WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, August 30, 2012

VIONGOZI WAJADILI NAMNA YA KUKABILI TATIZO LA AJALI ZA BARABARANI NCHINI


  • JIBU NI MOJA TU WANAWEZA KUSIMAMIA SHERIA IPASAVYO?

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uthibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(SUMATRA),akifafanua jambo katika mkutano wa kujadili namna bora ya kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani,Kulia kwa Mkurugenzi wa SUMATRA ni Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira Wizara ya Uchukuzi,Bi. Tumpe Mwaijande.Kulia kwa Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe.Pereira Ame
Silima (aliyevaa suti nyeusi)ni Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe na kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe. Dkt. Emmanuel J. Nchimbi(Mb).
 Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi,Said Mwema akichangia jambo katika Mkutano uliowakutanisha Waziri wa Uchukuzi,Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe(Mb) aliyevaa suti nyeusi,na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe. Dkt. Emmanuel J. Nchimbi(Mb) aliyevaa suti ya kaki.Mkutano huo ulifanyika Wizara ya Uchukuzi na kuwakutanisha SUMATRA,Jeshi la Polisi,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji(NIT), Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na viongozi mbali mbali wa Wizara ya Uchukuzi lengo likiwa kujadili namna ya kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani Nchini.
Waziri wa Uchukuzi,Mhe Dkt. Harrison G.Mwakyembe(Mb),akisisitiza jambo kwenye mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.Kulia kwa Waziri Mwakyembe (aliyevaa suti ya kaki) ni Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe. Dkt. Emmanuel J.Nchimbi(Mb),kulia kwa Waziri Nchimbi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Bw. Mbarak Abdulwakil  na kulia kwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani ni Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Said Mwema.

habari kwa Hisani ya Michuzi Blog

Sunday, August 26, 2012

UMUHIMU WA SENSA KWA TAIFA


HOTUBA YA MHESHIMIWA DK JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI KUHAMASISHA SENSA YA WATU NA MAKAZI, TAREHE 25 AG


Ndugu wananchi;
Imekuwa ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi. Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.
Ndugu wananchi;
Katika historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.
Ndugu wananchi;
Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka 2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.
Ndugu wananchi;
Shughuli yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida. Lakini, tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kuwepo. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya jitihada za makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini. Wamekuwa wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo baadhi yake hazina uhusiano wo wote na Sensa. Zipo sababu nyingine ambazo hata haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa hawatashiriki Sensa mpaka mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule Berlin, Ujerumani atakaporudishwa. Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa nchini zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita. Mwaka 1906 wana sayansi wa Kijerumani waliyagundua mabaki hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na kuyapeleka Ujerumani ambako yamehifadhiwa tangu wakati huo.
Ndugu Wananchi;
Kudai mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa kale waliokuwepo wakati huo wanafananaje. Huenda pia kikawa kivutio cha utalii. Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi. Watu wakisusia Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali hata watu wengine nchini na duniani watawashangaa. Lakini, jambo ambalo ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani? Mjerumani au wanajisusia wenyewe? Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata akirejeshwa huna manufaa ya moja kwa moja? Hasara anapata nani sisi au wao? Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza maneno yahusuyo Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa mambo yenye maslahi makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu. Tuachane nao hawatutakii mema na wala hawaitakii mema nchi yetu. Nawaomba tusitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni.
Ndugu Wananchi;
Wapo ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika orodha ya maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu. Wahusika wakuu hasa ni baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu wasikubali kuhesabiwa. Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi Waislamu wawaunge mkono katika msimamo wao huo. Nimesoma baadhi ya nyaraka na vipeperushi vyao kuhusu madai hayo. Nilipata pia bahati ya kukutana na kuzungumza na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati hizo. Nia yangu katika kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani hoja na madai yao. Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki, Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania.
Hawazikubali taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji wa takwimu hizo. Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya kuwa ni asilimia fulani Watanzania. Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu. Kwa maoni yao, taarifa hizo si za kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu wanazozijua watoaji wa taarifa hizo. Ili kuondoa upotoshaji huo, wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika hayo. Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya watu hutolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha Serikali. Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na wala siyo chanzo cha takwimu zilizotolewa na mashirika hayo. Walikozipata wanajua wenyewe. Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na ndiyo maana zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na wakipenda watoe tamko la kuzikataa.
Ndugu Wananchi;
Niliwaambia pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni kuionea na kutoitendea haki. Vile vile kuibebesha dhima ya kuongeza swali la dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili. Napenda, kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna hiyo kutambua unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea mifarakano isiyokuwa ya lazima kama ilivyo sasa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya kuliingiza swali la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na kiutekelezaji. Wakati wa ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu yaliulizwa katika Sensa. Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika Sensa ya kwanza ya mwaka 1967 kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya kikoloni. Baada ya hapo ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza maswali hayo kwani nia ya wakoloni kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale. Walitoa huduma kwa ubaguzi, sera ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na Mapinduzi. Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, bali kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sera hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa letu na watu wake. Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni wengi na hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa, sera mpya inawataka watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Nionavyo mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima kubwa. Tuendelee kuidumisha na kuienzi. Kufanya vinginevyo, na hasa kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu ni kuliingiza taifa letu ambalo lina sifa ya amani, upendo na utulivu, katika migogoro isiyokuwa ya lazima. Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na kudumisha sera yetu hii nzuri na sahihi.
Ndugu Wananchi;
Sababu ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji. Imechukua miaka kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Isitoshe Sensa ya majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali yaliyopo na marekebisho kufanywa baada ya hapo. Kuingiza mambo au jambo jipya sasa itakuwa viguku kiutekelezaji. Kutachelewesha zoezi zima na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Kwa vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo cha kutoa huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu wanaokereketwa na jambo hili waache kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze kuhesabiwa. Tujitokeze kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Sioni ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo na Waislamu. Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi Kuu ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo. Hata ukiamua uiite Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana sababu. Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa msingi wa dini kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na Waislamu. Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.
Ndugu Wananchi;
Katika maelezo yao kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Said na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa walinieleza kwamba kwa kawaida katikati ya Sensa moja na nyingine, hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani Demographic Survey. Huu ni utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya kaya ambapo taarifa za mambo mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa hukusanywa. Mara ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973, yaani baada ya Sensa ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978. Ni makusudio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016 ambapo baadhi ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa. Subira yavuta heri.
Ndugu Wananchi;
Nimehakikishiwa na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri na zoezi liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012. Lakini, mafanikio ya zoezi lenyewe yatategemea sana ushiriki wa watu ambao ndiyo walengwa na wadau wengine. Naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa kisiasa na kiutendaji wa ngazi mbalimbali waendelee kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika maeneo yao ya uongozi. Hawana budi kuhakikisha kuwa zoezi linakuwa na mafanikio makubwa. Wale wote wanaofanya vitendo vya kuvuruga zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
Nawaomba viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na kushirikiana na Makarani wa Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao. Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi wasijitokeze kuhesabiwa. Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema nchi yetu.
Ndugu wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi wa kisiasa, kusimamia na kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Sensa katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Shehia kwa kazi nzuri ya matayarisho na uendeshaji wa Sensa ya mwaka 2012. Nawatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu na adhimu kwa nchi yetu na watu wake.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu hawa kwa kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza kwetu ndiyo ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Ewe Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa kwa maendeleo yako na ya taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa kunisikiliza


