WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, January 11, 2014

HATIMAE SIMBA NAYO YAFUZU FAINALI MAPINDUZI CUP


Klabu ya Simba imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali ya kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga URA ya Uganda mabao 2-0.
 
mabao ya Simba kwenye mchezo huo yamefungwa na beki Joseph Owino pamoja na kiungo Amri Kiemba huku kiungo Owen Kasule wa URA akilimwa kadi nyekundu kwa kumchezea madhambi Ramadhani Singano.
 
Simba sasa itacheza fainali siku ya Jumatatu na timu ya KCC pia toka nchini UGANDA iliyoitoa AZAM kwa mabao 3-2.

Chanzo: Shaffih Dauda (P.T)

Mapinduzi Zanzibar yatimiza miaka 50


Rais wa Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Sheni (kulia) akimtunuku Dkt.Salim Ahmed Salim nishani ya Mapinduzi ya Zanzibar jana katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar jana.Picha na Michael Matemanga
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein atawaongoza maelfu ya wananchi wa Zanzibar, kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo leo.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali akiwamo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikililou Dhoinine wa Comoro na maseneta kutoka miji ya Lamu na Mombasa nchini Kenya, pamoja na mwakilishi maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa sherehe hizo ambazo ni kilele zitaanza saa 3.00 asubuhi baada ya viongozi wa kitaifa kuwasili, ambapo pamoja na mambo mengine Dk Shein atalihutubia taifa hilo.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, wananchi wa visiwa hivyo wanamtarajia Rais Dk Shein kuzungumzia hali ya kiuchumi, kisiasa na kudumisha usalama wa raia kutokana na vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, pia harakati za viongozi wa dini na wanasiasa kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.(P.T)

Alipoulizwa kuhusu kualikwa kwa aliyekuwa Sultan wa mwisho wa Zanzibar, Jamsheed Bin Abdullah, alisema kuwa sherehe hizo zilikusudia kuwaalika watu mashuhuri kutoka nchi za SADC na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), lakini bahati mbaya viongozi hao hawataweza kushiriki kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine.

Hata hivyo, alikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Salmin Amour Juma, iliwahi kutoa msamaha kwa sultani wa mwisho wa Zanzibar ikieleza kuwa mlango uko wazi na anaweza kuitembelea Zanzibar kama mwananchi wa kawaida.

Maadhimisho ya leo yanafanyika ikiwa ni miaka 50, baada ya Mapinduzi yaliyofanywa na Chama cha Afro Shiraz Party (ASP), Januari 12, 1964 chini ya hayati Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ).

Mji wa Zanzibar umepambwa kwa picha za viongozi kuanzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tangu awamu kwanza hadi ya saba, Bendera za Taifa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku mji ukiwa katika hali ya usafi.
Sherehe hizo zinatarajiwa kupambwa na mambo mbalimbali, ikiwamo vikundi vya ngoma za asili na michezo mbalimbali ya kijadi.

source Mjengwa blog

Monday, January 6, 2014

Nahodha wa Kilimanjaro II ahojiwa polisi Zanzibar



Zanzibar. Wakati watu saba wakiwa bado hawajaonekana baada ya boti ya Kilimanjaro II, kupata ajali na abiria kuzama baharini, nahodha wa chombo hicho alitoa taarifa za uongo kuhusu ajali hiyo imefahamika.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Mhandisi Abdi Omar Maalim, alisema taarifa iliyotolewa na nahodha katika kituo cha mawasiliano zilikuwa za uongo na hivyo kusababisha kazi ya uokozi kuchelewa.

Alisema baada ya boti hiyo kupigwa wimbi, abiria waliokuwa wamekaa juu waliteleza na kutumbukia baharini lakini nahodha katika ripoti yake alisema hakuna abiria waliotumbukia. Alisema hata alipotakiwa kupewa msaada na Kituo cha Mawasiliano cha Zanzibar, alisema hahitaji kwa sababu vitu vilivyotumbukia bahari ni vifaa vya uokozi na mizigo.

“Nahodha alitoa taarifa za uongo na kusababisha zoezi la uokoaji kutokufanyika kwa wakati mwafaka, baada ya kutokea ajali hiyo,” alisema Mhandisi Maalim.

Alisema ajali hiyo ilitokea saa 3:30 asubuhi lakini kazi ya uokoaji ilianza alasiri baada ya kupokea taarifa kutoka kwa abiria kuwa wenzao wamezama baharini baada ya meli kupigwa na wimbi.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman amesema nahodha wa chombo hicho alianza 

kuhojiwa na polisi juzi. Alisema kazi kubwa inayofanyika sasa ni kutafuta watu ambao bado hawajaonekana na baada ya kukamilika ataamua kama kuna haja ya kuunda tume ya kuchunguza ajali hiyo.

