WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 6, 2012

Hukumu Ya Godbless Lema: Tafsiri Yangu




Ndugu zangu,

Kuna kila dalili, kuwa tunakokwenda ni kubaya. Tumefika mahala sasa, kuwa kwenye siasa tunaingiza hulka za ushabiki wa Simba na Yanga. Hii ni hatari kwa taifa.

Jana alhamisi, kabla ya jua la saa sita mchana, habari zililipuka na kusambaa kote nchini; Mahakama imemvua Ubunge Godbless Lema.

Ni ukweli, Godbless Lema ni mbunge kijana na maarufu sana hapa nchini. Lakini, imefika wakati Watanzania tukubali na tuamini, kuwa Mahakama inafanya kazi kama mhimili huru wa dola hata kama kunahitajika, kupitia Katiba mpya ijayo, kuboresha mhimili huo ili uaminike zaidi.

Ni kwa mantiki hiyo, kuwa mahakama ni mhimili huru wa dola, tumeshuhudia  hata Serikali ikifikishwa Mahakamani na hata kushindwa kesi. Tumeshuhudia , katika historia ya nchi hii,  Wabunge wa CCM , bila kujali majina na umaarufu wao wakifikishwa mahakamani na kushindwa kesi.

Kwa Godbless Lema,  kutoa hadharani madai kuwa Rais wa nchi anahusika na hukumu yake ni kauli ya bahati mbaya sana anayopaswa yeye mwenyewe Lema, na chama chake, kuacha kuendelea kuitoa, hana maintiki. Inaidhalilisha Mahakama. Ni kauli iliyotolewa kwa haraka na isiyo na tija kwa taifa.

Tukubali kwa sasa, kuwa kule Arusha hukumu imeshatolewa. Kuna fursa pia ya kukata rufaa ya hukumu hiyo kwenye Mahakama iliyo juu zaidi. Hakika, kwa Godbless Lema na chama chake, huu ni wakati kutafakari hukumu hiyo na kuona ni namna gani ya kwenda mbele kisheria au kisiasa.

Haiwezekani kwa sasa kudai kuwa CCM inahusika na hukumu hiyo. Wakati kimsingi CCM imepata ’hasara nyingine ya kisiasa’  kwa matokeo ya  hukumu hiyo. Kwa anayechambua kwa undani sana, hukumu ya Lema ya kuvuliwa ubunge imekuja katika wakati mbaya sana kwa chama tawala, CCM.

Ni hukumu inayomtangaza na kumwongezea umaarufu Godbless Lema na chama chake cha Chadema.  Leo, bila kufuatilia mwenendo wa kesi husika,  kuna wanao-sympathy na Godbless Lema na Chadema, wakiamini CCM  imetumia Mahakama kumhujumu Godbless Lema na Chadema. Na kama Lema atasimama tena kuwania kiti hicho, basi, yumkini kura zake zitaongezeka maradufu. Lema ana hakika ya kura nyingi pia za ’ kuonewa huruma’.

Na ukweli mwingine ni huu, katika nchi yetu kwa sasa kuna kundi jipya la wapiga kura. Hawa naweza kuwaita ” Wapiga kura dhidi ya hali iliyopo”- Aina hii ya wapiga kura inaundwa kwa idadi kubwa na waliokuwa wapiga kura wa CCM katika chaguzi za miaka ya nyuma na ambao sasa hawaridhiki na hali iliyopo ndani na nje ya chama chao.

Ndio, hawa ndio waliokuwa wapiga kura wa CCM na ambao sasa  wanawachanganya sana CCM. Ndio hawa waliompigia kura Nassari Arumeru, ndio hawa waliowahakikishia viti vya udiwani Chadema kule Ruvuma, Mwanza na Mbeya.
  
Maana, ni wapiga kura wa kundi hili unaoweza kuwaona  wakijaa kwenye mikutano ya kampeni za CCM, lakini, kwa vile hawapati majibu ya maswali yao ya namna gani CCM na Serikali yake, si tu itakavyorekebisha, bali inavyorekebisha sasa ’ Hali iliyopo’, basi, siku ya kupiga kura wanatumbukiza kura zao kwa wapinzani. 

