WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, May 28, 2012

Uamsho Wakanusha Kuhusika Na Vurugu Zanzibar






THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266 
Tel: +255-777-419473 / 434145-
FAX +255-024-2250022
E-Mailjumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR

Tarehe 27MAY2012 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee 
Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika
Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na 
Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya
uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama
alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu
kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila
kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na
likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu
unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala
zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea 
kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali,
mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani
kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na
yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale
wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya
na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi 
zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa
Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya
dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia
haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya
kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na 
utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil
ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na 
kutetea haki za binadamu kwa watu wote.

WABILLLAH TAWFIQ 

Neno La Leo: Jambo La Zanzibar Ni Letu, Lakini...."



 Ndugu zangu, 

MFALME Suleiman aliambiwa ndotoni  aombe kitu chochote kwa Mola wake,  naye akajibu; “ Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” Hivyo basi, Mfalme Suleiman aliichagua hekima. Maana, niMfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, kuwa; “ Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima”.

Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepunguwa hekima ana hasara kubwa maishani. Hekima ni  tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze  kupambanua na kuamua kati ya yalo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.

Zimetufika habari; Zanzibar kuna moto unawaka. Si moto wa kuupuza.  Hekima inatuongoza katika kutambua, kuwa ukiupuuzia moto unaowaka kwenye nyumba ya jirani yako, basi, nyumba yako pia imo hatarini kuungua . Naam, ndio sababu ya kusema; Jambo la Zanzibar ni letu.

Ndio, ni letu hata sie tulio bara.  msiba wa Unguja ni msiba wetu. Hivyo, kadhia hii ya Zanzibar ni kadhia yetu. Ni wakati  sasa wa kutanguliza busara na hekima katika kutanzua kadhia hii.  Hoja ya msingi inasemwa kuwa ni suala la Muungano. Mengine ni makandokando yanayotokana na hoja ya msingi. Basi, tuujadili Muungano, kisha tuone kama kuna lingine. Maana, hata bila Muungano wa Serikali moja, sisi bado ni ndugu na majirani wa daima na milele. Tujadili basi aina iliyo bora ya Muungano ili tuendelee kushirikiana kama ndugu.

Binafsi nilifika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1988 ( pichani). Nilikuwa kijana mdogo sana. Zanzibar ndio kisiwa cha kwanza kupata kukitembelea. Tangu hapo niliipenda Zanzibar, nimefika Zanzibar mara kadhaa. Wenyeji ni wakarimu sana. Lakini, ukweli ni huu, tangu safari yangu ya kwanza Unguja miaka hiyo, wenyeji walinikumbusha, tena kwa kutamka kwa vinywa, kuwa mimi ni ' Mtanganyika'- mtu wa mlima. Hivyo, kwangu mimi, hoja ya Muungano nimeionja kwa karibu tangu mwaka 1988 nikiwa Zanzibar. 

Si jambo jema wala la kistaarabu kwa watu wachache kule Zanzibar kuchoma moto makanisa, baa na biashara za watu wa kutoka upande wa pili wa Muungano, lakini, vitendo hivi viovu vinavyopaswa kukemewa kwa nguvu zote haviwezi kumalizwa kwa nguvu za kipolisi au kijeshi, bali kwa kuzikutanisha pande zinazotofautiana kwenye meza ya mazungumzo.

Kwa hatua iliyopo sasa, bado Wazanzibari wenyewe wanaweza kukaa chini na kujadiliana kwa uwazi namna ya kwenda mbele. Lililo muhimu ni kuhifadhi amani na utulivu uliokuwepo.

Tayari kinachotokea Zanzibar kimeshakuwa na athari mbaya kiuchumi na kijamii. Kijamii, kuna mbegu za chuki zinapandwa. Ni jambo la hatari. Siku zote , chuki huzaa chuki, silaha huzaa silaha na hatimaye kupelekea uvunjivu wa amani wa muda mrefu. 

Katika dunia ya sasa ya teknolojia ya upashanaji habari, habari za uvunjivu wa amani Zanzibar zimeshasambaa duniani kote kama moshi wa kifuu. Watalii wa dunia wanataadharishwa sasa kutokwenda Zanzibar. Tunajua , baada ya kushuka kwa soko la karafuu, asilimia kubwa ya uchumi wa Zanzibar inatokana na mapato kwenye sekta ya utalii. Kadhia hii itapelekea kushuka kwa biashara ya utalii Zanzibar na hivyo kushuka kwa mapato.

Na mfano rahisi wa jinsi Mzanzibar wa kawaida atakavyoathirika, ni pale atakapoambiwa na wenye mahoteli asisitishe kupeleka samaki wake kwa vile wageni watalii wamehadimika. Na kuna vijana wengi wa Zanzibar ambao kipato chao kinategemea  sana shughuli za utalii. Nao watakosa cha kufanya, na mapato pia. Mazingira hayo huchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Na hasira pia ya wananchi, naam, midomo yenye njaa ni midomo yenye hasira. 