Alisema baada ya uhakiki wa majina ya abiria waliosafiri na boti hiyo wamegundua kuwa jumla ya watu 15 walizama baharini baada ya boti kupigwa na wimbi na kusababisha injini kuzimika.
Waziri Seif alisema hadi jana maiti tano zimepatikana na watu watatu wameokolewa.

Msimamizi Mwandamizi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mnazimmoja, Vuai Jabir Hassan aliwataja marehemu kuwa ni Rashid Said Ali (11) mkazi wa Ilala Dar es Salaam, Akram Khamis Issa (11) wa Mwanakwerekwe, Masoud Hamad (30) wa Wete Pemba, Nushra Khamis (9) na Fatma Asir Khamis (18) wa Magogoni Wilaya ya Magharibi Unguja.

Aliwataja waliookolewa kuwa ni Ali Maulid Haji (Mwanakwerekwe), Ali Salum Ali (Pemba) na Mahir Ali Issa (Mwanakwerekwe).

Wakati huohuo, huduma za usafiri kati ya Unguja na Pemba zimesitishwa kwa muda kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa katka Bahari ya Hindi. Habari zilisema hatua hiyo ni ya kiusalama.

source: mwananchi

Mwigamba, Kitila 'out' Chadema

 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa akitoa tamko la Kamati Kuu ya chama hicho kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. PICHA:SELEMANI MPOCHI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatimua, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, huku kikiwataka wanachama kutoshiriki mikutano ya nje na ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na mawakala wake kwa jina la Chadema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu jana mbele ya waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho, iliyokutana Januari 3 hadi 4, mwaka huu kujadili masuala mbalimbali likiwamo la wanachama hao.
ZUIO LA ZITTO
Mwishoni mwa wiki, Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando, aliiomba mahakama asijadiliwe katika kikao cha CC cha Januari 03, mwaka huu, kuhusu uanachama wake hadi hapo rufani yake itakapotolewa uamuzi na Baraza Kuu.
Wakati Dk. Slaa akisema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema uanachama na Ubunge wa Zitto utaendelea kuwapo kutokana na kesi iliyopo mahakamani na si kwa matakwa ya Chadema.

MASHITAKA DHIDI YAO
Dk. Slaa alisema washtakiwa wote walishtakiwa kwa mashtaka 11 yanayohusu ukiukwaji wa vifungu mbalimbali vya katiba ya chama, kanuni za uendeshaji kazi za chama, kanuni za kusimamia shughuli, mwenendo na maadili ya wabunge wa chana na mwongozi wa kutangaza kusudio la kuwania nafasi ya uongozi kwenye chama, mabaraza na serikali.

Alisema mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa mkakati wa mabadiliko, 2013, uliojikita katika kukashfu viongozi wakuu wa chama, kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘mtandao wa ushindi’ nje ya utaratibu wa chama ili kumwezesha Zitto kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa chama Taifa.

Mengine ni kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa chama na bila kupitia vikao halali vya chama, kujihusisha na vikundi nyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii, kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchinganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama na wanachama wake.

Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa mwongozo wa chama, kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya chama kinyume na mwongozo wa chama, kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama kinyume cha mwongozi wa chama.

MWIGAMBA AINGIA MITINI
Alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Mwigamba, hakutokea katika kikao hicho licha ya kuthibitisha kushirikia kwenye CC kwa ajili ya kujitetea kwa mdomo.

DK. MKUMBO AJITETEA
Alisema aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alihojiwa kwa mdomo na CC na kukiri baadhi ya makosa na mengine aliyakana huku akikataa kumtaja Mhusika wa Pili (M2) katika waraka wa mkakati wa mabadiliko 2013, uliodaiwa kuandaliwa nao hadi atakapopata ridhaa yake. Katika utetezi wake wa maandishi, alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka katiba ya chama, kanuni na mwongozo na kwa maneno yake mwenyewe alikanusha na kwamba mashtaka si ya kweli.

USHIRIKI WA ZITTO KATIKA MKAKATI HUO
Alisema licha ya Ziito kukanusha kuufahamu mkakati huo, lakini Dk. Mkumbo katika mahojiano na CC alikiri kuwa walimpa taarifa juu ya makakati huo na alikuwa anaufahamu.