Ndio, ni ukweli pia , kuwa ’ Ndani ya nyumba ya CCM’ kwa sasa  hakuna  amani na utulivu. Makundi na mbio za kuelekea kwenye  Urais 2015 zinawaacha wana-CCM wakivurugana wenyewe kwa wenyewe.

Focus sasa haiko kwenye kutekeleza ahadi lukuki walizowaahidi wapiga kura kwenye kampeni zilizopita. Kwa sasa kuna wenye kufikiria hatma zao za uongozi. Kuna waliojikita kwenye mnyukano wa kimakundi kwenye vita ya kuelekea Urais wa 2015.  CCM ya sasa inaonekana kuwa mbali na wananchi na kero zao zinazowakabili.  CCM ya sasa imeacha kuwa ' Kimbilio la Wanyonge' kama wakati mmoja alivyopata kukiri Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. CCM ya sasa ni kimbilio la ' wenye nacho' wakiwamo wafanyabiashara.

Ndio, CCM imeanza kulipa gharama ya wananchi kutoridhika na ’ Hali iliyopo’.  

Maggid Mjengwa,
Iringa.

Habari kwa hisani ya Mjengwa Blog

Thursday, April 5, 2012

ARUMERU MASHARIKI WAMEFUATA BUSARA ZA BABA WA TAIFA?


Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa anawaasa wananchi
kuchagua viongozi wanaowajaliwaache kuchagua viongozi kwa ushabiki wa vyama;
je sifa stahiki za viongozi bora zilitumika Arumeru mashariki?

Asante sana Marehemu Baba wa Taifa kwa ushauri mzuri ni kazi yetu sisi wenye nafasi za kuwaelimishawananchi kwa faida yako


Wednesday, April 4, 2012

MHESHIMIWA LIVINGSTONE LUSINDE KABLA NA BAADA YA UCHAGUZI ARUMERU MASHARIKI


Je Mheshimiwa Lusinde alikuwa amesahau kuwa siasa ni Mchezo mchafu ambao unachezwa kwa mbinu ya hali ya juu, mpinzani wako anatafuta kila mbinu ili utereze tu nayeakumalize,bila kuchafua mazingira ya uadilifu na demokraisa ya kweli?

Itakuwa ni vyema kama atakumbuka maneno ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya kuwaaga wabunge mwaka 2010 aliwahi sema kuwa Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu kwangu na kwa Serikali yetu.  Bunge letu limekuwa kielelezo kizuri cha ustawi wa demokrasia nchini.  Mmetoa hoja nyingi nzuri za kukosoa na kuishauri Serikali.  Ingawaje kuna baadhi ya nyakati maneno yalivuka mipaka ya staha,  lakini, napenda kuamini kuwa ilikuwa ni kwa nia njema!  Isitoshe elimu haina mwisho na wakati mwingine kukosea ndiyo kujifunza”.
narudia tena maneno hayo hayakustahili kusemwa na kiongozi kama yeye mwenye heshima kubwa ndani ya Taifa na chama chake; maneno yake yalivuka sana mipaka ya staha ambayo rais wetu alishawahi sema;
lakini pamoja na hayo yote tunamshukuru kwa kujitokeza hadharani kwa kupitia Clouds Redio katika kipindi cha Jahazi na kukiri kuwa alikuwa ameshindwa kuvumilia kwa namna alivyochokozwa na kutukana na upande wa pili; huu ni uungwana hata kama taifa litapokea msamahaa huu kwa hisia tofauti;
kwa wanasiasa wote na wale wote wanaopenda siasa, siasa inahitaji uvumilivu mkubwa sana, na kuweza kushinda ushindani ni nguvu ya hoja inatakiwa zaidi na sio ubabaishaji, siasa zilizo jaa ubabaishaji mwisho wake ni jazba na matusi na hatimaye mapigano

BAADA YA UCHAGUZI PICHA NA MAELEZO KWA HISAN YA MJENGWA BLOG. 
Mimi Mwanakijiji Ana Haya Kwenye Facebook Yake...

