WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, September 14, 2012

Neno La Leo: Ukimwona Tajiri, Tamani Kuwa Kama Yeye, Na Ukimwona Masikini....



Ndugu zangu,

JAMBO moja kubwa ni dhahiri, kuwa Watanzania bado tuna safari ndefu sana kufikia hatua ya kuitwa taifa la kisasa.


Tuyafanyayo mengi bado ni mambo ya hovyo hovyo, na wenye kuongoza kuyafanya hayo ya hovyo hovyo ni viongozi wetu. Lakini hatuna jinsi, hatua tunayopitia sasa ni lazima tuipitie. Hakuna njia nyingine ya kupita na kutufikisha kwa haraka tunakotaka kwenda. Tusisahau tu , kutunza kumbukumbu. Tufanye hivyo ili Watanzania wa vizazi vijavyo waje wajifunze kutokana na matendo yetu.


Tulikuliku ni aina ya ndege. Viongozi wetu wanaweza kujifunza kutoka kwa ndege huyu. Tulikuliku ana kanuni inayomwongoza. Mara ile tulikuliku anapotaga mayai, basi, hufanya maamuzi magumu ya kujinyonyoa manyoya yake.

Kwa pamoja, tulikuliku dume na jike watafanya tendo hilo.

Kwanini?
Wanajiwekea wenyewe mazingira ya kushindwa kuruka. Wanafanya hivyo ili waatamie mayai yao hata atakapotokea nyoka mpenda mayai wapambane nae hapo hapo. Kwamba wangebaki na manyoya, huenda wangemwogopa nyoka. Hivyo, wangeruka na kuacha mayai yakiliwa na nyoka.


Kwa kiongozi kujinyonyoa manyoya ina maana ya kukubali kushuka chini kwa watu. Kuyaelewa matatizo ya watu anaowaongoza. Kuwa tayari kupambana kuyatatua matatizo ya watu akiwa na watu.


Ilivyo kwa viongozi wetu wengi wa leo, ni kuwa, katikati ya dhiki kubwa ya wanaowaongoza, si tu wamefuga manyoya mengi, bali, hata pale wananchi wanapokabiliwa na adui maradhi, wao, viongozi, wana mbawa za kuwawezesha kuruka juu angani huku wakiwaimbia watu wao nyimbo za kejeli. Na bado watafanya hila ili kuwachonganisha na kuwagawa watu wao walio kwenye dhahma ya umasikini.

Na kuna mawili ambayo yaliwezekana kutumiwa na yakafanya kazi miaka ya sitini hadi themanini, na mawili hayo hata yanapotumika sasa, hayafanyi kazi tarajiwa. Maana, wakati umebadilika. Ni yepi hayo?

Naam, ni kwa kiongozi kutumia Uongo na kutishia nguvu za mamlaka. Kiongozi anayetaka kufanikiwa katika zama hizi ni yule aliye tayari na kuachama na mambo ya zama hizo; kuwaongopea watu wako na kutishia nguvu za mamlaka. Badala yake, kuwa tayari kufanya maongezi hata na wale ambao huko nyuma haikuwezekana kukaa nao meza moja.


Vinginevyo, Watanzania tungali na safari ndefu sana. Njia ina miba mingi, lakini ni lazima tuipite. Hakuna njia nyingine.

Nilipata kuandika, kuwa kwenye Uchina ya kale kulikuwa na mwanafalsafa kwa jina la Comfucius. Katika mafundisho yake mengi aliyopata kumpa mwanafunzi wake Tzu Kung, mojawapo linahusu dhana ya utajiri na mahusiano yake na umasikini. 



Comfucius anasema; ukimwona mtu tajiri(aliyefanikiwa kimaisha),basi tamani kuwa kama yeye, lakini, ukimwona aliye masikini, basi, jitafakari wewe mwenyewe.
 


Kwa mwanafalsafa Comfucius, dhana ya utajiri haikuwa na maana kuwa na mali pekee, bali, pamoja nazo, ni uwezo wa mtu kuishi maisha adilifu na yenye fadhila (virtues). Na katika fadhila zote, ile ya unyenyekevu na ukweli ndio chanzo cha fadhila nyingine zote.
 


Umasikini vilevile, yumkini unaweza kuwa na maana ya kukosa mali na uadilifu. Ndio, mwanadamu waweza kuwa na mali lakini ukakosa uadilifu. Ni dhahiri, katika hali hiyo, hata mwenye mali naye ni masikini sana. 



