WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 9, 2012

Sumaye usilalame, leta malalamiko-Mukama


Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Wilson Mukama
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakiwezi kutoa maoni yoyote juu ya kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kwamba chama hicho kinaandamwa na rushwa mpya za kimtandao, kwa kuwa kauli hiyo siyo rufaa wala malalamiko yaliyowasilishwa naye kwenye chama dhidi ya uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho.

Mukama alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE jana kutoa maoni ya CCM baada ya Sumaye kutoa kauli hizo katika mkutano na waandishi wa habari, ulioitishwa naye (Sumaye) jijini Dar es Salaam juzi.



“Hayo ni maoni yake. Siyo rufaa wala malalamiko,” alisema Mukama kwa kifupi.

Alisema CCM ni chama kikubwa, ambacho Tanzania Bara kina wilaya 149 na Zanzibar kina wilaya 12, hivyo hakiwezi kutoa maoni yanayotolewa na kila mwanachama kama hatakuwa amekata rufaa au kulalamika katika chama.

Hata hivyo, Mukama alisema kama waandishi wa habari wataona kauli zilizotolewa na Sumaye dhidi ya CCM kuwa ni za kweli, basi wafanye uchunguzi badala ya kuzimeza nzima nzima, kwani kuna kanuni ambayo inamzuia mtu kuzungumza kama hajafanya utafiti (uchunguzi).

Juzi Sumaye katika mkutano wake na waandishi wa habari aliouitisha mahususi kueleza yaliyojiri katika uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Wilaya ya Hanang’, mkoani Manayara, uliofanyika Septemba 29, mwaka huu na alieleza kuwa sasa CCM inaandamwa na rushwa mpya aliyodai imetoka kwa mtu kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na sasa kuna rushwa za kimtandao.

Alisema rushwa za kimtandao ni zile, ambazo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji katika safari za ndoto zake za kuwania uongozi ndani ya chama hicho.

Mwaka huu, alisema rushwa hiyo ndiyo iliyotumika katika uchaguzi huo wa Nec Hanang', ambako aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu alimwangusha.

Sumaye alisema mambo yaliyotokea katika uchaguzi huo, yalitokea pia katika chaguzi nyingine za CCM zilizofanyika katika maeneo mengi nchini, tofauti ikiwa ni viwango vya yaliyotokea na sura za watu waliohusika na matukio hayo.

Alisema katika sura ya kitaifa, uchaguzi wa CCM unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini umegubikwa sana na matumizi makubwa ya fedha za rushwa.

“Suala la rushwa katika nchi yetu na katika chama chetu siyo geni, lakini sasa nahisi tatizo hili sasa limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa. Mimi binafsi nilizungumza tatizo hili mara kadhaa,” alisema Sumaye.

Alisema mapambano dhidi ya rushwa ni agenda ya kudumu kwake na kwa hiyo ataendelea nayo popote atakapokuwapo.

“Hivi leo (juzi) tunavyoongea hali ya rushwa wakati huu wa uchaguzi imekuwa mbaya zaidi. Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapigakura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake, yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao. Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapigakura ni wapiga mihuri tu,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Zamani kulikuwa na rushwa ya mtu kuwahonga watu fedha wa eneo fulani ili achaguliwe, lakini leo hii kuna rushwa ya kimtandao.”

Alisema watu wanaochaguliwa kwa utaratibu huo, utumishi na uaminifu wao siyo kwa wale waliopiga muhuri kuidhinisha zile kura alizopata, bali ni kwa fedha zilizonunua zile kura na hasa kwa aliyetoa au waliotoa fedha, hivyo Watanzania kuwa na wawakilishi wa mtu au watu na siyo wa umma.

Kutokana na hilo, aliwaomba Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa wanavyotoka, kupiga vita hali mbaya aliyosema kuwa inadhihaki na kudhalilisha demokrasia na pia inayodhalilisha utu wa wananchi wanaopiga kura.

Alisema uchaguzi wa Nec Wilaya ya Hanang, uligubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho vingi, uharamia wa kuhamisha wapigakura usiku na maovu mengine mengi, ambayo hakuyataja.

Akijibu swali aina gani ya rushwa iliyotumika katika uchaguzi huo, alisema: “Ni ya mtandao” na kusema fedha hizo pamoja na mtu aliyezipeleka hamjui.

Alisema mtandao uliopo siyo mmoja, bali wenye mitandao wapo wengi.

Pia akijibu swali kuhusu madai kwamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alishiriki katika mtandao huo, Sumaye alimtaka mwandishi kwenda kumuuliza Lowassa suala hilo.

Hata hivyo, alisema hajakata tamaa na wala hatakata rufaa ya kupinga matokeo wala kupeleka malalamiko katika chama kwa sababu yaliyokuwa yanatendeka yalikuwa yanafahamika na kwamba hata vyombo vya habari vilitolea taarifa mara kadhaa.

“Narudia tena mimi nitabaki mwanachama mwaminifu wa CCM,” alisema.

Alisema Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alipokuja na kaulimbiu ya kuleta mageuzi katika chama, maarufu kama “kujivua gamba” yeye (Sumaye) ni miongoni mwa watu waliofurahishwa na pia alimpongeza kwa hilo.

Alisema kama kuna mtu atathibitika kuhusika na kashfa ya ufisadi ndani ya chama anatakiwa aadhibiwe na kuwapisha wanachama wengine, kwani anaharibu sifa nzuri ya chama.

Pia akijibu swali kwamba, kwa nini asimtafute Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kumlalamikia kuhusu yaliyotokea katika uchaguzi wa Hanang, alisema hawezi kufanya hivyo, kwa sababu yeye siyo katika aina ya watu wanaopenda kukimbilia Ikulu kwenda kulalamika kwa Rais na kwamba, siyo kila kitu lazima mtu akimbilie huko (Ikulu).

Alisema kuangushwa katika uchaguzi huo hakujadhoofisha ndoto zake za kisiasa, badala yake kumempa nguvu zaidi, kwani kugombea urais akiwa nje ya chama ni vizuri zaidi kuliko kuwa ndani ya chama.

Alisema yeye ni mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba, alishawahi kusema yeye hayuko CCM kwa ajili ya cheo na wala kukosa kwake Nec na hasa kwa njia iliyotumika hakumnyimi usingizi wala hakumzuii kugombea urais kwa tiketi ya CCM endapo ataamua kufanya hivyo.

“Lakini nataka kukumbusha kuwa hata Baba wa Taifa na mwanzilishi wa chama hiki aliwahi kusema kama chama kikiacha misingi yake atakiacha. Chama si mama yake. Kilichomuudhi Mwalimu wakati huo, pamoja na mambo mengine, ni hali ya rushwa katika chaguzi zetu. Hivyo, tusiandame watu bali tuandame maovu,” alisema Sumaye.

Akijibu swali kama bado ana imani na uongozi wa CCM hasa baada ya kubaini chama hicho kimegubikwa na rushwa, alisema bado ana imani na chama hicho kwani kama chama hakina matatizo.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuwa bado ana imani na viongozi wa CCM, bado hawajaweza kujisimamia vya kutosha kupambana na uovu, ambao alisema kina uwezo wa kubadilika licha ya kwamba, hajui lini mabadiliko hayo yatapatikana.

Alisema umma mpana wa Watanzania hautaki rushwa na unaumia sana na rushwa, hivyo akavishauri vyama vya siasa kujirekebisha kabla wananchi hawajasema sasa inatosha, kwani wakisema hivyo itakuwa ni hatari.
CHANZO CHA HABARI: NIPASHE

No comments:

Post a Comment