"Livingstone Lusinde akizungumza kwenye Clouds FM Jahazi anaomba radhi, msamaha kwa kauli na maneno ya matusi aliyoyatoa kwenye kampeni kule Arumeru Mashariki. Anasema ni maneno tu ya jazba ambayo hayana ukweli wowote. Kwa ufupi anasema anajutia kauli zake hizo. Asamehewe?"
Mungu Ibariki Tanzania

Monday, April 2, 2012

Anguko La CCM Arumeru: Tafsiri Yangu





Ndugu zangu,

Unaweza kuwatawanya watu kwa mabomu , lakini kamwe, mabomu hayawezi  kuitawanya mioyo ya watu yenye kutaka mabadiliko.

Habari kubwa usiku wa kuamkia leo ni anguko la CCM kule Arumeru Mashariki kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha Ubunge.

Tafsiri yangu;
Kuna wakati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipata kutamka; " CCM haina hati miliki ya kutawala". Mkapa aliusema ukweli wake ambao kwa bahati mbaya hupata tabu kuusimamia. Na hakika, idadi ya Watanzania wenye kutaka mabadiliko inazidi kuongezeka.  Na katika siasa za nchi hii ukiona wanawake watu wazima wanashiriki mikutano ya kampeni ya wapinzani, basi, ujue ni ishara ya mabadiliko yanayokuja.

Na ukweli mwingine ni  huu; vijana wengi zaidi wamekuwa mstari wa mbele katika kutaka mabadiliko hayo.  Kimsingi Arumeru Mashariki wamechagua mabadiliko. Na si kwamba Chadema ni chama bora na makini sana, la hasha, Watanzania wengi zaidi  vijana wanaonyesha kuichukia CCM. Miongoni mwao ni Wana-CCM.  Kiukweli, mvuto wa Chama Cha Mapinduzi kwa Watanzania na hususan vijana unazidi kupungua.

Na ajabu ya matokeo ya Arumeru?
Katika hali isiyo ya kawaida, kuna Wana- CCM waliyoyapokea kwa furaha matokeo ya chama chao kushindwa Arumeru. Tafsiri yake?  Ni kushamiri, si tu kwa makundi ndani ya chama hicho, bali, hofu ya kutokea kwa mpasuko ndani ya chama hicho katika mbio za kuusaka Urais ifikapo mwaka 2015.

Kitakachotokea sasa ndani ya chama hicho ni ‘ Witch hunting’- kutafutana uchawi. Bila shaka, kuna maswali yatakayoulizwa. Moja kubwa ni hili; kimeshindwa chama  au mgombea? Na msukumo wa swali hilo ni katika kumtafuta mchawi na kukitenganisha chama na mgombea katika ‘Anguko la Arumeru’.  Huo utakuwa ni mwendelezo wa ‘ Vita vya Panzi’ ndani ya CCM. Lakini, katika siasa, kuna wanaoamini pia, kuwa wakati mwingine kuna lazima ya kuwepo kwa ‘ Vita vya Panzi’ ili kujitenganisha na kumbikumbi.

CCM ifanye nini?

Jibu; ifuate njia ya Dr Harrison Mwakyembe
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Ipinda  hivi majuzi  Dr Mwakyembe alitoa kwa watu wake kauli ya ‘ Kichifu’ na iliyojaa hekima na busara. Alisema; “ Mimi sikubaliani na mtu yeyote anayesema kitu cha kwanza ni chama  chako…. Hapana, mimi kitu cha kwanza  kwangu siyo CCM , cha kwanza mimi ni Mtanzania, cha pili ndio tunaingia kwenye vyama. Mtu anayekimbilia chama kuwa cha kwanza hivi hicho chama kingetokea wapi kama siyo taifa?”. ( Dr Harrison Mwakyembe, Nipashe, Machi 31, 2012)

Na nilimwona na kumsikia Dr. Mwakyembe akiyasema hayo kwenye runinga.  Umati ule uliomshangilia Dr Mwakyembe ulikuwa wa wananchi bila kujali itikadi zao. Kulikuwa na Wana -Chadema pia, na kiongozi wa Chadema alipewa kipaza sauti kuongea kumkaribisha ‘ Chifu Mwakyembe’ aliyerudi nyumbani na mtazamo mpya wa kizalendo.

