MAISHA BORA KWA KILA MTAZANZANIA: TUYATEGEMEE KUPTIA KASI MPYA, NGUVU MPYA NA ARI MPYA? AU TUSUBIRI KAULI MBIU NYINGINE?
Mheshimiwa J.Kikwete - Rais wa Tanzania
Ni desturi kila kiongozi anapoingia madarakani huja na kauli mbiu, ambayo inakuwa ni dira ya utekelezaji wa majukumu yake katika kuwaletea maendeleo wananchi wake, tumeshuhudia kauli mbiu kama : Umoja ni Nguvu, na Utengano ni Udhaifu; Ruksa; Uwazai na Ukweli na hatimaye sasa tuna kauli mbiu ya “Kasi Mpya Nguvu Mpya na Ari Mpya” ambayo lengo la kauli hii kwa jamii ya watanzania ni kuwa na “Maisha bora kwa kila Mtanzania”.
katika tafakari yangu ya leo ikiwa ni salamu za kuaga mwaka wa 2010 na kuukaribisha 2011, maswali ya msingi je kauli hii mbiu inaweza kubadilisha maisha ya watanzania kutoka maisha duni na kuwafanya wayafurahie maisha yaliyo bora? Je serikali yetu inatumia kigezo gani katika kuhakikisha kuwa kauli hii mbiu inaleta changamoto na hata mabadililo katika maisha ya wananchi wake? Na katika kutekeleza Kauli hii mbiu Je tunao viongozi ambao wamejizatiti kuwatumikia wanainchi? Je tunao viongozi ambao wanajisuta wenyewe wanaposhindwa kuwatendea haki wananchi wao? (fear of justice): Kwa nini wataalamu wetu wengi wanaikimbia nchi yetu na kwenda kufanya kazi nchi nyingine? Je wananchi nao wanatimizaje wajibu wao katika kutekeleza kauli Mbiu hii kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe? Je Kauli mbiu hii imelenga maisha bora kwa wale ambao tayari wako ndani ya mzunguko wa ari,kasi, na nguvu mpya kutokana na uwezo, wa mali ambazo wamezipata kwa njia ambazo zina utata/sio sahihi?
Ni ukweli ambao haufichiki kuwa Serikali yoyote duniani, inayoendeshwa kwa misingi ya demokrasia, lengo lake la kwanza ni ulinzi wa maisha ya wananchi wake na furaha yao, na si uharibifu wake. Kulinda maisha ya wananchi wake ni lengo pekee kwa serikali ya kidemokrasia kwa sababu serikali ipo kwa ajili ya watu na imechaguliwa na watu na inapata madaraka kutoka kwa watu. Aidha, ridhaa ya serikali yoyote kuendelea kukaa madarakani haitokani tu na katiba na sheria iliyoiweka madarakani; bali ridhaa ya wananchi kutawaliwa inatokana zaidi na matendo mema ya serikali hiyo kwa wananchi wake.
Serikali ina changamoto ya kuhakikisha ufisadi nchini unaondolewa ili utajiri wa nchi yetu uwanufaishe wananchi, wakiwemo wafanyakazi. Kama mwandishi mmoja alivyowahi kumnukuu Albert Einsten kuwa : “Ulimwengu pamekuwa mahali pa hatari sana kuishi lakini haitokani na uovu unaotendeka, bali inatokana na wale wanaouona uovu ukitendeka lakini hawachukui hatua yoyote.” Swali je viongozi wetu wanao utashi na uwezo wa kukwemea maovu haya, hata kama watendaji wa maovu haya ni watu wa karibu nao: kama marafiki na ndugu au watoto?
Nakumbuka kauli mbiu hii (Kasi Mpya Nguvu Mpya na Ari Mpya) ilivyotolewa ilishangiliwa sana na watanzania ilionyesha kuwa na manufaa kwa umma, tatizo ni kuwa furaha hiyo kwa Watanzania kama kawaida imeanza kuzimika kama kibatari kwenye upepo, kwa vile utekelezaji wa kauli mbiu hii hauonyeshi kufikia malengo yake. Inafika mahali ambapo wananchi wanaanza kusema kunatofauti gani ya kule tukiko toka na hapa tulipo?
Kimantiki ni rahisi sana kwa gari ambalo gurudumu zake tayari zinazunguka kupandisha milima kwa haraka kuliko lile ambalo lilikuwa limesimama litahitaji nguvu zaidi na wakati zaidi katika kuupandisha mlima ule ule; Wakati mwingine msaada wa ziada utahitajika, lakini kwa bahati mbaya iwapo gari ambalo lilikuwa katika mwendo litakuwa tayari limeshakamilisha kupanda mlima halitaweza kutoa msaada wa haraka; na kama kwa bahati mbaya hata vioo vya kuangalia pembeni pengine havifanyi kazi, ni vigumu sana kujua kama mwenzake aliyemwacha nyuma anakuja au limeshindwa kabisa kupandisha mlima. Hii ni taswira ya viongozi wetu na serikali yao mambo yanapowaendea vizuri hawajali maisha ya wananchi wao mpaka wakati wa chaguzi tena.
