TUNAVYOJIANDAA KUSHEREKEA MIAKA HAMSINI (50) YA UHURU WA TAIFA LETU JICHO LANGU LIONAVYO;
JE SERIKALI YETU NI KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU KATIKA KUTATUA KERO ZA WANANCHI WAKE?
Katika mwaka huu wa 2011 serikali yetu ya Tanzania imekabiliwa na matatizo mengi ambayo yameendelea kuwakwera wananchi wake na kuendelea kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo ya nchi hii. Baadhi ya matatizo hayo ni;
· Ufisadi wa muda mrefu
· Tatizo la Umeme
· Tatizo la Maji safi
· Tatizo la barabara
· Tatizo la viongozi kushindwa kufanya maamuzi kwa haraka
Kumekuwa na tatizo kubwa sana la umeme ambalo ambalo kwa upande mmoja limechangiwa na hali ya hewa kwani sehemu kubwa ya nishati hupatikanaji wake unategemea upatikaji wa maji(mvua) ili kuweza kuendesha ,mitambo yake ambayo kwa miaka kadhaa sasa inaendeshwa kwa nguvu ya maji;
Je pamoja na tatizo la uhama wa umeme kutoka na tatizo la uzalishaji wake je watumiaji wa umeme wamekuwa waaminifu katika kulipa gharama halisi? Tunafahamu kuwa kuna watumiaji ambao hawalipi umeme kama wanavyotumia; Kila siku hupanga mission na wafanyakazi wasio waaminifu kucheza na mita au na bili za umeme. Huu nao ni ufisadi ambao unarudisha nyuma maendeleo ya kuwa na umeme wa uhakika;
Kama watu hawalipi umeme wanaoutumia nategemea hilo shirika litajiendesha na nini? Tunaweza kuliondoa tatizo hili kama pande zote mbili zitashirikiana pamoja na kwa ukaribu sana tusikimbilie tu kuwalaumu wahusika na kama wateja nao ni mafisadi wa kuiba matumizi ya umeme nao wanachangia kutokana na kutokuwa wakweli tunaishia kujiumiza wenyewe na kurudisha maendeleo yetu nyuma na ni wazi kuwa maendeleo hayawezi kuja kwa njia za mkato ili tuendelea inabidi tuchangie kwenye uchumki wa nchi yetu kwa vitendo.
Sisi kama taifa tunajua kuwa hatuna viongozi wazalendo, ndiyo maana kila siku tunalia na umeme,maji, hospitali,shule. Sasa kama taifa limekosa vitu vyote hivi kweli kuna maisha bora hapo? Halafu tunaimbishwa kuwa maisha bora kwa kila mtanzania ni sera na yako njiani yanakuja, mmm hebu tuendelee kusubiri; lakini swali la msingi hapa sijui tutayasubiri hadi lini?
Je serikali yetu jamani ni KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU yaani inahitaji kusaidiwa kwa nini? Au inajifanya KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU ili isiwajibishwe?
Lakini serikali inatakiwa kujua kuwa pale inapojifanya KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU KATIKA mazingira ya kawaida inajitengenezea maadui ambao wanaanza kujenga chuki dhidi ya serikali yao; ni ukweli kuwa chuki dhidi ya serikali yoyote duniani haitokei hivi hivi tu bila sababu. Wananchi hawawezi kuamka asubuhi na kuanza kuichukia serikali yao. Watu hawawezi kuwa na sababu ya kumchukia mtawala kama mtawala hawapi wananchi sababu ya kumchukia. Kwa kawaida kuna sababu kadhaa zinazoweza kuwafanya raia kuichukia serikali iliyoko madarakani.
Na moja ya sababu hizo ni pale serikali inapojifanya KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU katika kusikiliza matatizo ya wananchi wake, bubu katika kusema ukweli na kukemea maovu, kiwete pale inaposuasua katika kutekeleza majukumu yake kwa haraka na kuishia kuwa na tume nyingi za uchunguzi ambazo mwisho wa uchunguzi hakuna hatua ya maendeleo inayofanyika, na kipofu pale ambapo inayafumbia macho maovu ya watendaji wake na kuwabariki waarifu katika kuendelea kufaidi rasilimali na kodi za walalahoi.