Kuifuata njia ya Mwakyembe itawasaidia CCM kurudisha umaarufu wao. Maana,  moja ya sababu za wananchi walio wengi kuichukia CCM ni hulka yake ya kuwabagua wapinzani na kuwaona ni watu wasiofaa kushiriki uongozi wa nchi.

WaTanzania wengi sasa wanatambua, kuwa si kweli wapinzani ni watu wabaya. Ni maadui. Kwamba watasababisha vita na vurugu. Wananchi wameona pia kazi njema inayofanywa na upinzani. Ghiliba hii ya CCM kuwachonganisha wapinzani kwa wananchi imepitwa na wakati. Badala yake, inachangia kupunguza kura za CCM.

Na CCM isipobadilika sasa, na Chadema ikabaki kama ilivyo sasa bila kusambaratika, basi, CCM  itakuwa na wakati mgumu sana ifikapo 2015, maana, kuna ‘Jeshi kubwa’ la vijana linalojiandaa na kushiriki uchaguzi wa 2015.  Jeshi hili linaundwa na vijana wengi wasio na ajira wala hakika ya maisha yao ya kesho. Wanaiona CCM kama sehemu ya matatizo yao. Wana kiu ya kumpata mkombozi.

Na wanafunzi hawa wa Shule za Kata wamegeuka kuwa ‘ agitators’ wazuri wa mabadiliko. Ikumbukwe, shule za kata ziko vijijini. Siku hizi hata  waliokuwa wakiitwa ‘ wajinga’ wa vijijini wamepata walimu wa kuwafungua macho. Watoto wao wenyewe wanaosoma au waliomaliza shule za kata na kubaki vijijini kwa vile hata uwezo wa kujisomesha elimu ya juu hawana. Hawa hawana mapenzi na CCM.

Na katika vijana mia moja hii leo, utapata kazi kubwa kuwapata 20 wanaoipenda CCM. Huu ndio ukweli wa hali halisi. CCM ibadilike na kuwa chama cha kisasa kilicho tayari hata kuongoza nchi pamoja na wenzao wa upinzani. Yumkini jitihada za CCM kuangamiza upinzani zaweza kuwa na madhara makubwa endapo CCM itapata bahati mbaya ya kuondolewa madarakani 2015.  Maana, anguko hilo laweza pia kumaanisha kifo cha chama hicho.

CCM haipaswi sasa kufikiria mikakati ya kuangamiza upinzani ili watawale daima. Dhana ya ’ CCM Daima’ ni ndoto iliyopitwa na wakati. Katika Tanzania ya sasa kuna wengi wenye kuombea  kubaki hai na kushiriki kuzifuta ndoto kama hizo.
  
CCM ya sasa inapaswa kupanga mikakati ya kuendelea kuongoza dola huku ikishirikiana hata na wapinzani. Ingawa hata huo ni mtihani mgumu wenye kukihitaji chama hicho kuwa na watu makini zaidi badala ya waendekeza fitina na majungu.

Na hii ni tafsiri yangu.


Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
Habari kwa hisani ya Mjengwa blog

CHADEMA YASHINDA UCHAGUZI MDOGO ARUMERU MASHARIKI


Kwa Mujibu Wa Facebook Ya Zitto Kabwe: Chadema Yashinda Arumeru Mashariki

Zitto Kabwe anaandika usiku huu: 
"Moja ya Usiku Mzuri sana kwenye Historia ya chama chetu. Tumeshinda Madiwani mikoa yote nyeti na zaidi tumeshinda Ubunge Arumeru. Hakuna raha kwenye siasa kama kuongeza Mbunge katikati ya kipindi cha Bunge. Twamshukuru mola. Hongera viongozi wenzangu na wanachama wetu na watanzania kwa ujumla kwa kutupa nguvu. Its a 'snow ball effect' ! Watch our steps"
Habari kwa hisani ya Mjengwa blog

Sunday, April 1, 2012

"KUDADADEKI" NA UCHAGUZI MDOGO ARUMERU YA MASHARIKI


TUMEJIFUNZA NINI KUTOKANA NA UCHAGUZI MDOGO ARUMERU MASHARIKI?