Ni ukweli ambao haufichiki kuwa kama viongozi wetu wanavyosema; maisha bora hayawezi kuja watu wakiwa vijiweni;hayawezi kunyesha kama mvua, ni suala la mchakato. Lakini wananchi wameanza kuona mambo tofauti yanayotokea kwa viongozi wao. Viongozi wa nchi wao maisha yameanza kuwa mazuri baada ya muda mfupi. Wananchi wanashuhudia baadhi ya viongozi walioingia madarakani karibuni ambao walikuwa hoi kabisa lakini sasa wanaishi kama vile wako kwenye paradise ya peke yao.
Viongozi wetu wanageuka mchwa na kusahau waliko toka; wengi hujiingiza katika Wimbi wa wizi wa mali za umma na ufisadi wa kutisha. Ni vema viongozi wetu, hasa mawaziri, wakaingia kazini kutatua kero ambazo kila mmoja anazifahamu. Kama msanii Mrisho Mpoto alivyoimba katika moja ya nyimbo zake,Mwaka 2005 walitupima viatu na leo wanarudi tena kutuuliza tunahitaji viatu vya aina gani; sisi hatutaki mnapokuja kwetu tena mtuulize, bali tunataka mnaporudi mje na viatu vyetu tena ambavyo vinatutusha .
La msingi tunapoanza mwaka 2011 kukbukuke kuwa maisha bora ya Mtanzania yatapatikakna kama serikali itaweza kuboresha:
· Elimu kwa watoto wetu, Utajiri mwingi wa Taifa utumike kujenga shule bora kwa watoto wetu, kujenga mazingira bora ya kusomea na mahitaji yote yanayomjenga mtoto kiakili. Kama Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alivyosema “Elimu bora ndiyo urithi pekee unaoweza kulifanya Taifa kuweza kuboresha maisha ya watu wake”. Na elimu bora ndiyo chemchemu ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
· Hali halisi ya shule nyingi wanafunzi wanakaa nchi kutokana na ukosefu wa madawati ,tatizo la vyoo mashuleni haviko vya kutosha na kama viko sio visafi Kwahiyo ,wanafunzi wetu wanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizo kutokana na kutokuwepo na vyoo safi .kuna tatizo la msingi la uwiano wa walimu na wanafunzi. Idadi ya wanafunzi ni kubwa kuliko uwezo wa walimu; tatizo la pili walimu wengi hawana uwezo mkubwa wa kufundisha hivyo hupelekea watoto kumaliza shule wakiwa hawafahamu chochote kama vile kusoma, kuandika hata kuhesabu
- Kuna tatizo la huduma za afya hali halisi ni ile amabayo iko kwenye hopsptiali na zahanati nyingi hapa nchini akina mama wajawazito wanakufa sana hasa wakati wa kujifungua,sababu kubwa ni ukosekanaji wa wakunga na vifaa au wakunga hawapati mafunzo ya kutosha: tatizo pia tunaliona kwa watoto wetu wanafariki kila kukicha kutoka na kutokuwa na Zahanati nzuri na kubwa yenye huduma bora pamoja na ukosekanaji wa madawa,
- Tatizo la wataalamu wetu wengi hasa katika sekta ya afya wanvyokimbilia nje ya nchi hii ina dhihirisha kuwa Wataalamu wetu hawathaminiwi na hii inatugharimu sana; pengine wamesomeshwa na pesa za walala hoi lakini hawarudi nchini kuisaidia jamii.
Maisha Bora kwa sasa inawezekana, hili halina pingamizi ila tu utekelezaji wake unahitaji viongozi wetu wavue ubinafsi na wafikirie vizuri, waseme kile ambacho wanaweza kukitenda na si kutumia umasikini wa watu kwa kuwapa matumaini yasiyotekelezeka. tukumbuke kuwa mabadiliko sio rahisi yanahitaji kujitoa muhanga kutekeleza majukumu bila kuogopa vitisho, wala upendeleo: je tunao viongozi wa namna hii katika serikali yetu?
Ni jukumu la serikali ili kufanikisha hii ahadi inatakiwa kuwamulika mawaziri wanaotia mashaka katika kufanikisha sera na adhima ya maisha bora. kwamba ni vyema mtu anayetoboa jahazi akatoswa mapema, kwani kulelewa na kushangilia huku akiendelea na hujuma zake, mwisho wake ni abiria wote, pamoja na nahodha kuzama na kupoteza maisha. Kikwete, wakati wa kuwatosa wote wanaokuangusha ni sasa na usijali urafiki, uswahiba au undugu na watu wa aina hiyo na hapo utakuwa umeokoka na kulitendea haki taifa la Watanzania.
Je picha hizi hapa chini zinatupa mawazo gani kuhusu Watanzania? Wanafurahia maisha bora? Wanalaani serikali kwa kushindwa kuwajali? Au wana sema yote sawa tu? Au wanafurahia mafanikio ya Kasi Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya: Ni mambo yepi yanahitaji mabadiliko ya haraka kama yako?