“Ukweli huu unathibitishwa na mawasiliano ya barua pepe iliyotumwa na Zitto kwa mtu anayejiita Chadema Mpya 2014 wa Oktoba 27, mwaka 2013, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kikao cha CC kilichowavua madaraka,” alisema.

Alisema kuhusu tuhuma za ufisadi ndani ya chama licha ya Dk. Mkumbo kuonyeshwa taarifa mbalimbali ambazo yeye na Zitto walishiriki kupitisha kwenye CC, nyaraka za manunuzi, hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote.

MAAMUZI YA CC
Dk. Slaa alisema mkakati huo haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama pekee, bali ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi.

Alisema kwa maoni ya CC, chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wanachama kama tumaini lao la ukombozi.

Alisema CC imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbalimbali zilizoandaliwa na Zitto ama mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu.

Alisema mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbalimbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambako alidai Zitto alishiriki moja kwa moja.  
 
CHANZO: NIPASHE

JK: Tofauti ya maoni ya Katiba si dhambi

 
Rais Kikwete akihutubia mjini Unguja katika kilele cha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Jakaya Kikwete, amesema kutofautiana maoni ya mabadiliko ya Katiba, si dhambi kwani hadi sasa Tanzania haijapata Katiba nyingine na kwamba yaliotolewa ni maoni ambayo yatajadiliwa na Bunge la Katiba na hatimaye kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana kwenye viwanja vya Maisara Sulemain mjini Unguja katika kilele cha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete aliamua kuzungumzia jambo hilo baada ya UVCCM kuponda mapendekezo ya rasimu ya Pili ya Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, kuhusu mabadiliko ya mfumo wa Muungano kutaka uwe wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.

“Kazi ndiyo imeanza, kama ni mkoko ndiyo kwanza unaalika maua, wananchi wenyewe wataamua kwa ridhaa yao lipi wataliafiki na lipi watalikataa lisiwamo kwenye Katiba mpya ijayo, wananchi kaeni na wabunge wenu ili kujua mnalolitaka na msilo litaka,” alisema.

Aidha, alisema kuna baadhi ya watu wanapita na kupotosha umma kwa kusema kuwa Katiba mpya imekamilika, jambo ambalo si la ukweli na kuitaja hatua inayofuata ni rasimu hiyo kujadiliwa na Bunge la Katiba na baadaye kupigiwa kura na wananchi, hivyo maoni yanayotolewa kuikosoa Tume siyo dhambi.

Alisema bado wananchi wanayo nafasi pana ya kuendelea kutoa maoni yao na kutaka aina ipi ya Katiba na kwamba si lengo la Taifa kuunda Katiba ya kundi fulani au watu kuzuiwa kutoa maoni yao.

Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Rais Kikwete aliwataka vijana kuendelea kuyathamini na kuyaenzi kwani yalitokomeza unyanyasaji, dhulma na ukandamizaji uliofanywa na wakoloni.

Alisema yalikuwa ni Mapinduzi yaliyoondoa matabaka, uonevu na ukandamizaji wa haki kwa walio wengi ambao walibaguliwa na kunyimwa fursa za kibinadamu.

Wakati huo huo, Rais Kikwete, ameisifu Zanzibar kuwa ni nyota inayong’ara ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria katika Afrika.

Rais Kikwete amesisitiza kuwa siyo tu kwamba Zanzibar inaongoza katika Afrika, lakini ni mfano wa kuigwa duniani.

Aidha, ameisifu na kuipongeza Zanzibar kwa kuvuka lengo la Shirika la Afya Duniani (Who) la kuhakikisha kuwa wananchi hawatembei umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya afya.

Zanzibar imeshuka kutoka umbali wa kilomita tano kama inavyopendekezwa na Who hadi kufikia kilomita tatu.

Rais Kikwete pia amekisifu Kikosi Maalum cha Kupambana na Magendo (KMKM) cha Zanzibar kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya majini na kudumisha utulivu ambao Tanzania imeushuhudia katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele cha sherehe zake kitakuwa Januari 12, mwaka huu.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza mwishoni mwa wiki na mamia ya wananchi, maofisa na askari wa KMKM baada ya kuifungua rasmi hospitali kubwa na ya kisasa ya kikosi hicho kwenye eneo la Kibweni mjini Zanzibar.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kikazi katika Zanzibar, alifungua rasmi hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kuhusu mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye nyanja mbalimbali, Rais Kikwete alisema Zanzibar imekuwa na mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kipindi hicho.