  • Siasa zisizo na mvuto wa maendeleo ya kuwakomboa watanzania;

  •  siasa za kupakana matope badala ya kunadi sera za kuwakomboa watanzania.

  • Kampeni zilizojaa matusi au maneno yasiyofaa kwa tija ya maendeleo ya mtanzania

  • Malumbano, vijembe, matusi na kashfa kati yamiongoni mwa vyama vinavyoshiriki.

  • Tumeona aina ya viongozi wabunge ambao tunawategeme watuvushe kwenye maisha bora na kutujengea mazingira ya maisha bora katika karne ya teknolojia na sayansi kwa mwendo huu ni ndoto kufika huko.

KAMPENI NI NINI?

Kwa kifupi, Kampeni zilianza zamani. Katika vitabu tumesoma kuwa zilianza enzi za wanafalsafa mahiri duniani Socrates na wenzake.

Wakati huo ilikuwa ni njia mbadala ya kumwondoa madarakati kiongozi asiyefaa.

Katika Tanzania yetu tunaweza kujifunza jinsi Mwalimu Nyerere alivyofanya kampeni ya kudai uhuru kwa kuunganisha nguvu za watanzania wote kuonyesha na kuwashawishi wananchi wazawa kukubali kuwa mkoloni mtawala wa wakati huu alikuwahafai kwa maendeleo yetu na kwa uhuru wetu. Kwa mtazamo chanya hizo zilikuwa kampeni kwa vile zilihusisha kuwashawishi wananchi kuunga mkono juhudi za wapigania uhuru kumwondoa mkoloni. 

Kampeni kama wengi walivyowahi sema ni wakati ambao vyama vinavyowania uongozi katika ngazi yeyote ile vinatakiwa kunadi sera za vyama vyao kwa ajili ya maendelo ya mwananchi wa kawaida; kwa maneno mengine ni fursa njema kueneza sera bora za Kujinadi kunajumuisha kutaja sifa zako na uwezo wako kwa nini utakuwa kiongozi bora kuliko mpinzani wako na hivyo unastahili kura zao


Kujinadi pia kunajumuisha kutaja mapungufu ya mpinzani wako kwa nini hana sifa ya kuwa kiongozi bora na hivyo hastahili kura yao.

Busara ya kawaida inatueleza kuwa watu wanahitaji taarifa za msingi kuhusiana na msimamo na sera za mgombea. Wanahitaji kampeni yenye taarifa nyingi za kuelewesha kwa kina masuala muhimu yanayogusa vipaumbele na kero zao.

Tatizo ni nini? Kwa nini kama taifa tunaendlea na kampeni chafu kila wakati?

Vyama vingi vya siasa vinafikiria kuwa siasa chafu matusi ni tiketi bora ya ushindi; vyame vingi vya siasa ushindani wao wanajipima kwa kupiga kampeni chafu badala ya kueneza sera na kuwaacha wananchi wapime.

Viongozi wengi wa vyama wanashindwa kujenga hoja za kweli kuhusu mapungufu ya chama kingine; wanakosa vielelezo vya hoja zao; namna gani atatekeleza ahadi za kumkwamua mwananchi wa kawaida na kivipi anaona  mapungufu ya kiutekelezaji na uwezo mdogo wa kiongozi anayeshindana naye?

kampeni nyingi zinazofanyika ni si za kupata viongozi bora bali bora viongozi.  Uthibitisho wa hoja hii kampeni hazizingatii maadili, na uadilifu wa kiongozi mtarajiwa maana yake mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi.


Je nini tumejifunza katika Mwelekeo wa kampeni Arumeru Mashariki?