Jambo hili limesemwa sana na wataalam na wananchi wengi kuwa; Hakuna utawala mbaya kama utawala wa kifisadi ambao ni wa kiujanjaujanja tu. Utawala wa aina hiyo hudumu kwa kuvunja sheria au kuzipinda bila kumjali maendeleo ya wanyonge ambao hawana sauti; isipokuwa wale wenye uwezo na walioko madarakani kila mmoja ananufaika na uzembe wa mwingine na kila mmoja akilinda ubovu wa mwingine. Mara nyingi mafisadi hulindwa wakati maskini hunyanyasika na kuumizwa, na hata kidogo walichonacho inabidi watumie nguvu nyingi kweli kukilinda angalia nini kinatokea kati ya wamachinga na serikali za jiji na halafu angalia nini kinatokea kati ya wafanyabiashara wakubwa wakwepa ushuru na serikali.
Serikali yetu ikibadilisha msimamo wake na kuwa serikali ambayo sio KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU itajijengea heshima kubwa sana kwani itafanya jambo kubwa moja la kheri sana la kushughulikia kero na matatizo mbalimbali ya wananchi na ninauhakika yataondoka
Kwa hali ambayo tunayo sasa na tunavyoelekea kusherekea miaka hamsini ya Uhuru wetu (50;)Kwa mtazamo wangu, ukimya huu wa serikali unaleta au kukaribisha hatari, serikali ibadilike mara moja na kusikia kilio cha wananchi wake, ukimya huu utaleta tafsiri zisizo rasmi na majibu yatokanayo na tafsiri hizo yanaweza kuwa ya uvunyaji sana wa sheria na kupotea kwa uvumilivu na amani ambayo Taifa hili imejivunia kwa miaka hamsini;
Tunahitaji viongozi wetu kuwa na vision; Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alijua mapema kabisa wakati wa ujenzi wa taifa letu kuwa ni lazima tuwe na nguvu ya umeme kuweza kuendeleza viwanda vyetu, matumizi ya majumbani na kuinua miji yetu.Kwa wakati wake kwa vision yake umeme wa Mtera ulitosha kabisa;
Lakini kwa sasa umeme wa maji wa Mtera, kihanzi etc hautoshi tena, je viongozi wetu wanavision gani? Kukaa chini na kulaumu kujifanya hawaoni? Au vision yao imekuwa matatizo yetu ndio mtaji wao!
Au tuungane na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, aliwahi kusema “Hatuwezi kuwa Taifa ambalo kila siku tunajadili mambo yaleyale na kurudia makosa yaleyale. Hatuwezi kuwa Taifa ambalo vichwa vya habari vya magazeti vinapambwa na habari za ufisadi tu. Tunapaswa kutoka hapo kwa kusahihisha makosa, na kama tukifanya makosa mengine, yawe makosa mapya.”
Lakini la msingi sasa viongozi wetu wanatufanyia nini cha kutufanya tuwe na maisha bora; ni ukweli kuwa maendeleo yetu yataletwa na sisi wenyewe, lakini tutajisaidiaje kama kweli serikali unashindwa kutupa nyenzo za sisi kujisaidia kusimama wenyewe; kama vile Umeme wa uhakika, maji safi, barabara na elimu bora kwa watoto wetu?
Viongozi wetu wa Serikali na vyama vya siasa ndio wenye dhamana ya kuongoza juhudi za kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini baadhi yao wamekuwa chanzo cha kuyumbisha nchi kutokana na kasumba mbaya za kutanguliza maslahi yao binafsi pamoja na kukumbatia unafiki na urasimu
Mabadiliko yanahitajika haraka ili kunusuru nchi yetu iliyo mbioni kupoteza mwelekeo sahihi. Tanzania ni nchi tajiri yenye rutuba, bahari, mito, maziwa, misitu na mbuga za wanyama, madini, Iweje sasa tuishi katika nchi yenye utajiri halafu tunaishia kuwa omba omba hata wa chandarua kwa ajili ya kujikinga na malaria?
Kwa hali yoyote ile maamuzi ya maendeleo yetu bado yako mikononi mwa serikali. Nina imani kama serikali Itaamua vema,katika upangaji wa sera zake za maendeleo na usimamiaji wa sera hizo na uwajibikaji katika utekelezaji wake maisha bora kwa kila mtanzania hayachelewa . Lakini ikiamua vibaya, athari zake zitaendelea kujulikana na tafsiri serikali yetu kuwa ni KIZIWI, BUBU KIWETE AU KIPOFU itashika kasi;
Viongozi wetu wanaweza kubadilika kwa faida ya wananchi na taifa lake.
No comments:
Post a Comment