KUFUATIA AJALI YA MELI YA “MV SPICE ISALANDER “SISI KAMA TAIFA TUFANYE NINI KUEPUSHA HALI HII ISITOKEE TENA?
Mwishoni mwa wiki kulitokea ajali mbaya ya kupinduka kwa Meli na kuzama, ajali ambayo imesababisha vifo vya watanzania wenzetu zaidi ya 200 wengi wao wakiwa wananwake na watoto, ajali ambayo ilitokea katika bahari ya Hindi katika eneo lenye mkondo mkali wa Nungwi ikiwa inaelekea Pemba;
Msiba huo ni mkubwa kitaifa kwani umekatisha maisha ya watanzania wenzetu ambao ni nguvu kazi yetu kwa maendeleo yetu; wengi wa aliofariki ni wazazi wa familia zetu na watoto ambao walikuwa wanaandaliwa kwa ajili ya maendeleo yetu ya kesho.
Kwa mara nyingine nachukua nafasi hii kutoa pole kwa kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa wazazi kwa msiba huu mkubwa. Na kwa viongozi wetu wakuu wa taifa letu Raisi wa Serikali ya Mapinduzi Ya Zanzibar pamoja na timu yake yote ya uongozi; Raisi wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania na timu yake vile vile;
Swali ambalo limenigusa sana siku hii ya leo ni hili kwa nini ajali hii ilitokea?
Ni kweli imekuwa ajali kama ajali ambayo imekuja bila hodi na haikuwezekana kabisa kuepukwa?
Je ni ajali ambayo imechangiwa na uzembe wa usimamizi wa wajibu wetu kama watendaji?
Je ni tatizo la uwajibikaji na kuweka rehani ya maisha ya watanzania kwa kuendekeza “ muhali” na kushindwa kusimamia na kukemea sheria katika atendaji pale panapohitaji kufanya hivyo?
Je ni tatizo la tamaa ya wamiliki wa vyombo na wasimamizi wa miradi hivyo kushindwa kufuata taratibu zinazoongoza biashaya zao?
Mwananchi wa kawaida atajiuliza lakini serikali zetu ziko wapi katika kuwajibika?
Au zinasubiri kuwajibika baada ya tatizo kutokea au hufanya kazi vipi ( management in crisis or management after crisis or crisis management)?
Leo naungana na kauli ya Waziri katika Afisi ya Makamo wa pili wa Rais, Mhe Mohamed Aboud Mohamed
“amesema,kuwa kamati maalum itaundwa ili kuchunguza juu ya ajali hiyo na ikibainika kuwa uzembe umepatikana sheria itachukua mkondo wake”. ..
”kuwa tatizo kubwa la wazanzibari ni muhali, na amesema ili utendaji mzuri uwepo, lazima suala hili la muhali liwekwe upande ili nchi ipige hatua za maendeleo, na ikibainika kuna watu wanafanya uzembe wa kikazi lazima hatua za sheria zichukuliwe”
Tunaipongeza kauli hii ya awali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainiika kufanya uzembe uliosababisha kuzama kwa meli ya Spice Islanders huko katika mkondo wa Nungwi na kusababisha vifo vya watu watanzania wenzetu zaidi ya 200.
Wasiwasi wangu ni huu kuwa, pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuangalia na kukagua kila mara vyombo vya usafiri ili kunusuru ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Je wakibainika kwa uzembe huu watachukuliwa hatua za kweli ambazo zitakuwa fundisho kwa wamiliki na watendaji wengine?
Tatizo letu kama taifa siku zote tume zinazoundwa zinaishia kuwa ni viini macho tu na hakuna msukumo wa kweli wa adhabu ambazo zinakidhi haja na haki kwa wafiwa;
Kwa nini meli hiyo ilipakia kupita uwezo wake? Kwa nini captain alikubali kuendelea na safari? Kama yuko hai inapasa awajibishwe kulingana na uzito wa madhara ambayo yametokea tusimwonee muhari;
Je tunaweza kuthubutu kama serikali ya China inavyothubutu kwa raia wake ambao wanasababisha hasara kwa taifa? Wao hawana mchezo;
Kama tukiweza kuthubutu kwa wavunjaji sheria, uwajibishaji huu tutaweza kuzilinda na kuzitekeleza sheria na kanuni ambazo zimewekwa kwa ajili ya vyombo vya usafiri ili kudhibiti na kuzuia ajali zisitokee, kwa bahati mbaya sana baadhi ya wamiliki wa vyombo hivyo huacha kufuata kanuni hizo ama kwa makusudi na masilahi binafsi.
Ni kweli kuwa ajali haziepukiki, lakini ajali nyingine husababishwa na uzembe wa wamiliki pamoja nawatendaji wake na hili ndilo lilitokea wiki iliyopita huko Nungwi.
Natoa wito kwa wadau wote kushikamana katika kuhakikisha vifo vinavyosababishwa na ajali vinapungua kama si kumalizika kabisa kama tukisimama pamoja na kukataa kuburuzwa na wenye mali na kuweza kuwakatalia wengine kupanda kwenye ambacho kimejaa kulingana na uwezo wake tutakuwa tumeweza kuthubutu kwa masilahi ya taifa.
udhaifu wa usimamiaji wa sheria na muhali umetupa wakati mgumu wa kujua meli hiyo ilikuwa na abiria wangapi? Kwa nini kunakuwa na taarifa ya idadi inayotofautiana? Huu ni uzembe ambao kwa kweli hautakiwi kuendelea kuvumiliwa;
Mwisho tunaiomba Serikali yetu ambayo ndio muhimili wa maisha bora ya raia wake na usalama wao kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa sheria zake; serikali lazima ithubutu katika kuwawajibisha wote waliohusika na kuwachukulia adhabu kali na kuacha MUHALI