Neno La Leo: Nilishaamua, Nitabaki Kuwa Mjamaa...







Ndugu zangu,

Kwa siku mbili mfululizo nilikuwa kijijini Mahango, Kata ya Madibira, Mbarali, Mbeya. Huko niliongozana na wageni kutoka Uingereza waliokwenda kushiriki kazi ya ujenzi wa Maktaba ya Kijamii kijijini Mahango.
Uzoefu nilioupata kijijini Mahango ni elimu yenye gharama kubwa. Hakika nimejifunza mambo mengi. Kijijini Mahango niliuona kwa karibu sana umasikini wa watu wetu. Kwa mfano, kwenye moja ya kitongoji nilimshuhudia mama anayelindia maji kwenye kisima chenye chemchemi yenye kutoa maji ya kujaa bakuli moja kila baada ya robo saa.

Mama yule kwa kauli yake alitamka huku akiwa ameshika tama; ” Hali yetu ni mbaya sana, hapa ndoo moja kujaa inaweza kunichukua saa moja na nusu”. Wakati akitamka hayo nilimwona binti wa mama huyo asiyezidi miaka kumi akiwa amesimama akimwangalia mama yake. Niliziona pia ndoo zilizopanga foleni bila wenye nazo. Bila shaka wamekwenda kujihifadhi na jua kali la mchana, na kufanya kazi nyingine pia.

Hali kama hiyo niliikuta pia kijijini Mapogolo. Kwenye ofisi ya Mtendaji Kata ya Miyombweni kilipo kijiji cha Mapogolo nilifanya mazungumzo na Diwani wa Kata Bw. Lokelo pamoja na  Mtendaji wa Kata Bw. Filipo. Nao  wakawa wamekunja mikono wasijue la kufanya, maana, bajeti ya Halmashauri ya kushughulikia na tatizo la maji haitoi matumaini ya kutatua tatizo la wananchi katika muda mfupi ujao. Fedha hazitoshi.

Kwenye Mkutano wa hadhara kijijini Mahango, Mwenyekiti wa Kijiji  alinipa nafasi adimu ya kuzungumza machache na wananchi. Nilisimama na kuwaangalia wananchi wale walioonyesha kwenye nyuso zao, kiu ya kutaka kunisikiliza; niliwaangalia akina mama na watoto migongoni, niliwaangalia watoto wale waliokaa mbele yangu. Niliwaangalia akina baba na vijana. Kwa jinsi watu walivyoitikia wito wa kukusanyika kushiriki kazi ya ujenzi wa Maktaba, kushiriki jambo la elimu, basi, nami niliyaona matumaini kwenye kusanyiko lile.