Kadhia ya Zanzibar inaweza pia kuathiri uchumi wa Bara hasa kwenye eneo hilo la utalii ukiachilia maeneo mengine. Mfano, kuna watalii wanaokuja Bara wakiwa na mipango ya kuunganisha safari zao hadi  Zanzibar. Kama Zanzibar hakuendeki na bara hakutaendeka pia. Hivyo, hata mapato ya bara yanayotokana na biashara ya utalii yatapungua.

Naam, huu si wakati tena wa kutanguliza propapanda. Ndio, propaganda iwekwe kando na diplomasia ichukue nafasi yake; mazungumzo, mazungumzo, mazungumzo.  Ndicho kinachohitajika sasa. Pande mbili zinazokinzana ziwe kwenye mazungumzo hadi zifikie muafaka ulio na maslahi kwa jamii pana.

Huu si wakati wa kutafuta mshindi, maana, hata tulipofikia sote tumeshashindwa. Ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Na maamuzi mengine tunayotakiwa kuyafanya sasa yasitokane na mazoea ya siku nyuma bali uzoefu mpya tunaoupata sasa.

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
kwa hisani ya mjengwa blog

Saturday, May 26, 2012

NIMEIPENDA HII NUKUU

Je nukuu hii ya Baba Wa Taifa ina ukweli wowote katika  maisha ya Watanzania leo?

Ni jambo la busara tukiendelee Kumwenzi kwa fikra zake na maono (vision) za kizalendo kwa Taifa la Tanzania na wananchi wake;


Monday, May 21, 2012

CCM Kama Barcelona! ( Makala, Raia Mwema Jumatano Iliyopita)



 Na Maggid Mjengwa,

KIJANA wangu wa miaka 16 amenieleza sababu moja kuu ya  Barcelona kushindwa kufanya vizuri msimu huu. Anasema; Barcelona wamekuwa wakiamini siku zote, kuwa kuna njia moja tu ya kucheza kandanda, na njia hiyo ni ya Barcelona!

Kwamba hata kama Barcelona walifungwa na Chelsea na wakashindwa kucheza fainali za Kombe la Mabingwa Ulaya,  Barcelona bado inaamini, kuwa tatizo si njia yao ya kucheza kandanda, bali ni bahati mbaya tu wameshindwa. Kwamba wao ndio  walistahili kucheza mechi ya fainali dhidi ya  Bayern Munich!

Barcelona wameshindwa kutambua, kuwa tatizo la Barcelona ni Barcelona yenyewe. Kwamba hata katika soka wakati umebadilika. Njia ya Barcelona kucheza kandanda ni  moja, na kuna njia nyingine nyingi za kucheza kandanda. Barcelona mpaka dakika ya mwisho hawakuwa na uthubutu wa kubadili njia yao ya kucheza kandanda, hivyo basi, kupelekea anguko lao.

Mfano wa kijana wangu wa klabu ya Barcelona ulinisukuma kwenye kuitafakari CCM na shida inayopata sasa, hususan kupoteza umaarufu miongoni mwa Watanzania na hasa zaidi vijana. Kama Barcelona, CCM nayo inaamini, siku zote, kuwa kuna njia moja tu ya kuendesha siasa katika nchi hii, na njia hiyo ni ya CCM!

Na hata CCM iliposhindwa kiti cha Ubunge Arumeru na viti vya madiwani maeneo kadhaa ya nchi, bado ndani ya CCM kuna wanaoamini, kuwa tatizo si njia ya CCM, bali kuna ‘mapungufu ya hapa na pale’ yaliyopelekea kushindwa kwao.

Kauli za hivi karibuni za baadhi ya Wana-CCM ikiwamo ya Kamati ya Abdulhaman Kinana kuwataka CCM wajiandae kisaikolojia na Katiba Mpya ikiwamo uwepo wa wagombea binafsi inaashiria CCM kuanza kuamka.

Maana, wakati  umebadilika. Na ndani ya CCM, Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete anaonekana ni mmoja wa walioliona mapema hili la mabadiliko ya wakati. Hatuwezi tena leo, kutumia nadharia za miaka 40 iliyopita kuendeshea mambo yetu ya leo katika dunia iliyobadilika. Upepo wa mabadiliko ya wakati  una tabia moja kuu; usipoendana nao, basi, utakupiga kikumbo.

Nimepata kuandika, kuwa vijana wengi leo wanaikimbia CCM na hawataki kuhusishwa nayo. Tujiulize; ni kwa namna gani vijana hawa watakuwa na mapenzi na chama kinachohusianishwa mara kwa mara, na kashfa kubwa za kifisadi. Kashfa zinazoathiri maisha yao? Kwao wao, wanayaona ‘madudu’ kwenye vazi la chama. Hatuyaoni?

Ni sawa na kisa kile cha ‘ Mfalme aliyetembea uchi’. Watu wazima walijipanga barabarani kusifia vazi jipya la mfalme huku wakiifumbia macho kasoro kubwa ya vazi hilo, kuwa lilimwacha mfalme nusu uchi. Na hata pale mtoto alipotamka; “ Jamani, mfalme yuko uchi!” Kuna waliofunika nyuso zao kwa aibu. Maana, mtoto aliusema ukweli wake.