Alitaja moja ya mafanikio makubwa kuwa ni katika sekta ya afya ambako miongoni mwa mambo mengine, Zanzibar imefanikiwa kufuta ugonjwa wa malaria.

Alikuwa anazungumzia takwimu za Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Duni Haji, ambaye alimweleza Rais Kikwete kuwa mwaka 2007, vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vilikuwa asilimia 3.1, lakini mwaka 2011 asilimia hiyo ilikuwa imeshuka hadi sifuri. 
 
CHANZO: NIPASHE

Boti ya Kilimanjaro yaua sita, nyingine wanne

 
Yusuph Ilembo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI)
Watu kumi wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti katika Bahari ya Hindi.
Katika ajali ya kwanza, watu sita walifariki baada ya boti ya Kilimanjaro II ilipokumbwa na dhuruba kali katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar wakati ikitokea Pemba kwenda kisiwani Unguja jana asubuhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Juma, alisema jana jioni kuwa maiti sita zilipatikana na kwamba abiria watatu waliokolewa wakiwa hai huku uokoaji ukiendelea.

Hata hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khalfan Mohamed Mshangi, alisema baadaye kuwa zimepatikana maiti tano na tatu zimetambuliwa.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Akram Khamis issa (11), mkazi wa Mwanakwerekwe; Masoud Hamad Abdallah (30), mkazi wa Wete na Nashra Khamis (9), mkazi wa Mombasa, Zanzibar.

Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa na abiria 396 wakiwamo watoto 60 na kwamba abiria ambao hawajapatikana ni 18.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yusuph Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa kazi ya kuwatafuta watu wanaohofiwa kupotea imeanza kufanywa na mabaharia kwa kushirikiana na wananchi.

Alisema boti hiyo ilipofika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa na wimbi moja kubwa na injini kuzimika na watu waliokuwa wamekaa juu wakiwamo watoto waliteleza na kuhofiwa kutumbukia ndani ya bahari.

Alisema kuwa boti hiyo baada ya injini zake kuzimika ilibakia ikielea baharini na kwamba Nahodha wake alifanikiwa kuziwasha tena na kuendelea na safari na abiria waliobakia walifika salama.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar Maalim, alisema wazamiaji waliondoka jana mchana kuungana na baadhi ya wananchi huko Nungwi kufanya kazi ya kutafuta watu wanaohofia kupotea baada ya ajali hiyo.

Hata hivyo, alisema ZMA itatoa taarifa baada ya kukamilika uhakiki wa majina ya abiria kwa meli zote zilizosafiri jana kutoka kisiwani Pemba pamoja na wazamiaji kufika katika eneo la tukio na kufanya kazi ya kutafuta watu hao.

MASHUHUDA WANENA
Baadhi ya mashuhuda waliozungumza na NIPASHE walisema mkasa huo ulitokea sasa 2:30 asubuhi wakati boti hiyo ilipofika eneo la Nungwi na kupigwa wimbi kali na kuelemea upande mmoja.

Suleiman Muhammed Said, abiria katika boti hiyo, alisema baada ya boti hiyo kuelemea upande mmoja, baadhi ya watu walidondoka baharini pamoja na mizigo na kwamba boti iliendelea na safari baada ya kukaa sawa.

Alisema boti hiyo iliondoka Pemba majira ya saa 2:00 asubuhi na kwa mujibu wa ratiba, boti ilitarajiwa kufika Unguja saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana na hitilafu hiyo, ilifika saa 6:00 mchana.

Alisema boti ilipoondoka Pemba, hali ya bahari haikuwa nzuri na ilipofika Nungwi hali ya bahari ilizidi kuchafuka na boti kuyumba.

Alisema hadi boti inafika bandarini, ndugu zake wawili hawakuonekana pamoja na mizigo waliyokuwa nayo katika boti hiyo.

“Nilikuwa na ndugu zangu wawili na mizigo, baada ya meli kutaka kuzama mizigo na baadhi ya watu walidondokea baharini, lakini meli ilipoibuka iliendelea na safari bila ya kuwatafuta,” alisema Suleiman huku akitokwa machozi.

Baadhi ya watu walifika bandarini Malindi waliangua vilio na sura zao kujaa na huzuni kutokana na kutowaona ndugu na jamaa zao.

Abdallah Mohammed Abdallah, aliyefika bandarini kumtafuta mtoto wake ambaye bado hakuwa na taarifa zake, alisema alipokea simu ya mtoto wake aliyekuwamo katika boti saa 2:30 asubuhi kuwa boti inazama.