Mahango Oyee!”
Nilitamka na nikaitikiwa kwa sauti kubwa. Haraka nikaamua niongelee umuhimu wa Ujamaa na Kujitegemea; kufanya kazi kwa ushirikiano. Nikaanza hotuba yangu fupi kwa kumnukuu Mwanafalsafa David Hume kwa maneno yake haya;

“MBEGU yako imekomaa leo, yangu itakomaa kesho. Ni jambo la manufaa kwetu sote kama  nitalima pamoja nawe leo, na wewe unisaidie kulima kesho. Siwezi kuwa na urafiki nawe kama naona kuwa hujengi urafiki nami. Msimu utapita, nasi tusipoaminiana na kushirikiana, basi, sote tutakula hasara.”  (Mwanafalsafa David Hume)

Nikasisitiza pia umuhimu wa kuzingatia ‘K’ tatu ili kufanikiwa katika tuyafanyayo; Kujitambua, Kujiamini na Kuthubutu.  Pale Mahango nikasisitiza pia umuhimu wa kuitanguliza Tanzania kwanza katika yote tuyafanyayo. Tusiendekeze sana tofauti zetu za kisiasa. Tuwajue maadui tunaopambana nao, tuyajue malengo yetu kwenye vita iliyo mbele yetu. Tukubaliane kupambana kwa pamoja kwa maana ya kufanya kazi kwa pamoja ili kuyafikia malengo yetu.

Maana, hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hatima yetu kama watu binafsi, kama vikundi vya watu na kama taifa, inatutegemea sisi wenyewe. Umasikini wa watu wetu ni umasikini wetu.
Naam, sijawahi kuficha imani yangu ya kisiasa, kwa maana ya itikadi yangu.  Na imani yangu inaimarika zaidi kadri ninavyozidi kutembelea na kukutana na watu wa vijijini.

 Kiitikadi mimi ni Mjamaa ninayeamini katika uwepo wa demokrasia na kutanguliza maslahi ya walio wengi katika jamii-   I am a  Social Democrat.  Na bado naamini kuwa hata sasa, mfumo  wa enzi za Mwalimu wa Ujamaa na Kujitegemea bado una nafasi katika jamii yetu.  Misingi ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni muhimili wa maendeleo ya nchi na watu wake. Ni udhaifu na kutokujiamini kwa kuionea haya misingi iliyoijenga jamii yetu na ambayo bado ina nafasi ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi kama itaimarishwa.

Maana, mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea uliofanyiwa mabadiliko ya kimsingi unaweza kutuhakikishia ulinzi wa maslahi ya nchi yetu. Ni kwa sera zenye kuhakikisha usawa wa watu. Sera zitakazohakikisha kodi inakusanywa na kutumika katika yaliyo muhimu na yenye kumsaidia pia mwananchi wa chini katika nchi yetu. Mwananchi aweze kupata elimu bora na huduma bora za afya, maji, miundo mbinu  kati ya mengineyo ya msingi.

Tuazimie sasa kuwajibika kwa pamoja kwa maslahi ya nchi yetu. Na tukifanya ajizi, tutaigeuza nchi yetu kuwa ‘ nyumba ya njaa’.  
Naam, Nilishaamua nitabaki  kuwa Mjamaa.
Na hilo ndilo Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

Saturday, August 25, 2012

Neno La Leo: Tunaposubiri Kuhesabiwa Na Dhana Ya Kiumbe Mzito



Ndugu zangu,

Kwa siku kadhaa nimekuwa nje ya mitandao. Hata magazeti, redio na televisheni zimenipitia kando. Jioni hii wakati nikipitia taarifa mbalimbali nimekutana na hili la hoja ya baadhi ya Waislamu kutaka sensa ya watu na makazi  itakayofanyika kesho Jumapili igomewe kwa vile haina kipengele ama dodoso linalotaka kujua dini ya mtu.

Kabla sijatoa maoni yangu juu ya hilo ningependa niitafsiri dhana ya ‘ Kiumbe mzito’ kama tulivyoambiwa na wahenga wetu. Huenda si wengi kati yenu wasomaji wenye kufahamu maana hasa ya usemi wa Wahenga kuwa  ‘ Kiumbe mzito’.

Ndio, Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu kwa usawa kwenye mambo mengi. Wala hakutaka kubagua; ona unyayo wa mwanadamu. U sawa, iwe kwa tajiri au masikini. Wewe na miye tumepata, ama wenyewe au  kusikia mtu akilalamika kuwa soli ya kiatu chake imechakaa, kwamba anakwenda kwa fundi viatu kubadilisha soli. Lakini, wewe au miye hatujapata kumsikia mwanadamu mwenzetu akilalamika kuwa unyayo wake umechakaa, anataka kwenda kwa fundi awekewe unyayo mwingine!