Chama cha Mapinduzi ni chama kikubwa, kikongwe na kinachotawala kwa sasa. Lakini, kwa sasa, si chama kinachopendwa, bali kinachozidi kuchukiwa sana na kundi kubwa la vijana. Huu ni ukweli ambao, wanafiki ndani ya chama hicho hawataki kuusema, wala hawataki kuusikia ukisemwa. Ndio, ukweli mwingine haufurahishi, lakini ni lazima usemwe ili kuwasaidia wahusika kujisahihisha, kama wana nia ya dhati ya kufanya hivyo.

Tunavyoenenda sasa, ili CCM ibaki salama katika chaguzi zijazo inahitaji mawili; mosi, Katiba iliyofanyiwa marekebisho makubwa, pili, kurudisha imani ya kundi la vijana kwa chama hicho. Kwanini?

Ni ama wanafiki au wasiojihangaisha kufikiri kwa bidii ndani ya CCM ambao bado wanaamini chama hicho kitaendelea kubaki madarakani daima. Maana, hakuna uchaguzi mkuu ambao umeanza kusubiriwa kwa hamu kubwa na kundi kubwa la vijana kama uchaguzi wa 2015.

Tunaojichanganya na vijana mitaani na kwenye mitandao tunalifahamu hilo. Kwa vijana wa sasa, kuchagua upinzani ni fasheni. Ni  kuondokana na ukongwe, ni vijana wangapi wasiotaka hilo? Vijana hawa, wanaweza kuiondoa madarakani CCM hata kwa Katiba ya sasa. Katiba mpya ni salama ya CCM. Na CCM ikianguka kwa Katiba ya sasa, basi, itakuwa ni sawa na nyumba ya karata.  Yumkini kitabaki kuwa chama kwenye vitabu vya historia.

Ni ukweli pia, CCM haiwezi kutegemea kubaki madarakani kwa muda mrefu kwa kura za wazee, maana, idadi yao inapungua kila kukicha. CCM haina jinsi, bali kuungana na Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, katika kuongoza mabadiliko haya ya kihistoria katika nchi yetu. Mabadiliko makubwa ya Katiba ambayo, mbali ya mambo mengine yaruhusu uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, Uundwaji wa Serikali ya Mseto na hata  kumpunguzia Rais nguvu nyingi za maamuzi alizo nazo. Kwa kufanya hivyo, kuna hadhi , heshima na imani kwa CCM  itakayorudi.

Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine  kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa.  

Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu.
Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka.

Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Ukweli, ndani ya CCM kuna wenye hofu ya kupoteza mamlaka ya kuongoza dola. Ni hofu hiyo inayowasukuma kuwa tayari kufanya lolote lile kuzuia mabadiliko ambayo wengi sasa wanataka yatokee katika nchi hii.

Hakuna busara nyingine yeyote kwa sasa bali ni kwa CCM kuruhusu na kuendesha kwa salama mchakato wa mabadiliko makubwa yanayotakiwa na umma. Mabadiliko hayaepukiki. Ni hali ya dunia kwa sasa. Ni kama wimbi la maji ya bahari. Limeshajikusanya. Kwa CCM chaguo ni moja tu, kuenenda na wimbi hilo la mabadiliko au kukubali kufunikwa nalo.

Hilo la mwisho laweza kuharakisha kifo cha CCM. Ni jambo baya, maana, hata kama Watanzania watachagua upinzani ifikapo 2015, nchi yetu inahitaji chama imara cha upinzani, na CCM inaweza kuvaa viatu hivyo. Nahitimisha.

Habari kwa hisani ya Mjengwa blog

Saturday, May 19, 2012

Kwa nini Rais Park Chung Hee alifanikiwa baada ya kuingia madarakani?


MAENDELEO YA NCHI YANATEGEMEA SANA MAONO (VISION) YA KIONGOZI AMBAYE YUKO MADARAKANI.


Give a person a fish: you have fed the person for today.  Teach a person to fish: you have fed the person for a lifetime.”

Kumpa mtu samaki utakuwa umemlisha katika siku ya leo.ukiweza  Kumfundisha mtu  namna ya kuvua samaki  utakuwa umeweza kumsaidia kumlisha katika maisha yake yote.

Teach the person how to process and package fish for export and market it, and you have stimulated economic development.

Ukiweza kumfundisha mtu namna ya kutengeneza na kusafirisha na kuweza kuuza samaki katika masoko ya nje; utakuwa umefanikiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi

Park Chung Hee alikuwa kiongozi wa Korea ya Kusini kuanzia mwaka 1961-1970 alipo uwawa.Park Chung Hee alikuwa dikteta lakini alikuwa Rais ambaye alifanya Korea ya Kusini leo hii kuonekana tajiri. Alipoingia madarakani mwaka 1961 alikuwa na vision na vipaumbele ya maendeleo ya nchi yake kwa kutilia mkazo maendeleo ya  Elimu, kukuza technologia (ICT),Kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanakuwa na nidhamu ya kazi (dicpline) na kusimamia ukaaji wa Nishati.


