiondoa katika kesi hiyo.
Mamia ya wabunge wa Kenya wanatarajiwa kuambatana na Kenyatta kama ishara ya kumuunga mkono.CHANZO BBC SWAHILI

Thursday, October 2, 2014

MATUKIO BUNGE MAALUM LA KATIBA LEO MJINI DODOMA

 .


1
2Wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wakishangilia leo mjini Dodoma mara baada ya matokeo ya upigaji kura kuonyesha kuwa Theluthi mbili ya Zanzibar imepatikana.
3Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Anne Makinda akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
4Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, mhe. John Shibuda akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
5Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. John Cheyo akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
6Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar  ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Pandu Ameir Kificho akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
7Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Selemani Nchambi akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
8Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
10 (1)Makamu wa Pili wa Zanzibar ambaye pia alikuwa ni mjumbe wa Buge Maalum la Katiba, Mhe. Balozi Seif Ali Idd akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
11Aliyekuwa Makamu wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza bunge hilo mjini Dodoma wakati wa ufungaji wa bunge hilo leo 2 Septemba, 2014.
13Waziri Mkuu wa Tanzania ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Mizengo Pinda akitoa akitoa neno la shukurani kwa wajumbe wa Bunge la Katiba na uongozi wao pamoja na uongozi wa nchi kabla ya bunge hilo kuvunjwa rasmi leo mjini Dodoma.
15Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta akiwashukuru wajumbe na Watanzania kabla ya kuvunja bunge hilo rsmi leo 2 Septemba, 2014 mjini Dodoma.
17 (1)Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakitoa maneno ya shukurani kwa wajumbe na Watanzania kabla ya kuvunja bunge hilo rsmi leo 2 Septemba, 2014 mjini Dodoma.
chanzo: matukiotz.com