Ndio, wewe na miye ama tumeshuhudia au kusikia kuwa upepo umeangusha mti, nyumba, ghorofa, gari na hata meli. Lakini, jiulize, je, umepata kumwona mwanadamu mwenzako anayetembea kwa miguu akiangushwa kwa upepo?

Binafsi hilo la mwanadamu kuangushwa na upepo sijapata kulisikia au kuliona kwa macho yangu. Mwanadamu hata awe mwembamba kiasi gani, haiyumkini akaangushwa kwa upepo. Na ukimwona mwanadamu mwenzako anaanguka barabarani, basi, ama ni mgonjwa, au ni mlevi. Na hilo la mwisho haliwezi kuwa na maana ya mwanadamu huyo kaangushwa na upepo, bali kaangushwa na  pombe alizokunywa.

Naam, kiumbe mzito.
Na kesho ndio siku yenyewe ya Watanzania kuhesabiwa. Kuna wenzetu hususan kwenye  Uislamu wenye kudai kuwa watagoma kuhesabiwa; Kisa? Hakuna dodoso lenye kutaka kujua dini ya mtu. Mimi naamini walioamua suala la dini ya Mtanzania lisiingizwe kwenye sensa walifanya uamuzi wa busara na wenye hekima sana.

Sisi ni Watanzania. Ni watu wamoja kwa asili. Na tujiulize kwanza; kwa nini tunahitaji kujihesabu. Ndio, sensa ina maana ya kujua idadi yetu kama Watanzania ili iisaidie Serikali katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi yetu. Mipango ya maendeleo ya nchi haibagui dini ya Mwananchi. Kama ni huduma ya maji, basi, maji hayo watakunywa Watanzania; wawe Waislamu, Wakristo, Wahindu au Wapagani. Hivyo hivyo kwa huduma nyingine muhimu za kijamii.

Bila shaka, Sensa ya watu na makazi ni mpango madhubuti wa Serikali kwa maendeleo ya watu wake na wenye kugharimu mabilioni ya shilingi. Si busara na hekima kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini kushiriki kuhujumu mpango huu wa Serikali kwa manufaa ya wananchi wakiwamo waumini wa dini mbali mbali na hata wasio waumini. Na kubwa zaidi hapa ni ukweli huu; kuwa nchi yetu haina dini.

Naam, kiumbe mzito, hata kama Sensa ingeingiza kipengele cha dini, basi, wangetokea wachache wa kuhoji; iweje leo watu wakaulizwa dini zao, ama ni njama za kutaka kuwabagua na kuwakandamiza zaidi kimaendeleo Watanzania wa dini fulani au ni mbinu ya kutaka kudhibiti kuongezeka kwa idadi ya waumini wa dini fulani. Ndio, kuna ambao wangepambana kutaka kipengele cha dini kiondolewe na hata kutishia kugomea sensa.

Naam, kiumbe mzito, na mgumu pia!

Shime Watanzania na hususan ndugu zangu Waislamu, kesho ikifika na tuwe tayari kuhesabiwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa maendeleo yetu.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

Sunday, August 19, 2012

TUNAWATAKIA WATANZANIA WOTE SHEREHE NJEMA YA EID


SALA YA EID KITAIFA ZANZIBAR 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, akijumuika na Waislamu, wananchi  na VCiongozi mbali mbali katika Sala ya Iddi El Fitr iliyosaliwa  Kitaifa katika Msikiti wa Mwembeshauri Mjini Zanzibar leo. Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais, Seif Sharif Hamad
       Waumini wakiwa kwenye Sala hiyo ya Eid mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,  akisalimiana na watoto wa Kiislamu walioshiriki katika Sala ya Iddi el Firti iliyowajumuisha waislamu kutoka mitaa mbali mbali katika Mji wa Zanzibar,na kusaliwa Kitaifa katika Msikiti wa Mwembeshauri Mjini Zanzibar leo. 

                        Picha na Ramadhan Othman IKulu.

Friday, August 17, 2012

YALIYOJILI OLIMPIKI 2012 TANZANIA TUMEVUNA TULICHOPANDA:



  • USHINDANI WA MICHEZO SIO SIASA NI UBUNIFU WA MAZOEZI NA KUJITUMA KWA WANAMICHEZO;


  • JE VIONGOZI NA WANAMICHEZO WANATUMIA KODI ZA WALALA HOI KWA AJILI YA KWENDA KUTEMBEA NA KUWASHANGILIA WENGINE?


  • KWA NINI NCHI NYINGINE ZA AFRIKA MASHARIKI ZIMEFANIKIWA NA SISI TUNAENDELEA KUBURUZA MKIA?


  • TUKIBADILISHA MSIMAMO NA MAWAZO FINYU OLIMPIKI YA 2016 TUNAWEZA KUSHINDA MEDALI NYINGI.