Kwa taathimini ya kiuchumi wakati Park anaingia madarakani uchumi wa Korea ya Kusini ulikuwa sawa na  hali ya uchumi tunaoulaamikia sisi watanzania yaani uchumi duni na maisha magumu;

Kutokana vision na uzalendo wake kwa kujitoa kwa utendaji bora  na usimamiaji bora wa rasilimalia za taifa lake  leo hii Korea ya Kusini ni moja ya nchi zenye uchumi imara dunia na inashindana na hata kuogopewa na nchi ambazo ni tajiri duniani.

Ni takribani zaidi ya miaka 30 toka alipouwawa lakini tafiti zinaonyesha kuwa amebaki kuwa na rekodi bora ambayo imeisaidia nchi yake katika umaarufu ambao Korea ya Kusini inafurahia leo; Park alisaidia sana katika kusimamia ukuaji wa uchumi na usambazaji wa kasi  wa uwiano wa kipato, ikilinganishwa na mataifa mengine.  Kwa usimamiaji wake bora wa maendeleo kwa wote, Rais Park ilijulikana kama "unforgettable" miongoni mwa Wakorea kwa sababu ya ujuzi wake na nguvu ya usimamiaji wa maendeleo kwa wote.

Kwa nini alifanikiwa katika kuboresha uchumi wa nchi yake?

Rais Park alikuwa na tabia moja mimi naiona ni nzuri ambayo iliwashangaza waandishi wengi  ndani ya ofisi yake kuwa kuta zilitapakaa na michoro ya takwimu, ikiwa ambazo zilikuwa zikionyesha  mwenendo wa biashara, ukusanyaji wa kodi na taarifa za maendeleo ya viwanda ambayo katika nchi yeyote ile ni nguzo imara ya maendeleo. Kiongozi yeyote mwenye  maono ya  namna hii lazima awe kiongozi bora kwa maendeleo ya nchi yake.

Swali hapa viongozi wetu wanatumia muda wao mwingi wakiwa ofisini wanakuwa wanangalia data za aina gani? 
Kusoma magazeti

Je viongozi wetu wanakuwa na muda wowote wa kufuatilia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia ofisi zao?

Jambo jingine ambalo ni msingi sana ambalo pengine viongozi wetu wanatakiwa kulitilia mkazo wanapo yaangalia maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu kwa  kuendelea kutilia mkazo katika kujenga uwezo wa kiufundi unaotokana na elimu ubora katika fani ya sayansi na teknolojia. Uwezo wetu wa kiufundi ni nguvu itakayo weza kutoa njia kadhaa za maendeleo ya kiuchumi na  mvuto wa makampuni ya kitaalam ya kimataifa kuwekeza ndani ya Taifa letu kwa faida ya Taifa:

Kama taifa “pengine” tuna tunatumia misaada vibaya, lengo la misaada ambayo nchi Hisani hutoa kwa taifa ni katika katika kutatua kero ya uchumi unaotusumbua na na kuyafanya maisha ya watanzania kuendelea kuwa duni. Matumizi bora ya misaada ya kigeni, katika miradi ya miundombinu sahihi ni suluhisho namba moja wa umasikini wetu.


Watendaji wetu kuanzia Kiongozi wa juu kabisa wa Serikali yaani Rais na wengine wote wanaomfuata wanatakiwa wawe na uwezo wa Kujenga kuboresha uchumi, kupitia sera za mitazamo yakimaendeleo kwa kukuza mifumo ya kiutawala na sera zinazolenga zaidi katika kusimamia maisha na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Nimejaribu kueleza hayo yote ili kuonyesha kuwa bila kuwa na uongozi wenye maono usiotafuta faida yake wenyewe, usiokuwa tayari kuwawajibisha watendaji wabovu na wanaokiuka maadili uvunja sheria  hatuwezi kutoka hapa tulipo, tutaendelea kufurahia  kauli mbiu ambazo hazina maana wala msingi mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Kama historia inavyo onyesha kuwa  Rais Park aliingia madarakani kwa kupindua uongozi ulikuwa madarakani lakini lengo lake lilikuwa maendeleo ya Korea kusini katika hali yeyote na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi chake kama kiongozi wa nchi.

Je kwa nini sasa Nchi yetu tunafarijika ndani ya demokrasia lakini tunashindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake?

Kama taifa viongozi wetu wangeweza kuiga namna bora ya usimamiaji katka kutekeleza majukumu yao:

Swali la msingi je kuna tija au mabadiliko yeyote yanayotokana na utaratibu huu wa usimamiaji?

Tofauti na Rais Park yeye alikuwa na wasiwasi mkubwa katika kupima matokeo,na alikuwa hana mchezo hata kidogo katika hili alikuwa hana msamaha kwa wale wote ambao hawakufikia malengo ambayo alikuwa amewapangia wengi waliathibiwa kwa kufukuzwa kazi bila huruma na hii ilikuwa inatoa changamoto kwa wale wote ambao walikuwa wamekabidhiwa madaraka kwa ajili ya Taifa kuwa wawajibikaji. kwani ufanisi ulukuwa unapimwa kwa uwajibikaji na sio propaganda za kisiasa.