Kuna kitu kinatokea katika jamii yetu. Wengine wanakiona, wengine hawakioni. Wengine wanakiona lakini hawataki kukiona. Na kuna wanaoonyeshwa , lakini wanashindwa kukiona. Tunafanyaje?
 
Hakuna kitu kingine bali ni watu ndio wenye kuifanya nchi. Kuna kitu kimetutokea waTanzania. Kinaendelea kuota mizizi. Na kwa vile kitu ndicho hufanya vitu, basi, mimi naviona vitu vya hovyo hovyo vikitokea katika jamii yetu. Na pengine, kwa vile tumeanza kuwa na hulka za hovyo hovyo, basi, vinavyotokea hatuvioni kuwa ni vya hovyo hovyo. 



Naam, vinatokea kila leo, na kuna wenye kusimama kuvitetea vitu hivyo vya hovyo hovyo. Ni kuanzia namna tunavyouza rasilimali zetu. Na wenye kuuza, ni viongozi wetu waliogeuka ’ madalali’ wa kutanguliza tenipasenti. Hawa wa kundi la pili ndio matajiri wetu wapya . Ni watu waliopungukiwa chembe nyingi za uadilifu, hivyo basi, nao ni masikini.
 


Na tumeimbiwa sana, kuwa nchi yetu ni masikini (japo wanamaanisha kipato pekee). Wenye kutuimbisha wanasahau, au labda hawajui, kuwa sisi ni masikini zaidi kwenye maadili. 



Ndugu zangu, 



Katika wakati huu tunaoenda nao, na tujifunze kutoka kwa mwanafalsafa Comfucius. Kwamba katika umasikini wetu huu kama taifa, basi, walau tujitahidi kujitafakari tulivyo huku tukiwaangalia wenzetu waliopiga na wanaondelea kupiga hatua za mafanikio ya kiuchumi.
 



Maana, nasi tutamani kuwa taifa la kisasa. Lakini hatuwezi kuwa taifa la kisasa kwa staili hii tunayoenda nayo. Oneni kule Marekani. Hawa ni matajiri wa kipato. Wanafanya kazi usiku na mchana kutimiza ndoto ya taifa lao. WaMarekani wanaijua ndoto yao na huungana dhidi ya yeyote anayetaka kuikwamisha. Na pengine ni katika kutimiza ndoto hiyo sisi tunalalamika kuwa Marekani ni taifa baya. 



Tujiulize; ni taifa gani litaishi bila kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu? Hivi, ni nini ndoto na maslahi ya kudumu ya Tanzania? Je, ni WaTanzania wangapi wakiwemo viongozi wanaijua sera ya Tanzania inapohusu uhusiano wake na mataifa mengine? 


Na hilo ni Neno La Leo:
 
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam
13, Septemba, 2011

Thursday, September 13, 2012

NIMEPENDA UPEO WA UKWELI WA MR. ZEMBWELA ALIPOHOJIWA MA MKASI TV; HEBU SIKILIZA


Waziri Mkuu Wa Zamani Misri Afungwa Jela


 

Mahakama nchini Misri imemhukumu kifungo cha miaka mitatu gerezani waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Ahmed Nazif.Nazif amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la ufisadi.

Bwana Nazif, ambaye alikuwa waziri mkuu kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka jana wakati mapinduzi ya kiraia yalipofanyika, pia ameamrishwa kulipa faini ya dola milioni 1.5.
Mwaka jana Ahmed Nazif alifutwa kazi kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kushtakiwa kwa kosa la kupata faida haramu kutokana na biashara alizofanya kinyume na sheria.

Nazif alikuwa mmoja wa maafisa wakuu katika serikali ya rais wa zamani Hosni Mubarak.Alikamatwa miezi kadhaa baada ya kuacha kazi mwezi Januari mwaka 2011, muda mfupi kabla ya rais Mubarak kuachia ngazi.

Maafisa kadhaa wa uliokuwa utawala wa Mubarak wamefikishwa mahakamani kwa aidha kosa la njama ya kuwaua waandamanaji au makosa kuhusiana na ufisadi.Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha jela mwezi Juni baada ya kuhusishwa na mauaji ya waandamanaji.