Rais wetu wa awamu ya Pili mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliwahi sema kuwa “Tanzania kwenye michezo ni sawa na kichwa cha mwendawazimu” kwa tafsiri rahisi ni kuwa Tanzania kwenye michezo ni  Ni aibu sana. Sawli ninaloendelea kujiuliza ni tatizo la viongozi, ubunifu wao umejaa kutu, au ni tatizo la serikali kuto kutoa kipau mbele kwenye michezo, au ni tatizo la wanamichezo wetu kutuzingatia maelekezo ya walimu wao na hali ngumu ya maisha yanayowazunguka?

Kama ni tatizo la viongozi kwa nini viongozi hao wasiachwe, na kama taifa  tuanze upya, kama mwana zuoni mmoja alivyosema “hakuna haja kuendelea kuwa wataliii na kutumbua pesa ya walalahoi kama posho ambazo wanazitumia wanashiriki masindano husika”


Tatizo la uozo na aibu ya kushindwa katika michezo ya kimataifa limedumu kwa muda mrefu sana kama mwandishi mmoja alivyowahi andika kuwa “Tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi leo Tanzania ikiwa awamu ya nne, ni medali mbili tu za fedha”.

Lazima tukubali kuwa tupende tusipende  kama Thadeo alivyowahi sema kuwa “mwenendo wa michezo nchini siyo mzuri sana, kwani bado hatujafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, mwenendo sio mzuri kwa sasa, "

Je kushindwa kwetu kunachangiwa vile vile na ubinafsi wa viongozi wa michezo ambao wanafikiria zaidi faida binafsi na sio faida kwa taifa?

Tathimini ya mashindano ya olimpiki:

Michuano ya olimpiki ni michuano mikubwa kuliko yote duniani pamoja na kwamba ni mashindano yanayofanyika kila baada ya miaka minne, yakitoa nafasi kubwa kwa wadau kujiandaa,tumekuwa tukishikwa na kigugumizi kila mwaka kwani maandalizi yetu yamekuwa daima ni ya kuchechemea tu; Je, nini kinatukwaza? Yawezekana ni ukosefu wa mipango na kujituma katika kuitekeleza, tukiachia tu kila mmoja kwenye nyanja yake aoneshe nguvu zake. Je, katika wingi wa vipaji vilivyosambaa kote mikoani Bara na Visiwani, wanakosekana wanamichezo 100 wa kufuzu?


Uzuri wa Tanzania ni kwamba inavyo vitu vyote vya msingi kwa ajili ya maendeleo katika nyanja zote, michezo ikiwamo. Wapo watu waelewa wanaoweza kutoa uongozi mzuri na wamebarikiwa kwa rasilimali nyingi. Ili yote haya yafanikishwe lazima kuwe na dira ambayo inaweza tu kuwekwa Watanzania wakiwa na ndoto moja itakayowaongoza mwelekeo mmoja.

Mwandishi mmoja aliwahi sema kuwa Katika vijiji vingi Tanzania kuna vipaji vya ajabu kwenye michezo karibu yote 25 ya Olimpiki. Ni jinsi tu ya kuvikuza na kufungua fikra za wachezaji na kuwaingiza kwenye hali ya kisasa ya sayansi kiutandawazi. Katika Olimpiki hakuna michezo ya kutoka sayari nyingine, ni michezo ya kawaida tu – kuogelea, kulenga shahaba, soka ya wanawake na wanaume, tenisi, vishale, mpira wa pete, kikapu…yote inachezeka.
Mwanazuoni mmoja aliuliza kuwa ni katika msingi huo, naona kwamba kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kuiletea Tanzania medali za fedha kutoka Olimpiki, si tiketi ya wawili hao kuwa viongozi wa michezo. Medali za Olimpiki zitabaki ndoto ikiwa Tanzania haitasafisha nyumba yake – kwa wadau kuondoa woga, ubinafsi na kuacha kula vilivyotengwa kwa ajili ya watoto wa Olimpiki. Hakuna tena muda wa kupoteza, hivyo basi, ujenzi wa ndoto hiyo uanze sasa.

Anasema matayarisho mabovu ya wanariadha na ukosefu wa uongozi kutoka kwa mameneja katika mashirika ya michezo ndio sababu kubwa ya utendaji wa Tanzania wa kuvunja moyo katika michezo ya Olimpiki mwaka huu.

Anasema serikali ingechukua uongozi kutoka mashirika ya michezo, hata kama ni kwa muda, kama ilivyofanya kwa timu ya taifa ya mpira tangu mwaka 2007.

Maro alisema “mashirika ya michezo pia yanahitaji kupewa mafunzo ili kuwa na stadi zinazofaa za uendeshaji. "Uwezo wa viongozi wa mashirika ya michezo ni mdogo sana, aliiambia Sabahi. Wanaweza wakaweka rekodi za riadha na masumbwi, lakini hii haitoshi. Lazima wawe na uwezo wa kuandika mapendekezo ya gharama na kupanga michezo, badala ya kungojea serikali."

Kocha wa Riadha, Samwel Tupa analaumu maandalizi mabovu. Kwani hatukujua miaka minne iliyopita kuwa kuna Olimpiki mwaka huu? Umefika wakati wa kuingizwa watu wenye fikra mpya kwenye Kamati yetu ya Olimpiki. Haiwezekani, kwa ' Taifa Kubwa' kama letu kushindwa hata kufika fainali ya mchezo wowote kwenye Olimpiki. 