Serikali yetu ina hili tatizo la ufuatiliaji na uwajibishaji wa mara moja; uwajibikaji na uwajibishaji hauko katika kamusi yaviongoziwetu. pengine hili linatokana na namna watendajiwanavyopatikana; Je watendaji wetu wanapatikanaje? kupitia elimu yao? utashi wa kisiasa wa chama kilicho madarakani? au kwa misingi ya urafiki na undugu?

kama majibu ya maswali hapo juu yatalenga zadi katika utashiwakisiasa, urafiki na undugu basi uwajibishai wowote utafanyika baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi; na vision za viongozi wetu zitabaki zaidi za kwenye makaratasi ambazo zinakosa sana kipaumbele na kuthubutu.

Je baraza jipya litaleta ufumbuzi wa tatizo la umasikini?

 “watanzania wana matumaini makubwa na serikali yetu, tusiwaangushe. Njia pekee kwetu sisi ya kutowaangusha ni kufanya kazi kwa bidii”.

Nionavyo mimi Katika baraza la jipya tunao Mawaziri ambao wanaweza wakaivusha Tanzania  na kupeleka katika nchi ya ahadi iliyojaa maisha bora kwa kila mwananchi. mawaziri kama Dr.Mwakyembe, Prof. Tibaijuka, Sitta na kadhalika.

Ngoja nimchambue kidogo utendaji mzuri wa Dr. John Pombe Magufuri,   pamoja na mapungufu yake kama binadamu; Magufuri ni miongoni mwa viongozi wachache ambaye daima huwa anathubutu  na daima amekuwa akijielemisha ili kuzielewa zaidi sheria za nchi na wizara husika;  ni msimamiaji mzuri wa sheria katika utendaji wake  sio mnafiki katika utendaji wake hata kama wakati mwingine maamuzi yake yanakuwa kero kwa kwa watendaji wenzake na wananchi ambao wanakiuka sheria za nchi na zinasababisha utumiaji wa nguvu na ugumu wa utendaji na utoaji wa hudumu ya uhakika kulingana na sera au maagizo ya serikali kuu;

Kimsingi kama nilivyoainisha hapo juu inawezekana magufuli akawa na madhaifu yake lakini huwezi kuondoa ukweli kuwa ni miongoni mwa mawaziri wachache sana ambao tunao wanaofanya vizuri kazi za kusimamia hata kuchukua hatua kali kwa wakati. Hilo hata wananchi wa kawaida wanalijua na jamii ndio inayo msafisha daima.

Angalia jinsi anavyosimamia sheria namba 18 ya mwaka 2007 ambayo ilisainiwa na Rais mwenyewe ambayo inakataza watu kuingilia eneo la hifadhi ya barabara kwa kujenga makazi au kufanya biashara; pamoja na Mheshimiwa Rais na waziri Mkuu kumpunguza kasi lakini msimamo wake uko pale pale.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Sadiki aliwahi sema kuwa “Hatukatai hata kama ana upungufu wake, basi apewe sifa katika yale mazuri anayoyafanya, lakini ukweli ni wazi kuwa Magufuli ni kiongozi mchapakazi na msimamizi mzuri wa sheria na hilo halipingiki,” Akiendeleza sifa hizo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alisema siku zote utendaji kazi wa Magufuli unafuata sheria na taratibu “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, wengi tunamtambua Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, tunakuomba uendelee kufanya hivyo hivyo wala hutofeli na ukiendelea na moyo huo sote hatutafeli,” aliongeza Kabaka.

Tunacho washauri Mawaziri katika baraza hili jipya wanatakiwa wachukue tahadhari mapema wasiendelee kufanya kazi na watendaji wabovu; Kumbuka, samaki mzuri akichanganyika na samaki waliooza lazima achafuke uvundo.Mawaziri wetu wanatakiwa wajipange upya waache porojo za kujitetea kwa maneno wajitete kwa vitendo ambavyo vina tija kwa wananchi kwa maendeleo ya Taifa; Tuna imani na nanyi kama mawaziri wapya  tunawatakieni kila la kheri na fanaka katika kumsaidia mheshimiwa Rais wetu katika  kutimiza kauli mbio ya maisha bora kwa wote.


Viva baraza letu la mawaziri tunaamini kuwa baraza hilo litakuwa la kiutendaji zaidi. Litachukua mazuri ambayo Rais Park wa korea ya kusini aliyatumia katika kuboresha uchumi wa nchi yake. Nafikiri inawezekana kuiga na kuleta katika tamaduni yetu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

JE KILIMO CHA TANZANIA NI UTI WA MAENDELEO YA WANANCHI?


 Kilimo katika mataifa mengi yalionaviwanda vingi kwa sasa kilikuwa ndio 
chimbuko la ukuajiwa uchumi; waingereza walifanikiwa kuleta mapinduzi ya viwanda baada ya kujiimarisha na kuleta mapinduzi ya kilimo

kwa kipindi kirefu sasa nchi yetu pamoja na kuwa ardhi yenye rutuba nzuri na hali ya hewa nzuri kwa mikoa mingi tumeendelea kuwa omba omba wa chakula  na mbaya zaidi wanachi wetu wanaendelea na uhaba wa chakula hata katika mikoa ili yenye kila neema ya kilimo.