Jambo la kwanza linalosikitisha kwa wengi walioshiriki kufanya kampeni ni  vyama ambavyo vinadadi wagombea wake ktutumia muda mwingi sio katika kunadi sera zenye tija kwa wananchi wa Arumeru bali vinatumia na kupoteza muda mwingi kuendeleza malumbano yasiyo na maana, na kwa msingi huu ni kumnyima haki ya msingi ya kujua na kutafakari sera ambazo angeweza kuziona pengine zitaweza kufaa katika kumsaidia kumletea maendeleo. Katika hilo kwa kweli tunahitaji viongozi ambao wangekuwa (great thinkers) kwa maendeleo ya wananchi sio viongozi ambao wanaweza kusimama kwenye jukwaa na kudadi maneno kama “kudadadeki”


Vyama vya siasa nchini vinashindwa kuelewa kuwa siasa sio ugomvi wala sio vita, siasa ni nguvu ya hoja; siasa ni mchezo wa masumbwi na unatakiwa ufuate sheria za mchezo na sio kucheza kinyume cha utaratibu. Na jambo moja kubwa katika siasa ni mchezo ambao unafanyika chini ya demokrasia. Kinachoendelea Arumeru mashariki sijui ni democrasia gani inatumika, iliyokosa maadali ya kunadi sera: 

Kampeni za matusi zinajenga misingi ya  vurugu na mwisho wa siku kura zitapigwa sio kwa kupima sera bali upenzi wa vyama kitu ambacho kama tutakuwa wakweli kinarudisha nyuma maisha bora kwa kila mtu: je hilo ndilo tunalolitamani liendelee katika nchi yetu?

Kisiasa, kampeni ni jitihada au mpangilio maalumu unaofanywa na chama au vyama kwa lengo la kushawishi mchakato wa utoaji maamuzi katika kundi fulani. Katika nchi zinazofuata mifumo ya kidemokrasia, kampeni za kisiasa mara nyingi humaanisha kampeni za uchaguzi.

Je ni chombo gani kinachosimamia maadili ya kampeni wakati wa chaguzi?

Je ni kweli kuwa chaguzi zetu zimetawaliwa na hujuma na chama chenye nguvu ndicho daima kinachoshinda?

Je ni kweli kuwa wakati wa chaguzi hakuna uwanja sawa wa kisiasa kutoka kwa vyombo vya kusimamia na kuratibu uchaguzi?
Ndipo tunapofika kwenye hoja ya msingi na kufikiria kuwa utawala wa sheria katika chaguzi ni dhaifu na:

Je vyombo hivyo havina meno binafsi na haviko huru vya kutosha?
Kwani tunasikia malalamiko daima kuwa chaguzi zinatawaliwa na rushwa na hujuma nyingine miongoni mwa vyama husika?
Je tume ya uchaguzi na msajili wa vyama wanawezaje kuimarisha demokrasia ya kweli katika kufanikisha kampeni huru na zenye tija kwa wananchi?

Tukururu inawajibikaje katika mazingira haya ina msaada wowote au inaangalia upepo unavyovuma?

WAJIBU WA MWANANCHI WA KAWAIDA KATIKA KIPINDI HIKI NI NINI?

Nafikiri kama nilivyowahi kuandika katika moja ya makala yangu wananchi wanahitaji sana elimu ya uraia, ili waweze  kuepuka hujuma na sera uchwara zinazotolewa na wanasiasa kwa faida zao binafsi nakuwa na uwezo wa  kuzidhibiti kampeni za matusi na sinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.


Elimu ya uraia itawasaidia kuwajengea wananchi uwezo wa maamuzi na kwa uwezo huu wananchi watakuwa na nguvu na kuwashikisha adabu wanasiasa uchwara wasio na hoja, ili vyama vinapokuja kwenye uchaguzi vijipange.  Ndio maana wakati mwingine naashiria kusema kuwa hata kinachoendelea bungeni wakati mwingine chimboko lake ni hili wanasiasa wetu wanakosa hoja za nguvu za kumkwamua mwananchi hawajipangi sawa sawa ni sawa na hoja zinazo kurupushwa kutoka usingizini. 

Je makapeni manager vya vyama wanakazi gani katika kuhakikisha kuwa wanadadi sera zinazotakiwa?