Kama mwariri wa gazeti la Tanzania Daima alivyowahi sema kuwa “ tukiwa miongoni mwa wadau wa maendeleo ya michezo nchini, tunasikitishwa na matokeo ya aibu kwa nchi yetu kwani tumeshindwa hata na nchi kama Libya na nyinginezo za Afrika ambazo muda mwingi, zimekuwa kwenye migogoro ya kisiasa.

Ni wakati sasa kwa serikali yetu kujifunza kutokana na makosa haya, kwani wakati nchi nyingi duniani zikiwekeza kwenye sekta ya michezo kwa vitendo, sisi viongozi wetu wamekuwa wakifanya hivyo kinadharia zaidi, hivyo kushindwa kung’ara kimataifa.

Wahenga walisema ‘kuvunjika kwa koleo, sio mwisho wa uhunzi’, hivyo kushindwa huku kuwe somo na chachu ya kujipanga zaidi kwa ajili ya mashindano mengine ya kimataifa, zikiwemo fainali zijazo za Olimpiki zitakazofanyika mwaka 2016.

Kwa kutumia mbinu, mikakati na mipango kama iliyotumiwa na mataifa jirani ya Kenya, Uganda, Ethiopia na Afrika Kusini yaliyopata medali huko London, kupitia wadau tutaweza kujiweka sehemu sahihi kimaandalizi kutung’arisha siku za usoni.


Serikali kupitia wizara husika, viongozi wa vyama vya michezo, wanamichezo, wadau na mashabiki kwa ujumla, kila mmoja achukulie matokeo ya kufanya kwetu vibaya kwa uchungu na kuamsha harakati mpya za kupata mafanikio siku zijazo. Tunaamini, hiyo ndio njia pekee itakayowezesha kufufua morali iliyokufa miongoni mwetu kufuatia matokeo hasi waliyopata wawakilishi wetu.”

Nakubaliana kabisa na mawazo ya mhariri wa Tanzania Daima kwa maoni yake mazuri lakini lazima tukubali kuwa “ kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi” lakini hii koleo yetu nafikiri imevunjika kiasi kwamba hatuwezi kuitengezeza kiurahisi. Kama taifa hivi sasa tunahitaji kusafisha wahunzi wa koleo yetu ya michezo wanaongoza kwa sasa. Nafikiri tunao masonara wazuri tu ambao hawajepatiwa nafasi ya kuonyesha ujuzi wao; lazima tukubali kuwa sasa ni wakati wa kusafisha nyumba yetu hebu tuanze na hii nyumba inayoitwa “TOC”;

Serikali inatakiwa kuandaa sera nzuri ya michezo 2016 olimpiki vison tukifanya hivyo nina imani kabisa kuwa tutaweza kuwa na timu nzuri ambayo itatuletea ushindi na medali mpaka ya dhahabu; tukiamua na tukianza kujisafisha na kugundua udhaifu wetu tutafanya vizuri zaidi ya Kenya, Uganda na Ethiopia.


Na nina imani kubwa kuwa waandishi wa michezo wananafasi kubwa ya kutelimisha na kutuonyesha mapungufu kama taifa katika swala nzima la michezo;  mabadiliko yeyote yale yatapatikana kama waatalamu wataweza kutufichulia udhaifu wa viongozi wanaohusika, wanamichezo wenyewe na Taifa kwa ujumla;

LAZIMA TUKUBALI KUKOSOLEWA KWA MANUFAA YA HESHIMA YA KIZAZI KIJACHO.

Monday, August 13, 2012

TAFSIRI YA KUJIUZURU KATIKA UTENDAJI WA SERIKALI ZETU:


JE KUJIUZULU KWA WATENDAJI WETU WA NGAZI ZA JUU NI SOLUHISHO LA TATIZO?





CHANGAMOTO KWA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA M. KIKWETE NA DR.ALI MOHAMED SHEIN;

Taafsiri ya kujiuzulu  kwa maneno ya kawaida  ni kuacha (Dhamana) ya utendaji ambayo kiongozi ambaye amepata shinikizo la Kujiuzuru analazimika kuachia madaraka ikiwa ni sehemu ya  uwajibika wa pamoja kiserikali kutokana kushindwa kutekeleza majukumu ambayo kiongozi muhusika alitakiwa kuyatenda au kuyasimamia kulingana na kiapo chake cha kazi.

Katika nchi ambazo zimeendelea kiuchumi na kisiasa dhana hii ni jambo la kawaida na hutekelezwa bila shinikizo kubwa sana. Kinyume chake Katika  nchi nyingi za zinazoendelea  Tanzania ikiwamo tunajua utekelezaji wa dhana hii huwa mgumu sana na ukitendeka inakuwa baada ya shinikiza kubwa wakati mwingine kutoka kwa wananchi hii inatokana sana na kulindana kisiasa.

mheshimiwa edward lowasa alilazimika kujiuzuru

JE KUKIMBILIA KUJIUZURU NI SOLUHISHO LA TATIZO?