Chanzo:  http://www.bbc.co.uk/swahili/habari

Wednesday, September 12, 2012

Magufuli Akagua Barabara Ya Kilwa



 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akijiridhisha kwa kupima kiwango cha lami inayowekwa upya katika barabara ya Kilwa na Kampuni ya Kajima ya Japan leo jijini Dar es salaam. Wengine wanaoshuhudia kutoka kulia ni mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki, Balozi wa Japani nchini Tanzania Masaki Okada na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Kajima.
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli (mbele) akiwa amefuatana na balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam na viongozi wengine wa wizara akikagua moja ya sehemu ya barabara ya Kilwa inayojengwa upya na kampuni ya KAJIMA  ya Japan kutokana na barabara hiyo iliyokamilika hapo awali kuwa chini ya kiwango na serikali ya Tanzania kuikataa na kuiagiza kampuni hiyo iijenge upya kwa gharama zake.
  Wafanyakazi wakiendelea na ujenzi wa barabara ya Kilwa leo jijini Dar es salaam
 Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akikagua ujenzi wa daraja la Kigamboni akiwa ameambatana na viongozi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki (wa pili kutoka kulia) Mbunge wa Kigamboni Dkt.Faustine Ndugalile (wa tatu kutoka kulia) leo jijini Dar es salaam. Daraja la Kigamboni linajengwa na kampuni ya China Railways Engineering kwa gharama ya shilingi bilioni 214 na linatarajia kukamilika kabla ya mwaka 2015


 Mmoja wa wafanyakazi wa daraja hilo ambaye jina lake halikupatikana mara moja akiendelea na zoezi la kupiga picha huku akiwa amesimama kwenye mtando unaopitisha umeme mwingi bila kuchukua tahadhali wakati waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli alipokua akikagua maendeleo ya ujenzi wa  daraja hilo leo.
Picha na Aron Msigwa -MAELEZO

Thursday, September 6, 2012

Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi- Makala Yangu Raia Mwema Jana Jumatano



Na Maggid Mjengwa,

HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.

Mwandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa, Daud Mwangosi ameuawa. Polisi wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Jumapili ya Septemba 2, 2012 itabaki katika kumbukumbu za Watanzania kwa mamilioni kwa kufikiwa na taarifa za kutisha za mauaji ya mwandishi wa habari. Haya yanaingia katika historia kuwa ni mauaji ya kwanza kwa mwandishi wa habari kufanyika hadharani tangu nchi hii ipate Uhuru.
Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na walifanya nini siku walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa ile ya mauaji ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa ilinikuta nikiwa Iringa, umbali wa mwendo wa saa moja  kwa gari kufika eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.

Jioni ile nilikuwa nikifundisha soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa zile kwa simu,  nilisitisha mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa zile.  Nilipowaambia kuwa nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa habari ameuawa Mafinga, mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; “ Kwanini?”
Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa kujiuliza sasa; KWA NINI?

Mwandishi wa habari ni mjumbe katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi kuwa na hofu ya kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya  kutumia silaha.  Ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa kazini kwenye maeneo hata ya vita.

Askari asiyejua kutofautisha kati ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa Msalaba Mwekundu aliyeshika mkoba wa Huduma ya  Kwanza na raia anayefanya vurugu au adui aliyeshika silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni askari makini.

Polisi katika nchi ni  moja ya viungo muhimu vya dola kuu. Polisi ni mkono mrefu wa dola ( State's extended arm). Inapofika mahali, mkono huu muhimu unapoonyesha udhaifu wa ndani katika mfumo wa utendaji kazi wake, basi, umma nao unakosa imani na mkono huu mrefu. Ndipo hata raia wa kawaida niliyemsikia kwenye runinga ya ITV akitamka; ” Kama polisi si makini, basi ni heri wasiwepo watuache wenyewe tuendeshe mambo yetu, maana sisi wananchi tunaishi kwa amani na utulivu”.
Kauli kama hizi ni kiashiria cha umma unaopungukiwa imani na dola na viungo vyake, ikiwamo polisi. Hili haliwezi kuwa jambo jema.

Na hakika, kama  Taifa,  tunafanya makosa kuamini,  kuwa  nchi yetu ni ya amani kwa vile wananchi wetu hawagombani.

Kama watu hawagombani basi maana yake ni nchi ina amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya amani.  Maana, kama watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na uadilifu wa viongozi; mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu mengine  wanayotendewa au wanaotendeana wanajamii,  basi, amani hiyo itakuwa ni ya muda tu.

Maana, kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea uvunjifu wa amani, hiyo  itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na  hofu.

Hivyo basi, kwa hilo la mwisho, itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi ya hofu. Na hofu hiyo haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu hufikia ukomo wa kuhofia. Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka! Ndipo hapo tunapoona nchi zinalipuka na watu kuchinjana.

