Mbowe asisitiza Ukawa bado wamoja, Lembeli, Bulaya wakaribishwa rasmi.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kililifunika jiji la Mwanza, baada ya kufanya mkutano mkubwa wa hadhara uliokusanya maelfu ya wakazi wa jiji hilo katika viwanja vya Magomeni.
Mkutano huo uliohudhuria na viongozi wote wa juu wa Chadema pamoja na waliokuwa wabunge wawili wa CCM, James Lembeli (Kahama) na Esther Bulaya (Viti Maalum) waliopokelewa rasmi baada ya kujitoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkutano huo ulikusanya wafuasi kutoka Mwanza na mikoa ya jirani ikiwamo Shinyanga (Kahama) na Mara (Bunda).
Kabla ya mkutano huo kuanza, wafuasi wa chama hicho walisimamisha kwa muda shughuli mbalimbali za wakazi wa jiji hilo baada ya kufunga barabara ya Makongoro kutoka uwanja wa ndege walikowapokea viongozi wao hadi katikati ya jiji.
Misururu ya waenda kwa miguu, pikipiki maarufu ‘bodaboda’ na magari yalisimamisha shughuli hizo kutokana na kuwapo katika msafara wa kuwapokea viongozi hao wa Chadema.
Wabunge hao waliohama CCM na kujiunga na Chadema waliokuwapo katika msafara huo hivyo kuongeza mbwembwe za wafuasi hao.
Hata hivyo, polisi wa usalama barabarani walijipanga vyema na kuhakikisha usalama unakuwapo kwa waenda kwa miguu na watumiaji wengine wa vyombo vya moto.
MBOWE
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wamefanya mkutano huo kwa lengo la kuwafahamisha wanachama na wapenzi wa chama hicho kuhusu siku atakayotangazwa mgombea atakayesimamishwa kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tunawashukuru wakazi wa Mwanza kwani mmeonyesha jinsi mnavyotaka mabadiliko katika nchi hii, mmeteseka sana…tumenyimwa uwanja wa CCM Kirumba uliojengwa na Watanzania hadi tunatumia uwanja huu ambao umesababisha watu kuzimia kutokana na wingi wa watu,” alisema Mbowe.
Mbowe pia katika mkutano huo aliwatambulisha Lembeli na Bulaya pamoja na kuwakabidhi kadi za Chadema na wao kuzikabidhi zile za CCM walizokuwa nazo.
Mbowe pia aliwaeleza wananchi na wanachama wa Chadema kuwa Ukawa bado wamoja.
Hata hivyo, alisema baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo wa CUF, NCCR-Mageuzi na NLD hawakuwapo kwenye mkutano huo kwa kuwa walikuwa wakiendelea na shughuli mbalimbali za vyama vyao.
Alisema CUF watakutana Julai 25 kuamua suala hilo na kuwa NCCR-Mageuzi na NLD nao watakutana wakati wowote na baada ya hapo vyama vyote vitakutana kutoa maamuzi juu ya mgombea watakaye msimamisha kugombea urais.
LEMBELI
Akizungumza kwenye mkutano huo baada ya kutambulishwa, Lembeli alisema:
“Lazima sasa safari tuliyoitegemea itafanikiwa kwa wapinzani kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, nimewachukia kwa muda mrefu mafisadi na wezi ndani ya CCM, leo hii nimeamua kutangaza rasmi kuachana nao,” alisema Lembeli na kuongeza:
“Kabla sijajiunga Chadema Jumapili iliyopita nilisali sana na familia yangu ili njiachane na chama cha umasikini katika nchi na kwenda chama chenye neema, siku iliyoifuata nikaamua kutangaza kujiunga nanyi,” alisema Lembeli.
BULAYA
Alisema atashirikiana na viongozi wa Chadema mkoa wa Mara kuhakikisha anachukua Jimbo la Bunda Mjini na kumtoa Stephen Wasira ambaye amekaa madarakani kwa vipindi vyote vya marais wa nchi hii,” alisema Bulaya.
PROF. SAFARI
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, alisema chama hicho kimejipanga kukabiliana na nguvu ya mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, muda wa kampeni utakapowadia.
Alisema Chadema wana ‘silaha’ za kumwangamiza mgombea huyo wa CCM, kutokana na kufahamu mambo mengi aliyonayo ya kifisadi ndani ya chama chake.
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alisema chama hicho kimejipanga kuwashitaki wagombea wake watakaotangaza kujitoa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa kuhongwa na wapinzani wao.
“Mtu akichukua fomu, atasainishwa fomu maalum mbele ya mwanasheria kisha akijitoa tu kwa kuhongwa, ataipata kwani sheria itasema naye,” alisema Dk. Slaa.
JOHN MNYIKA
John Mnyika Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, alisema chama hicho kinawakaribisha wabunge hao wapya pamoja na wengine wenye nia nzuri na maendeleo ya nchi yao.
“Tumekubaliana kwa pamoja kuchukua utawala wa nchi hii ili kuwakomboa Watanzania wanaoteseka na maisha magumu yaliyosababishwa na utawala wa CCM,” alisema Mnyika.
SALUM MWALIMU
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema:
“Chadema tumebalisha staili ili kukabiliana na ‘goli la mkono’ la CCM…kwani Wazanzibar wanaunga mkono umoja wetu wa Ukawa kutokana na wao kuhitaji muundo wa serikali tatu.”
HALIMA MDEE
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, alisema ‘goli la mkono’ lililosemwa na CCM litafungwa na Chadema badala ya wao.
“Hilo goli tutalifunga sisi, kwani hawa wabunge wawili tuliowakaribisha tayari wameingia katika ufalme wa Watanzania waliochoka maisha ya chama tawala,” alisema Mdee.
ARCODO NTAGAZWA
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Arcardo Ntagazwa, alisema Chadema siku zote inaanza na Mungu na kumaliza na Mungu, hivyo wana uhakika wa kuchukua Ikulu mwaka huu.
LISSU
Mwanasheria wa Chadema na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema hawana shaka na mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli, kwani tayari wamemuandalia ‘silaha’ ambazo zinaweza kummaliza katika kampeni muda ukifika.
CHANZO: NIPASHE