Kwa nchi yetu Tanzania Pengine kama wanazuoni wengi walivyowahi sema kuwa "Kukimbilia kujiuzulu siyo suluhu sana ya tatizo. Kwasababu kama ni hivyo, watu wanaweza kuharibu mambo kwa makusudi wakitegemea watajiuzulu na kukaa pembeni." Kwani dhana hii ya kujiudhulu haihusishi adhamu ya ya moja kwa moja kama ya kushitakiwa kwa utendaji huo mbovu uliobainishwa. Tatizo langu daima ubaki kuwa je tunapomshinikiza kiongozi kujiudhru tunakuwa tayari tumeshabaanisha tatizo, na hata akichaguliwa kiongozi mwingine kushika nafasi anajua anatakiwa kufanya nini? Je tatizo ni mtu au ni mfumo? Kama ni mtu basi ni sahihi kumshinikiza kiongozi mwenye dhamana kuachia ngazi; lakini kam tatizo ni mfumo wa utawala nina mashaka kama kweli kujizuru kunasaidia kuondoa tatizo linalopigiwa kelele kwa wakati husika.

Tatizo linalokabila taifa letu kwa sasa mfumo wetu wa utawala umevamiwa na ufisadi. Swali la kujiuliza ni moja tu je huu ufisadi ni utamaduni wetu? au ni ugonjwa tu umeingia ambao unatakiwa kutibiwa mara moja kwa njia ambazo wengi wamezisema na wengine kuzitumia ? tupende au tusipende inaonekana ni mfupa uliotushinda Jibu lipo wazi tunajua tatizo lakini hatujui chanzo cha tatizo

MHESHIMIWA DR.IBRAHIM MSABAA ALILAZIMIKA KUJIUZURU;

Mheshimiwa Mtei aliwahi sema kuwa “Nilifanya kazi Mwalimu Nyerere, alikuwa kiongozi ambaye hasiti kuwachukulia hatua viongozi waliokuwa wakimwangusha katika utendaji wake,” nafikiri itakuwa ni vyema kwa viongozi wetu wa ngazi za juu kama wataweza kuwachukulia hatua za uwajibikaji za haraka sana watendaji wote wabovu wanao haribu mfumo mzuri wa utawala, na hatimaye kulipeleka taifa letu katika nyia ambayo sisi hatuko tayari kwenda huko kwa manufaa yao binafsi.

TUKITAFAKARI SAKATA LA KUZAMA MELI MV.SKATIG JE TATIZO NI WAZIRI AU MFUMO MZIMA?


MHESHIMIWA HAMAD MASOUD ALILAZIMIKA KUJIUZURU KUFUATIA AJALI YA MELI MV.SKATIG

Katika sakata hili wanazuoni wengi wamebainisha tatizo ambalo tunakabiliwa nalo kama taifa sio swala la kujiuzuru kwa viongozi, tunatakiwa kwanza tuimarishe mfumo wetu wa utendaji kwa maneno mengine mfumo ambao tunao wa kiutawala ni dhaifu. Na kielezo kimoja kati ya vingi ni pale viongozi wetu wanaziona nyadhifa zao ni sawa na hati milikizao! Hivyo kwao  hawawajibiki kuishi au kuongoza kulingana na maadili ya uongozi. Wamesahau kabisa kanuni za uongozi kuwa “Cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu kwa faida yangu binafsi au kwa faida ya familia yangu”.

DR.Bana,Mallya na Prof. Mpangala kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam waliwahi sema kuwa tunatakiwa kubadilisha mfumo hasa kwa kujenga utamaduni wa kujiuzuru Bali kuimarisha  maadili ya kazi na uongozi kwa watumishi wa serikali na pale kosa linapofanyika wahusika  wafikishwe mahakamanimara moja.

Emmanuel Mallya alisema licha ya kuwa mabadiliko yamefanyika lakini sio suluhisho kutokana na nchi kuwa na mfumo mbovu wa utawala.  
Alisema mawaziri  waliokumbwa na kashfa mbalimbali walitakiwa kusimamishwa kazi ili wachunguzwe na kama ingebainika hawana hatia wangerudishwa kazini.  “Kama wangekutwa na hatia wangefunguliwa mashitaka, hii ingewafanya wengine kuogopa kutafuna mali za umma kwa kuhofia kuwa watasimamishwa kazi na kuchunguzwa”

Dk Bana alishawahi sema kuwa dawa ni kubadilisha mfumo mzima wa utawala.  