Tumefika mahali hata wawakilishi wa wananchi kwa maana ya wabunge , wanatiwa mbaroni na polisi katika mazingira ya kudhalilisha, tulishuhudia hili likimtokea Mbunge wa Viti Maalumu, CUF, Tabora Mjini.  Mbunge ni mwakilishi wa wananchi. Mbunge ni mjumbe aliyetumwa na wananchi. Ana kinga ya kikatiba.
Kwa polisi kumdhalilisha  mjumbe wa wananchi ina maana pia ya kuwadhalilisha waliomtuma. Haya ni matendo ya aibu.

Kilichomtokea mwandishi Daud Mwangosi ni aibu pia ya Taifa hata kimataifa. Kupunguza aibu hii ni kufanyika kwa uchunguzi huru, na kwa wote watakaobainika kuhusika na aibu hii wachukuliwe  hatua za kisheria. Na wenye kustahili kuwajibika wawajibike kulinda heshima ya  serikali iliyo madarakani.
Hii ni nchi yetu. Katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania. Kuna umma uliopo na unaokuja. Umma  unaotegemea sana busara katika uongozi wetu.

Tuanze sasa kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa kufanya na kuamua yale yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa vipo leo na kesho havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama nchi itakuwapo daima.

Tusifike mahali  tukabaki tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi, ya makundi yao na vyama vyao,  wakashinikiza au kuelekeza yale  yenye kuchochea machafuko makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.

Na tunafanyaje pale tunapowaona viongozi  wa kisiasa na watendaji wakifanya maamuzi yasiyo na busara na kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza uhai na hata kuchochea machafuko?
Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.

Na katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu  na kujenga mazingira ya chuki na  uhasama, lakini ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu na kuondosha mazingira hayo ya chuki na uhasama. Na nchi yetu kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo katikati ya mazingira ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa vyama vya siasa au wanajamii.

Kihistoria, Watanzania tumeishi kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama miongoni mwetu unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila. Tunaziona sasa, dalili za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa,  kutaka kupandikiza miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti zetu za kidini na kikabila, tofauti zetu za kiitikadi.  Wanafanya hivyo mara ile wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya kisiasa. Hawa ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.

Katika nchi zetu hizi, ni wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha malengo yao,  huwa tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na kuwavutisha bangi ili washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila.  Tumeyaona hayo Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.

Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.
Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu.  Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru.

Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna  mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko  haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.
Maana, tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa.

Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika.

Tuesday, September 4, 2012

Tafakuri Ya Usiku; Je, Uwezo Wetu Wa Kufikiri Umepungua?


 



Ndugu zangu,

Yanayotokea nchini mwetu yanatutaka sio tu tufikiri, bali, tufikiri kwa bidii. Lakini swali ni hili; Je, uwezo wetu wa kufikiri umepungua?
 

Yumkini si kwa aliyekuwa na 

ujasiri wa kuipiga picha hiyo hapo juu. Alifikiri sana pia. Na si kwa aliyekaa chumba cha habari na kuumiza kichwa, kisha akaamua picha hiyo ipambe sura ya mbele ya gazeti la Mwananchi la juzi. Hapa Iringa gazeti hilo liligombaniwa kama njugu, na bila shaka sehemu nyingine za nchi. 

Naam, siku hizi utasikia ikisemwa; " Tumefika pabaya!" Mwingine atasema; " Tunakokwenda ni kubaya!". Lakini, ni Watanzania wangapi wenye kuuliza maswali haya; " Tumefikaje hapa?" Na " Je, tunaendaje?" Maswali hayo yanamtaka mwanadamu afikiri kwa bidii. 


Wakati mwingine nafikiri, kuwa Watanzania tumechoka kufikiri. Hata kwenye maswali magumu yenye kutuhusu tunataka wengine wafikiri kwa niaba yetu. Unaweza kukutana na Mtanzania mwenzako ukamwuliza; " E bwana ee, unafikiri nini juu ya jambo hili?". Jibu lake; " Kwani wewe unaonaje?"- Ni moja ya maswali yenye kuashiria anaykujibu swali lako amechoka kufikiri.
 

Na wakati mwingine tatizo si kutofautiana kifikra, bali kutofautiana namna au jinsi ya kufikiri. Swali moja, lakini unaweza kuona namna tunavyotofautiana katika kuchagua njia ya kulisogelea ( approach) swali husika. 


Na kuna wenye kukimbilia kutafuta njia za mkato. Ndio, majawabu ya mkato. Na baadaye itakuwaje? Inshallah na BwanaYesu Asifiwe!
 