  • Je tatizo letu hasa ni nini?
  • Je wanasiasa wanajitetea vipi kuhusu hili?
  • Nini kifanyike kuondoa tatizo hili la kuwa ombaomba hata katika vitu ambavyo tunaiweza?


HEBU TUWASIKILIZE WANASIASA NA MAELEZO YAHO KUHUSU TATIZO NA MAFANIKIO YA KILIMO HUSUSA NDANII YA NCHI YETU





Tuesday, May 8, 2012

Mawaziri Watoa Ahadi Za Asali Na Maziwa


 MAWAZIRI na manaibu waziri wapya, wameeleza mikakati yao ya kukabiliana na changamoto wakati wa kutekeleza majukumu yao, huku Umoja wa Ulaya (EU), ukiweka bayana kuwa umefurahishwa na mchakato mzima uliomfanya Rais Jakaya Kikwete afanye mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri.

Mawaziri hao walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana katika hafla ya kuwaapisha iliyofanyika Ikulu.

EU ambao ni wafadhili katika Mfuko Mkuu wa Bajeti ya Serikali (GBS), umewapongeza wabunge kwa jinsi walivyoibana Serikali bungeni na kumwagia sifa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utouh, kwa kazi nzuri.

Katika mkutano wa Saba wa Bunge, wabunge waliibana Serikali wakitaka iwawajibishe mawaziri wanane ambao wizara zao zilitajwa katika ripoti ya CAG kwamba zilihusika na ufisadi wa fedha za umma hatua ambayo ilimfanya Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa katika baraza hilo na kuwatupa nje sita.

Mawaziri waliowajibishwa ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Mustafa Mkulo (Fedha), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na Mhandisi Omary Nundu (Uchukuzi), huku wawili, Profesa Jumanne Maghembe akihamishwa kutoka Kilimo, Chakula na Ushirika na kwenda Maji na George Mkuchika akihamishiwa Ofisi ya Rais, Utawala Bora akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
 
Mawaziri walonga

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi baada ya kuapishwa alisema atapambana na changamoto zilizopo katika wizara hiyo.

Alizungumzia pia mgomo wa madaktari uliotokea hivi karibuni akisema atafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa suala hilo halitokei tena... “Changamoto ni nyingi lakini niwahakikishieni kuwa tutapambana nazo.”

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema wizara hiyo ina matatizo mengi lakini hawezi kuwa mwarobaini wake bali, atapambana na matatizo hayo ili Uchukuzi iwe ni wizara inayoeleweka na kama ikishindikana atasema.

“Nachukulia kawaida mgawanyo wa kazi, tunaomba muda wa kujua matatizo na kuyarekebisha, tutakuwa tukitoa taarifa,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema vipaumbele ni vingi vya kufanyia kazi akigusia kusimamia Bandari, Reli na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwamba maeneo yote hayo yanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema umeme ni kipaumbele muhimu kwake akisema sasa anashangaa kwa nini nchi haina megawati 1,500 za uhakika.

Alisema atahakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika na kujitahidi kuwa na megawati zipatazo 5,000  ambazo zitasaidia kukuza uchumi na kupunguza makali ya umeme kwa wananchi.

“Mimi siyo mwanasiasa, nimesomea Jiolojia na ninamudu nafasi hii. Haiwezekani hadi sasa ni asilimia 14 tu ya Watanzania ambao wanapata umeme tena usio wa uhakika. Nitakachokifanya ni kuongeza watumiaji wa umeme na kupunguza gharama zilizopo.”

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema akishirikiana na wizara nyingine atashughulikia tatizo la mfumuko wa bei ambao unaathiri wananchi wenye kipato cha chini. Pia aliahidi kupunguza gharama za ufanyaji biashara na kuondoa urasimu.

“Lazima tupunguze gharama za ufanyaji biashara. Pia tutaangalia yale yaliyozungumzwa bungeni na kuyafanyia kazi,” alisema Dk Kigoda.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema uteuzi wake ni changamoto kubwa akisema ana shaka kwamba wizara anayokwenda ina matatizo lakini akasema lazima wananchi wapate faida ya rasilimali zao na kwa kufanya hivyo ataanzia kwenye ripoti ya CAG  kusafisha njia.

“Watanzania watuangalie utendaji wetu wa kazi. Lazima tuondokane na tabia ya ripoti kuvumbua uovu na kuziacha tu zikapita. Nitahakikisha ripoti ya CAG haipuuzwi. Wizara hii watu wanakula vibaya hivyo nitawashughulikia na haya matatizo ya vitalu na wizi wa nyara za Serikali yote nitayashughulikia.”

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alisema Watanzania wategemee Katiba bora ambayo watakuwa wameshiriki kikamilifu kuiandaa... “Tutapokea mawazo ya wananchi kwani ushirikishwaji ndiyo utakaotufikisha.”

Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema jambo la kwanza atafuatilia mwenendo wa matumizi ya fedha za Serikali pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watendaji.