Katika kufanikisha kuboresha mfumo bora wa utawala mti ukigolewa ungolewe wote pamoja na mizizi yake; watendaji wote katika kila ngazi wanatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kufanya hivi tutaweza kukomesha tabia ya ubinafsi inayoota mizizi ndani ya Taifa letu na kuleta kichefuchefu katika kuimarisha maadili ya kazi na maadili ya uongozi. Kwa msingi huu tunarudi pale pale kuwa “Kujiuzulu siyo utatuzi wa tatizo”,

Pamoja na kauli ya waziri wa uchukuzi wa jamuhuri ya Muungano mheshimiwa Dk Mwakyembe kuhusu ajali kuwa “Watanzania hawana sababu ya kumtafuta mchawi wa ajali hiyo kwani imetokea kwa bahati mbaya… Tukubali kwamba ajali hii ni bahati mbaya. Maofisa wetu wametuthibitishia bila kuwa na shaka kwamba meli ilikuwa nzima na haikuzidisha abiria, kujiuzulu siyo suluhisho, tushikamane katika kipindi hiki kigumu.”

Lakini je anakubali kuwa meli hiyo ilikuwa sio chakavu na kama kiongozi wa ngazi ya juu anatoa ushauri kuwa ilikuwa sahihi kwa taifa kutumia meli ambayo ilishasimamishwa kufanya kazi huko marekani? Na hivyo usajili wake ulukuwa sahihi? Na kama hivi ndivyo kwa nini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeisimamisha meli pacha nyingine ambayo haikuhusika na ajali?

Nakubaliana sana na maelezo ya  Kepteni Magamba alisema kuwa anayepaswa kulaumiwa katika ajali hiyo ni kiongozi wa safari za meli. Kiongozi huyo (Port State Controller) hupokea taarifa kutoka mamlaka ya hali ya hewa na kuruhusu meli iondoke au isiondoke. Kiongozi huyo husimamia usalama wa meli ndani na nje ya bahari kwa kushirikiana na eneo meli inapoelekea. “Meli kabla ya kuondoka lazima ifuate taratibu zote, nahodha hupata kibali kutoka Sumatra (clearance) na kuipeleka kwa ‘Port State Controller’ ambaye tayari anakuwa ameshapata taarifa za hali ya hewa,” alisema Magamba.

KWA NINI KAMA TAIFA BADO TUKO KWENYE MFUMO MBOVU WA UWAJIBIKAJI?

Kama alivyowahi sema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliitaka Serikali kuangalia upya uwajibikaji, utendaji na mwenendo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) akidai kuwa taasisi hiyo imeshindwa kuwajibika ipasavyo kudhibiti vyombo vya usafiri.

Mwenyekiti wa APPT Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Lipo tatizo katika uingizaji, ukaguzi na usajili wa vyombo vya usafirishaji wa majini… Serikali na mamlaka zinazohusika na usajili hazifanyi kazi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi waliyopewa na matokeo yake ndiyo kuruhusu vyombo vibovu kubeba roho za watu.”


Lazima tukubali kuwa tuko katika mfumo mbovu wa uendeshaji wa shughuli za serikali mfumo mzima ni mbovu (the whole system is dysfunctional). Na kama tukigundua hivi kama taifa tutakuwa tumefanikiwa kuondoa tatizo la utendaji katika shughuli za serikali. Mimi binafsi bado nafikiri kuwa watendaji wetu wakuwa kwa namna moja au nyingine wanatakiwa kuwa kama Marehemu Park Rais  wa Korea ya Kusini ambaye alikuwa anahakikisha kuwa watumishi wote ambao wamepewa dhamana lazima watekeleze wajibu wao na kama wakishindwa wanawajibishwa mara moja. Mfano mwingine tusiende mbali wanatakiwa kuwa kama Marehemu Baba Wa Taifa Julius Nyerere au Marehemu Sokoine ambao walikuwa hawana mchezo na maadili ya watumishi ambao wako chini yao; tukiiga mifano yao tunaweza kama taifa kubadilisha kabisa mfumo wa uwajibikaji.




Viongozi wetu wengi hivi sasa uwajibikaji wao ni wa maneno tu, ni mahodari wa kusema lakini ni wabovu wa vitendo kwa kiasi kikubwa. Kama alivyo wahi sema baba wa Taifa Hayati mwalimu Nyerere kuwa kwa nchi ili iweze kuendelea inahitaji: Ardhi, siasa safi na uongozi bora; hivi vitatu vikikamilika tunazungumzia uwajibikaji wa kweli na sio wa kuoneana aibu; kwa sasa taifa letu au linakosa viwili kati ya hivyo vitatu na mafanikio yetu yanabaki kuwa ngonjera;

Kama tutafanikiwa kubadilisha mfumo wa utawala na usimamizi wa shughuli za kila siku za serikali hata inapotokea kiongozi ambaye amepewa dhamana anawajibishwa italeta tofauti ya uwajibikaji; kwa hivi sasa kijiuzuru kwa viongozi wetu inabakia katika nadharia ya siasa zaidi ambayo bado haibadilishi mwelekeo wa uwajibikaji wa kweli;


Nafikiri ni wakati muafaka kwa viongozi wetu wa juu 
kufikira zaidi jinsi ya kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa serikali kwa manufaa ya wananchi wake.

MUNGU IBARIKI TANZANIA