“Nilipokea simu ya mtoto wangu, alikuwa akilia na kuniambia baba baba tunakufa, meli huku inazama, baada ya hapo simu yake ikawa haipatikani” alisema Abdallah.
Aidha alisema alifika bandarini kupata taarifa sahihi, lakini hakupewa jibu linaloridhisha kutokana na boti kufika bila kumuona mtoto wake. Mmoja wa abiria aliyekuwa anasafiri na boti, Salama Husseni alisema:

“Tulianza safari vizuri ila tulipofika Nungwi mawimbi yalikuwa makali sana, boti yetu ilizidiwa ndipo hali ya wasiwasi ikatujaa abiria wote ila tunamshukuru Mungu hali ilikaa sawa baada ya muda na amani ikarejea.”

AZAM MARINE KIMYA
Hata hivyo, waandishi wa habari walifika katika ofisi za Kampuni ya Azam Marine inayomiliki boti hiyo ili kupata taarifa sahihi, uongozi ulikataa kuzungumza badala yake kuwafukuza.

Jijini Dar es Salaam, NIPASHE ilifika katika ofsi za kampuni hiyo na kukuta msongamono wa abiria ambao walikuwa wakikata tiketi kuelekea Zanzibar.
Hata hivyo juhudi za kumpata msemaji wake zilishindikana baada ya kudaiwa yupo nje ya ofisi.

Wanne wafa Rufiji
Wakati huo huo, watu wanne wamekufa maji na wengine 12 kuokolewa baada ya boti ya Mv Nyaulele waliyokuwa wakisafiria kutoka wilayani Rufiji kwenda Mafia mkoani Pwani kupinduka na kuzama majini katika Bahari ya Hindi usiku wa manane kuamkia jana.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, alidhibitisha tukio hilo na kusema boti hiyo ilikuwa ikitoka Rufiji kwenda Mafia juzi saa 11:00 jioni na ilipofika katikati ya safari ilikumbana na dhoruba kisha kupinduka na kuzama baharini.

Matei alisema kwa kujibu wa taarifa zilizopo polisi, boti hiyo ilikuwa na abiria 16 na mizigo kadhaa midogo midogo ya kawaida ya abiria.

Aliwataja abiria waliofariki kuwa ni Swaumu Muhidin, Tano Shaban ambaye amegundulika kuwa ni mwalimu wa shule moja wapo ya msingi Rufiji, Hadija Ntayala na mtoto mdogo mwenye umri kati ya miezi minne na sita, Najma Yusufu.

Imeandikwa na Rahma Suleiman, Beatrice Shayo, Zanzibar; Kamili Mmbando, Dar na Julieta Samson, Pwani. 
CHANZO: NIPASHE

Thursday, January 2, 2014

Waziri wa Fedha afariki dunia

marehemu Dk William Mgimwa akisoma bajeti ya wizara yake bungeni. 

Dar es Salaam na Iringa. Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki dunia jana katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.
Habari zilizopatikana jana kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema Waziri Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea, jambo ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara (Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu... Natoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Steven Muhapa alisema jana kuwa wamepokea kwa mshituko kifo cha mbunge wao.
Muhapa alisema halmashauri yake imepata pigo la mwaka, kwani walikuwa na mipango mingi ya kutekeleza chini marehemu Mgimwa lakini sasa imeyeyuka... “Alisaidia sana kutuletelea wafadhili kutekeleza ahadi mbalimbali alizoahidi... ni mapenzi ya Mungu.”
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema Mkoa wa Iringa umepoteza mtu muhimu, mahiri na mchapakazi... “Pamoja na kwamba alikuwa CCM, hakubagua mtu. Niliwahi kumpa ushauri mara kadhaa akauchukua ushauri wangu na kuufanyia kazi.”
Mwenyekiti PAC
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amemwelezea marehemu kwamba alikuwa ni mtu mnyenyekevu na hakuwa na ubaguzi katika kutekeleza wajibu wake akiwa kiongozi wa Serikali.
“Kwa kipindi kifupi nilichofanya naye kazi kwa karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha, nikiwa mkaribishwa kama Waziri wa Fedha kivuli, kisha kwenye kamati ndogo niliyounda kuhusu miradi ya umeme ya Mchuchuma, Liganga na Ngaka na baadaye akiwa Waziri wa Fedha, jambo la msingi nililoliona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa aliyonayo kwa watu wengine.
“Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti za kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi kuliko wengine wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu.”
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Florence Majani, Joseph Zablon (Dar) na Geofrey Nyang’oro (Iringa).

source: mwananchi