Maggid Mjengwa,
 
Iringa

Monday, September 3, 2012

Taarifa Ya Jukwaa La Wahariri Kuhusu Kuuawa Kwa Mwandishi Daudi Mwangosi




TAARIFA YA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI
  UTANGULIZI:

1. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
2. Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa akiwa kazini jana, Septemba 2, 2012, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
3. Tukio hili linaiingiza Tanzania katika historia mbaya ya ukiukwaji na ukandamizwaji wa uhuru wa habari, kwani ni kwa mara ya kwanza tunashuhudia mwandishi wa habari AKIUAWA WAKATI AKITEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KIHABARI.

4. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Mwangosi kabla ya kufikwa na mauti saa 9.30 alasiri katika kijiji cha Nyololo, Mufindi, alizingirwa na kushambuliwa na polisi waliokuwa katika eneo la tukio. Na hata alipopiga kelele za kuomba msaada, hakusikilizwa na matokeo yake aliuawa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
5. Kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania, TEF tumechukua hatua za haraka za kuunda timu ya uchunguzi wa suala hilo, ambayo itakwenda mkoani Iringa mapema kadri itakavyowezekana, ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Lengo la uchunguzi huo ni kuweka kumbukumbu sahihi (documentation) ya tukio hilo la aina yake katika historia ya nchi yetu.

6. Matokeo ya uchunguzi huo pamoja na mwingine unaofanywa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa hatua ambazo TEF inachukua dhidi ya Jeshi la Polisi katika siku chache zijazo.
MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF

Kwa kuzingatia taarifa kutoka Iringa na zile za vyombo vya habari vya jana (Jumapili, Septemba 02, 2012) na leo (Jumatatu, Septemba 03, 2012), TEF ina mtizamo na msimamo kama ifuatavyo:

1. Kwanza tunalaani vikali tukio la kupigwa, kisha kuuwawa kwa mwandishi Daudi Mwangosi ambalo limeigusa tasnia ya habari kwamba sasa pengine waandishi wa habari ni malengo “target ya polisi” wanapokuwa kwenye kazi zao.

2. Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo zinategemeana.
3. Kwa matukio ya aina hii, tunadhani wakati mwafaka kwa uongozi wa Jeshi la Polisi nchini kuwajibika, kuazia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na uongozi wa Makao Mkuu, akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema.
4. Tunasema hivi kwani kuna kila dalili kwamba polisi wanahusika kwa namna moja au nyingine na tukio au/na matukio yaliyosababisha kifo cha Mwangosi, kwani kitendo cha kumzingira tu na kumshambulia kinathibitisha kwamba hawakuwa na nia njema hata kidogo dhidi ya mwandishi huyu.
5. Taarifa ambazo TEF tunazo, pia zinadai kwamba kulikuwa na mpango wa polisi wa “kuwashughulikia waandishi wa habari watatu” (Mwangosi) akiwa mmojawapo na hilo lilionekana likitekelezwa kwa polisi kumshambulia mwandishi huyo, baadaye alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha
6. Hili linatiliwa nguvu na tukio jingine la polisi kumpiga na kumjeruhi mwandishi mwingine, Godfrey Mushi ambaye ni mwakilishi wa gazeti la Nipashe mkoani Iringa. Mwandishi wa tatu ambaye hadi tunapoandika taarifa hiyo yumo katika mpango wa ‘kushughulikiwa na polisi’ ni Francis Godwin ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
7. Vitendo vya aina hii havivumiliki na havipaswi kuachwa kuendelea kwani ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa habari nchini. Hatuwezi kuendelea katika mazingira ambayo polisi wanageuka kuwa chombo cha mauaji ya raia badala ya kuwa walinzi wa raia.
8. Kwa maana hiyo, mbali na uchunguzi ambao utafanywa na polisi, tunatoa wito kwa Serikali kuunda chombo huru, ambacho kitabaini ukweli, na matokeo yake yatangazwe kwa umma, huku wahusika wa aibu hiyo wakichukuliwa hatua za kisheria. Tunasema hivyo, tukifahamu kwamba tayari kuna jitihada za kuficha ukweli na kueneza propaganda za uongo kuhusu tukio zima.

9. Mwenendo wa aina hii wa chombo cha dola kuamua kutumia silaha kuua na baadaye kupanga mbinu chafu za kuficha ukweli ni hatari kwa Taifa, na unaiweka demokraisia ya nchi yetu njia panda, huku tukielekea katika hatari ya Taifa kutumbukia katika uovu.

IMETOLEWA NA:
NEVILLE MEENA,
KATIBU MKUU – JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF) SEPTEMBA 3, 2012