Katika kampeni nyingi nafikiri wamekuwa wakifanya kazi za uenezi zaidi na sio kuvisaidia vyama vyao katika ushindani wa hoja nzuri na nzito nz zenye mvuto wakati wote wa kampeni;

Kampeni manager ndio dira ya kutumainiwa katika chaguzi yeyote; ni viongozi ambao wanatakiwa watembee mbele zaidi kimawazo, kifikra na kimwelekeo; wao ndio marubani wa ushindi;

Katika nchi za wenzetu kutokana na ushindani wa hoja makapeni manager wanakuwa makini ukiaukwaji wa maadili, lugha za matusi automatically zitamwajibisha kichama na kuachia nafasi yake yenye heshima kubwa;


Tumeona katika chaguzi zetu nao hushindwa kuzuiaa na kuratibu mchakato mzuri unaofaa wa uelezaaji wa sera bora kwa jamii.
Kampeni yaweza kuwa ni kuwaelezea wananchi mambo utakayowafanyia na namna utakavyotekeleza. Hii ni pamoja na kueleza ilani yavyama vyao, vipaumbele vyao, huduma za afya na utakavyokomesha rushwa na maisha bora kwa mtanzania

Makapeni Manager wa vyama “Pengine” wanafikiria zaidi kuwa  kuzungumzia mabaya ya wenzao badala ya sera ndiyo kufanikisha mchakato mzuri na utakaowezewsha chama chao katika mbio za uchaguzi ambao unaoshindaniwa.   

KAMA TAIFA NINI KIFANYIKE KUEPUSHA HALI KAMA HII KUENDELEA KUJITOKEZA TENA NA TENA?

Kwa ujumla, suala hili la kampeni linahitaji msukumo mkubwa na labda mapinduzi fulani kwa sababu hivi sasa Watanzania hawamchagui kiongozi wala chama kwa sababu ya sera zake au uchapakazi wake bali wanafuata ushabiki tu. Kwa msingi huu wananchi watendelea kubariki na kushangilia matusi kwa vile tu yanakikashifu chama na watendaji wa chama tofauti hata kama hakutakuwa na tija yeyote katika maisha yao, kama Mheshimiwa waziri Mkuu mstaafu Jaji
Warioba alivyowahi sema kuwa “Siasa nyingine zinajenga chuki, siasa za kinafiki siwezi kuziunga mkono, tufikie wakati tutofautishe mambo binafsi na mambo ya umma,”
Kama taifa hakuna kisichowezekana katika kuleta mageuzi ya kweli ya kufanya kampeni za kiustaarabu, zenye maadili na zenye tija kwa Taifa tuwe  wazalendo wa kweli kukubali kuwa tunaweza kufanya kampeni ambazo hazitahusisha matusi, BALI KAMPENI ZILIZOJAA NGUVU YA HOJA NA USHINDANI WA KWELI KWA MAENDELEO YA TAIFA.

Maggid Mjengwa na Uchambuzi Wa Habari: JK, Shivji Na Wanahabari Wetu


Ndugu zangu,

Yamepita majuma kadhaa sasa bila kuwasilisha fikra zangu kupitia ’ Neno la Leo’, ’ Uchambuzi wa Habari’ au ’ Tafsiri Yangu’.



Kwa mwanadamu ni vema wakati mwingine kukaa chini; kusoma na kusikia ya wengine huku ukitafakari.



Katikati ya taarifa ya habari ya televisheni jana usiku nilianza kujiuliza; ” Hivi nchi hii hatuna televisheni nyingine ’ Ya Kitaifa zaidi’?” Mimi nilitarajia, kuwa katika siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo kule Arumeru tungeletewa habari moto moto kutoka huko, ikiwamo uchambuzi pia. Wapi?


Niliposikia kuwa ’ Sasa tunawaletea habari za Afrika Mashariki’ nili-tune BBC News!



Kwenye taarifa ile ya habari jana usiku nilimsikia Rais Jakaya Kikwete akizungumzia juu ya tasnia ya uandishi wa habari hapa nchini. Kati ya mambo mengine, JK aliweka wazi, kuwa ameambiwa kuwa waandishi wengi hawana ajira ya kudumu.
Kwamba wanafanya kazi kwa kupokea posho tu- These journalists can easily become mercenaries- anasema JK. Kwamba waandishi wa aina hii wanaweza kiurahisi kugeuka mamluki.