Alisema ili aweze kufanikiwa katika hilo, atasimamia vizuri fedha za umma ili zitumike katika shughuli zilizokusudiwa jambo ambalo linaweza kupunguza ufujaji wa fedha za Serikali. Alisema mkakati mwingine ni kuimarisha thamani ya shilingi.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Maselle alisema Watanzania wategemee mabadiliko makubwa katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kuboresha shughuli zao na kuleta tija kwa kundi kubwa la watu.

“Wachimbaji wadogo wanafanya kazi katika mazingira magumu, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa malalamiko ya hapa na pale, mkakati uliopo ni kuweka utaratibu madhubuti ambao utaweza kuwalinda katika shughuli zao,” alisema Masele.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni, Amos Makala alisema Wizara yake ina changamoto nyingi ikiwemo upande wa michezo, hivyo atashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa maendeleo ya michezo yanapatikana.

Alisema kutokana na hali hiyo watendaji wake wanafanya kazi kwa ufanisi zaidi jambo ambalo linaweza kusaidia kukuza michezo nchini.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema taifa linakabiliwa na changamoto nyingi hasa za ukosefu wa nishati ya umeme jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa malalamiko mengi hivyo kuahidi kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa nishati hiyo inapatikana jambo ambalo linaweza kupunguza adha ya mgawo.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema atahakikisha kunakuwa na elimu ya sayansi ili kuzalisha watafiti wazalendo katika masuala mbalimbali akisema elimu hiyo itasaidia pia sekta ya mawasiliano katika nyanja mbalimbali za mawasiliano, sayansi na teknolojia.

“Mkakati wangu ni kuhakikisha kunakuwa na kipaumbele katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi mbalimbali iwe ya elimu ya juu au binafsi ili kuhakikisha kuwa ripoti zake zinafanyiwa kazi.”

Alisema, lengo ni kupiga hatua za kimaendeleo pamoja na kuhakikisha kuwa tafiti hizo zinaleta tija kwa maendeleo ya taifa ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zilizojitokeza ili ziweze kufanyiwa kazi katika maeneo husika.

Alisema hali hiyo inaweza kufumbua matatizo mbalimbali ambayo Serikali inapaswa kuyarekebisha jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa taifa zima.

“Tafiti hizo zitaweza kutoa dira ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini jambo ambalo linaweza kuboresha utendaji kwa wafanyakazi na kukabiliana na changamoto za kimaendeleo zinazojitokeza,” alisema.

Kwa upende wake, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema hana kinyongo na hatua iliyochukuliwa na Rais... “Sina kinyongo miaka mitano ya Nishati na Madini si mchezo.”

Mawaziri walioapishwa jana ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Hussein Mwinyi (Afya na Ustawi wa Jamii), Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Hawa Ghasia (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi), Mathias Chikawe( Katiba na Sheria), George Mkuchika (Ofisi ya Rais, Utawala Bora) na Celina Kombani (Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma).

Wengine ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk William Mgimwa (Fedha) na Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini).

Naibu waziri ni Adam Malima (Kilimo, Chakula na Ushirika), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii), Gregory Teu (Viwanda na Biashara), Pereira Ame Silima (Mambo ya Ndani), Charles Kitwanga (Ofisi ya Makamu wa Rais), Jerryson Lwenge (Ujenzi), Dk Seif Radhid (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge (Maji), George Simbachawene na Steven Maselle wote Nishati na Madini, na Januari Makamba( Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine ni Dk Charles Tizeba (Uchukuzi), Amos Makalla (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Angela Kairuki (Sheria na Katiba), Janeth Mbene na Saada Mkuya Salum wote Fedha.

EU yamwaga sifa

Wakizungumzia hatua hiyo, mabalozi wa EU wamesema kubadilishwa kwa mawaziri, ripoti ya CAG na mapendekezo ya wabunge kuhusu ripoti hiyo imeonyesha demokrasia ya kweli kwa Tanzania.

Balozi wa EU nchini, Filiberto Ceriani Sebregondi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuzindua wiki ya umoja huo kwa mwaka 2012.

Balozi Sebregondi alisema umoja huo umefurahishwa na mchakato ulivyokwenda kuanzia kwa CAG mpaka mabadiliko ya mawaziri na kusema huko ndiko kuendeleza demokrasia ya kweli.
Alisema kutokana na mabadiliko, watakutana hivi karibuni na kujadili namna ya kusaidia Bajeti ya Serikali ya Tanzania... “Tunafurahi na mabadiliko hayo kwa kuwa yataleta manufaa kwa jamii na hivi karibuni tutakaa na kutangaza kiasi tutakachochangia katika Bajeti ya Tanzania ya mwakani.”

Balozi wa Ujerumani nchini, Klaus Peter Brandes alisema wamefuatilia na kuona majibizano yaliyokuwa yakifanyika bungeni na wamefurahishwa na mazingira aliyowekewa CAG katika kufanya kazi.

“Tumefuatilia na kuona majibizano bungeni, Serikali imefanya vizuri, tunafurahi kwa CAG kufanya alichoagizwa kwa maendeleo ya Tanzania nasi hivi karibuni tutaangalia mataifa yetu tutachangia kiasi gani kwa ajili ya bajeti ijayo,” alisema.