JK akaonyesha hofu yake ya kufa kwa taaluma hii. Naam, JK yuko sahihi. Na alipokuwa akiyatamka hayo kuna makofi yaliyokuwa yakipigwa, japo si ya ukumbi mzima. Kuna ambao waliguswa na ukweli huo, si tu wanahabari, bali wamiliki wa vyombo vya habari.



Na ukweli huo wa hali ya wanahabari wetu unafahamika. Lakini, kama taifa, tunafanya nini wakati “ Fourth Estate”- mhimili wa nne wa dola unaundwa na vibarua wapokea posho za siku wakati Wabunge wanakamata laki tatu na zaidi kama posho ya siku kukaa bungeni?



Huko nyuma nimepata kuanzisha mjadala wa umuhimu wa kuwepo kwa ruzuku kwa vyombo vya habari ili navyo viweze kupata nguvu ya kuendesha shughuli zao ikiwamo hata uwezo wa kuwasafirisha wanahabari wao kwenye matukio badala ya gharama hizo za usafiri kutegemea ‘ bahasha’ za wanasiasa na wamiliki wa makampuni ya biashara, ambao , masharti yasiyoandikwa ya wao kutoa bahasha zao, ni namna wanahabari hao watakavyoripoti habari za kuwapamba na zitakazowafurahisha watoa bahasha.

Vinginevyo, kwa mwandishi asiyejua kumpamba mtoa bahasha, na badala yake akamchafua, ana hatari ya kushushwa njiani, hata kama ni katikati ya pori la mbuga ya wanyama ya Mikumi. Maana yake? Akome ubishi!
Si tuliambiwa shuleni , kuwa ubepari ni unyama, ongeza sasa, na ufisadi pia.


Naam, wanahabari unganeni. Huu si wakati wa kulilia huruma za watawala ikiwamo wanasiasa. Huu ni wakati wa kupambana kudai ruzuku ya Serikali kwa vyombo vya habari. Ni ruzuku, pamoja na mauzo ( kama ni magazeti) na matangazo ndivyo vitakavyowafanya muwe huru. Vinginevyo, mtaendelea kuachana na jukumu la kuutumikia umma wa Tanzania na badala yake mtabaki kuwatumikia wanasiasa, wafanyabiashara na makampuni makubwa.

Yumkini, kwa mwanahabari kumtumikia kafiri yaweza kuwa na maana ya kuwaangamiza ndugu zake kwa mamilioni. Na kwa maana ya JK, mwanahabari wa aina hii atakuwa amegeuka mamluki-
mercenary.


Katika kitabu chake, " The Intellectuals At The Hill" ( Wasomi wa Mlimani); Profesa Issa Shivji alipata kuandika yafuatayo juu ya uandishi wa habari; " Uandishi wa habari huenda usifikiriwe kuwa ni taaluma adimu.
Na pengine usipewe kipaumbele katika kamati za mipango. Lakini bado, mwanahabari, kama mwasilisha wa taarifa, aweza pia akawa mwangamizaji katika jamii ya kidemokrasia. ( Au, waweza wakawa wasaidizi wa tawala za kidikteta kama wawasilishi wa taarifa potofu.)


Lakini katika nchi zetu demokrasia ni suala la kuhubiri zaidi kuliko vitendo wakati wanahabari si kitu chochote zaidi ya kuwa maofisa uhusiano kwa "kigogo" huyu au yule. Ni nadra kwa yeyote yule ( wakiwemo wanahabari wenyewe ) wenye kuchukulia kazi ya uanahabari kwa umakini, achilia mbali kwa uwajibikaji." Prof. Issa Shivji ( The Intellectuals at the hill, Uk 176) (Tafsiri hiyo ni yangu)



Na
kuna wakati Rais Yoweri Museveni alipata kuulizwa; " Mheshimiwa Rais unapoamka asubuhi unafanya nini kabla ya kwenda ofisini? Museveni alijibu;" Mimi huanza siku kwa kufungulia taarifa ya habari ya BBC London!".


Hata kama ni jibu la kusikitisha, lakini, namwelewa kabisa Yoweri Kaguta Museveni.