Balozi wa Sweden, Lennarth Hjelmaker alisema: “Tumeona kuwa ripoti ya CAG imeonyesha ukweli na wote tunaunga mkono kilichotokea katika mabadiliko ya mawaziri na mchakato wa bungeni Dodoma.

Habari hii imeandaliwa na Boniface Meena, Festo Polea na Ibrahimu Yamola
 Chanzo; http://www.mwananchi.co.tz

Sunday, May 6, 2012

SIMBA YAMCHAKAZA MPINZANI WAKE WA JADI YANGA MABAO 5 - 0

MATUKIO YA MCHEZO KATI YA SIMBA NA YANGA

SIMBA BINGWA




















PICHA KWA HISANI YA  JOHN BUKUKU FULLSHANGWE BLOG NA KAMANDA RICHARD MWAIKENDA.

Saturday, May 5, 2012

ZITO KABWE NA SALAMU KWA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI


Zitto: Mawaziri Hakuna Sherehe Bali Waanze Kazi



Juhudi za kurejesha misingi ya uwajibikaji katika utumishi wa umma zimeanza kuzaa matunda Baada ya Rais kutekeleza shinikizo la Bunge la kuwafukuza kazi baadhi ya Mawaziri ambao Wizara zao zimetuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na utendaji mbovu. Mawaziri 6 wamefukuzwa kazi baada ya kugoma kujiuzulu wao wenyewe, manaibu Waziri 2 wamefukuzwa pia.
Ndugu George Mkuchika alitakiwa kujiuzulu, akajiuzulu lakini Rais amemrudisha kwenye Baraza Kama Waziri wa Utawala Bora. Yeye nampongeza kwani hakuwa na makuu ya kuanza kujitetea Kama wengine. Atakuwa ametoa funzo kwa wenzake.
Kwa kawaida wateule hufanya sherehe kwa kuteuliwa kwao. Nitawashangaa watakaofanya sherehe safari hii kwani hakuna cha kufurahia. Nitawashangaa Watakaokwenda kuapa na Maua kwa furaha kwani furaha itakuwa ya muda mfupi tu. Mkutano wa Bunge wa Bajeti ni mwezi ujao tu na Wateule wote watakuwa kikaangoni. Too short honeymoon.

Hakuna cha kusherehekea kwa sababu nchi in changamoto nyingi sana. Changamoto ya kuzalisha umeme wa kutosha na kuusambaza kwa wananchi wengi, changamoto ya kukuza uchumi wa vijijini na kukuza uzalishaji viwandani ili kutengeneza ajira kwa vijana, changamoto ya kuongeza mapato ya Utalii kutoka katika hifadhi zetu na kuvutia watalii zaidi katika nchi yetu.
Nimewapigia simu wateule wengi na kuwaambia, siwapi pongezi Bali nawatakia kazi njema. Nawatakia uwajibikaji mwema. Uwajibikaji ndio msingi wa kupambana na rushwa, uvivu na uzembe.

Kwa Waziri wa Fedha, ambaye mimi ni Waziri Kivuli wake (Kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni hataniwajibisha pia), namwambia uteuzi wake ni changamoto kubwa sana katika maisha yake.
Hivi sasa eneo lenye Bajeti kubwa kuliko zote nchini ni huduma kwa Deni la Taifa (services to national debt). Lazima kuangalia upya Deni la Taifa. Hivi sasa Deni la Taifa ukijumlisha na Dhamana za Serikali (government guarantees) limefikia tshs 22trn mpaka Desemba 2011. Nimewahi kutaka ukaguzi Maalumu katika 'account' ya Deni la Taifa. Linarejea wigo huu. Tunalipa takribani 1.9trn tshs kwa mwaka kuhudumia Deni la Taifa. Zaidi ya Bajeti ya miumbombinu, Afya, Maji, Umeme nk.

Mfumuko wa Bei, misamaha ya kodi na kodi zinazozuia watanzania kujiajiri ni changamoto kubwa sana Wizara ya Fedha lazima ihangaike nayo.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na hasa usimamizi wa Hisa za Serikali katika kampuni binafsi ni masuala yanayohitaji masuluhisho sasa na sio baadaye.

Kwa Mwalimu wangu dkt. Mwakyembe, utakumbukwa kwa Jambo moja tu. RELI. 'make Railways system work'. Hutakuwa na 'legacy' nyingine isipokuwa Reli maaana Bandari bila Reli ni sawa na Bure.
Tunatumia zaidi ya tshs 300bn kwa mwaka kukarabati barabara wakati tunahitaji tshs 200bn kukarabati Reli iweze kusafirisha mzigo kwenda Bandarini na kukupa Bandarini.
Ndio maana nasema hakuna Jambo la kusherehekea maana wajibu mliopewa na Rais ni mtihani mkubwa kwenu katika kukitumikia Taifa letu. Msipowajibika, mtakumbwa na fagio la chuma!

Mkisha kula kiapo, kimbieni kazini. Nothing to celebrate. Hit the ground running.

ZITO ZUBERI KABWE
Dar-es-Salaam
Jumamosi, Mei 5 2012